The Chant of Savant

Tuesday 7 February 2017

Akina Mgoshi Machungu kujidai Hollyweed

          Baada ya rahis mpenda sifa na vimwana, Don Trumpet, kuipiga tafu Bongolalaland kwa kuruhusu wabongo kuingia kayani kwake bila visa, kijiwe kinapanga kwenda kule hasa Holyweed kujinoma kama hakina akili nzuri. Pamoja na upenyo huu, sijui kama magaidi hawataanza kutuonea wivu na kutaka kutunyotoa roho kwa wivu.
            Mgoshi Machungi anaingia yote 36 yakiwa nje kwa furaha. Anasalimia na kutujuza habari njema. Anasema “wagoshi mimesikia jinsi Tiampu aivouhusu wabongo kuingia Maikani bia visa? Sijui wenzangu mmeipokeaje hii habai njema?”
            Kapende anajibu “hapa hakuna cha kusherehekea hasa vinginevyo uwe mwanasiasa au muuza bwimbwi kama si fisadi anayeweza kuwa na  njuluku za kulipia pipa na hoteli kwenda kustarehe kule. Hii ni danganya toto. Huenda kuna kitu ameona anachotaka kuja kuchukua kwa kujifanya mwekezaji wakati ni mchukuaji.”
            Msomi Mkatatamaa anajibu “huenda anataka kudhibiti hii  urani iliyogunduliwa Kusini ili maadui zake wasiweze kuifaidi na kutishia woga ambao Marikani imekuwa ikitumia kutisha mataifa mengine hasa Irani ambayo imeshupaa kuwa haitishwi.”
            Mbwamwitu anamchomekea Msomi “nimesikia hii kitu ingawa sijui kama hata wamachinga wataruhusiwa kwenda kule kufanya biashara kama vile kuuza kanda na kununua kanda za wasanii wa kule.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anamchomekea “bila shaka mama ntilie nao wajiandae kukwea pipa kwenda kuwapikia watasha waliochoshwa na kunyotolewa roho na Makidonald Janki yaani vyakula vibovu tokana na ujinga na uvivu wao. Nasikia watasha wanakula kila kitu hata nyanya chungu na mchunga. Ila wakija huku hujifanya hivi si vyakula anavyoweza kula mtasha wakati kwa wanavipwakia kama hawana akili nzuri.”
            Kabla ya kuendelea, Kapende anachomeke “ nadhani hapa na vyangu wa Bongo hao ndiyo usiseme wanajiandaa kutia timu hasa ikizingatiwa kuwa Don mwenyewe anapenda vimwana kama jamaa yangu Njaa Kaya. Wakiingia kule watapeta hasa ikizingatiwa kuwa uchangu kule unaruhusiwa kisheria. Jamaa yangu mmoja alinitonya kuwa machangu hulipia ndude zao kodi kama wafanyabiashara walipiavyo maduka na biashara zao nyingine halali.”
            Mipawa naye anaamua kutia timu na kusema “ hii kitu inaweza kushabikiwa sana na kuonekana nzuri tu bila kufikiri. Tangu lini Marikani ikapenda kaya yoyote duniani wakati falsafa yake inajulikana kuwa hakuna rafiki wala adui wa kudumu bali maslahi?. Wabongo–tokana na ujuha na ulimbukeni na upenda dezo–wanaweza kujisifia wamepata wasijue wamepatikana. Hapa lazima nitahadharishe. Wauza bwimbwi msithubutu. Kwani kwa Trumpet hawana mchezo na bwimbwi kama hapa kayani ambako bwimbwi lilihalalishwa baada ya kifo cha nzee Nchonga. Huoni walivyowakamata akina Akasha pale Kenya na El Chappo kule Mexico?”
            Kabla ya kuendelea Kanji anakula mic “kama Tramp naruhusu Tanjania kwenda Amerikani mimi sasa kwenda fanya pango vekeza kule. Tafanya pango unganisa Bombey na Vashington ili fanya biasara kuba kuba. Kama veve natumia akili wizuri hapa naweza kuwa tajri veve na vatu vako vote.”
            “Wenzako tunashangilia wabongo kuruhusiwa kuingia kwa Joji Kichaka kama taifa kumbe mwenzetu unakamia kwenda kule kwa faida ya Ughabacholini na si kaya yetu. Ama kweli kunguru hafugiki walisema wahenga! Wakati sisi tukidhani wewe ni mwenzetu kwa kutudanganya na kutuita ndugu zako, kumbe bado roho yako iko Bombei!” anasema Mchunguliaji huku akipokea gazeti toka kwa mheshimiwa Bwege.         
            Mheshimiwa Bwege anakatua mic “dog achana na Kanji. Kwani ulikuwa hujui sera za hawa jamaa ambao alituletea mkoloni mwingereza halafu akatuachia wakazaana kama magugu? Mie hapa nafikiri kwenda kwa Joji Kichaka kuoa mitoto ya kitasha. Lazimanilipize kisasi. Kila mara naona mabinti zetu wakichezewa na watasha wanaojifanya watalii, acha nami niende kule niwachezee binti na dada zao hata mama zao. Maana naambiwa kuwa watasha si wabaguzi kama wamanga au magabacholi wa hapa. Nasikia kule wote wanaitwa wamakonde bila kujali nani alitoka wapi. Jamaa yangu anayeishi kule alisema kuwa watasha wakiamua kubagua wanabagua kila mtu ambaye si mtasha bila kujali ni gabacholi, mmanga au mjep au mchainizi.  Pia naambiwa akina mama wa kitasha wanapenda sana wanaume wa kiswahili kwa vile wanajua kupenda na kuwanyenyekea.”
            Kabla ya kuendelea Msomi anakatua tena mic “waswahili kwa kushobokea vya wengine. Kwani hapa wanawake wameisha au ni kutafuta matatizo? Hamjui kuwa mama wa kitasha anaoa Mswahili bali haoelewi kama mlivyozoea. Mgoshi Machungi najua udenda unakutoka kwa kuwazia mitoto ya kitasha. Hamjui mnachokimbilia kama kweli mtajaliwa kwenda zenu kwa Trampet. Sijui kama mtaweza kupewa vijibwa mvipeleke kujisaidia au kufanya mazoezi huku mkiviruhusu kulala vitandani mwenu na kulia kwenye vyombo vyenu kama watasha wafanyavyo. Kuchunga mbwa kwa mswahili wapi na wapi. Kubalini. Mmezoea kuchunga mbuzi na ng’ombe lakini si mbwa.”
            Mijjinga aliyerejea hivi karibuni toka kijiji anakula mic “mie wala sina mpango wa kwenda kwa Trampet hasa ikizingatiwa kuwa aliwahi kusema kuwa lazima Afrika itawaliwe zaidi. Aliendelea kusema kuwa waswahili hawana akili ya kuweza kujitawala.”
            Kabla ya kuendelea Kapende anakatua mic ‘kwani alikosea? Huoni tulivyoruhusu magabacholi kuja hapa kujiibia watakavyo na kutajirika wakati sisi tukiendelea kuwa makapuku? Hii ni nini kama si ujinga?”
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.
 
 

No comments: