The Chant of Savant

Sunday 5 February 2017

Hotuba ya Magufuli suto kwa Afrika

           Hivi karibuni rais John Pombe Magufuli alionyesha upekee kama kiongozi wa nchi kwa kuwa kiongozi wa kwanza wa  Tanzania kuhutubia mkutano wa wakuu wa Nchi Huru za Kiafrika kwa Lugha ya Kiswahili jambo ambalo lilipokelewa kwa hisia tofauti. Wapo walioona kama ni kujidhalilisha au kukwepa kutumia Kiingereza Lugha ya mtawala wetu wa kikoloni wa zamani huku wengine–hasa wenye kujitambua na kupenda taifa lao–wakimsifu kwa ujasiri na uthubutu huu wa aina yake. Wale ambao bado mabakia ya ukoloni hayajawatoka vichwani walidiriki kusema kuwa rais hajui Kiswahili bila kujua kuwa andiko lake kwa ajili ya shahada yake ya uzamizi (PhD) aliliandika kwa lugha hiyo. Niliwasoma kwenye mitandao wakikejeli kitendo hiki cha kishujaa bila kujua kuwa walikuwa wakifichua ujinga na kujikana kwao.
            Hata hivyo, ujinga na ulimbukeni na woga wa kutumia lugha ya Kiswahili ambayo ni moja ya lugha kubwa za kimataifa kwa baadhi ya wenzetu havikuanza jana wala havitaisha kesho. Zipo nchi tena jirani ambazo watu wake wanaonea aibu Kiswahili kwa kushabikia Kiingereza ambacho nacho hawakijui zaidi ya kukiongea kwa lafudhi za lugha zao asilia.  Wengi hukwepa kutumia Kiswahili au kikionea aibu kutokana na imani mfu kuwa lugha hii ni ya wale ambao hawajaelimika jambo ambalo si kweli. Hivyo, tunampa moyo rais Magufuli asikate tamaa bali aendelee kukienzi na kukitumia Kiswahili popote aendapo ili kutangaza Kiswahili kama lugha ya taifa na ya Afrika yenye asili yake Tanzania.
             Hata hivyo, Magufuli si wa kwanza kukosolewa na kuonekana wa ajabu kwa kutumia Kiswahili kwenye jukwaa la kimataifa.  Kwa mfano, mwaka 1964 marehemu profesa Ali Mazrui gwiji wa sayansi ya jamii alipendekeza Kiswahili kitumike kuwa lugha ya Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU). Badala ya kuungwa mkono, pamoja na usomi wake wa kupindukia, alizomewa na kuonekana kama hakuwa ameelimika vilivyo. Ajabu ya maajabu ni kwamba wengi waliomzomea walikuwa na viwango vidogo vya elimu ikilinganishwa na Mazrui mwenyewe.  Watu wenye mawazo mgando, ya kikale na kikoloni wanaweza kuona kama rais Magufuli kuhutubia Umoja wa Afrika (AU) ni jambo la ajabu bila kujua kuwa ni njia moja ya kuonyesha kujitambua, kujithamini na kuchangia kwa Umoja wa Afrika na kuondokana na masalia ya ukoloni ukiachia mbali kukuza Kiswahili kama lugha ya  taifa na kimataifa ya kiafrika hata kama ina baadhi ya maneno ya lugha za kigeni.
            Kwanini viongozi wa mataifa makubwa kama China, Japan Urusi na mengine hutumia lugha zao hata kama viongozi hawa wanakimanya kiingereza? Wanafanya hivyo ili kuonyesha wanavyojitambua. Tunapaswa kujivunia hatua hii aliyofikia rais Magufuli kwa kupeperusha bendera ya Tanzania na lugha yetu ya taifa. 
            Wapo wanaokosoa hotuba ya Magufuli kwa kuangalia udhaifu uliojitokeza ambao si kosa la rais yaani kutotoa nafasi kwa mkalimani kutafsiri. Ikizingatiwa kuwa hii ni hotuba ya kwanza kwa rais Magufuli kwenye jukwaa kubwa kama hili, hivyo anaweza kujifunza na kushughulikia mapungufu haya. Hata hivyo, ukisikiliza namna wasikilizaji walivyokuwa wakimshangilia, ni wazi ujumbe ulikuwa ukiifikia hadhira yake barabara. Watanzania na waafrika walio wengi wana kasumba ya kujivunia vya wengine wakati vyao wakividhalilisha. Unaweza kuona udhaifu huu kwenye namna ya watu wetu wanavyotetea dini nyemelezi za kigeni huku wakitukana mila zao na kutukuza za wenzao hata kama zinafanana au ni mbovu kuliko zao.
            Lazima waafrika tufikie mahali tujikomboe kutoka kwenye kongwa za kikoloni kama vile kutumia lugha zao bila ulazima au kuamini kuwa sehemu takatifu duniani ziko ughaibuni ukiachia mbali kupachikwa majina ya kigeni na kuomba kwa baadhi ya lugha za kigeni kana kwamba Mungu hajui wala hakutupa maarifa ya kuunda lugha zetu. Wakati mwingine tunawalaumu wazungu na waarabu waliotuletea ukoloni wao tukaugeuza kuwa wetu wakati sisi wenyewe ndiyo tunauendeleza na kuutukuza tokana na kutojitambua, kutojiamini na ujinga.
            Tumalizie kwa kumpongeza rais kwa kuanza kujikomboa mwenyewe ili liwe somo kwa wengine hasa viongozi wenzake wa Umoja wa Afrika (AU) ambao walionyesha kongwa za ukoloni katika uchaguzi uliopita wa Mwenyekiti wa AU kwa kupiga kura kwa kulalia kwenye mgawanyiko wa kikoloni baina ya makoloni ya zamani ya kifaransa na kiingereza ambapo waziri wa mambo ya kigeni wa Chad Moussa Fakhi Mahamat alimshinda mwenzie wa Kenya Amina Mohamed.
            Tunawasihi watanzania wajenge mazoea ya kuithamini lugha yao kama tunu yao. Kwani si mataifa mengi ya kiafrika yenye lugha zenye hadhi na kusambaa kijiografia kama Tanzania. Rais Magufuli ameanza. Naamini hata majirani zetu wanaoona Kiswahili kama ni lugha ya wasiosoma, watabadilika na kuanza kujiamini na kujithamini na kutumia Kiswahili kama Waafrika. Hakika hotuba ya Magufuli kwa AU ni suto kwa Waafrika walio wengi ukiachia mbali kuwa jambo la kupongezwa na kupigiwa mfano.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

3 comments:

Anonymous said...

Salaam Mwalim Mhango,
Kuna wakati ilisemakana kwamba Waziri mkuu wa zamamni wa Uingereza Bibi Margret Thatcher alisikika akisema kwamba "race ya watu weupe imekuja kwa ajili ya kuwastaarabisha race zingine".Kama ni kweli Bibi Thatcher aliyaomgea hayo ni wazi kwamba nia na madhumuni ya wakoloni wote walio tawala race zingine ilikuwa ni kufuta kwa kadri wawezavyo utamaduni,mila,desturi na dini za walio watala na utaona kwamba kwa ushahidi ulikuwepo ardhini wakoloni hao wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kwa nia na mdhumuni yao hayo.Na cha kuhuzunisha na kusikitisha zaidi ni kwamba Waafrika kuanzia zama za ukoloni hadi hii leo katika ukolni mambo leo bado tunaendelea kukumbatia kwa nguvu zetu zote mila zao,desturi zao,utamaduni wao na dini zao hapa inabidi tuwaongeze Waarabu ambao walishiriki kikamilifu katika nia na madhumuni ya race hiyo ya watu weupe.

Mwalimu Mhango,umeeleza na umefafanua zaidi,haya ya upande wangu ni nyongeza ndogo tu katika maandishi yako haya.Tunakubuka wazi utaratibu wa kijamii kwa walio endesha utaratibu(crime)wa utumwa ni kumfuta Mtumwa kwa kila kitu ambacho alichokimiliki kama mwanadamu huru na kumpandikiza upya program ambazo wamiliki wa watumwa hao walivyotaka wao kwa masilahi yao ya kijamii na kiuchumi mtumwa huyo awe.Na hatimae mwanadamu huyu(mtumwa)hakuwa na alichobaki nacho isipokuwa ni kujinasibisha na Bwana wake tu na kujiona nae ni sehemu ya Bwana huyo kwa mila,dsturi,utamaduni na dini,na kwa vile sehemu zote hizo nne MIHIMILI YAKE MIKUU NI LUGHA katika kujieleza kutekeleza katika maisha ya kila siku hatimae Mtumwa huyu akajikuta hana alichobaki nacho kama ni UTAMBULISHO wake zaidi ya utambulisho wa Bwana wake.
Inaendelea.............

Anonymous said...

Na ndio maana Waafrika tumefika hapa tulipofika kwa kuthamini kila kitu cha wakoloni hawa na hususa kukumbatia Lugha zao.majina na Lugha zao na tumekuwa tukiwaona na tukiwashangaa wale Waafrika ambao wanataka kujikomboa kutoka katika utamaduni wa kitumwa na akili za kitumwa.Kwa hiyo hatuoni ajabu hii leo kwa Rais wa Tanzania Magufuli kuwapa waafrika wa aina hiyo ELECTRIC SHOCK YA KIAKILI kwa kuongea Lugha ya Kiswahili katika Mahafali ya kimataifa.Na kwa wale wenye wivu na lugha ya Kiswahili waelewwe wazi tu kwamba hakuna lugha yoyote ile duniani ni bora kuliko lugha nyingine na hakuna Lugha yoyote ile ni duni kuliko Lugha nyingine muda wa kudumu Lugha hiyo inatumika katika mawasiliano ya kila siku.Na kwa vile waafrika kutumia kwetu lugha za Wakoloni wetu au lugha za kienyeji(Makabila)ndio moja ya sababu ya kutuchelewesha ndoto yetu ya kuwa Afrka Moja.Kwa hiyo na iwe Lugha ya Kiswahili ndio chanzo cha kutufikisha katika lengo la kuwa lugha inayotumika Barani mwetu.Je kwa wale wenye utamaduni wa kitumwa na akili za kitumwa wapo tayari kujikomboa au wataendelea tu kupigania masilahi ya Mabwana zao na kukumbatia kwa nguvu zao zote Mila,utamaduni.desturi na dini za Mabwana zao hao???!!!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anonymous,
Habari za siku nyingi; na karibu tena. Nashukuru kwa mawazo yako mapana na ya kina. Ni kweli tumeendelea kukumbatia utumwa kwa hiari zetu kwa ajili ya maangamizi yetu. Tunao watu wanaitwa wasomi japo si wote. Wengi ni makasuku wa kukariri vya watu ukiachia kuwa na mataifa yanayojisifia ujinga kuwa yanajua kiingereza au kifaransa wakati hayajui lugha zao wenyewe kama vile Kiswahili. Ukisoma makala yangu iliyotoka kwenye gazeti la kila siku la Kenya la Daily Nation, nimeliongelea hili kwenye uchaguzi wa mkuu wa AU. Karibu mataifa yote ya kiafrika yalipiga kura kwa kuzingatia mgawanyiko wa lugha za mabwana wao yaani Kiingereza na Kifaransa. Ndiyo maana nchi kama Burundi zilipiga kura kuunga mkono mgombea wa Chad huku zikimtosa mgombea toka EAC. Ni kinyaa kuona Afrika inavyozidi kujipeleka yenyewe utumwani na kwenye ukoloni tena kwa kujitakia. Nimeyadurusu haya kwenye kitabu changu cha AFRICA REUNITE oR Perish.