Hakuna ubishi
kuwa mauaji ya padri Evarist Mushi yalijulikana kabla ya kutekelezwa kama
alivyosema kardinali Polycarp Pengo. Pengo alikaririwa hivi karibuni akisema,
“Tumekuwa tukipokea vipeperushi toka kwa watu wanaojiita Uamsho, wakisema
mapambano yanaendelea,”
Pengo alitoa
hata ushahidi kwa kuonyesha kipeperushi walichotumiwa. Kwa maneno mengine ni
kwamba serikali ilikuwa ikijua kilichokuwa kinaendelea ingawa haikutaka kuchukua
hatua? Uko wapi mkono mrefu wa sheria? Uko wapi umakini wa vyombo vya usalama?
Je nchi yetu ni salama? Sababu? Nadhani ni wakati muafaka kuitaka serikali ijibu
madai ya Pengo. Si serikali tu. Hata Uamsho wanapaswa kujibu madai haya bila
kuchelewa. Kwani kutofanya hivyo kutaonyesha moja kwa moja walivyo nyuma ya
mauaji ya kinyama na kishenzi ya padri Mushi.
Ukiachia mbali
na kitisho cha Uamsho, kuna mtu anayeweza kukamatwa na kueleza vizuri maagizo
yake juu ya kuua viongozi wa kidini hasa wa kikatoliki. Katika pita pita zangu
kwenye mtandao wa Jamii Forum, niliwahi kukutana na link hii
http://www.jamiiforums.com/jukwaa-la-siasa/403448-majibu-kwa-hoja-ya-uchochezi-ya-ustaadh-ilunga-serikali-inamuogopa.html
Na link
nyingine ni http://www.youtube.com/watch?v=NL9AkL0goTU
Sina wasi wasi.
Vyombo vya usalama vinajua mambo haya. Haiwezekani mtu akurupuke na kuweka
maagizo haya kwenye mitandao bila wao kuwa na habari. Kwa yeyote aliyebahatika
kusikiliza mahubiri ya huyu anayejiita ustaadh Hassan Ilunga, atakubaliana nasi
kuwa mtu huyu ni hatari kwa usalama wa taifa.
Kwanza, mtu
huyu anaonekana kama aliyekata tamaa kiasi cha kutaka umaarufu kwa kuchochea
umwagaji damu chini ya chuki za kidini baina ya waislam na wakristo. Ingawa
wengi wanaweza kumpuuza na kumuona kama hamnazao, tukubaliane kuwa kuna hamnazo
wenzake wanaoweza kuona mahubiri na maagizo yake kuwa ya kidini wakati siyo.
Pili, mhusika
anaonekana kutokuwa na elimu ya kutosha kiasi cha kuhatarisha usalama wake na wa
taifa kwa kutaka sifa zisizokuwa na msaada si kwake tu bali hata wale
wanaomsikiliza na kuyazingatia maagizo yake.
Tatu, huyu
Ilunga kama ni mzima kiakili, alipaswa kubanwa aeleze lengo la maagizo na
mahubiri yake. Kwa mfano, katika moja ya mahubiri yake anasema kuwa akiuawa
shehe basi auawe na padri. Ni bahati nzuri kuwa hakuna shehe aliyekwisha kuuawa
Tanzania ukiachia mbali yule shehe anayeonekana kuabudiwa na Ilunga aitwaye
Abdul Rogo aliyeuawa huko Kenya mwaka jana.
Je mauaji ya
Mushi ni kulipiza kisasi cha mauaji ya Rogo? Maana, kwa mantiki ya hoja za
Ilunga ni kwamba waislamu wote ni ndugu na atakapouawa mmoja mahali popote basi
ni halali kuua mkristo sehemu yoyote duniani. Je huyu ana tofauti na makundi ya
kigaidi kama Al Qaida au Al-Shabaab ambayo Rogo alikuwa akiitetea kwa udi na
uvumba huku akimsifia Osama bin Laden kwa kumuita shehe?
Je mauaji ya
Zanzibar ni mwendelezo wa kampeni za Al Qaida katika Afrika Mashariki? Maana
ukisiliza mahubiri ya Rogo ukayaunganisha na ya Ilunga unapata jibu moja kuwa
Al-Qaida imeishafungua cell Tanzania na Kenya.
Je vyombo vyetu
vya usalama hata vya Marekani havijui njama hii ambayo imevishwa udini?
Nne, ni ajabu
kuwa ustaadh Ilunga haelezi chanzo cha chuki baina ya waislam na wakristo. Wala
hatoi suluhu ya chuki hii ya kupandikizwa na kuundwa na wachumia tumbo wanaotaka
kuishi kwa kutumia mgongo wa dini hasa uislam.
Tano, kwanini
serikali haikuchukui tahadhali hasa pale padri mwingine Ambrose Mkenda
alipojeruhiwa kwa risasi hapo Desemba 25, 2011? Je ni sababu zipi zilizoifanya
serikali kuendelea kutochukua hatua kama vile kuwakamata kuwahoji hata
kuwafungulia mashitaka watu wanaoeneza chuki za kidini kama Ilunga?
Sita,
yalipochomwa makanisa huko Zanzibar jambo ambalo limerudiwa siku tatu baada ya
kuuawa kwa padri Mushi, kwanini serikali inaendelea kuzungusha bila kuchukua
hatua mujarabu?
Kama msomaji
atajipa muda wa kusikiliza mahubiri ya Ilunga, atakubaliana nami kuwa, kama
vyombo vya dola vingekuwa na nia ya kutafuta waliotekeleza mauaji ya Padri
Mushi, basi ina pa kuanzia ambako si pengine bali kumuweka nguvuni Ilunga ili
awataje wenzake na kwanini wanafanya hivi.
Tunaweza
kuendelea kujidanganya kuwa mauaji ya Zanzibar yanasukumwa na udini bila kujua
kuwa kumbe yanaweza kubeba hata msukumo wa kisiasa hasa ikizingatiwa kuwa kuna
wenzetu wengi upande wa pili wasioridhika na Muungano kiasi cha kutaka uvunjike
kwa gharama na namna yoyote ili wapate madaraka ambayo wameyakosa kutokana na
Zanzibar kuwa kwenye Muungano.
Tusidanganywe
na vurugu za kidini tukasahau kuwa maadui wa taifa hasa mshikamano wanaweza
kutumia upenyo na sababu yoyote kutudhoofisha ili wafanikiwe. Hata haya mauaji
ya Buseresere ni ushahidi kuwa vyombo vya dola havifanyi kazi zake vilivyo.
Maana hii si mara ya kwanza kwa chokochoko zenye harufu ya udini kutokea
Tanzania. Nani mara hii kasahau kadhia ya uvunjaji mabucha ya nguruwe uliotokea
chini ya utawala wa Ali Hassan Mwinyi baada ya baadhi ya waislam kudhani kuwa
kwa vile rais alikuwa muislam basi wangepitisha ajenda zao za siri? Ni bahati
nzuri kuwa wakati ule baba wa taifa Mwalimu Nyerere alikuwa hai na alimtaka
Mwinyi wazi wazi kutoa msimamo wake ambao ulikuwa ni kuanzisha falsafa ya RUKSA.
Leo Nyerere
hayupo. Watanzania tupo na urathi wake upo. Historia siku zote ni mwalimu mzuri.
Kwa vile tatizo hili si mara yake ya kwanza kujitokeza, tungeshauri serikali na
viongozi wake waache woga na uzembe. Kazi ya serikali yoyote ni kulinda uhai na
mali za wananchi wake. Anapouawa mmoja kwa uzembe wa serikali, ingekuwa ni
kwenye nchi za wenzetu, serikali ingetimuliwa madarakani. Kwa vile Tanzania
hatujakomaa kwa kiwango hiki, kuna haja ya kuikumbusha serikali kuwa kulinda
uhai na uhuru wa raia zake ni wajibu namba moja. Hivyo, tunatoa taarifa kama
hizi kuisaidia serikali kutimiza wajibu wake wa kulinda uhai, uhuru na mali za
raia.
Kwa kuanzia
tumetoa taarifa kuhusiana na Ilunga ambaye akishughulikiwa vilivyo licha ya
kuacha kueneza sumu yake, anaweza kutusaidia kuwajua wenzake. Pia tunaweza kujua
lengo lao la kufanya wanayofanya.
Kwa ukumbusho
ni kwamba uislam hauruhusu matumizi ya vurugu na nguvu kuueneza. Ndiyo maana
mtume Muhammad (SAW) alisifika kwa uvumilivu wake. Hawa wanaohubiri vurugu
wasipewe nafasi. Hata waislam wa kweli wanapaswa kuwalaani na kuwafichua wao na
hila zao. Kwa ufupi ni kwamba mahubiri ya Ilunga yanaelezea maandalizi ya kifo
cha padri Mushi. Je watafuata wangapi? Je serikali inataka wafe wangapi ndipo
ichukue hatua? Je serikali ina lipi la kutueleza ni kwanini isiwakamate akina
Ilunga? Je inangoja wahubiri mapinduzi ya serikali ndipo istuke?
Tukubaliane. Na
wakristo ni watu. Je wakiamua kulipiza kisasi au akatokea Ilunga wa kikristo
serikali itamlaumu nani? na katika vita ya namna hii inapoanza haina macho.
Watakaoumia ni pande zote hasa maskini, wanawake, wazee na watoto. Tuchukue
hatua haraka. na hakuna haja ya kuogopa machafuko wakikamatwa wachochezi hawa
kama wanavyoota. Waulize akina Ponda walipokamatwa si wamejikuta peke yao huku
walichotegemea kisitokee.
Chanzo: Dira Februari 24, 2013.
3 comments:
Kumbuka "makafiri" ndio wanaotengeneza bunduki! Osama alitamba mpaka walipomuondolea uvivu.
Ndugu Mhango mbona unaniacha ninaning'inia hapo juu peke yangu? Wallahi watu wanaweza kunifikiria kuwa nimeanza kutafuna mirungi:-)
Sijakuacha ukining'inia. Kuna kipindi watu wanatoa comments zenye kuharisha na kuchafua hewa hivyo hulazimika kuzifyeka bila kujali watasemaje. Pole sana ndugu yangu. Kuna kipindi natamani nitoe mawazo yangu lakini huchelea kuona kama najipigia debe.
Kila la heri ndugu yangu.
Post a Comment