KWA wanaokumbuka, Makamu Mwenyekiti mpya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Philip
Japhet Mangula, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, watakubaliana nami kuwa
aliondolewa kwenye nafasi ya ukatibu kwa aibu ya aina yake.
Pamoja na kukitumikia chama kwenye nafasi ya ukatibu chini ya uenyekiti wa
Benjamin Mkapa na kusuka mpango wa kuiwezesha CCM kushinda, Mangula alitupwa nje
na Rais Kikwete pindi aliposhika wadhifa huo.
Wachambuzi wengi wa mambo, wakati ule, waliona kama Rais Kikwete alikuwa
ameonesha kigeugeu katika kupangua watendaji wa Mkapa na kuweka wake wakati
akijua fika kuwa ni Mkapa na Mangula waliomsaidia kushinda na hata wakati
mwingine kusaka fedha haramu kama za EPA kama ilivyowahi kudaiwa na mwanasheria
aliyesimamia dili hili zima, Michael Bhyndika Sanze.
Mengi yalisemwa juu ya urais wa Kikwete kuanzia shutuma za wizi wa pesa ya
umma kutoka kwenye Benki Kuu chini ya kashfa ya EPA ambayo Kikwete aliizima
baada ya kukabidhiwa mikoba.
Yalisemwa pia ya Kikwete na kampeni zilizotumia pesa ya EPA kuwahonga wapiga
kura baada ya kuwachafua wagombea walioonekana kuwa tishio, hasa Salim Ahmed
Salim ambaye uzalendo wake ulitupwa kando na kuitwa Mwana Hizbu, hata Mwarabu
wakati ni Mtanzania safi.
Kwa wanaojua mchezo mzima, kilichomponza Mangula hakijulikani wazi na bado
kimeacha maswali kwanini Kikwete alimtema haraka, hivyo huku akimkingia kifua
Mkapa?
Si Mkapa, Mangula wala Kikwete waliowahi kukanusha shutuma hizi nzito pamoja
na Dk. Willibrod Slaa kuwataka wafanye hivyo mara nyingi.
Laiti Mangula angejua kuwa mambo yangebadilika haraka namna ile, angekata pua
na kuunga wajihi wakati ule kabla ya kutimuliwa na kuadhirika kiasi cha
kurejeshwa chamani kama zana nyingine yoyote.
Kwa wanaofahamu jeuri ya Mangula na alivyotupwa, wameshangaa jinsi
alivyokubali kuramba matapishi yake sawa na Kikwete aliyemtupa nje baada ya
kupata uenyekiti. Maana aliwahi kusema kuwa wastaafu wasikae Dar na kufungua
NGOs, waende vijijini.
Je, nini siri ya Rais Kikwete na Mangula “kurudiana”? Je, Kikwete amegundua
kosa lake au Mangula amepunguza hasira zake? Je, hii ni ndoa ya mashaka au
mwisho wa uhasama?
Kwa wanaojua maisha ya watumishi, wanaoachia ngazi bila kuiba vya kutosha,
bila shaka watakubaliana nami kuwa Mangula amelazimishwa na ukata kukubali
kumtumikia Kikwete hasa wakati huu ambapo watu angalau waadilifu, au wenye
madhambi yaliyofichika na wenye busara ni wachache ndani ya CCM.
Kwa upande wa Kikwete, naye kama Mangula amelazimishwa na ukata wa uadilifu
kiasi cha kuramba matapishi yake. Je, ndoa hii itafana na kufanikisha kile
walichodhamiria ambacho ni kuifufua CCM ili iweze kuwa ‘fit’ kuelekea uchaguzi
2015?
Kila mti utaujua kwa matunda yake. Maneno ya Mangula wakati wa kuwashukuru
wajumbe kwa kumpitisha nadhani yanaweza kutufungulia kijidirisha cha kuchungulia
kilichomo moyoni mwake. Alikariri, “Isifike mahali CCM ikatangaza tenda ya
uongozi,” Je, hapa Mangula alikuwa akimpiga kijembe bosi wake ambaye ilidaiwa
aliingia madarakani kwa pesa, tena pesa yenyewe chafu au maswahiba wa Kikwete
wanaoutafuta urais kwa pesa chafu itokanayo na usaliti na wizi kwa taifa?
Je, Mangula alilenga kupeleka ujumbe gani? Je, Mangula alikuwa akitubia
dhambi ya kuiba pesa na kuitumia kama hongo aliyoishiriki wakati wa kuitafutia
CCM ushindi wa urais wa Kikwete? Je, alikuwa akiwakumbusha wale wanaotaka urais
kuwa kipindi hiki hatashiriki mchezo mchafu kama huu?
Je, Mangula amekubali nafasi husika kwa masharti ambayo ni siri ya wawili
kiasi cha kuwa na jeuri ya kutamka maneno yanayoonekana wazi kumgusa bosi wake
ambaye ni hasimu wake wa zamani kimsimamo? Hakika ndoa hii ya wawili inaacha
maswali mengi kuliko majibu.
Je, Mangula ambaye aliondoka kwenye ukuu kwa aibu ana jipya gani la kuleta
katika CCM? Mangula baada ya kutemwa na Kikwete alijaribu kugombea uenyekiti wa
Mkoa wa Iringa akabwagwa na Deo Sanga mwaka 2007.
Baada ya hapo alijaribu kugombea ujumbe wa NEC jina lake halikurudishwa. Kwa
wafuatiliaji wa mambo kitendo cha Mangula kujishusha hadi kugombea cheo kidogo
kama kile kilionekana kama mtego kwa CCM, ingawa wakati ule si Kikwete wala CCM
waliojali.
Je, ni kitu gani ameifanyia CCM hadi kumkumbuka? Je, ametubu dhambi zake au
waliomtema wamejikuta wamebanwa kiasi cha kukuta kuwa Mangula ndio muarobaini?
Hata hivyo Mangula ambaye ameonesha kushindwa tena kwenye nafasi ndogo anaweza
kuleta jipya gani zaidi ya kutafuta riziki? Je, atakubali kuacha msimamo wake na
kile anachoamini ili kuishi?
Wahenga walisema: mtumikie kafiri upate mradi wako. Je, haya yanajidhihirisha
kwa Mangula? Kwa wanaojua tabia ya Kikwete, wanatia shaka kama ndoa hii itadumu
hasa ikizingatiwa alivyomtema Yusuf Makamba baada ya kugeuka mzigo na kumteua
Wilson Mukama ambaye aliishia kuwa mzigo hata zaidi ya Makamba.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 21, 2012.
|
|
1 comment:
Yaani huna cha ku comment
na mwenye blog hebu tuondole huo upuzi hapo wa matusi
Post a Comment