The Chant of Savant

Thursday 27 June 2013

Tamaa, upofu, uroho na roho mbaya vitaliangamiza taifa

MATUKIO  ya kushambuliwa kwa mkutano wa CHADEMA kule Soweto Arusha na kupigwa na kuumizwa vibaya kwa wananchi wakiwamo viongozi wa chama hicho hayawezi kupita bila kulaaniwa kwa sauti kali. 
Tanzania ilisifika kuwa kisiwa cha amani. Kwa sasa bila shaka inaanza kusifika kama kisiwa cha vurugu, ubabaishaji, ufisadi, kujuana, kulindana, kukomoana  na hata kudhulumiana.  Hivi ni dhuluma kiasi gani kwa kikundi fulani chenye kuamini kuwa madaraka ni staili yake kuwaumiza na kuwahujumu wananchi wasio na hatia? 
Ni upuuzi na ukosefu wa akili kiasi gani kwa kikundi kidogo cha watu kujiona kama ndicho chenye kujua na kumiliki kila kitu hata ikiwamo akili?
 Je kwanini sisi kama taifa hatutaki kujifunza toka tawala ovu na zandiki zilizofanya haya lakini bado zikaangushwa kwa aibu na kejeli? Walikuwapo akina Muamar Gaddafi (Libya), Hosni Mubarak (Misri) na Saddam Hussein (Iraki). 
Waliogopewa sana na kuamini kuwa wao na waramba viatu wao waliumbika kuwatawala na kuwanyonya wengine wasijue arobaini yao ilikuwa imewadia. Kwanini hatupendi kusoma alama za nyakati kuwa wakati tulio nao si ule wa mwaka 47 ambapo kikundi kidogo cha watu kingeweza kuteka taifa na kulitenda litakavyo? Ni vizuri kutambua kuwa vijana wa sasa si wa kuburuzwa kutishwa wala kuchezewa mahepe.
Ni ajabu kuwa tumegeuka taifa la wakandamizaji na wababaishaji kirahisi hivi. Nani hajui kuwa kwa sasa tumo msambweni tukielekea kuzimu ambapo ulaji umechukua nafasi ya huduma? 
Leo tunaambiwa kwa mfano deni la taifa linazidi kuumka huku wahusika wakitumia kwa hisrafu na kuiba kama vile hakuna kesho. 
Nani hajui, kwa mfano, kuwa hoja ya  kurejesha fedha zilizofichwa Uswizi imeuawa kwa vile wahusika ni wakubwa au marafiki zao. 
Je ni kosa kuyashupalia haya? Je ni kosa kudai ukombozi? Je kupiga mabomu mikutano au kukata watu mapanga kwa vile wanapinga dhuluma ni jibu? 
Hata wenzetu wanaolia na kukumbuka maafa kama Rwanda walianzia huku. Hakika hawa walipaswa kuwa somo kwetu.
Inashangaza kuona kuwa Tanzania imegeuka nchi ya kulipuliwa na mabomu ya kigaidi na hakuna anayekamatwa kwa vile wahusika wana watetezi wao wenye mamlaka. Tunasema hivi si kwa chuki wala uchochezi bali kujibu kilio kilichotolewa na wahanga kule Arusha kuwa walimuona aliyerusha bomu na kutaka kumkamata lakini polisi wakamkingia kifua na kumtorosha. 
Je kama polisi na huyu gaidi lao si moja walimtorosha ili iweje kama siyo kuficha ushahidi? 
Laiti wangemtorosha kunusuru uhai wake ili ahojiwe na kuwataja wenzake ingeingia akilini. Ajabu badala ya kushughulikia kuwasaka waliolipua bomu, polisi inawashughulikia CHADEMA. 
