The Chant of Savant

Wednesday 5 December 2012

Hapa hakuna cha NEKI mpya wala nini!

TUKIWA kijiweni tukitafakari jinsi mafisi na mafisadi walivyopanguana na kupangana kule Idodomya, si Dk. Mpemba kaja na mpya.
Anaingia akiwa anaimba: ‘Uangusho uangusho uangusho Karumekeenge naye yumo ati!’ Hatumuelewi kwanza. Mara Dk. Mbwamwitu anaamua kumtolea uvivu. Anasema: “Ami leo kunani au nawe umejiunga na Uangusho baada ya kuchoshwa na ndoa ya Maalim Madefu wa Kaafu?”
Mpemba kaguswa pabaya! Anakwanyua mic na kuchonga: “Kwanza mie si mwanachama wa Kaafu. Pia si wa kundi hili la kigaidi la Uangusho ambalo hakika miye naona la magamba.”
Mbwamwitu hakubaliani naye. Anamuuliza: “Sasa kama wewe siyo hao alkaida, sorry Uangusho, mbona unaimba wimbo wao hata kama unawaita makenge?”
Mpemba anajibu: “Miye sijasema eti Uangusho makenge ati. Lau wangekuwa makenge tusingewahofu hawa. Hawa alkaida ati. Nisemacho ni kwamba Karumekenge aliyepitishwa na hao mafisadi wenzake kuwa rahisi wa Zenj ameumbuliwa nao hao wenzake.”
Kabla ya Mbwamwitu kudakia, Dk. Mgosi Machungi anatia buti. “Shisi hatikieewi inaposema Kaumekenge naye yumo. Kwani huyo Kaumekenge ni nani hadi akushughuishe?”
“Yaani wewe hujui Karumekenge ni nani?”
“Yatosha jamani mshamjua kuwa ni yule Amii aliyepitishwa kuwa rahisi wetu wakati hakufaa na sasa ameamkia kwenye Uangusho,” alisema Mpemba huku akibwia gahawa yake.
Kabla ya Dk. Mpemba kuendelea, Profesa Msomi Mkatatamaa aliingilia kati. “Ami kumbe hukuwa unaujua mchezo mzima! Hawa wanasiasa uchwara walioondoka kwenye ulaji wa bure wakiwa wanautaka, wanatafuta mwanya wa kutengeneza nyufa ili waonekane wakombozi hali itakapokuwa mbaya.” Anabwia kahawa yake na kutazama huku na huku na kuendelea:
“Ingawa wanaweza kujiona wajanja kwa hujuma na upuuzi wanavyofanya, moto wanaotaka kuuwasha hawawezi kuuzima. Si wao na hao vibaraka wao wala mabwana zao. Tunapaswa kuwashughulikia mapema kabla hawajatugawa kwa tamaa zao.”
Kila mtu ameweka mkono kwenye tama akisikiliza mapwenti ya Msomi wetu kijiweni. Kabla ya kuendelea, Dk. Kidevu anamuuliza swali. “Pworofwesa, unataka kutwambia kuwa hata manyang’au mafisi na mafisadi nayo yameanza kustukiana kiasi cha kuanza kuzomeana kama walivyomfanyia Karumekenge aliyewatusi kuwa wana ubongo wa samaki?”
Dk. Mipawa halazi damu, anakwanyua mic. “Nazani kama magamba yaliyomzomea Karumekenge yana ubongo wa samaki, basi yeye anao wa kenge kama jina lake.”
Wanywa kahawa hawana mbavu kwa jinsi Dk. Mipawa anavyowapaka mafisi kwa maneno makali yenye lafudhi ya Kisukuma.
Wakati watu wakiendelea kuvunjika mbavu, Dk. Mgosi Machungi anakatua mic. “Dokta Mpemba hemu tiambie. Hivi nkwanini nyinyi huko mnapenda kutumiana?”
Kabla ya kuendelea Mpemba anajihami. “Yakhe sasa haya nmatusi. Twatumiana vipi wakati watu wajinga wajinga wataka waonekane wajua wakati hawajui kitu kama huyu juha Karumekengee.” Anavuta sigara kali yake na kumpasia kichungi Mbwamwitu na kuendelea:
“Kama magamba yatumiana nyuma ya pazia usiseme ni sote. Wao kwelii watumiana tena kwa siri na wazi wazi. Sie wananchi twapinga kutumiwa ndo maana wale watu toka vi-island walimzomea Karumekenge.”
Dk. Mgosi Machungi kanogewa, anaamua kukwanyua mic tena. “Kama huyu Kaumekenge ndiye Uangusho yawezekana ndiye aitoa bendera yetu kwa Waiani kufanyia biashaa yao ya haramu, hebu tijaribu kufikii pamoja.”
Dk. Mchunguliaji haniangalii mwenyekiti lau nimruhusu, maana tangu mada ianze inaonekana kama mwenyekiti sina kazi na kama ninayo basi mimi boya. Anyways, I have decided to let the vent. The whole schemata are supposed to look like that in such kind of circumstance.
Lo! Nimevutiwa hadi nikaonyesha usomi wangu.
Anyways, Kikameruni kinajua kung’ang’ania ubongo. Dk. Mchunguliaji aliendelea: “Kumbe Dk. Mgosi ulikuwa hujui hili! Mbona kila mtu anajua ni nani alichuuza bendera yetu kwa wanaharamu wale.”
“Mimi naona tuachane na mambo ya Karumekenge na ukenge wake wa kuangusha akijitia Uamsho. Hebu jamani tuchambue hii NEKI mpya iliyoundwa juzi na wabaya wetu,” alipendekeza Dk. Mipawa.
Dk. Machungi anadakia: “Ie NEKI kwei neki. Maana ukiangaia mijitu yenye kia uchafu kama Phil Jaff Mangu na Zaki Mengjii unashangaa na kugundua kuwa kumbe kazi ya inzi ni kucheezea kinyesi. Hivi hawa waiosababisha wizi wa HEPA wana jipya gani zaidi ya kuja kusuka wizi mwingine?”
“Du! Mgosi sikuwezi kwa kukumbuka mambo makubwa kama haya. Tena jana nilisoma kwenye gazeti la Tanzania Ever, Dk. Silaha akizidi kumkaba shati Phil Mangu,” alichomekea Dk. Mbwamwitu.
Profesa sasa kafika mwake. Anakatua mic na kuanza kutoa lecture. “Nadhani wengi hawajui kuwa haya ni maandalizi ya wizi wa njuluku nyingine kwa ajili ya uchakachuaji na uchafuzi ujao. Ingawa baada ya Mangua kukamilisha wizi wa HEPA na kusababisha ushindi, Njaa Kaya alimpiga kibuti na kumteua mropokaji Yusuf Ma-rope kwa kuogopa Mangua angemsumbua kutokana na kujua ubovu na wizi wake.”
Anachukua kashata na kuila na kuendelea huku akikohoa kuweka koo vizuri. “Hapa hakuna cha NEKI mpya wala nini, bali ni kukusanya wezi wazoefu ili wafanikishe ujambazi mwingine.
Mada ikiwa inaanza kukolea si likapita gari la Karumekenge likimuwaisha Airport. Wote tulisimama na kuanza kulisindikiza kwa wimbo ule ule ulioanzia Idodomya. Uangusho Uangusho Uangusho Uangusho Uangusho hadi wapita njia wakaanza kutujalia.
Baada ya kuona ndata nao wanaanza kujisogeza wakidhani nasi tumepagawa kama akina Shehena Pondwa, tuliamua kuvunja kikao. Uangusho Uangusho nanyi mandata Uangusho kama Karumekenge.
Nadhani kaya yetu sasa ya Uangusho maana kila mtu anaangusha mwenzake. Ngoja nami niende kuangusha.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 5, 2012.

No comments: