BAADA ya mnywa kahawa mmoja fyatu ambaye zamani alikuwa memba wa kijiwe chetu kuja na mpya kuwa wahishimiwa wabungwe warambwe bakora kama wataboa, kijiwe kimekaa kama kamati na kupendekeza adhabu nyingine kwa watakaofanya madudu.
Dk. Mgosi Machungi anaingia na gazeti la Tz Ever. Hata hasalimii. Analianzisha, “Wagoshi, kwei sasa nimeamini kuwa mapinduzi yanaanza kunukia,”
Dk Mbwa Mwitu anadakia, “Dk Mgosi, hata salamu hakuna! Inaonekana hii imekuingia sana. Maana salamu zako ni mapinduzi uliyo nayo kichwani mwako,”
Dk. Mbwa tiheshimiane, imeniingia nini hiyo. Acha kunishongeza kwa waheshimiwa uulize ninachomaanisha,” Anampa Mbwa Mwitu nakala ya gazeti la Tz Ever ili ajioneee kilichomsibu.
Mbwa Mwitu analipokea gazeti kwa haraka haraka ikichukuliwa kuwa kijiweni wanunuzi wa magazeti si wengi.
Kusoma kichwa cha habari tu anasita na kusema, “Kweli Mgosi ulikuwa na haja ya kutosalimia na kuhemkwa. Yaani huyu mama anataka eti wahishimiwa wa mjengoni warambwe bakora wakiboa! La illah ill-allah!”
Wakati akishangaa Dk Mipawa anadakia, “Unashangaa nini? Mbona pendekezo zuri tu. Kama wao walitunga sheria ya kuwapiga wengine bakora kwanini wao wasipigwe iwapo wote ni wana kaya na tuko sawa?
Mie napendekeza zaidi. Hata kama mkuu akifanya madudu kama ilivyo naye arambwe bakora. Mbona mzee Mchonga alimraba bakora waziri Fundukura wakati alipotuhumiwa kupokea mlungula? Unadhani leo angekuwa mkuu si wengi wangevimba makalio.”
Kijiwe hakina mbavu.
Wakati tukiwa tunavunjika mbavu, Dk Mpemba alinyaka mic na kulonga, “Mie nansapoti sana huyu mama. na kama angekuwa hajaolewa mie ningemuoa ili ajenshauri jinsi ya kukomboa watu wetu.”
Mpemba anaendelea, “Mie naona viboko havitoshi ati. mbona Uchina wapiga risasi bila kujali ukubwa wa cheo cha ntu? Kama siyo kutawaliwa na vibaka, wanafiki na wehu tungekuwa tunapiga risasi wanaoibia umma hasa mafisadi,”
Dk Kapende hangoji, “Leo Dk Mpemba umenikuna sina mfano,” Kabla ya kuendelea Dk Mchunguliaji anaingilia, “Dk Kapende hiyo lugha kaka. Amekukuna wapi na vipi?” Kapende anacheka na kusema, “We unaona wapi na vipi?”
Profesa Msomi Mkatatamaa ameishaanza kuhisi utani unaweza kuvuruga mada. hangojei Kapende ajibiwe. Anakatua mic, “Waheshimiwa tukubaliane. Kuna haja ya kuwa na katiba yenye meno badala ya hili gunia lenye kila matundu ya ujambazi tulilo nalo. Hivi kwa mfano wahishimiwa wanaosinzia au kuongopa mjengoni unategemea wafanywe nini?”
Hangoji ajibiwe. Anaamua kujijibu mwenyewe, “Mie naona wangechapwa bakora kabla ya kupewa adhabu nyingine kama kufukuzwa uheshimiwa na kutakiwa warejeshe nusu ya mishahara waliyolipwa. Pia kuna majambazi wa kielimu ambao wamo mjengoni kwa vyeti vya kughushi.
Ingekuwa si heshima yangu kwa haki za binadamu, hawa ningeshauri wavuliwe nguo na kurambwa bakora kabla ya kupigwa mawe na hatimaye kuchomwa moto,”
“Profesa huna haja ya kuhofia haki za binadamu. Mafisadi si binadamu bali binsheitwani Audhubillillahi minna shaitwan rajiim,” Anadaki Dk Madevu.
“Hapana. Ni binadamu. Hivyo, kwa vile kaya yetu haijaondoa adhabu ya kunyotoa roho, tunaweza kuwanyonga tena baada ya kuwavisha suti na kuwapa mlo mzuri ilmradi watokomee na kuwa somo kwa wengine,”
Akiwa anakunywa kahawa yake ili aendelee kutoa pwenti ndata kama watatu hivi walipita wakiwa na bunduki zao. Nadhani ni wale wasio na kazi bali kuzurura mitaani na likitokea tukio la ujambazi hasa wa kutumia silaha wanakimbia na silaha zao.
Mpemba anawaona na kuongea kwa sauti ya chini, “Mie naona na hawa ndata nao wapaswa kupigwa bakora na kuchomwa moto kwa wanavyoua watu siku hizi. Maana mie sasa naogopa wao kuliko hata hayo majambazi,”
Kila mtu anageuka kuangalia ndata wakipita bila hata kujali kuwa kuna watu walikuwa wakiwananga.
Mipawa anasema, “Nao siku yao ya kuonja wanachofanya ipo karibu. Hamkusikia huko Ngala ambako nasikia wawili walinyotolewa roho baada ya kumnyotoa mtu asiye na hatia roho! Taratibu tutafika tu ilmradi kila mtu amheshimu mwenzake bila kujali nyadhifa wala kipato,”
Msomi amepata upenyo anarejesha mada kwenye mstari. Anasema, “Mie vitani huwa sihangaishwi na mbwa bali aliyemfuga. Hao ni viumbe wadogo sana wasiwahangaishe. Tuhangaike na hawa walioishiwa wanaopenda kuitwa wahishimiwa kama wezi wa miwa.
Nirejee kwenye kilichoandikwa na gazeti kuhusu kuwapiga bakora wahishimiwa. Ni wazo zuri hasa ikizingatiwa kuwa litatoa somo na fundisho kwa wengine.
Hivi wapuuzi kama Badworse aliyenaswa akipokea rushwa au wale wanaotuhumiwa kuomba rushwa kwenye halmashauri za wilaya ni vibaya kuwapiga bakora tena hadharani? Hivi wale wanaojigeuza makuwadi wa makampuni ya uchukuaji kwa vile wanapewa vijidole vichache tukiwakata vichwa tutakuwa tumekosea?”
Dk Machungi hajivungi. Anakatua mic, “Poofesa mie nakuunga mkono. Sioni haja ya kuwanea huuma majizi kama akina Endeea Chenge au Eddie Owassa ambao mazambi yao yametisababishia mgao wa umeme. Mie hawa natamani kuwapiga zongo hadi wabebe mimba,”
Wanakijiwe wamamshangilia utadhani kafunga goli kweli. Mgosi Machungi kusifiwa hivyo kaamua kuendelea, “Hivi mtu kama Azao Nyaandu kwei akipewa mimba itakuwa ni kumuonea? Timesikia anavyomiika kampuni ya utaii wakati yeye ni wazii wa utaii.”
“We mgosi achia hapo,” Anaingilia Mbwa Mwitu.
Walevi hatuna mbavu kwa jinsi Mgosi alivyoamua kuwatia mimba wanaume bila kujali lolote.
Baada ya profesa Msomo Mkata tamaa kuona watu wote wameshikilia kucheka, aliamua kurejea na kula mic, “Mgosi umesema kweli ingawa hili la mimba sijui litawezekanaje. Kweli kama hii ya huyu waziri wa wanyama kuwa na kampuni ya kuchuuza wanyama si kinyaa jamani?
Nashangaa bado mkuu atakuja na kujichekeshachekesha bila kumwajibisha mshikaji wake. Hivi hawa watu huwa wanampa nini huyu bwana jamani? Nina wasi wasi wasije kuwa makuwadi wa biashara yake na jamaa zake au hata washirika. Vinginevyo upuuzi kama huu ungemuondoa mtu dakika ile ile ulipofumka,”
Kijiwe kikiwa kimekolea si gari la Nyaranyalandu likapita. Tulilitupia mimawe kama hatuna akili nzuri. Kama siyo wale polisi kuingilia, huenda jamaa angekuwa ima maiti au mjamzito wa mingumi yetu. Eti leo ni Jumatano? Kachape kazi siyo mkeo.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 19,2012.
No comments:
Post a Comment