Najua habari
hii haitawafurahisha walevi walio wengi hasa wanaopondwa na matatizo ya ukapa wa
kutengenezwa na sisi wenye maulaji yetu. Wapo watakaoniona kama najidai na
kuwakoga. Hawa nawashauri wakajinyonge maana kutesa ni kwa zamu. Wapo
watakaoniona kama limbukeni na mtu wa kushangaashangaa. Pia, wapo watakaoniona
mtu wa watu na wa maana hasa wale wanaoandamana nami kwenye matanuzi yangu. Wapo
watakaoniita Vasco da Gama yule habithi wa kireno aliyekuja pwani yetu akavamia
miji yetu na kupora na kuishia zake Ureno. Yote poa tu mradi kelele za mpangaji
hazimnyimi usingizi mwenye nyumba kama alivyowahi kusema jamaa yangu Njaa Ka...
we koma! Wapo watakaoniona kiherehere kama vitoto vya shule vinavyopachikwa
mimba kama alivyowahi kusema mkulu.
Kwa vile mimi
ni kichwa maji nisiyejali wala kusikia, sasa nawapa utamu wa jiji la Paris.
Wenyewe wafransii huliita Pari au Parie. Sisi tuliosomea hapa huwa
tunasema kwa kifransii, “Paris est la mere de tous capitales mondiale.” Yaani
Paris ni mama wa majiji yote duniani.
Hakuna kitu
kilinichekesha kama bi mkubwa wangu alipotaka kubonga kifransii kwa lafudhi ya
ki-matching guys. Badala ya kusema Bonjour Monsieur Presidaa alisema, “Banjua
plizidaa,” Ilibidi mwenyeji wetu acheke kwa chati kama vile alifurahi wakati
alikuwa akishangaa inakuwaje bi mkubwa hakupiga shule angalau ya kumwezesha
kuzinyaka concepts nyepesi haraka kama salamu. Watasha huwa hawana dogo. Si
alinipa laivu kuwa kwa vile amegundua kuwa bi mkubwa wangu hajapiga shule hivyo
angempa nafasi kwenye shule moja lau apigwe msasa. Nilivimba kwa hasira ingawa
nilichekacheka kama kawa. Huyu angejua bi mkubwa wangu asivyopenda kusoma
asingeniudhi kwa kutoa wazo kama hilo. Asome kupata nini iwapi NGO yake
inamuingizia mshiko wa kutosha kiasi cha kuajili wasomi wanaomtumikia kama mke
wa mfalme? Wenzetu bado wanadhani elimu ni ufunguo wa maisha. Hii ni kwao. Kwetu
pesa na mamlaka ni ufunguo wa maisha. Simpo! Nilimjibu nini Monsieur Normal? Top
secret as usual.
Twende kwenye
mada ya mose wa lero. Kama kawa, niliondoka kwenye kaya nikiwa nimeandama na bi
mkubwa ili naye akashangae shangae na kujipiga viwalo vipya. Yeye pia
aliandamana na mashoga zake ili nao wafanye first shopping bab kubwa. Kitu
kimoja kilimkera bi mkubwa hadi akanilalamikia ingawa niliogopa kumwambia rais
kwa vile huu si ustaarabu wao. Kilichomkera ni ile hali ya kwenda kufanya
shopping kwenye mitaa ya Rue St. Honore, Loire Valley,Mont St. Michel , Faubourg
du Roule, Marais Republique na mingine mingi yenye majina magumu
bila barabara kufungwa kama Uswazi. Bi mkubwa na mashoga
zake waliwaacha hoi wafaransee kwa kulipa cash tena kwa dorali na si madafu.
Hakuna mtaa niliupenda kama ule wa Marais Republique. Nina mpango wa kununua
bungalow pale ili nikistaafu nikumbuke urais wangu wa kijiwe. Hayo
tuyaache.
Pia wapo jamaa
zangu ambao sikutaka watajwe kwa vile walevi wanaweza kuanza kuhoji uhalali wa
kuandamana nao. Najua hapa wanoko wataanza kusema niliandamana na washikaji
zangu, vitegemezi na nyumba ndogo. So what? Kutesa kwa zamu na maulaji siku hizi
ni mali ya familia. Au siyo? Hivyo, wale wanoko waliongojea kusikia majina ya
nilioandamana nao kwenye utalii wangu jijini Paris walie na kusaga meno. Mie
siyo kama akina Mchonga waliozoea kutaja orodha ya watu waliokuwa wakiandamana
nao. Hivyo, niliandamana na walaji wangapi na akina nani ni top secret.
Tusameheane. You know what? Ukila na kipofu usinshike nkono.
Wengi wanauliza
kwanini nilipenda kutembelea jiji la Paris. Kwanza Paris ni karibu na Uswizi
hivyo akina Mbwa Mwitu na Mgosi Machungi wenye vijisenti vyao Uswizi waliweza
kuchukua High speed train na kuchungulia akaunti zao haraka haraka.
Wengine walipata fursa ya kufungua akaunti mpya kwa vile tulishaonyesha wazi
kuwa hatutakubali kusikia wambea wanaosema eti tuwakamate walioweka vijisenti
Uswizi wakati ni maendeleo kwa kaya.
Sababu nyingine
ya mashiko iliyofanya nitembelee Fransee ni ukweli kuwa nilisoma na bwana nkubwa
Francois Hollande kwenye chuo kikuu cha L’ Institut d'études politiques de Paris
(Paris Institute of Political Studies), wakati ule nikisomea mambo ya siasa
baada ya kutoka zangu Kivukoni. Pia yeye ni rika langu ingawa yeye ni dogo
kwangu kwa miaka minne. Kitu kingine kilichofanya tuwe washikaji na huyu jamaa ni
ile hali ya kupenda totoz wakati ule tukisoma. Nani angeamini kuwa bado mshirika
wangu Hollande anaishi na mchumba na si mke? Yeye ni mtu wa totoz. Huwa hakawii
kupenda na kuacha. Haya ndiyo mambo ya kisasa. Sitaki niseme mengi ingawa hayo
machache yanatosha kuonyesha ushikaji wetu ambao haukuanzia barabarani. Hivyo,
tuna mengi tunayofanana.
Jiji la Parii
usipime! Siyo kama hii mikweche ya majiji uchafu mtupu. Barabara zake ni mikeka
mitupu. Hakuna misongamano wala vurugu kama Uswazi. Kwa nilivyopenda jiji hili
la Paris kuna siku nitahamia kule baada ya kugundua kuwa sina jinsi ya kubadili
mikangafu yetu ya miji. Nadhani ningekuwa mkulu ningefunga mtu aitwaye meya. Ila
kwa vile wote wana uvivu wa kufikiri nani amfunge nani? Heri kuwafunga wanaodai
gesi ibaki umachingani.Ili sisi tule nini na tupate ten percent wapi? Senzi
kabisa!
Huwa nashanga
watu wanaopenda kulalamika kuwa deni la kaya ya kijiwe linatuna ila uchao. Yaani
kuongezeka kwa tutrioni kumi na ushei watu wanapiga kelele utadhani jambo la
ajabu. Hivi kazi ya ukuu ni nini kama siyo kutumia kama huha akili nzuri? Nani
kawaambia kuwa mali ya umma inauma? Kwanini lisitune iwapo matumizi na matanuzi
ndiyo fasheni kwetu sisi wenye maulaji? Hivi mnadhani kwenda nje namna hii
tunatumia mawe? Tunatumia pesa yenu jamani na mlitupa ulaji ili tule migongoni
mwenu. Ila nawashauri msikonde kwani mwaka 2015 sitagombea ukuu wa kijiwe wala
kaya. Hivyo, nakula vya mwisho mwisho kwa usongo wa hali ya juu
nikijua kuwa ulaji ukishanitoka maulaji kama haya nitayasikia kama siyo kuyasoma
magazetini.
Lo! K umbe niko
kwa Mfugambwa siyo Pariii! Kumbe naota! Ukisoma stori hii usiipe uzito maana ni
ndoto! Acha niamke!
Chanzo: Tanzania Daima Januari 23, 2013.
No comments:
Post a Comment