Hali ni mbaya na yenye kutia kinyaa hadi kufikia baadhi ya walevi wa madaraka kusema eti waliolipua bomu ni CHADEMA ili kupata huruma ya wananchi. Hoja dhaifu  na ya aina yake kwa uhovyo. 
Yaani CHADEMA wawaue viongozi wao ili iweje na hiyo ‘huruma’ iwasaidieje kama siyo utaahira wa aina yake? Waingereza wana msemo : Go tell it to the birds. 
Tunadhani badala ya kuingiza siasa kwenye mambo nyeti na mazito kama mashambulizi haya ya kigaidi, serikali iwajibishwe kutuletea wale waliotenda uovu huu. Inashangaza kuona Watanzania wanageuka mateka kwenye nchi yao huku wakiuawa na kuteswa kutokana na kukataa kwako kulala kitanda kimoja na uovu. 
Wako wapi waliomteka na kumtesa Dk Steven Ulimboka na Absalom Kibanda? 
Wako wapi waliomuua Daud Mwangosi? Kwani hawajulikani?
 Je nani anahangaika kuwakamata iwapo walitumwa kutekeleza amri za wakubwa zao walioishiwa? 
Je hili ni jibu na hali itaendelea hivi hadi lini? 
Tumegeuka taifa la kulalamika lalamika. Ni jukumu la wananchi kujiletea ukombozi na kuhakikisha hatima zao zimo mikononi mwao. Tuwawajibishe watawala wetu waache kutuchezea.
Hakuna kitu kilitushangaza kama matamshi ya kizembe  kama yale yaliyotolewa na Waziri wa Nchi  Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) aliyekaririwa hivi karibuni akirusha lawama kwa wahanga akidai kuwa kumekuwapo na tabia ya wananchi kuchukia jeshi la polisi. Lukuvi anayetuhumiwa kughushi vyeti na sifa za kitaaluma ameonyesha ukweli kwa mada hii. 
Hivi Lukuvi hajui kuwa wananchi wanachukia jeshi la polisi kutokana na kushindwa kuwahudumia?
Ameshindwa kutambua kuwa wananchi wanaona kila uchao  mauaji na manyanyaso yanayotekelezwa na polisi huku wakilipwa kwa kodi za hao hao wanaowaua kama Swala mbugani? 
Imefikia mahali hata wanyama pori wana amani kuliko Watanzania. Je Lukuvi alitaka wananchi wawapende polisi kwa kuendelea kuwaua na kuwadhulumu? 
Je huku ni kufilisika kimawazo kiasi gani? Wengi walidhani kuwa wasemaji ambao ni makada wa chama tawala angalau wangekuwa wastaarabu wakatoa hata salamu za rambirambi badala ya kutonesha donda. 
Kwanini hawajifunzi toka nchi ambapo vyama tawala vilipigwa teke na kutokomea kwenye kaburi la sahau?
Tuhitimishe kwa kulaani kitendo cha wanasiasa uchwara kutetea ugaidi kwa vile unawanufaisha wao baada ya kuishiwa kisiasa. 
Hata hivyo wafahamu kuwa Watanzania si mataahira wala mawe yasiyobadilika. Kuna siku yaja watalia na kusaga meno. 
Kama taifa na jamii tusipoangalia tamaa, upofu, uroho na roho mbaya vitaliangamiza taifa. Tafakarini.
Chanzo Dira Juni27, 2013.

5 comments:

Jaribu said...

Kama ulivyozungumzia hapo juu, shida ni kwamba huwezi kuwalaumu viongozi wa CCM kuwa ni genius material kwa sababu hata shahada zao ni kufeki au kugawiwa. Inabidi nikubaliane na mmoja wao aliyezungumzia kasoro za kufukua hoja kutoka kwenye makalio. In their feeble minds, wenyewe wanajiona wamecheza kama Pele, lakini sisi tunawadeku tu.

Mtwangio said...

Mhango wache niongelee kuhusu saikolojia ya Mtanganyika(Matanznia)alivyolelewa kabla na baada ya uhuru.Tulipokuwa chini ya wajerumani, wajerumani walitutawala kwa utaratibu wa mabavu kwa kututia hofu na woga kwa utamaduni wa ukali,makelele na ukatili kiasi ambacho wananchi wa Tanganyika chini ya utawala wa ujerumani walikua kama kundi la kondoo ambao wanalindwa na mbwa mahiri wa kulinda kondoo hao.Kwa hiyo Mjerumani alikuwa ni chanzo cha kumjengea hofu na woga Mtanganyika kiasi alibaki kama kondoo tu kwa kusubiri hatima aidha kwa kunyolewa sufi,kuuzwa au kuchinjwa kwa masilahi ya Mjerumani.Lakini hata hivyo watanganyika walihisi jeuri,uenevu,ukandamizaji na udhalilishaji wa Mjerumani na matokeo yake tulipata waliojitoa muhanga kwa ajili ya kupambana na Mjerumani kwa hiyo tuliwapata mashujaa kama akina kinjikitile Ngwale akina Mkwawa kuweza kujieleza kwamba hatutaki kutawaliwa.lakini mbegu hizo za mashujaa hao hazikuweza kupandikiza ushujaa kwa watanganyika na hatimae Mjerumani aliendelea kuwatawala watanganyika mpaka pale masilahi yao yalipogongana na mataifa ya wakoloni wengine wa kizungu na tukajikuta watanganyika tupo chini ya himaya ya Muingereza ambaye alitumia utaratibu wa fimbo na karoti ambao ulifanikiwa kumfanya abaki kama mlinzi wetu na katika muda wote huo watanganyika tayari walishaathirika na utawala wa kijerumani kwa kuishi katika hofu na woga.Kutona na hali hiyo tulijijengea utamaduni wa kwamba mtawala au serikali si ya kuifanyia mchezo kwa vyovyte vile iwavyo aidha kwa kuipinga au kuikosoa utakiona kilichomtoa kanga manyoa,na kwa mtanganyika kila panapokuwa na madaraka au alama ya madaraka tayari ameshajijenga kutojiamini na kuwa na hofu na woga ambao mtawala anauona kirahisi ndani ya macho na moyo wa mtanganyika huyo na hii ndivyo ilivo hadi hii leo kwamba saikolojia ya mtanganyika ni ya hofu na woga na kutojiamini, na watawala wetu wanalijua hilo na kwa vile CCM imebaki madarakani kwa miaka mingi wanaujua udhaifu wa mtanganyika kwamba akileta blaa blaaa tu anajua matokeao yake wapi atapokunyia.kwa hiyo watawala wetu na wana siasa wetu hawana hofu ya aina yoyote ile na wananchi wao kwamba wanaweza wakawatoa madarakani kwa njia ya aina yoyote ile na inapotokea kuona kwamba kuna chama cha upinzani kinaweza kuwang'oa madarakani wanatumia umafia wa hali ya juu kuhakikisha kwamba chama hicho kinasambaratika au kukosa kuaminiwa na wananchi kwa uzushi mkubwa wa kidini au kikabila.Mhango uliona wapi au ulisikia wapi kwamba Rais akiwa madarakani anakuwa na kinga ya kutoshitakiwa na akiwa nje ya madaraka pia anakua na kinga ya kutoshitakiwa na hatimaye wanafanya chcochote kile katika ufisadi,uonevu,dhuluma na kutowajibika mbele ya nchi yao na wananchi wao.Marais kama Mwinyi,Mkapa na Kikwete wanastahiki kusimamishwa mahakamni kwa kutowajibika kwa nchi yao na wananchi wao na kutumia madaraka yao vibaya kwa masilahi yao wao wenyewe binafsi,familia zao na waramba viatu wao.Sasa swali linalojiuliza kwa nguvu je ni nani atakaewasimamisha mahakamani Marais hao?Na uwezi kuamini mafao ambayo wanayoruzukiwa au waliyotengewa baada ya kuacha madarka ni mapesa kiasi gani sasa mimi najiuliza ni nini walichoifanyia nchi au wananchi mapaka wawe na haki ya mafao hayo mpaka kifo chao wakati mapesa waliyotuibia ni mengi tu wao na familia zao?

Mtwangio said...


Na mimi sidhani kwamba viongozi wa CCM wanahofu kwamba wakitolewa madarakani wanaweza kusimamishwa mahakamni bali kama ulivyosema" tamaa,upofu,uroha na roho mbaya"hivi ndivyo vinawafanya wafanye kla njia wabaki madarakani na kwa vile hawana hofu ya kwamba wananchi wanaweza kuwatoa madarakani ndio maana wanakifanyia chama chochote kile ambacho kinahatarisha kuwepo kwao madarakani.Mana swali la kujiuliza ni hili kwa nini wananchi kama wananchi bila ya kujali kwamba wewe unahusika na chama gani wakubali matokeo yote hayo ya kigaidi ambayo yaliyofanywa na serikali na viongozi wa CCM?je ni kweli ni waoga kiasi hiki kwa nini tusitoke kwa maandamano ya usalama na amani tukapinga vikali ugaidi huu wa CCM na serikali yake?Je tumekuwa ni watu wanafiki,wasema pembeni na kuwa na hamasa ya kulipuka na na hesabu ya kushuka chini ikifika sifuri ndio kana kwamba hakuna lilitokea?Na maisha kuendelea kama kawaida?Na tukumbuke wazi kwamba wakati wa Bwana Mungu na malaika wake kushuka kuja kuwatetea wanyonge na wadhulumiwa wakati huo umeshakwisha na wala wakati wa miujiza kwamba CCM itatoka madarkani muujiza huo haupo na hautokuwepo na Tanzani itabaki daima kama Tanzania mpaka dunia hii itakapotoweka, viongozi na waongozwa watakuja,watakuwepo na wataondoka na Tanzania itabaki kama ni Tanzania mikononi mwa watanzania ambao wanastahiki kheri kwa kuhudumiwa na viongozi wao kama kweli wana sifa ya uongozi na wala sio majmbazi mafisadi na wenye roho mbaya kuanzia awamu ya pili mpka hii tuliyokuwa nayo.

Mhango umekuwa na matumaini kwamba watanganyika nao wanaweza kuwaondoa viongozi wao madarakani kama walivyoondolewa akina Zine El Abidine Ben ali,Mubaraka,Abdallah Saleh na Ghadhafi -sikumtaja Saddam hussein kwa hoja kwamba hakuondolewa na watu wake bali kwa masaada wa mataifa makubwa kwa kulinda masilahi yao na wala si masilahi ya wananchi wa iraq-Kwanz anakubali kwamba dhuluma,uonevu na kunyanyaswa unapoendelea kwa muda mrefu toka kwa watawala ni lazima wananchi watatafuta ufumbuzi wa kuiondoa hali hiyo na kwa kuindoa hali hiyo inahitajika kuwepo na maandalizi ya kisaikolojia ya wananchi hao kwa utaratibu ufuatao:
1-Kutambua na kuelewa kwamba viongozi wao waonevu,wanyanyasaji,mafisadi na wenye kuwadhulumu haki zao zote kama wananchi.
2-Kuwa tayari kujitolea muhanga kuwatoa viongozi hao madarakani kwa kumwaga damu endapo viongozi hao hawpo tayari kutoka madarakani kwa njia ya kidemokrasia.kwa kujitolea muhanga huko maana yake ni kukubali kufa kwa ajili ya nchi na wananchi na kwa mustakbali wa vizazi vijavyo na kuingia katika kitabu cha historia kama mashujaa.

Mtwangio said...

Naam mhango nadhani mimi na wewe tunakubaliana kabisa kwamba wananchi wa Tanganyika wanatambua na kuelewa kipengele namba 1,lakini kwa kipengele namba 2 wananchi wa Tanganyika hatukulelewa katika utamaduni huo wa kufa kwa ajili ya nchi na wananchi wenzetu na kwa vile hatukulelewa katika utamaduni huo na kwa vile CCM imebaki madarakani kwa miaka mingi kwa kuendelea kuwatia woga na hofu na kuwaishisha katika shimo la umasikini ambalo hawawezi kujikomboa muda wa kudumu CCM itabaki madarakani,wananchi hao wamebaki kupigania daily bread yao na kujali familia zao na kwa hili CCM wanalijua na wanaliendelea hadi mwananchi wa Tanganyika amefikia kutojiamini kwamba anaweza kuleta mabadiliko katika nchi yake.

Mhango mafanikio ya kung'olewa viongozi na wananchi wao Mashariki ya kati yametona na utamaduni wa malezi kwamba mwananchi anaweza kufa kwa ajili ya nchi yake na wananchi wake na akazingatiwa kama ni shujaaa ambae hatosaulika katika historia ya nchi hiyo ukiongezea malezi yao ya mafunzo yao ya kidini kwamba inapotokea kupigania haki na ukafa katika kupigania haki hiyo unazingatiwa ni kama shahidi mbele ya Bwana Mola na pepo inakuhusu kwa kuchanganya ushujaa wa nchi na pepo wananchi hao wapo tayari kufa wakati wowote ule endapo wanaona haki haitendeki.Mhango nilisema kwamba tuwalenge vijana mustakbali wa Tanganyika upo mikoni mwa vijana na wao ndio wanaoumiliki pamoja na kuishi vijana hao katika shimo la umasikini na hofu na woga ni juu yetu kuwaonyesha njia na kuwatanabahisha kwamba wanaweza kuleta mabadiliko kabisa na ya uhakika bila ya kutegemea vyama vyao kwa njia ya kidemokrasia na hata kwa kumwaga damu kuwaondoa watawala hao muda wa kudumu kutakuwa na maandalizi ya kushikamana kwa kujaliana kwa kujipanga nakuona kila kijana ni mkono wa kijana mwingine naamini kwamba wanaweza kuwachelewesha lakini hawawezi kuwasimimisha!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mtwangio umenifumbua macho. Maana pamoja na ujanja wangu sikuwa najua chanzo cha ukondoo wa Watanganyika. Hata hivyo, tukubaliane kuwa binadamu ni kiumbe anayebadilika kila wakati na kulingana na wakati. Inakuwaje watu wetu hwabadiliki? Ingawa nakubaliana nawe na chanzo cha ukondoo. Nataka nikupe muendelezo wake. Kinachofanya watanzania wasiingie mitaani kuondoa huu uoza ni kwamba ufisadi wa Tanzania ni wa kimfumo kiasi cha kugawiana na kufanya kila mtu hasa walio wengi kutokuwa na shida zinazoweza kuwalazimisha kuingia mitaani. Hebu fikiri mtu hana pesa anakwenda kwa ndugu yake fisadi anamkatia uchache siku inapita. Kesho akibanwa tena anakwenda kwa mwingine hivyo hivyo mwaka unakatika. Unadhani mtu wa namna hii anaweza kuingia mitaani ikilinganishwa na wakenya au wamisri ambapo kila mtu anabeba msalaba?
Hata hivyo baada ya kuingia utawala unaokula kwa miguu na mikono tena bila kunawa, nadhani kamchezo haka katakufa kiasi cha watu kuamka na kufanya kweli. Hakuna watu walikuwa makondoo kama wamisri au walibya.
Hivyo Mtwangio, tusiwakatie tamaa wala kuwalaumu Watanganyika. Watabadilika hata kama hawataki. Mabadiliko ni kama mimba lazima izaliwe iwe ni kwa operesheni, uzazi wa kawaida au kutoka na kumuua mjamzito.