Tuesday, 29 January 2013

Katiba Mpya - Madaraka ya Rais yapunguzwe


INGAWA Katiba Mpya haijaandikwa na Watanzania wametakiwa kutoa maoni yao, kuna mambo muhimu kuliko mengine ambayo tunapaswa kuzingatia katika kuandika Katiba Mpya.
Leo tutaongelea mamlaka ya kupita kiasi ya rais yanayoweza kumfanya awe fisadi na dikteta hata bila kutaka.
Historia ya uhuru wa Tanzania inaonesha kuwa tumekuwa na rais ambaye anaonekana yuko juu ya sheria. Tunaweza kusema kuwa ni rais mfalme kwa lugha nyepesi.
Hii ni kuanzia awamu ya kwanza hadi ya sasa. Tutajaribu kuonesha upungufu ya kuwa na rais aliyeko juu ya sheria na mwenye madaraka yasiyoweza kudhibitiwa (unchecked powers).
Chini ya utawala wa Awamu ya Kwanza wa hayati Mwalimu Julius Nyerere pamoja na uadilifu wake, kuna kipindi tulikuwa na Rais (Nyerere), Mwanasheria Mkuu (Joseph Warioba), Mkuu wa Majeshi (David Msuguri na wengine kutoka Mara), Gavana wa Benki Kuu (Charles Nyirabu) na Katibu wa rais (Joseph Nyerere ambaye ni mjomba wa Nyerere) kutoka mkoa mmoja wa Mara kwa vile rais alikuwa anatoka kule na alikuwa na mamlaka kikatiba kumteua amtakaye.
Chini ya utawala wa Awamu ya Pili tulianza kuona nguvu za mke wa rais zikiibuka bila kuwa kwenye katiba.
Hali ilianza kuwatisha baadhi ya watu hadi Nyerere akaamua kulijadili suala hilo na kutaka kiongozi yeyote asikubali kushauriwa na mkewe.
Hii ilikuwa wakati ambapo vimemo vya kutaka mikopo ya daladala au kununua viwanja kutoka kwa First Lady vilianza kuwa kitu cha kawaida serikalini hadi ikawa kashfa. Ili tusionekane tunazusha, rejea hali ilivyokuwa mbaya hadi Nyerere akaseme ikulu inanuka rushwa.
Utawala wa Awamu ya Tatu chini ya Benjamin Mkapa, madaraka ya First Lady yaliumuka zaidi kiasi cha kuwa kile Wazungu huita power to reckon with. Maana mke wa rais naye alianzisha sijui tuite kampuni au chama chake chini ya kivuli cha NGO.
Kwa mara ya kwanza ilionekana mke wa rais alianzisha NGO. Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) ilizaliwa na kujihusisha zaidi kwenye shughuli zilizotiliwa shaka kwa kuwa ilionekana kumnufaisha mke wa rais na watu wake wa karibu. Tulilalamika na hakuna aliyetusikiliza kwa vile rais anaonekana kuwa juu ya sheria.
Matokeo ya mchezo huu uliishia na kumfanya rais wa wakati ule kukabiliwa na kashfa kubwa mbili. Moja ya watu wake wa karibu kutuhumiwa kuingiza Kampuni ya Net Group Solution kuendesha Shirika la Umeme la taifa (TANESCO) na kujitwalia mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira.
Mchezo wa First Lady kutumia madaraka ya rais kujinufaisha chini ya kivuli cha NGO umeonekana kuendelea hata alipoingia Rais Jakaya Kikwete, ambaye mkewe ameanzisha mfuko wa WAMA, ambao una kila dalili za shaka kuwa mali ya mke wa rais kwa manufaa yake binafsi sawa na EOTF.
Mchezo huu umepanuka hadi kuhusisha ndugu na watoto wa rais. Rejea kuibuka kwa Ridhiwan Kikwete na Seleman Kikwete katika duru za chama.
Ukiachia udhaifu huo tulioonesha hapo juu, kuna udhaifu mwingine wa kimfumo ambapo, mosi, rais wetu halipi kodi ila anaweza kufuja kodi ya umma bila kuwajibishwa kama ambavyo utawala wa Mkapa na Kikwete unasifika kwa kutumia pesa nyingi kusafiri nje bila umuhimu wowote.
Ajabu mtu kama huyu asiyelipa kodi anawahimiza wengine walipe kodi ale, ukiachia mbali serikali yake kutoa misamaha ya ajabu ya kodi wakati nchi inaendelea kuwa maskini na kuwa ombaomba.
Pili, anamteua amtakaye hata kama hafai ambao wamekuwa wakikipendelea wazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama anavyodaiwa mlezi wa vyama vya siasa, John Tendwa, ambaye anajulikana alivyo mshirika wa rais na kada wa chama chake.
Tendwa sasa anadaiwa na kuonekana na vyama vya siasa kuwa kama muuaji wa vyama hivyo na si mlezi.
Anakwenda hatua mia mbele kwa kuwateua wakuu wote wa mikoa na wilaya, wakurugenzi wa mashirika mbali mbali, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa vyombo vya dola.
Pia, anateua wabunge wasiomwakilisha yeyote isipokuwa yeye. Hawa husaidia kukuza idadi ya forum inapotokea kukawa na upungufu katika kuunga mkono hoja za serikali. Ambao wanaonekana kuwa ni mzigo kwa taifa kwani zaidi ya kumwakilisha rais na matumbo yao hawawakilishi Watanzania.
Tatu, imefikia mahali hata rais anaandamana na watu awatakao nje ya nchi na kufanya orodha ya majina yao siri.
Nne, yuko juu ya sheria ndiyo maana anafanya hayo bila kushughulikiwa. Rais kama binadamu yeyote mwenye udhaifu lazima atatumia madaraka vibaya ukiachia mbali kulewa madaraka.
Tano, bajeti ya ofisi yake ni suala la usalama wa taifa na utashi habanwi wala kulazimika kuwajibika akivuruga ofisi ya rais na mamlaka yake.
Sita, hatakiwi na sheria kutangaza mali zake kwa vile yuko juu ya sheria. Rejea kwa Kikwete kuendelea kutotaja mali zake huku akisifika kuwalinda mafisadi kama wale wa Kiwira.
Edwarad Lowassa (Richmond) na Andrew Chenge (rada) na Rostam (Kagoda na EPA), ambayo rais mwenye alituhumiwa kuwa aliasisi na kutekeleza mkakati huo ili kupata pesa ya kutafutia urais (asikanushe wala kuwa tayari kutoa maelezo) kutaja baadhi tu.
Madudu yanayotendwa na rais kutokana na kuwa na madaraka yasiyo na mpaka ni mengi kiasi kwamba nafasi haiwezi kutosha kuyaeleza japo yapo mengi. Jambo la muhimu ni kwa Watanzania kuhakikisha madaraka ya rais yanapunguzwa na kuwa na uwajibikaji wa kikatiba.
Wengine wameishafanyia hili majaribio na kufanikiwa. Mifano ni nchi jirani ya Kenya na Afrika Kusini ambapo madaraka ya rais yamepunguzwa na kuwajibishwa kikatiba. Bila kupunguza madaraka ya rais tutatendelea kuwa shamba la bibi. Tutaendelea kuwa umma wa watu maskini huku rais akitumia madaraka yake kujineemesha na marafiki na jamaa zake.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 30, 2013. 

No comments: