Hivi karibuni
rais Jakaya Kikwete alikaririwa akisema kuwa uvumilivu sasa kwisha.
Alisema, “Serikali
haitavumilia vurugu wala ukabila kwa namna yoyote ile…. Mwaka 2012 vurugu zenye
sura ya kidini zilianza kujitokeza ila sasa nasema kwamba hatutazivumilia kwa
namna yeyote ile, inatosha,” Je Kikwete amekumbuka blanketi asubuhi? Je uzoefu
wa kufanya mambo wa Kikwete unasemaje? Je Kikwete anasogeza muda ili amalize
ngwe yake na kuliacha tatizo pale pale kama ambavyo amefanya kwa matatizo
mengine kuanzia ufisadi, ujambazi, kuporomoka uchumi, muungano, udini, ukabila,
ukanda, mitandao kwenye chama chake na mengine mengi?
Ni
kweli kuwa mwaka jana taifa letu liligeuka gumzo kimataifa baada ya chomaji
makanisa uliotokea baada ya watoto kufanya utoto kutokana na kufundishwa imani
potofu na za kishirikina.
Je baada ya
haya kutokea serikali ilifanya nini cha mno iwapo vyanzo vya kadhia hii yaani
mihadhara inayoendeshwa na watu wasio na taaluma si ya kidunia wala ya kidini
imepigwa marufuku zaidi ya kushamiri?
Leo tunajua
fika kuwa Kikwete hajasukumwa na dhamira ya kutatua haya matatizo ya udini na
ukanda bali kutaka kuingiza kipato kitokanacho na kuuza gesi ya Msimbati. Hii ni
baada ya watu wa Mtwara kuja na hoja kuwa lazima gesi iwanufaishe wao kwanza na
miundo mbinu yote lazima ijengwe Mtwara. je watu wa Mtwara
wanaohofia nini zaidi ya ufisadi na upendeleo? Je Kikwete katika maelezo yake
ametoa majibu ya tatizo hili yanayoingia akilini? Nadhani watu wa Mtwara wanajua
ujambazi wa Richmond, Dowans na mwingine unaohusisha nishati. Pia wanajua
udhaifu wa serikali ambayo kimsingi, kuna dhana imejengeka kuwa imo mikononi mwa
mafisadi ambao Kikwete aliwahi kukiri kuwa na orodha yao na asiwaghulikie kwa
sababu ajuazo.
Hebu tuangalie
nukuu nyingine ya Kikwete, “Unawezaje kuwa
na nchi moja na taifa moja wakati kila mmoja anadai rasilimali kutoka kwenye
eneo moja ibakie na kunufaisha watu wa eneo hilo tu. Huwezi kuwa na nchi moja na
yenye umoja wakati kuna nchi ya gesi asilia kule Mtwara, kuna nchi ya kahawa
kule Kilimanjaro, kuna nchi ya chai na ndizi kule Bukoba,”
Kama
inawezekana kuwa na watanzania walio juu ya sheria na wale ambao wako chini ya
sheria lolote lawezekana. Watanzania si wajinga kiasi hiki. Kikwete anapaswa
aambiwe ukweli kuwa hawezi kueleweka kwa vile amekuwa mfadhili na muhimili
mkubwa wa haya madudu. Kama watu wanaona jinsi pesa inavyoibiwa na watu walio
karibu na rais na rais hachukui hatua unadhani watamwamini? Hivi nani asiyejua
kuwa Richmond iliyoingizwa na swahiba mkuu wa Kikwete, Edward Lowassa ililiweka
taifa msambweni kiuchumi? Je Kikwete amefanya nini kuonyesha uongozi na
uwajibikaji? Nani hajui sakata la rais mstaafu Benjamin Mkapa mkewe
watoto wake na wakwe zake kujitwalia migodi ya makaa ya Kiwira huku Kikwete
akiulizwa atachukua hatua gani anajibu” Mwacheni mzee Mkapa apumzike. Wananchi
wa Mtwara hawako tayari kuona gesi yao inabinafsishwa ima kwa Kikwete au
marafiki zake? Kumbuka ni kusini huko huko walioanzisha vita ya maji maji wakati
wengine walikuwa wakigwaya. Wanajua wanachotaka na jinsi ya kukipata. Hivyo,
dawa si kuwatisha wala kuwaongopea. Wanajua kuwa sekta ya nishati ndiyo
inayoongoza kwa ufisadi na kutoa kipato kwa mafisadi. Wanajua kuwa Tanesco
haikubinafishwa kwa vile ilikuwa haiwezi kujiendesha bali uroho na upogo wa
watawala. Wanajua kuwa mgao na ulanguzi wa umeme vimesababishwa na ufisadi
unaolindwa na kutendwa na watawala na mawakala wao. Wanajua kila kitu.
Wamajua kuwa
Kikwete anawadanganya na hana nia ya kufanya lolote kwa faida yao. Wanajua kuwa
hata mwaka 2006 alipowaambia kuwa ana orodha ya mafisadi, majambazi
na wauza unga na asiwashughulikie ilikuwa ni danganya toto. Hapa hakuna cha
kugawa nchi wala nini? Kama ufisadi umeigawa nchi kwanini gesi ya Msimbati iwe
tatizo?
Si uzushi wala
upendeleo kusema kuwa serikali yetu imefuga hisia za udini, ukabila, ufisadi,
ukanda na hata mitandao nchini mwetu. Maana kumekuwa na watu wanaoota ndoto za
mchana kuwa kuna siku Tanzania itatawaliwa kaiislam au kikiristo au kikanda au
kikabila. Ila wanasahau kuwa uislam haujawahi kutawala popote ukiachia mbali
baadhi ya watawala kuutumia kufikia malengo yao. Mfalme Constantine aliutumia
Ukristo kutawala Rumi, Ezana (Kush) huku watawala wa Ottoman, Mughal na Safavid
nao wakiutumia uislam kujiimarisha kwenye madaraka. Kuna watu
wanaoota kuwa juu ya sheria wakifaidi keki ya taifa huku wengine wakifa njaa.
Kinachofanya
serikali ilaumiwe ni ile hali ya kuruhusu kila mtu kujifanyia atakavyo bila
kufuata sheria. kwa mfano, madhehebu ya dini yalipaswa kusajili kwa sharti kuwa
yakienda kinyume na matarajio ya serikali yanafutiliwa mbali. Leo tuna maaskofu
wengi feki wanaotumia dini kuwaibia maskini na kuwadanganya. Wanazuka k ila
uchao. Tuna mashehe wengi wanaoibuka na kutangaza vitu vya ajabu kama hawa
wanaotaka kuangusha Bakwata au kutaka kueneza uislam wa kihafidhina ambao hata
mtume hakuuacha.
Hata hivyo,
inapaswa watu wa namna hii kuambiwa kuwa tulipopigania uhuru tulipigania uhuru
kama watanzania na si waislam wala wakristo, wamakonde, wana CCM na upuuzi
mwingine. Mtu yeyeto aweza kuingia dini yoyote na kutoka lakini hawezi kufanya
hivyo kwa uraia wake kirahisi hivyo. Kwenye kujiunga na dini hakuna maombi wala
masharti sawa na uraia. Mbona wakati tukiingizwa kwenye mfumo wa kikoloni au
kupelekwa utumwani hizi dini zinazotaka mamlaka leo hazikutusaidia zaidi ya kuwa
wakala wa mateso yetu? Kuna haja ya kusoma historia kuepuka aibu ya kiakili kama
hii. Hivyo, hawa al muthnaka wanaoota mchana kudhani Tanzania inaweza kutawaliwa
kidini, washikishwe adabu mara moja.
Tumalizie na
kadhia ya gesi asili Mtwara. Serikali isiposhughulikia ufisadi na ubaguzi wa
kimaeneo yatatokea mengi kama hili la Mtwara. Jibu si kuwatisha watu wa Mtwara
bali kuwatendea haki sawa na watanzania wengine.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 23, 2013.
No comments:
Post a Comment