Saturday, 18 February 2017

Serikali izuie bendera madhabahuni na vyeo bandia

  Image result for tanzanian flag
 
              Kwa walioangalia mahubiri ya Josephat Gwajima baada ya kuachiwa toka Central police station, watakubaliana nami kuwa ana bendera ya taifa na ya Israel kwenye jukwaa lake. Siku zote tunaonywa kuchanganya dini na siasa. Je huyu anayetumia bendera kwenye mambo ya kidini wakati hana stahiki ya kuwa na bendera anadhamiria nini? Je kama makanisa na misikiti yote watafanya hivyo, tofauti ya dini na siasa ambayo Tanzania imeitengeneza itakuwapo?
            Hata ukisikiliza mengi ya mahubiri ya Gwajima ni ya kisiasa. Cha mno anajaribu kujipigia debe ili kuwa karibu na rais John Pombe Magufuli ambaye hata hivyo anaonyesha msimamo wa kutotaka kuchezewa. Ni ajabu kuwa Gwajima amekuwa mwepesi wa kusahau kuwa ni jana tu alikuwa shirika la Edward Lowassa dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Sasa baada ya mtu wake kushindwa, Gwajima anajitahidi kwa kila hali kujifanya anampenda na kumuunga mkono Magufuli kwenye wakati wa kuvuna wakati alimpiga kiatu kwenye kulima (uchaguzi). Je Gwajima anadhani kuwa Magufuli naye ni msahaulifu au msanii kama yeye?
            Ukiangalia ujio wa Gwajima na wenzake kama yeye waliojivisha vyeo vikubwa vya kidini, unagundua mambo mengi mojawapo likiwa ni kutojiamini. Wakati umefika wa kuondokana na viongozi wa kidini wa kujipachia madaraka ili kuepusha watu wetu kuzidi kuibiwa na kutapeliwa tokana na ujinga na shida zao. Kimsingi, kinachoendelea nchini licha ya kuwa ushirikina, ni ufisadi wa kiroho ambao madhara yake ni makubwa sana. Mtu asiye na shahada hata ya kwanza anaamka na kujiita daktari na lecturer na mamlaka zinamvumilia. Hili haliwezekani. Serikali zilizopita tokana na kuongozwa na watu wasioelimika na kusoma vilivyo, ziliwavumilia wasanii hawa kiasi cha kutosha. Magufuli daktari wa falsafa anajua uchungu wa elimu. Hivyo, tunamshauri atumbue ufisadi huu. Kwanini kwa mtu kujiita mheshimiwa Mbunge lazima achaguliwe au ateuliwe lakini si kwa askofu na vyeo vingine vya kiroho? Tunajenga taifa la namna gani kwa kuruhusu udhalilishaji wa taaluma? Je hatutoi motisha kwa watu kudharau elimu na kutafuta vyeo na stahiki za kisomi hata kwa njia ya kughushi ambalo ni tatizo kitaifa linalowahusisha wanasiasa wengi; na sasa viongozi waroho wa kiroho wa kujipachika? Kwanini wanaojifanya madaktari wa kutibu watu wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka wakati matapeli wanaojiita au kupeana udaktari uchwara wanaachiwa? Nadhani waziri wa Elimu anapaswa kuliangalia hili kwa makini hasa ikizingatiwa kuwa naye ni msomi wa kumenyekea na si wa kupewa.
            Japo ni kielelezo cha ujinga wa aina yake kwa mtu asiyesomea shahada yoyote kujipachika shahada husika, kwa wajinga na vihiyo hili si tatizo. Kuwasaidia ni kuhakikisha hakuna mtu anaruhusiwa kutumia cheo cha heshima wala kujipachika au kughushi. Kwanini wachungaji kama hawa wa kujipachika hawakuwapo wakati wa utawala wa Mwl Julius Nyerere? Jibu ni rahisi kuwa Nyerere hakuruhusu ujinga na ufisadi kama huu wakati wake kwa vile alikuwa ameelimika na kusoma vya kutosha.
            Tukirejea kwenye suala la kutundika bendera, bendera ina stahiki na namna za matumizi yake. Wapo maafisa wa serikali walioruhusiwa kutumia bendera ya taifa kama alama kuu ya utaifa wetu. Sasa hawa wachunaji wamepewa na nani mamlaka na kwa sheria gani kutumia bendera yetu kwenye shughuli zinazotia kila aina ya shaka ukiachia mbali kuwa si wote wanaoamini kwenye maigizo yao? Kuna taasisi zinazoruhusiwa kupeperusha bendera ya taifa kama vile ofisi za serikali, taasisi za umma kama vile shule na nyinginezo lakini si makanisa wala misikiti; kwa vile taifa letu halina dini japo linaundwa na watu wenye dini tofauti na kinzani. Hatuwezi kuruhusu wafanya biashara ziwe za bidhaa au kiroho watumie bendera yetu. Kufanya hivyo, licha ya kuidhalilisha ni kubariki biashara hizo hata kama nyingine ni haramu. Siku hizi dini umegeuka uchochoro wa kila tapeli kupatia mkate wake. Tutaishi kwa mahubiri kweli? Nashauri serikali itenge mahubiri kuwa ni jumapili na ijumaa. Zaidi ya hapo wahusika lazima walazimishwe kufanya kazi nyigine. Wale waliojipachika wasimamishwe haraka ili kuepuka utapeli huu kuendelea kuumiza watu wetu wengi wajinga na washirikina. Ni ajabu katika karne ya 21 bado kuna watu wanaaminishwa kuwa kuna anayeweza kutenda miujiza wakati miujiza yenyewe ni kuwaibia na kuwageuza majuha wa kawaida tu kama si mabuzi ya kuchunwa. Huwa nasema kila mara kuwa Yesu licha ya kuwa maskini, alisema tajiri hawezi kuuona ufalme wa mbinguni. Rejea kisa cha Zakayo. Ajabu ya maajabu leo wachunaji wengi ndiyo wakwasi wa kutupa. Je wataweza kuwatumikia mabwana wawili yaani mali na Mungu kweli wakati Yesu wanayejidai kumhubiri alishaweka mambo sawa? Je nani anamdanganya nani hapa?
            Tumalizie kwa kuishauri serikali imalize kadhia hii ambayo wachunaji wengi wameitumia kujipatia utajiri wa haraka ama kwa kufaidi misamaha ya kodi au kuwaibia watanzania wajinga na maskini wenye matatizo wasiojiamini. Hali imekuwa mbaya hadi matapeli wanaosifika toka kwenye mataifa kama Nigeria wamejipenyeza kwenye nchi yetu chini ya kivuli cha kuhubiri. Enough is enough.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili kesho.

3 comments:

Anonymous said...

Salamu Mwalimu Mhango,
Sikuwa na taarifa yoyote ile ya kujua kwamba nchi yetu Tanzania imerudisha mahusiano ya kibalozi na Nchi ya Israel,isipokuwa nilipomsikia kupitia mitandao ya kijamii Mchungaji Gwajima akiongea katika kanisa lake mbele ya waumini wake kwa shangwe ya hali ya juu sana kwa serikali ya Tanzania kwa kufanya hivo.Na wakati huo huo akimsifu na kumbariki sana Rais Magufuli kwa kuchukua maamuzi hayo magumu,maamuzi ambayo eti yaliwashinda viongozi kuanzia awamu ya kwanza hadi ya nne.Katika mahubiri yake hayo ambayo kwa msikilizaji na mfuatiliziji wa mahubiri wa watu hawa wa kidini Gwajima hakujificha na wala hakumeza mate wala kufumba macho kwa kuweka bayana kwamba yeye ni katika wale wafuasi wakereketwa wanaojulikana kama WAKRISTO WAZAYONI(Zion Christians).Na makao makuu ya waumini hawa yapo nchini Marekani waumini hawa ambao wamejitwalia kutokana na maagizo ya Bibilia haki ya itikadi ya kuwapigania na kuwatetea Wayahudi na Taifa la kiyahudi kwa hali na mal.Leo hii tunashangazwa kwa kuona kwamba kuna mwakilishi rasmi wa Wakristo Wazayoni nchini kwetu na wanapeperusha bendera ya Taifa la Israel pamoja na Bendera ya nchi yetu katika magari yao,majumbani mwao maofisini mwao na katika makanisa yao.Inapotokea kwa Gwajima kuwaahidi wafuasi wake kwamba atamwita Balozi wa Israel nchini Tanzania kuja kuongea katika Kanisa lake je hapa anataka kutueleza nini sisi Watanzania na kwa kufanikiwa kwake kumwita Balozi huyo je nini Balozi huyo atawafahamisha nini wafuasi wa Gwajima?Gwajima huyu ameuweka utajiri na rasilimali zote za Tanzania chini ya matakwa ya Israel kana kwamba yeye ndie mmililki wa utajiri na mali hizo za nchi na kudai kwamba nchi yoyote ile yenye uhusiano wa kidiplomasia na nchi ya Israel itabaririkiwa!!!.Wakristo Wazoyoni si kundi la kidini tu bali ni kundi la kisiasa per exellence!!Na taifa kama la Israel halisiti hata kidogo kutumia TAATHIRA ZAKE ZA KISIASA,KIUCHUMI NA KIJASUSI KWA KUWATUMIA WATU WA AINA HII POPOTE WANAPOPATIKANA.Kwa hiyo watu kama akina Gwajima na mfano wake hata kama wanajifichia chini ya uchungaji lakini muda wa kudumu wanaweka wazi itikadi yako hii ya UKRISTO UZAYONI tunaishauri serikali iwe makini kutowafumbia macho na makanisa yao.
Inaendelea..........

Anonymous said...


Mwalimu Mhango,nakumbuka sana katika maandishi yako mara nyingi umekuwa ukiwaongelea sana hawa "wachunaji wa kiroho"athari zao na hatari zao kwa taifa letu hii ukiongezea uongezeko la uoza na uvundo wa wachununaji kutoka Nigeria ambao kwao wao hawasiti kufanya maovu ya aina yoyote yale kwa kujifichia chini ya Jina la Yesu.Haiwezekani kamwe kwa Mwalimu Nyerere kufanikiwa kuziweka dini au kuzirudisha dini mahala pake na zikabaki humo humo makanisani na misikitini leo hii tumefikia mahala kwamba dini zimeingia katika siasa kwa nguvu na mapana yake yote na wengi wa viongozi waliokuja baada ya Mwalimu Nyerere kutokemea au kuwa wakali kwa kuingizwa dini katika Siasa.Na matokeo yake tuaona baadhi ya wanasiasa nao wanaongelea ufalme wa Mbinguni ili wakubalike mbele ya wananchi na kuchukliwa kama ni wacha Mungu.Kiasi mpaka imekuwa ni utaratibu rasmi kusikia katika ufunguzi za hotuba za wanasiasa wetu za majukwaani MAAMKIZI YA KIDINI!!!!!

Mwalimu Mhango,kwa maoni yangu tatizo hili litaendelea kuwa sugu muda wa kudumu baadhi ya wanasiasa wetu nao wamekuwa katika kundi lile lile ulilosema kwamba wengi wa wananchi wetu ni WAJINGA NA WASHIRIKINA.Kwa kusema hayo ni kwamba hata kama viongozi hao wamefanikiwa kusoma kiasi gani na kupata shahada za juu kwa kiasi gani lakini muda wa kudumu wanaathiriwa na dini na ushirikina basi bado watakuwa katika kundi la wajinga tu kwani ujinga nao una nyanja nyingi.Kama ulivyo mfafanua Mtume Yesu kwamba aliishi masikini na alikufa masikini na ujumbe aliufikisha na aliukamilisha na hivyo hivyo mitume karibu yote ukisoma historia zao hawakutafuta utajiri wala hawakuomba ujira na wala hawakuishi katika aina yoyote ile ya Ukwasi zaidi ya kuwahudumia watu wao na wao wenyewe wengi wao kazi yao ilikuwa ni uchungaji wa wanyama na sio uchunaji wa wanadamu kwa hiyo nakubaliana nawe kabisa kwamba kama ni mahubiri yawe siku za Ijumaa na Jumapili kama katika zama zile za Mwalimu Nyerere,lakini wahubiri wa leo kwa matendo yao wanathibitisha wao wenyewe kwamba ni wahubiri FAKE wanao watumia wajinga na washirikina kujikusanyia utajiri wa dunia kwa njia za utapeli,uwongo,ulaghai na hata ushirikina.Kwa hiyo kuwaita kwako kwamba ni wachunaji na si wachunganji wanastahiki kwa kusema ukweli.

NN Mhango said...

ANON
Nakubaliana na mengi ya mawazo yako. Akina Gwajima si viongozi wa kiroho bali waroho. Ni wajinga wa kawaida wanaoendeshwa na matumbo yao kiasi cha mabwana zao wanaowatumia kuwachagua wka vile ni wepesi na rahisi kutumika kutokana na ujinga na tamaa zao. Nakubaliana nawe kuwa viongozi na baadhi ya wasomi wetu ni wajinga na washirikina wa kaiwaida. Nitatoa mfano mdogo hapa. Jaribu kuangalia mantini ya mtu mwenye PhD kama Magufuli kutapeliwa na mjinga kama Makonda. Au angalia hili. Msomi kama Dk Gharib Bilal kuzidiwa kete na mjinga kama Kikwete. Hiyo ndiyo Tanzania yetu. Huwa naandika ninayoandika kwa uchungu na kutaka kujaribu kujipambanua na ujinga na ushirikina vilivyosheheni nchini mwetu. Kuhusu kuchanganya dini na siasa, nadhani awamu ya tano ni kiongozi. Angalia ilivyoamua kujenga makao makuu ya BAKWATA bila kueleza ni kwa misingi gani na kasma gani ya fedha.