Wednesday, 5 October 2016

Kijiwe chalaani upumbavu wa Iringa Mvumi


          Kitendo cha kinyama kilichotendwa na wananchi wa kijiji cha Iringa Mvumi kimeacha kijiwe na simanzi, hasira na hata kutaka kulipiza kisasi. Baada ya kuzinyaka kuwa maafisa wa Kituo cha Utafiti wa udongo na maendeleo ya ardhi Seliani mkoani Arusha waliteketezwa kwa moto na wauaji waliowadhania ni wanyonya damu, kijiwe kinatoa amri kwa lisirikali kuhakikisha wote waliotenda unyama huu wanashughulikiwa kikamilifu.
            Mpemba anaingia na gazeti la Uvumi Leo. Analitupa mezani huku akisonya na kusema “yakhe twendaapi kama baadhi ya wenzetu wawezajichukulia sharia nkononi na kuua watu wasohatia kama ilivotokea kule kwa akina Agwe jana? Wallahi mie sikujua kuwa hata baada ya kupata uhuru bado kaya yetu ina watu wajinga na wakatili kama hawa.”
            “Kaka unashangaa hawa wauaji uchwara waliosukumwa na ujinga, ujuha na upumbavu siyo! Hiyo ndiyo kaya yetu. Hushangai kuona wachovu wanavyoshabikia kuua vidokozi na vibaka huku wakinyenyekea na kushobokea mibaka kama ile ya Escrow, Epa, UdA, Kagoda, na mingine mingi iliyotamalaki na kutapakaa kayani? Hushangai vibinti vyetu vinavyonyotolewa na ngoma kutokana na ujinga na umaskini?” anajibu Kapende huku akionyesha wazi kuchukia.
            Mgoshi Machungi anakula mic “waahi angekuwamo ndugu yangu ningekwenda Ushoto kumtafuta shemtwashua na vijana wetu tiende kue tiwachome nao moto kama siyo kuchoma wake zao kama wangetokea kukimbia. Hata kama ni wajinga, hawa siyo binadamu kusema ue ukwei.”
            Mijjinga anakula mic “japo hawa wauaji na washenzi siwatetei, siwezi kuwalaumu wao peke yao. Nawalaumu walioteka uhuru wetu huku wakichezea kaya yetu kiasi cha kuacha wachovu wetu wawe wajinga na wakatili wa kutupa kiasi hiki. Wana bahati. Laiti waliokufa wangekuwa ni jamaa zao majambazi. Bila shaka wangekitokea hiki kijiji siku moja na kulipiza kisasi kwa kuua wauaji wenzao kama wadudu.”
            Msomi Mkatatamaa anasalandia mic “siwezi kuficha hasira, mshangao, uchungu na kichefuchefu nilivyopata baada ya kusikia habari hizi za kijima kwenye redio. Kwanza, nilidhani nilikuwa nimesikia vibaya. Pili, nilishani haya mambo yametokea sehemu nyingine duniani lakini si Bongolalaland. Hivi kweli bado kuna watu duniani wanaamini kwenye hekaya za mumiani, vibwengo na majini! Ama kweli, aliyesema kuwa aliyeroga kaya hii aliishafariki hakukosea. Je tunajifunza nini kutokana na kadhia hii? Kwanza, tunajifunza kuwa watu wetu ni wakatili wanaoweza kufanya lolote ima kwa woga au kutafuta mlo. Rejea wanavyoua watu wenye ulemavu wa ngozi. Pili, tunajifunza kuwa watu wetu walio wengi ni wajinga wanaoweza kuamini kila kitu. Rejea kutamalaki kwa dini za kishirikina, waganganjaa wa jadi na matapeli kila aina bila kusahau hata vyama vya siasa.”
            Anapiga chafya na kuendelea “huu ni ushahidi tosha kuwa kaya yetu iko hatarini. Leo tunaua wenzetu kwa imani chafu na haba kama hizi. Kweli kesho tutashindwa kuuzana kama walivyofanyiwa mababu zetu waliouzwa utumwani? Mnadhani wote walikamatwa kwa nguvu? Wapo waliouzwa na ndugu zao sawa na viongozi wengi waliopita waliouza kaya hii kwa wachukuaji waitwao wawekezaji ukiachia mbali maafisa wa serikali wanaoendelea kuuza kaya hii ima iwe ni kwa kupewa kitu kidogo kama vile kuuza uraia na vyeti vya kuzaliwa vya wananchi na mengine mengi.”
            Mipawa anampoka Msomi mic “mie nangoja kuona hatua zitakazochukuliwa katika kuadhibu huu ujinga na jinai ya mauaji ya watu wasio na hatia. Nangojea kusikia nini sirikali itafanya kuhakikisha haki inatendeka na hili linakuwa somo kwa wengine wenye mawazo mgando na ya kinyumenyume kama hawa. Ama kweli, agwe wameamua kututia aibu kama kaya. Napendekeza wote waliohusika na unyama huu wakamatwe na kuchukuliwa hatua mara moja ili haki itendeke na liwe somo kwa wengine.”
            Sofia lion aka Kanungaembe anakwanyua mic “naomba nikuchomekee kidogo. Napendekeza kila kijiji kiwe na kituo kidogo cha polisi ili yanapotokea mazonge kama haya polisi waweze kusaidia kuzuia mauaji ya watu wasio na hatia.:
             “Nami vacha nichomekee veve dada yangu. Naunga kono na guu veve. Ile pesa silingi milioni hamsini kijiji napewa basi kijiji natumia kulipa polisi.”
            Mheshimiwa Bwege aliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kula mic “wote mmetoa mapendekezo ya msingi. Ila mmesahau jambo moja kubwa; yaani kumuua adui aliyesababisha mauaji haya tunayoongelea yaani ujinga. Nakumbuka zama za mchonga, angalau kulikuwa na elimu ya ngumbaru. Mnategemea nini kaya inapokuwa na wajinga wengi? Bila shaka haya ndiyo matokeo yake. Kama kundi dogo la wezi linateka kaya kama mlivyoshuhudia sehemu mbalimbali kama vile bandari, viwanja vya ndege, mipakani, TRA, uhamiaji na kwingineko huku kila mchovu akitegemea usongo wa dokta Kanywaji mnategemea nini? ili kuondokana na ujinga na ujima huu, tuache kumbebesha mzigo dokta Kanywaji. Tumbane atuletee katiba mpya ambayo itaeleza upya haki za wachovu. Vinginevyo tujinyamazie na kuacha kulalamika. Kwani kwa mwendo huu, watakufa wengine wengi tu.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si daladala likapata panchali. Acha tutimke–kwa ujinga wetu–tukidhani ni bomu la nyuklia!
Chanzo: Tanzania Daima jumatano leo.

No comments: