TUKIWA kijiweni tukitafakari jinsi mafisi na mafisadi walivyopanguana na
kupangana kule Idodomya si Dk. Mpemba kaja na mpya.
Anaingia akiwa anaimba: Uangusho, uangusho, uangusho, Karumekeenge naye yumo
ati! Hatumuelewi kwanza.
Mara Mbwamwitu anaamua kumtolea uvivu. Anasema, “Ami leo kunani au nawe
umejiunga na uangusho baada ya kuchoshwa na ndoa ya Maalim Madefu wa Kafu?”
Mpemba kaguswa pabaya! Anakwanyua mic na kuchonga, “Kwanza mie si mwanachama
wa Kaafu. Pia si wa kundi hili la kigaidi la Uangusho ambalo hakika miye naona
la magamba,”
Mbwamwitu hakubaliani naye. Anamuuliza, “Sasa kama wewe siyo hao alkaida
sorry Uangusho mbona unaimba wimbo wao hata kama unawaita makenge?”
Mpemba anajibu, “Miye sijasema eti uangusho makenge ati. Lau wangekuwa
makenge tusingewahofu hawa. Hawa alkaida ati. Nisemacho ni kwamba Karume -kenge
aliyepitishwa na hao mafisadi wenzake kuwa rahis wa Zenj ameumbuliwa nao hao
wenzake.”
Kabla ya Mbwamwitu kudakia, Dk. Mgosi Machungi anatia buti, “Shisi hatikieewi
inaposema Kaumekenge naye yumo. Kwani huyo Kaumekenge ni nani hadi
akushughuishe?”
“Yaani wewe hujui Karumekenge ni nani wakati ni mtoto wa Abdi aitwaye Ama..
Yatosha jamani mshamjua kuwa ni yule jamaa aliyepitishwa kuwa rahis wetu wakati
hakufaa na sasa ameamkia kwenye uangusho,” Alisema Mpemba huku akibwia gahawa
yake.
Kabla ya Dk. Mpemba kuendelea Profesa Msomimkatatamaa aliingilia kati, “ Ami
kumbe hukuwa unaujua mchezo mzima! Hawa wanasiasa uchwara walioondoka kwenye
ulaji wa bure wakiwa wanautaka wanatafuta mwanya wa kutengeneza nyufa ili
waonekane wakombozi hali itakapokuwa mbaya,”
Anabwia kahawa yake na kutazama huku na huku na kuendelea, “Ingawa wanaweza
kujiona wajanja kwa hujuma na upuuzi wanavyofanya, moto wanaotaka kuuwasha
hawawezi kuuzima. Si wao na hao vibaraka wao wala mabwana zao. Tunapaswa
kuwashughulikia mapema kabla hawajatugawa kwa tamaa zao.”
Kila mtu ameweka mkono kwenye tama akisikiliza mapwenti ya Msomi wetu
kijiweni. Kabla ya kuendelea, Dk. Kidevu anamuuliza swali, “Pworofwesa, unataka
kutwambia kuwa hata manyang’au mafisi na mafisadi nayo yameanza kushtukiana
kiasi cha kuanza kuzomeana kama walivyomfanyia Karumekenge aliyewatusi kuwa wana
ubongo wa samaki?”
Dk. Mipawa halazi damu, ankwanyuma mic, “Nadhani kama magamba yaliyomzomea
Karumekenge yana ubongo wa samaki basi yeye anao wa kenge kama jina lake,”
Wanywa kahawa hawana mbavu kwa jinsi Dk. Mipawa anavyowapaka mafisi kwa
maneno makali yenye lafudhi ya kisukuma.
Wakati watu wakiendelea kuvunjika mbavu, Dk. Mgosi Machungi anakatua mic,
“Dokta Mpemba hemu tiambie. Hivi nkwanini nyinyi huko mnapenda kutumiana?”
Kabla ya kuendelea Mpemba anajihami, “Yakhe sasa haya ni matusi. Twatumiana
vipi wakati watu wajinga wajinga wataka waonekane wajua wakati hawajui kitu Kama
huyu Karumekengee,”
Anavuta sigara kali yake na kumpasia kichungi Mbwamwitu na kuendelea, “Kama
magamba yatumiana nyuma ya pazia usiseme ni sote. Wao kwelii watumiana tena kwa
siri na wazi wazi. Sie wanannchi twapinga kutumiwa ndo maana wale watu toka
vi-island walimzomea Karumekenge.”
Dk. Mgosi Machungi kanogewa anaamua kukwanyua mic tena, “Kama huyu Kaumekenge
ndiye uangusho yawezekana ndiye aitoa bendera yetu kwa waiani kufanyia biashaa
yao ya haramu, hebu tijaribu kufikii pamoja.”
Dk. Mchunguliaji haniangalii mwenyekiti lau nimruhusu. maana tangu mada ianze
inaonekana kama mwenyekiti sina kazi na kama ninayo basi mimi boya. Anyways, I
have decided to let the vent. The whole schemata are supposed to look like that
in such kind of circumstance. Lol! Nimevutiwa hadi nikaonyesha usomi wangu.
Anyways, kikameruni kinajua kung’ang’ania ubongo.
Dk Mchunguliaji aliendelea, “Kumbe Dk Mgosi ulikuwa hujui hili! Mbona kila
mtu anajua ni nani alichuuza bendera yetu kwa wanaharamu wale.”
“Mimi naona tuachane na mambo ya Karumekenge na ukenge wake wa kuangusha
akijitia uamsho. Hebu jamani tuchambue hii NEKI mpya iliyoundwa juzi na wabaya
wetu,” Alipendekeza Dk. Mipawa.
Dk. Machungi anadakia, “Ie NEKI kwei neki. Maana ukiangaia mijitu yenye
uchafu kama Phil Jaff Mangu na Zaki Mengjii unashangaa na kugundua kuwa kumbe
kazi ya inzi ni mbaya. Hivi hawa waiosababisha wizi wa HEPA wana jipya gani
zaidi ya kuja kusuka wizi mwingine?”
“Du Mgosi sikuwezi kwa kukumbuka mambo makubwa kama haya. Tena jana nilisoma
kwenye gazeti la Tanzania Ever Dk. Silaha akizidi kumkaba shati Phil Mangu,”
Alichomekea Dk Mbwamwitu.
Profesa sasa kafika mwake. Anakatua mic na kuanza kutoa lecture, “Nadhani
wengi hawajui kuwa haya ni maandalizi ya wizi wa njuluku nyingine kwa ajili ya
uchakachuaji na uchafuzi ujao.
Ingawa baada ya Mangua kukamilisha dili ya HEPA na kusababisha ushindi, Njaa
Kaya alimpiga kibuti na kumteua mropokaji Yusuf Ma-rope kwa kuogopa Mangua
angemsumbua kutokana na kujua dili ya Hepa.”
Anachukua kashata na kuila na kuendelea huku akikohoa kuweka koo vizuri,
“Hapa hakuna cha NEKI mpya wala nini bali ni kukusanya wazoefu ili wafanikishe
ujambazi mwingine.
Mada ikiwa inaanza kukolea si likapita gari la Karumekenge likimuwaisha
Airport. Wote tulisimama na kuanza kulisindikiza kwa wimbo ule ule ulioanzia
Idodomya. Uangusho, uangusho, uangusho, uangusho, uangusho hadi wapita njia
wakaanza kutujalia.
Baada ya kuona ndata nao wanaanza kujisogeza wakidhani nasi tumepagawa kama
akina Shehena Pondwa tuliamua kuvunja kikao. Uangusho uangusho nanyi mandata
uangusho kama Karumekenge. Nadhani kaya yetu sasa ya uangusho maana kila mtu
anaangusha mwenzake. Ngoja nami niende kuangusha.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 21, 2012.
|
|
2 comments:
Kumbe wengi wenye ubongo wa samaki
Hasa wale walioishia Form Four na wanapenda kujiita "Doctor"
Post a Comment