The Chant of Savant

Wednesday 12 October 2016

Kijiwe chataka scorpion askopioniwe


1475740986581.jpg 
            Tukio la kinyama la mchovu mmoja kutobolewa macho baada ya kupora na kutupwa barabarani ili agongwe na magari limeudhi kijiwe hakuna mfano. Leo kila mwanakijiwe anaongelea unyama huu tena bila huruma wala kuchelea chochote.            Anayeanzisha mjadala ni Kapende anayesema “jamani mnasemaje kuhusu tukio la mwenzetu kutobolewa macho kinyama na mnyama anayeendekezwa lupango badala ya kuskopiniwa naye? Mwenzenu hadi usawa huu sijaelewa mantiki ya kumhifadhi bazazi na habithi huyu. Je hii ni haki kwa mhanga ambaye maisha yake yameharibiwa milele. Hakuna kinachokera kama kuona mhusika akiendelea kuona, kutabasamu, kula na kulala bure badala ya kutendewa kama alivyotenda.”
            Mgoshi Machungi anajibu “kama yeye aimskopion mwenzake hadi akapoteza macho, kwanini naye asiskopieniwe ii aonje adha ya kazi na matokeo ya unyama wake? Huyu angekamatwa na kufungwa kamba na kufanyiwa kitu mbaya kabua ya kukatwa mkono, mguu mmoja na kutobolewa macho yote halafu akaachiwa aonje utamu wa maisha. Ingekuwa Ushoto tingemtoa na kumtoa hadi anyatuke loho.”
            Sofia Lion Kanungaembe anamchomekea Mgoshi “hata mimi sina huruma na mnyama huyu. Naungana na wale wanaotaka atobolewe macho ili haki itendeke na liwe somo kwa maskopioni wengine ambao hawajakamatwa.”
            Msomi Mkatatamaa anapinga wazo la jicho kwa jicho. Anasema “je kama wote tutaamua kufanya jicho kwa jicho tutakua na vipofu wangapi kayani? Isitoshe, huyu jamaa hajapatikana na hatia na kuhukumiwa na mahakama kama sheria inavyosema. Lazima tuheshimu utawala wa sheria na kuhakikisha mhusika anashughulikiwa kisheria na kuepuka kutenda yale tunayopinga na kuchukia. Je kama scorpion akitobolewa macho, hili litamrejeshea macho mhanga? Bila shaka jibu ni hapana. Hatuwezi kuwa kaya ya makatili tukawa salama ingawa tunao maskopioni kibao ambao unyama wao tumeamua kuupuuzia au kuuvumilia kama jamii.”
            Naungana nawe Msomi hapa. Nadhani tusilaumu hawa vijana. Unategemea nini midawa na bangi vinapohalalishwa kiasi cha kuwabangua akili? Nani wazazi wao kama siyo sisi? Nani viongozi wao kama siyo wao? Nani wanalinda mitandao yao kama si ndata? Unategemea nini kaya inaporuhusi kila mchovu kuchuma bila kutoa maelezo? Nadhani hapa ndipo mzizi wa maovu, unyama, rushwa, ufisadi na ubinafsi ulipojichimbia. Ukateni basi badala ya kupapasa juu juu. Kamateni waliolea kadhia hii tokana na ima ujinga au uroho wao au sababu zozote ziwazo badala ya kuwaenzi na kuenzi jinai yao,” anajibu Mijjinga huku akiwasonya hao anaowatuhumu kuharibu kaya yetu.
            Mipawa anapinga, “mnaongelea kufuata sheria na kuwa mtuhumiwa. Kwani yeye alifuata sheria alipofanya unyama huu au aliidharau? Sheria inapaswa imdharau kwanza apewe stahiki yake. Naona huyu abanwe nyeti zake aseme lini alijifunza huu unyama, kwanini, ameufanya kwa muda gani. Ashughulikiwe hadi awataje washirika zake hata wahanga wa unyama wake. Vinginevyo mascorpion ambao hawajatiwa nguvuni wataendelea kunyanyasa raia wema kana kwamba hakuna lisirikali. Tukatae uskopioni huu na tuhakikishe tuchimbua mizizi yote ya unyama huu.”
            Mzee Maneno anachomekea, “yakhe mie nshangaa. Hivi hawa ndata wetu walikuwapi hadi huyu habithi afanye unyama bila kuchukuliwa hatua wala kushughulikiwa vilivo? Je hawa walipwa kwanini ; na waliponkamata kwanini wasimpe dawa yake huko huko korokoroni yakesha watu wakaendelea na mengine? Kwani hawakusikia rahis alivosema kuwa hawana haja ya kumwachia jambazi silaha au huyu hakuwa nayo wakati kila ntu ajua anayo hadi sasa?”
            “Ami umeniacha hoi. Hiyo silaha gani unayoongelea ambayo sisi hatuioni wala haijaonyeshwa kwa pilato?” anauliza Mchunguliaji aliyekuwa bize akisoma gazeti.
            “Fumbo nfumbie njinga mweleve ang’amua ati. Wataka nsema nkubwa alimaanisha uhai au nin?” Mpemba anajibu huku akicheka.
            Kanji akwanyua mic “veve fikiria kama mimi. Iko chukia hii jana na kama nafanyia kitu baya mimi haiko pinga. Ile nafanyia kijana nyingine bay asana sana dugu yangu. Mimi naona ile kijana natoa jicho nalia chozi kuba kweli kweli. Kama data naamua basi maliza yeye ili ionje tamu ya kazi nafanyia hii mtu maskini.”
            Mheshimiwa Bwege naye hajivungi; anasema “nakubaliana na mzee Maneno kuwa huyu hayawani ana habari na ushahidi muhimu unaoweza kutusaidia kujua ukubwa wa tatizo ili kulishughulikia vilivyo na kunusuru maisha ya watu wema na wasio na hatia.  Kwa kuanzia angetobolewa macho ili aweze kusema vizuri. Lazima abanwe ili aeleze ukweli wote ili tuondokane na kadhia hii mara moja. Nadhani hata ndata kuna wanachojua ambacho kiliwafanya wachelewe kubaini unyama huu kwa muda ulipotendeka. Sijui kama aliyetobolewa macho angekuwa ndata kama huyu scorpion angekuwa hai akibembelezwa kwa kulala na kula bure akisherehekea ushindi wa unyama wake. Kweli kaya yetu ni Danganyika aka Bongolala.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita karandinga la magereza likimpeleka scorpion lupango. Acha tulitoe baruti ili tumtoe na kumtoboa macho afaidi kama alivyowafanyia wenzake! Kama siyo ndata kutuzuia mkarandinga ukaishia, huenda jamaa angekuwa kipofu kama siyo maiti kwa sasa. Hivyo, tutoe onyo kwa masikopioni ambao hawajakamatwa kukaa mkao wa kuliwa. Hatutakubali tukio jingine kama hili; kama noma na iwe noma. Wenye masikio wamesikia; na wenye macho wamesoma.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: