How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 19 June 2013

Tuvunje Muungano au tuungane kweli kweli

Zanzibar watataka serikali tatu kwa vile si mzigo kwao. Pesa ya kuendesha serikali ya Tanganyika haitatoka Zanzibar ingawa pesa ya kuendesha serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar siku zote imetoka Bara. hivyo kwa watu kama hawa ambao hawataonja machungu ya kuwa na utitiri wa serikali kuwa na serikali tatu si tatizo. Pia wazanzibar wangependa serikali tatu ili kuendelea kuukana utanzania na kuukumbatia uzanzibari.  Kama na watanganyika watachangamkia utaifa wao wa asili hakuna shaka utanzania utabakia kuwa kwenye shubaka na nyaraka na thamani yake itatoweka. Kitendo cha namna hii ni kuvunja muungano hata kama hatutaki kusema wazi. Kama tumeridhika na hili basi tukubali kuvunja muungano badala ya kuutetea mchana na kuuvunja usiku. Huu ni unafiki na kutojiamini. Tuachane na muungano na kushikilia maslahi binafsi kama ambavyo ilivyo. Tuseme wazi kuwa maslahi yetu kama bara au visiwani ni zaidi ya muungano ili dunia ituelewe na tupumue au vipi?  Je kuna haja gani kuwa na utaifa usio na mwenye kuubeba kama ambayo itakuwa kwa utanzania ambao hata hivyo umebakia kubebwa na watu wa Bara huku wa Visiwani wakiuepa kwa gharama yoyote vinginevyo kuwepo na maslahi kama uwaziri ubunge au fursa za kuchuma?
Bara watataka serikali moja ili kuondoa mzigo unaowakabili hadi sasa wa kugharimia uendeshaji wa serikali mbili hasa ukilinganisha vyanzo vya uchumi baina ya pande mbili. Ni ajabu kuwa waliokusanya maoni kutoliona hili! Ni ajabu kuwa wabara wanazidi kuongezewa mzigo ili kuwaridhisha wavisiwani. Pia itakuwa ni ajabu kama tutakuwa na serikali tatu bila muungano kuvunjika kulaleki!
Kuna ushahidi wa kutosha kuwa waanzilishi wa muungano waliamua kuwa na serikali mbili ili baadaye waelekee serikali moja pamoja na kutofautiana mwanzoni kutokana na hali ya kisiasa ya wakati ule. Kwa mujibu wa Jaji Mark Bomani alikaririwa hivi karibuni akisema, “Hayati Karume yeye alipendekeza nchi mbili kuungana na kuwa nchi moja mara moja. Hayati Nyerere yeye alisita kidogo kwa kuogopa kwamba ingeonekana Zanzibar imemezwa na Tanganyika na hivyo pengine kuelekeza maasi Zanzibar.” Wakati ule ilikuwa inaingia akilini. Je baada ya kukaa pamoja kwa zaidi ya miaka arobaini bado tunahofia kumezwa? Mbona Kilwa iliyokuwa na hadhi sawa na Zanzibar hailalamikii kumezwa wala Lamu Malindi na Mombasa nchini Kenya? ni ajabu kuwa tunaongeza wingi wa serikali na kujipa moyo kuwa ndiyo kudumisha muungano wakati tunauvunja kijanja!
 
Je kwa kuongeza serikali ya tatu badala ya kupunguza ya pili tunaimarisha muungano au tunaendekeza kila upande na maslahi yake? Kama kweli tunaamisha kuhitajiana basi tuungane na kuwa na serikali moja badala ya utitiri wa serikali ambazo kwa nchi ombaomba kama yetu zaweza kuwa chanzo cha kusambaratika. Muungano ni sawa na ndoa. Kinachoendelea ni sawa na ndoa ya maslahi au chuma ulete ambapo wanandoa hutumiana kwa maslahi tofauti. Ndoa halisi ni kuwa mwili mmoja na kitu kimoja badala ya vipande vipande.
Tufanye kama Marekani. Nchi zilizotengeneza Marekani au Kanada zilipoungana zilibakia kuwa majimbo na nchi zimeshikana na hakuna anayedai kumezwa. Hawaii ni sawa na Zanzibar. Lakini bado haidai wala kujihisi imemezwa na California au Texas kwa sababu ni nchi kubwa ndani ya muungano wa Marekani. Prince Edward Island nchini Kanada ni kijisiwa kidogo lakini hakijawahi kulalamika kuwa kimemezwa na Ontorio au Nanavut kwenye shirikisho pana la Kanada.  Kimsingi, hii hofu ya kumezwa ni ya si ya msingi na haina maana kwa vile kama tutaungana kweli kweli wote tutakuwa watanzania badala ya sasa ambapo tuna wazanzibari, watanganyika, watanzania, wapemba, waunguja na kesho tutakuwa na waMnemba. Kama kweli tunahitajiana haya madai ya Uzanzibari kama utaifa ya nini iwapo watanganyika kwa miaka zaidi ya 40 wameridhika kuitwa watanzania bila kulalamikia utanganyika.  Muungano mara nyingi hujengwa kwa kile waingereza huita give and take and good will. Unapata hiki na kupoteza kile. Unatoa kile unapokea hiki na mambo yanakwenda.
Tuhitimishe kwa kusisitiza kuwa bila kuwa na serikali moja muungano wa Tanganyika na Zanzibar utaendelea kuwa mzigo na kitendawili ambacho baadaye kinaweza kudhoofisha Tanzania. Tuamua tuwe na serikali moja au tuvunje muungano ili kuwe na nchi mbili ambazo kila moja itakuwa na serikali moja. Hivyo, kuondoa mzigo kwa walipa kodi wa nchi hizi. Kuwa na serikali tatu hata mbili ni sawa na kuwa hermaphorodite yaani mnyama mwenye jinsia mbili ambaye si jike wala dume bali kituko. Kama sote ni wamoja kihistoria na kijiografia, kwanini tunaogopa kuungana na kutengeneza nchi moja yenye nguvu na ustawi? 
Chanzo: Tanzania Daima Juni 19, 2013.

6 comments:

Mtwangio said...

Mimi kama mwananchi wa Tanganyika nataka nirudishiwe nchi yangu na nijidaie uraia wangu nikiwa nchini mwangu au nje ya nchi kama wanavyojidaia wazanzibari wakiwa ndani ya nchi au nje ya nchi,kamwe uwezi kumsikia mwananchi wa kawaida wa visiwani akijitambulisha kwamba yeye ni mtanzania pale anapoulizwa nchi yake au uraia wake utamsikia akijbu kwa majivuno kwamba yeye anatoka Zanzibar na mzazibari!Sasa mimi sina haja ya kusema kwama huyu ni mwananchi mwezangu tunatoka taifa mmoja na tunajidaia uraia mmoja,Nahitaji serikari yangu ya Tanganyika ambayo itanihudumia mimi kama mtanganyika na kuendeleza maendelo ya nchi yangu ya Tanganyika bila ya kubeba jukumu la kuingalia au kuisaidia nchi nyingine kwa hoja kwamba tupo katika muungano.Kwangu mimi kama mtanganyika serikali tatu ni unafiki wa kisiasa na kuendelea kulinda masilahi ya wanasiasa,viongozi wa Tanganyika na Zanzibar na kulinda masilahi ya wafanya biashara wakubwa wakubwa na wadogo wadogo toka visiwani ambao wanamiliki njia nyingi za uchumi nchini mwangu Tanganyika.Watanganyika bado tumelala, hatujajitambua kwamba ni watanganyika na bado tunajiita tu watanzania kwa sababu ya muungano kwa hiyo wakati umeshafika wa kurudishiwa nchi yetu na uraia wetu na wale wanasiasa wa Tanganyika ambao bado wnataka kuikalia nchi nyingine au kujifanya kama ni kaka mkubwa kwa nchi nyingine wakati huo umeshapita.Tanganyika ni ya watanganyika na kama kuungana na nchi nyingine basi maamuzi hayo yaamuliwe na watanganyika wenyewe na isiwe tuamuliwe na wanasiasa wetu au serikali yetu kwani tumeshafikia umri wa kukomaa vya kutosha kuweza kufikiri,kuona,kuchagua,kuamua na kujua masilahi yetu yapo wapi na ni nani wa kuweza kubadilishana masilahi.Hoja ya kusema tunashirikiana kihistoria na kijiografia tusiipe uzito sana au iwe ni sababu ya ukaribu wa muungano tumeishi na visiwa vya Ngazija(Comoro),Seychelles,Mauritius na vinginevyo kama majirani wema kwa salama na amani na tuuvunje muungano tutaishi na visiwa vya zanzibar na Pemba kwa salama na amani kama tunavyoishi na majirani wengine.Hofu zingine ambazo zinajitokeza au zinazoelezewa hazina msingi wowote wa kusema tuendelee kuuenzi muungano.Mwisho namalizia nikisema kwamba nyinyi wanasiasa na mliokuwepo madarakani hamuyaoni walaa hamuyajui ambayo wananchi wa kawaida wanayoaona au kuyaishi katika muungano huu na kama mnayajua na kuayaona kwa nini mjifanye amuyaoni wala kuyajua kwa masilahi yenu binafsi bila kuangalia masilahi ya wananchi ambao ndio wanaufanya muunagano uwe na maana.

Ahsante sana Mhango kwa machango wako huu mkubwa katika swala hili la muungano lakini mimi kama ni mtanganyika sina haja nao.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Usemayo Mtwangio ni kweli tupu. Heri tuvunje kitanda cha muungano na kugawana mbao ili nasi tujisikie huru na kuwepo. Maana tangu hiki kiini macho kiitwacho muungano ambao kimsingi ni mgongano na mnyonyano, watanganyika tulipoteza utaifa wetu kwa kukumbatia utanzania ambao una uzanziari ndani yake wakati wazanzibari hawakuukumbatia ingawa ndiyo walipaswa kuliko sisi.
Wakati wa kufumua muungano umefika na ni huu.Nadhani akina Warioba walikusudia hili la kuuvunja muungano kwa kuwatumia wananchi wenyewe.

Mtwangio said...

Mhango sijui kosa nililifanya wapi maana comment yangu iliyotokea ni paragraph ya mwisho kabisa katika comment ambayo niliyoituma nami naamini wazi kwamba wewe si mtu wa kumziba mtu mdomo kwa kutochapisha comments za wasomaji wako.Comment niliiandika kama ifuatavyo naomba kama hakuna usumbufu upande wako uiweke kwa utaratibu ambao nilioukusudia nao ni huu:

Mhango nimekusoma na pia nimekuelewa vyema kwa uchambuzi wako,hadharisha yako,matamanio na hata matumaini na matarajio yako ya kuutakia kheri muungano.Mimi naandika kama mtanganyika ambaye sina ridhaa wala sioni kuna haja ya kuendelea kuwepo kwa muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar,naelewa wazi maoni yangu haya si mageni kwako lakini naandika kama mwananchi wa kawaida wa tanganyika ambaye zaidi ya miaka 40 ya muungano huu sijanufuika kwa chochote kile au hata Tanganyika kunafaika na Zanzibar kwa chochote kile zaidi mimi ni kama mwananchi wa Tanganyika kuona kwamba wazanzibari na wapemba wamenufaika na wanaendelea kunufaika vya kutosha na muungano huu japo wamekua na makelele na malalamiko ya aina yote ya kudai kuonewa,kunyanyaswa na kudhulumiwa katika kuwepo kwao katika muungano huu wa zaidi ya miaka 40!

Mhango nakariri tena nikisema kwamba naandika kama mwananchi wa kawaida wa Tanganyika ambaye anaungalia muungano kwa masilahi ya mwananchi kwanza kabla ya wanasiasa na viongozi waliopo madarakani,kama ujuavyo lazima muungano wowote ule kwanza uagalie na kulinda masilahi ya mwananchi katika muhungano huo,lakini iwapo masilahi yanapatikana zaidi kwa upande mmoja na upande mwingine unakuwa ni kuelemewa na mzigo huo sio muungano sahihi na kama ulivyotolea mfano ulipoandika ukisema "kinachoendelea ni sawa na ndoa ya masilahi au chuma ulete ambapo wana ndoa hutumiana kwa masilahi tofauti".Naam, hivyo ndivyo ulivyo muungano huu wa zaidi ya miaka 40 wananchi wa zanzibari kama ni wananchi wapo katika ndoa hii kwa masilahi yao ya wazi na makubwa sana na mwananchi wa tanganyika amekua sawa na chuma ulete.Hapa nitafafanua zaidi kwa vile katika muungano wowote ule duniani wananchi wana uhuru na haki sawa ya kuishi na kufanya shughuli zao za kuendeleza na kuboresha maisha yao,hata kama hatua kwa hatua kama zilivyowekewa sheria baadhi ya nchi za ulaya ya mashariki zilizojiunga na umoja wa ulaya.kwa hiyo ukiangalia wimbi la watafutaji kutoka visiwani kuja Tanganyika ni kubwa zaidi kuliko uhamiaji wa kutoka Tanganyika kuhamia visiwani na kwa uhuru huo basi wazanzibari na wapemba wamejizatiti kiuchumi na kijamii kuliko watananganyika waliopo visiwani!

Mtwangio said...

Leo hii utakuta wafanya biashara wetu wakubwa wakubwa na wadogowadogo amabao wanashika njia za uzalishaji ni kutoka visiwani na hata sheria ya kumiliki ardhi Tanganyika ni tofauti na iliyopo visiwani,mzazibari ananua na kumiliki ardhi kama ni alivyo mtanganyika na kwa upenyo huo wazanzibari wameshaanza kutolea macho kwa kuelekeza majuhudi yao pia katika kununua na kumiliki ardhi Tanganyika,lakini sheria ya ununuzi na kumiliki ardhi ya zanzibar inamuhukumu na kumchukulia mtanganyika kama mgeni sawa na mgeni toka nchi yoyote ile ya ugenini!Sasa kutokana na kanuni ya kiuchumi ni kwamba wafanya biashara wakubwa wakubwa na wenye kumiliki ardhi kwa kiasi kikubwa daima hawapo tayari kusikia au kutaka na kuona muungano unavunjika kwani kuvunjika kwa muungano kwao wao ni pigo kubwa kwa masilahi ya vitega uchumi vyao na hasa kwa vitega uchumi hivyo haviwezi vikahimili na kuleta matunda kwao walipotoka visiwani.kwani swala ambalo linajiuliza lenyewe kwa nguvu na kwa kasi kwa nini wazazibari na wapemba hawawekezi kwao walipotoka na kwa nini wasijenge kwao walipotoka na badala yake wanawekeza na kujenga Tangayika?Je katika joto hili la miaka yote hii ya ukereketwa wa wazanzibari kutaka kuvunja muungano wawekezaji hawa wa kizanzibari na kipemba watakuwa na utulivu kweli wa kisaikolojia?Nina shaka na hilo na kawabu lake lipo wazi kwa hiyo hawa wanakuwa ni nguvu inayofanya kazi kizani ya kutaka kuona muungano hauvunjiki na hatimae ndio sauti zinazosikika kwa matakwa ya kuongolea kero za muungano na wala si kuvunjika kwa muungano,na nguvu hizi huwa na mashaka kwamba hujipendekeza kwa wanasiasa wa Tanganyika kwa aina moja au nyingine kuona kwamba muungano unabaki hai na kwa wazanzibari wenziwao inakua ni sauti ya kuwaunga mkono wale wanaojiita "muhafidhiina"kwa kushikia bango kwamba kuoongelewe kero za muungano na wala si kuvunja muungano.

Mtwangio said...

Mimi kama mwananchi wa Tanganyika nataka nirudishiwe nchi yangu na nijidaie uraia wangu nikiwa nchini mwangu au nje ya nchi kama wanavyojidaia wazanzibari wakiwa ndani ya nchi au nje ya nchi,kamwe uwezi kumsikia mwananchi wa kawaida wa visiwani akijitambulisha kwamba yeye ni mtanzania pale anapoulizwa nchi yake au uraia wake utamsikia akijbu kwa majivuno kwamba yeye anatoka Zanzibar na mzazibari!Sasa mimi sina haja ya kusema kwama huyu ni mwananchi mwezangu tunatoka taifa mmoja na tunajidaia uraia mmoja,Nahitaji serikari yangu ya Tanganyika ambayo itanihudumia mimi kama mtanganyika na kuendeleza maendelo ya nchi yangu ya Tanganyika bila ya kubeba jukumu la kuingalia au kuisaidia nchi nyingine kwa hoja kwamba tupo katika muungano.Kwangu mimi kama mtanganyika serikali tatu ni unafiki wa kisiasa na kuendelea kulinda masilahi ya wanasiasa,viongozi wa Tanganyika na Zanzibar na kulinda masilahi ya wafanya biashara wakubwa wakubwa na wadogo wadogo toka visiwani ambao wanamiliki njia nyingi za uchumi nchini mwangu Tanganyika.Watanganyika bado tumelala, hatujajitambua kwamba ni watanganyika na bado tunajiita tu watanzania kwa sababu ya muungano kwa hiyo wakati umeshafika wa kurudishiwa nchi yetu na uraia wetu na wale wanasiasa wa Tanganyika ambao bado wnataka kuikalia nchi nyingine au kujifanya kama ni kaka mkubwa kwa nchi nyingine wakati huo umeshapita.Tanganyika ni ya watanganyika na kama kuungana na nchi nyingine basi maamuzi hayo yaamuliwe na watanganyika wenyewe na isiwe tuamuliwe na wanasiasa wetu au serikali yetu kwani tumeshafikia umri wa kukomaa vya kutosha kuweza kufikiri,kuona,kuchagua,kuamua na kujua masilahi yetu yapo wapi na ni nani wa kuweza kubadilishana masilahi.Hoja ya kusema tunashirikiana kihistoria na kijiografia tusiipe uzito sana au iwe ni sababu ya ukaribu wa muungano tumeishi na visiwa vya Ngazija(Comoro),Seychelles,Mauritius na vinginevyo kama majirani wema kwa salama na amani na tuuvunje muungano tutaishi na visiwa vya zanzibar na Pemba kwa salama na amani kama tunavyoishi na majirani wengine.Hofu zingine ambazo zinajitokeza au zinazoelezewa hazina msingi wowote wa kusema tuendelee kuuenzi muungano.Mwisho namalizia nikisema kwamba nyinyi wanasiasa na mliokuwepo madarakani hamuyaoni walaa hamuyajui ambayo wananchi wa kawaida wanayoaona au kuyaishi katika muungano huu na kama mnayajua na kuayaona kwa nini mjifanye amuyaoni wala kuyajua kwa masilahi yenu binafsi bila kuangalia masilahi ya wananchi ambao ndio wanaufanya muunagano uwe na maana.

Ahsante sana Mhango kwa machango wako huu mkubwa katika swala hili la muungano lakini mimi kama ni mtanganyika sina haja nao.

Mtwangio said...

Kama nilivyosema hapo juu kwamba sidhani kwamba wewe si mtu wa kuziba mdoma kwa kuchapisha comments za wasomaji wako.Lakini endapo utaona kwamba kwa comments zilizokamilisha paragraph yangu ya mwisho kwamba haziendani na kufikisha fikra kama ipaswavyo nitaheshimu maamuzi yako ya kufikisha paragraph yangu ya mwisho katika fikra nzima niliyoitaka kuifikisha.