The Chant of Savant

Saturday 11 February 2017

Mlevi kuleta FBi kupambana na bwimbwi Bongo

          Baada ya Mkoa wa Dar-Si-Salama chini ya munene wake Po Makondakonda kujitutumua kupambana na biashara ya bwimbwi, mlevi niemeamua kuwaunga mkono. Nitatumia umaarufu wangu na elimu yangu ya juu sana ya mambo ya sheria na usalama kuwasaidia namna ya kushinda vita hii hatari na ngumu. Hivyo nitatoa mapendekezo yafuatayo kabla ya kuingiza the big gorilla, Federal Bureau of invasion (FBi).
            Kwanza, mapambano dhidi ya wauza bwimbwi al maaruf barons au kingpins kwa Kinyasa, yaanze kisayansi na si kisiasa, kukurupuka au kutafuta sifa. Mfano, lazima ufanyike uchunguzi wa kina na wa kitaalamu wa kubaini wauzaji ndipo wakamatwe. Hapa wale wanaoita vijidagaa kutafuta umaarufu na kuuridhisha umma wanapaswa kupata somo. Sina haja ya kuonekana kama nawakandia au kuwakong’ota. Iko wapi vita ya kupambana na shisha iliyoanzishwa kwa nguvu ya soda? Si bado watumia shisha wanaendelea kutesa. Mmeshindwa shisha; mtaweza bwimbwi?
            Pili, nguvu kubwa ielekezwe kwenye mapapa na si vidagaa vinavyogalagazwa mbele ya vyombo vya habari ili kuonekana mapambano ya kupambana na bwimbwi yapo na yanafanikiwa wakati si kweli. Juzi tuliltewa wasanii njaa wanaohangaishwa na njaa ya umaarufu na njuluku kiasi cha kugeuka kuwa taxi kisiasa. Maskini, wakati wakipiga kampeni tena baada ya kubwia bwimbwi hawakushughulikiwa. Sasa uchakachuaji umeisha. Jasho linawatoka. Wako wapi wanasiasa ambao microphone wa mjengo aliwahi kusema wanakula bwimbwi tena njengoni? Je ni wanasiasa wangapi na vyama vingapi vimekuwa vikifadhiliwa na wazungu wa bwimbwi? Kwani hii siri? Wako wapi wafanyabiashara mashuhuri wanaojulikana kuwa kingpins wa bwimbwi wanaosifika kufadhili wanasiasa na vilabu vya michezo?
            Tatu, zitungwe sheria kali dhidi ya kitu hii. Sijui kama zilizopo zina makali ya kuweza kupambana na kitu hiki hasa ikizingatiwa kuwa utawala uliopita ulihalalisha kila jinai. Naona yule anatoa mimacho akidhani nazua. Umesahau namna mashushu walivyofanya upelelezi na kukusanya orodha ya wauza bwimbwi wakubwa wakampa Njaa Kaya ambaye aliwahi kukiri alikuwa nayo asiifanyie kazi tokana na kuogopa kuvuruga ulaji? Kwanini asibanwe akatoa hii orodha ili kurahisisha kazi ya kuwasaka wauza bwimbwi? Au waliotangaza vita hii hawajui hii kitu ambayo hata kunguru wanaijua?
            Nne, ili kushinda vita dhidi ya bwimbwi tunapaswa kuwa wakweli kwa nafsi zetu. Mfano, huwezi ukapambana na biashara ya bwimbwi bila kuwa na sheria inayokupa mamlaka ya kukamata mali yoyote inayotuhumiwa kupatikana tokana na biashara hii haramu.  Ukiachana je mapilato wetu ni wasafi hasa ikizingatiwa kuwa wengi waliteuliwa na Njaa Kaya kwa kuangalia udini, urafiki na ushikaji? Anayebishia hili ajiulize wale mapilato vihiyo waliwezaje kuupata ujaji kama siyo kujuana? Je hawa wanaweza kutoa haki bila kununuliwa na wazungu wa unga? Naona yule anasonya. Sina maana kuwa majaji au mapilato wote ni makanjanja. Hasha. Ila wapo wengi ima feki, makanjanja, vihiyo na mafisadi tena wanaojulikana kwa majina.
            Tano, hakuna mashamba ya poppies Bongo. Hii maana yake ni kwamba bwimbwi linatoka ughaibuni hasa kule kwa Watalibani. Je linaingizwa kupitia wapi kama siyo kwenye viwanja vyetu vya ndege, mipakani na kwenye bahari zetu? Je hawa wanaosimamia maeneo haya wameshughulikiwa? Ni wangapi wanafahamika? Ukitaka kuwajua huna haja ya kuhangaika. Wapo vijana walioajiriwa jana lakini wana ukwasi wa kutisha. Unadhani wameupataje kama siyo kuruhusu bwimbwi lipite kwenye maeneo tajwa? Ukiachi hilo, inakuwaje wazungu wa bwimbwi wasijulikane wakati mateja yamejaa kila mtaa? Kamateni mateja yote yawapeleke yanakopata kago nako waeleze anayewasambazia kago. Ukiachia hilo, nenda Masaki na kwenye maeneo ya matajiri uone waja wenye kutia kila shaka walivyonunua mihekalu bila kuwa na historia ya njuluku. Kamata mahekalu haya na kuwabana wawambie walivyotengeza njuluku ya kuyanunua. Simpo. Hata wachovu mitaani wanawajua wauza bwimbwi ila wengine hawawataji kwa vile ni wafadhili wao. Mkikaa vizuri na wachovu wanaochukia kitu hii mtapata habari kibao. Je mtawahakikishia usalama dhidi ya wauzaji ambao ni wakatili hakuna mfano?
            Nimalizie kwa kuwapa mfano hai toka kwenye kaya ya nyayo pale jirani. Baada ya wauza bwimbwi waitwao Akasha kuwaweka mifukoni wanasiasa, polisi, majaji na kila yoyote mwenye nafasi, tokana na hofu ya kupoteza uchaguzi, lisirikali kule liliwaita FBi wakawategea ntego na kuwakamata na kuwasafirisha kwa Joji Kichaka. Nanyi kama mmeshindwa si mniambie niwaunganishe na FBi? Muve na zuva rakanaka.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: