Wednesday, 1 February 2017

Serikali inaposhindwa kujua faida ya mradi wa DRT

Image result for photos mabasi ya mwendo kasi
            Hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli  akiwa ameandamana na makamu wa rais wa Benki ya Dunia (WB) kwa Afrika, Makhtar Diop alizindua awamu ya kwanza ya magari yaendayo kwa kasi jijini Dar es Salaam (DRT). Mradi huu wa kipekee katika Afrika Mashariki na Kati ni jambo la kujivunia kama litaleta faida na kukidhi matarajio ya watanzania.
            Pamoja na hadhi ya mradi husika ambao umejengwa kwa mkopo toka Benki ya dunia, wapo wanaooanza kushuku uwezekano wake wa kufikia malengo. Mmojawapo ni rais mwenyewe ambaye vyombo vya habari vilimkariri akimtaka waziri wa usafirishaji amueleze faida itakayopata serikali kutokana na mradi wa husika. Hili liliwashangaza wengi hasa wanaojua namna taifa letu lilivyofikishwa lilipo kifisisadi. Kama rais, nasi tunauliza, je huu mradi unaweza kuwa na faida kisiasa japo si kiuchumi? Tunaweza kujivuna kuwa tuna mradi mkubwa na wa pekee barani Afrika. Je hilo ndilo wanalotaka watanzania ambao ndiyo wenye fedha inayokopwa kwani watailipa siku moja?
            Tukiangalia waliopewa kuendesha mradi huu ambao sasa unaitwa UDART mbali na utata unaoghubika zoezi zima, tunapata shaka kama watanzania watapata faida waliyotarajia tokana na mradi huu unaojengwa kwa fedha yao. UDART ni muunganiko wa kampuni ya iliyokuwa ya Usafiri Dar Es Salaam (UDA) pamoja na  Dar Es Salaam Rapid Transit (DART).  Kuungana si jambo geni. Ila inapokuja kuwa muungano huu ni wa watuhumiwa na asasi ya kiserikali, unapata taabu na kushindwa kuelewa mantiki ya muungano huu rangi mbili.
            Kwa wanaojua historia ya namna UDA ilivyouawa na kutwaliwa kifisadi huku serikali zilizopita na hata ya sasa zikiendelea kupiga dana dana, watakuwa wanashangaa mantiki ya watwaaji wa UDA kuaminiwa kuendesha mradi mkubwa wa umma kama huu wakati hawana hata chembe ya imani tokana na kashfa ya utwaliwaji wa UDA. Ni vigezo gani vilitumika kuteua UDA kuendesha mradi wakati ni watuhumiwa  wa kuhujumu umma ambao hawajawahi kukanusha kwa kutoa ushahidi unaoingia akilini kuwa walijitwalia iliyokuwa shirka la Usafirishaji Dar Es Salaam (UDA)? Kwa vile walioua UDA; na hatimaye kuitwaa bado wako pale pale, je hii haiwezi kujenga dhana kuwa hata DART itauawa na kutwaliwa kama UDA hasa ikizingatiwa kuwa walioko nyuma ya hujuma hii si hawa tunaowaona wakijiita wamilki na wakubwa wa UDA wakati historia zao hazionyeshi chembe ya ujasiriamali wala namna ambavyo wangeweza kuwa na mtaji wa kununua UDA kama wanavyodai. Kama ukimdurusu Simon Kisena, hupati historia yoyote inayoonyesha ana uwezo wa kuwa na fedha zinazodaiwa kulipwa kwa serikali kama manunuzi ya hisa zake ambazo nazo ni utata mtupu. Tunapaswa kujua mchakato na namna watuhumiwa kama hawa walivyopata tenda ya kuendesha mradi wa wananachi wale wale waliowaibia shirika lao. Tunapaswa kujua na vyanzo vya fedha iliyotumiwa kununua hisa kama kweli ziliuzwa.
            UDA ni bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote kama serikali itaamua kutimiza wajibu wake. UDA ni jipu linalopaswa kutumbuliwa haraka bila kujali ni nani wako nyuma ya hujuma hii kwa taifa. Huu si wakati wa kulindana na kuoneana aibu. Najua rais alisema kuna makaburi hatayafukua kwa kushindwa kuyafukia. Pamoja na msimamo huu, nadhani kelele za waathirika–yaani wananchi–zitaendelea kumuandama hadi atende haki kama alivyoapa kufanya. Na hakika; umma unaotaka haki na kuchukia maovu, hautanyamaza kumkumbusha rais na serikali yake kutekeleza wajibu wao bila upendeleo wala uonevu.  Inashangaza kwa taifa kuendelea kuchukua mikopo toka kwenye taasisi za kimataifa na nchi mbali mbali na kuishia kuwapa mafisadi wanaojulikana miradi itokanayo na fedha hii waihujumu kwa kisingizio cha kuiendesha. Wezi wa UDA hawana udhu wa kuweza kusimamia mradi wowote wa taifa.  Historia ya utwaliwaji wa UDA inaonyesha uchafu sawa na kashfa nyingine kama vile IPTL, Kagoda, EPA, ESCROW, Lugumi na nyingine nyingi ambazo serikali inaonekana kuzigwaya kutokana na vigogo walioshiriki kuzitenda. Mbunge wa Kawe Halima Mdee alinukuriwa hivi karibuni akipinga wizi wa UDA akisema “naliambia Bunge msije mkathubutu, maana nimesikia mara zile Sh bilioni 5 alizolipa Simon Group zipangiwe matumizi, naomba niwaambie sisi kama Jiji tunatambua mamlaka yetu, sasa kama hatujitambui na Serikali inataka kuingilia, hatuwezi kutumia hii shilingi bilioni 5 kuhalalisha haramu kuwa kitu kitakatifu.”
            Mwisho, inashangaza mantiki ya serikali kutumia jumla ya shilingi 39.6bn ambazo zililipwa kwa kampuni ya kichina Beijing International Engineering Group (BCEG) kujenga miundo mbinu ya mradi na kuruhusu kampuni yenye thamani ya blioni 5 kuwa mbia katika kuendesha mradi huu. Je mgawanyo wa hisa baina ya UDA na DART ni upi? Je ni UDA hii hii ambayo Mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa fedha za serikali (CAG) alishauri hisa zake zirejeshwe kwa serikali na kuchunguza namna UDA ilivyotwaliwa kifisadi?. Kashfa ya UDA imegeuka donda ndugu kwa taifa letu. Alipoingia rais Magufuli na tumbuatumbua yake, wengi walidhani angekuwa na ujasiri na uzalendo wa kutumbua jipu hili. Ukweli ni kwamba hatafanya hivyo. Ushahidi uko wazi kuwa kitendo cha serikali yake kuridhia waliohujumu umma kwa kuiba Shirika lake la UDA ndiiyo hao hao walioaminiwa kuendesha mradi tena mkubwa kuliko ilivyokuwa UDA yenyewe. Swali muhimu hapa ni: Kama serikali haijui faida ya mradi wa DRT, nani anajua sasa?
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: