The Chant of Savant

Saturday 15 October 2016

Barua kwa mzee Mchonga Nyerere

 
            Baba tena wa kaya, nakusalimu kwa heshima na taadhima. Japo najua hutajibu, naamini unanisikia. Japo huweza kupokea salamu zangu, bado nakuheshimu tena kuliko wengine walio hai ambao uliwakingia kifua hadi ukaambiwa umebeba kinyago cha mpapure. Na kweli, kilikuwa kinyago cha mpapure ile mbaya. Maana kilitutenda tena vibaya. Kwani kilitupapura si haba hadi tukaparurika na kupigika huku kikiendelea kujisifu na kujifanya kijuaji wakati ni kilaza cha kawaida tokana na matendo yake machafu. Kinyago kile kiliuza kila kitu ulichosimamia hadi na chenyewe kikajibinafsisha kwa wachukuaji kilichowapa jina zuri la wawekezaji. Hata hivyo baba, Mungu si Mlevi;kwani alikipiga laana kikaondoka kimechafuka ile mbaya. Hata siku hizi sikisikii kikipayuka na kujivuna kama wakati ule kilipokuwa kwenye ulaji kikasahau kuwa kuna kesho tena yenye mazonge.
            Sasa ni miaka 17 tangu baba yetu mpendwa uliyependa taifa kuliko hata familia yako, Mzee mwenyewe Mchonga mwana wa Burito tangu uondoke kimwili duniani. Wengi wanakukumbuka hasa wale wanyonge uliowajali na kuwasemea ingawa wenye kusaka ulaji hukusanifu kwa kutembelea kaburi na familia yako pale wanapohitaji tafu tokana na umaarufu na utaua wako usiomithalika uliotokana na uadilifu na upendo wake wa dhati. Tunakukumbuka baba hasa walevi na wasio nacho. Japo Mchonga umeondoka kimwili, kiroho tuko nawe daima hasa wanyonge uliowapigania na wengine kuwakomboa hadi wakawa wazito japo wanakusanifu.
            Tokana na kuyoyoma miaka mingi tangu uondoke, ngoja nikupe taarifa muhimu japo chache.
Kwanza, wale ulioamini wangevusha walevi wako, waliwazamisha na kuwauza kwa udoho udoho na vitu vya hovyo kama vile majumba na akaunti kwenye mabenki. Zile nyumba ulizotaifisha tokana na kujengwa na njuluku za walevi, nyingi zilitwaliwa chini ya kidhabi uliyempa tafu ukiamini ni mwema usijue shetani anatamwingilia na kumuacha mchafu. Lile jina la Mr Clean ulilompa liligeuka kuwa kinyume. Sasa ametokomea kwenye sahau ya kisiasa kiasic ha kuona aibu asijue la kufanya. Viwanda vilipigwa mnara tena kwa bei ya kutupwa. Ni sasa tu tunapoanza alifu na kijiti baada ya kuja kwa Daktari Joni Kanywaji Makomeo ambaye anaonekana kueleewa somo lako barabara.
            Baada ya kuondoka kwa aibu wale uliowakingia kifua na kuwanadi, walichukua wale uliowaita wezi na mafisadi walioonyesha ukwasi wa kutisha hadi wakawa na jeuri ya kukodisha pipa kwenda kuchukua fomu za kugombea ulaji. Kama kile kinyago cha mpapure nao walituumiza kweli kweli. Kwani, badala ya kuuza kaya waliigawa kwa mabwana zao. Baada ya kutimka, tulitegemea wanyee debe Keko au Segerea; lakini mzito anaonekana kuwakingia kifua akidhani ni huruma na si hujuma.  Kuingia kwa bazazi huyu na genge lake kulinajisi na kuibaka kaya hakuna mfano. Tulishuhudia kashfa kama vile EPA, Escrow, UdA na madude mengine ya kutisha. Je unaweza kuamini kuwa kaya ilifikia mahali pa kuendeshwa kwenye autopilot kwa miaka ipatayo kumi? Ni juzi tu tuligundua kuwa kumbe pale bandarini mita za mafuta, flow meters zilifungwa kiasi cha weze kuiingia bila kulipiwa kodi? Kama haikutosha, kidhabi huyu aliizunguka dunia hadi akaiitwa Vasco da Gama, yule habithi wa kireno aliyezunguka dunia akipora na kuharibu ustaarabu wa walevi kila alipotia mguu.
            Ticha Mchonga, tena kabla sijasahau, elimu uliyoanzisha na kupigania nayo ilibakwa ile mbaya hadi kufikia wazito na walevi wa kada ya chini kughushi vyeti vya kitaaluma. Kwa sasa kaya yako inasifika dunia kwa kuwa na vihiyo na vilaza wengi waitwao madaktari wakati walikimbia umande.
            Mambo hayakuishia hapo. Maadili uliyoanzisha yaliishia kuwa madili ambapo kila mwizi aliweza kujiibia kwenye kaya iliyogeuzwa shamba la bibi. Hiyo mosi. Pili, waliibuka matajiri wa ghafla bin vu ima baada ya kuuza mibwimbwi au kutumia vyeo vya marafiki na wengine wazazi wao huku walevi wakizidi kupigika. Siku hizi si ajabu kuona kibaka akiabudiwa na kuitwa mheshimiwa wakati ni mhalifu. Ama kweli, tunazimiss zama zako za uwajibikaji na maendeleo. Hata hivyo, good news, ni kwamba dokta Kanywaji anajitahidi kuwabana ingawa amegoma kubadili mfumo. Kwa sasa kila kitu kinategemea usongo wake. Wenye akili japo walevi tunahoji; Inawezekanaje akafanikikwa kuirejesha kaya yako bila kufumua na kuufuma upya mfumo zandiki na mbovu uliopo. Tumempigia kelele arejesha Katiba Mpya hadi makoo yanauma. Hata hivyo, hatutachoka hadi kieleweke.
            Mwisho, yule rafiki yake kidhabu uliohoji ukwasi wake, alitimkia upingaji, akagombea ulaji na kupigwa chini. Yuko huko akipiga kelele na kuzidi kuubomoa upingaji uliochanganyikiwa na kujichanganya.
Nimalizie kwa kukutaarifu kuwa bi mkubwa wako, Mary, bado anadunda japo uzee unapiga hodi. Tunaendelea kumuenzi na kumheshimu kama maza wetu. Nakutakia uendelee kulala salama huko uliko ila tunakukumbuka sana baba yetu hadi unafikia kuwa na nguvu na ushawishi kuliko walio hai.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

2 comments:

Anonymous said...

We are not deify him but he is our Prophet who will live among us.They say,leaders are coming and going and some of them are forgotten by their people and the country remains,but for our Prophet Mwalimu Nyerere will be remembered by his People as long as Tanzania as a country will remain.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

What nuggets! Thanks for such a vision. I fully concur with you; the man was a leader that many coming generations will treasure.