Tuesday, 14 February 2017

Mihadarati: Barua ya wazi kwa Kikwete

            Mheshimiwa Luteni Kanali na rais mstaafu, Jakaya Mrisho Kikwete, naomba nisikuite dokta kwa vile sikumbuki wewe kusomea shahada ya juu ya PhD. Najua unazo PhD za heshima ambazo kisomi, huwa wanaopewa hawaruhusiwi kuzitumia hasa ikizingatiwa kuwa wewe ulipewa kama rais lakini si kama Kikwete.  Hivyo, tofauti na wengine wanaokuvisha kilemba cha ukoko, nimeamua kueleza kwa cheo chako ulichokisotea. Hayo tuyaache.
            Shikamoo; na habari za ustaafu? Unaendeleaje na matibabu ya ugonjwa ulisema uligundulika miaka michache iliyopitwa ambao nakupongeza kwa kuuweka wazi? Mimi ni mzima mwenye afya. Nakufahamisha; mimi ni shabiki wako na aliyefurahia kipindi cha utawala wako. Sina tofauti na wale uliokuwa ukiandamana nao ughaibuni kwenye ziara zako za mara kwa mara kwenda kwenye matanuzi hadi ukabatizwa jina la Vasco da Gama yule habithi wa kireno aliyesaidia ukoloni kuenea duniani.
            Mheshimwa Kikwete, leo nakuandika rasmi waraka huu wa wazi kwa lengo la kukuomba na kukusihi usaidie kuliokoa taifa letu toka kwenye hatari na mkwamo vitokanao na kushindwa kupambana na biashara haramu ya madawa ya kulevya ambayo bila shaka unaijua vizuri. Hivyo, rasmi, nakuomba utoe orodha ya majina ya wauza madawa ya kulevya uliyotangazia umma kuwa unayo; na ulipewa na vyombo vya usalama. Nakumbuka ilikuwa mwaka 2006 ulipotoa kauli hii ya kuwa na orodha hii muhimu katika mapambano haya magumu dhidi ya midarati nchini. Hata wabunge bungeni wameomba hili lifanyike.  Ninapoongea, wale vijana wasanii uliozoea kukutana nao na kuwapa ujiko hadi ukaambiwa kuwa chama chako na serikali yako vilikuwa vya wasanii sasa baadhi yao wako mbele ya mahakama wakipmbana na kesi zihusianazo na mihadarati. Juzi juzi wengi walisweka kwenye vituo vya polisi wakidaiwa kuwa wanabwia unga jambo ambalo liliibua hisia tofauti miongoni mwa watanzania. Suala hili limewagawanya watanzania baina ya wale wanaounga mkono jitihada hizi za kupambana na mihadarati ambazo zimeanzishwa na kijana wako Paul Makonda mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam. Pia wapo walioona kama huu ni usanii mwingine wa baadhi ya wapambe wa rais kulinda ulaji wao. Wengine walisema kuwa hii ni danganya toto na nguvu ya soda ya kisiasa tokana na namna zoezi lenyewe linavyoendeshwa. Kama haitoshi, hata waheshimiwa wabunge bungeni walitoa pofu kweli kweli wengine wakilaani kitendo hiki cha kuonea watumiaji badala ya kukamata wasambazaji na wauzaji. Wengine walikipongeza wakisema ni mwanzo mzuri ingawa waliilamu serikali kwa kutotimiza wajibu wake hasa serikali zilizopita ikiwemo yako. Wapo waliokwenda mbali hadi kudai walioanzisha wimbi hili jipya la kupambana na mihadarati kwa wasanii kwa kukamata vidagaa wakati wakiacha mipapa kuwa walichagiwa na wauza unga kwenda kutanua Marekani, Ufaransa na kwingine.  Wengi wanahoji mantiki ya kukamata vijidagaa wakati mapapa wanajulikana.
            Naomba ufanya yafuatayo:
Mosi, nakuomba chonde chonde utoe ile orodha ya wauza madawa ya kulevya uliyosema ulipewa na vyombo vya usalama mabayo umekaa nayo kwa zaidi ya miaka kumi. Kwa vile ulipoondoka madarakani hukukabidhi madaraka rasmi, sikumbuki kusikia kuwa ulikabidhi orodha hiyo kwa rais Magufuli aliyechukua madaraka baada yako. Nakumbuka uliwaambia watanzania kuwa una orodha za wauza unga, majambazi, wala rushwa, hata wezi wa bandarini kutaja wachache.
            Kwa vile ushastaafu, nashauri ile orodha uitoe kwa rais John Pombe Magufuli aliyesema hana simile na biashara hii. Alikaririwa akisema kuwa hata kama mkewe akijihusisha akamatwe bila kujali ni mke wa rais. Hii maana yake ni kwamba rais–kama hafanyi usanii–hataki mchezo na mihadarati.
            Pili, kama utaweza, naomba ueleze ni kwanini uliamua kutowakamata watuhumiwa baada ya kupewa orodha uliyokiri kuwa nayo. Umma ungependa kujua sababu za kutofanya hivyo ili uweze kuzifanyia kazi na kuepuka wewe kugeuzwa kuwa sehemu ya jinai hii.
Tatu, naomba uelezee ni kwanini hukumpaulinzi marehemu Amina Chifupa alipoamua kuweka mambo hadharani kiasi cha kuhatarisha usalama na maisha jambo ambalo lilikuwa wazi. Je uliamua kuwasamehe wauza unga kama ulivyofanya kwa wezi wa EPA uliowaamuru warejeshe fedha na mambo yaishe wakati kufanya hivyo ni kinyume cha sheria jambo ambalo una bahati halikufika mbali. Kwani ingekuwa ughaibuni ungekuwa impeached kwa kuvunja katiba.
Nne, kama kiongozi mstaafu, nakuomba utoe kauli dhidi ya balaa hili kwa taifa ili lau watanzania waache kuishi kwa kudhani nawe ni sehemu ya tatizo badala ya kuwa suluhu. Kwa sasa ni rahisi kwako kufanya hivyo, hasa ikizingatiwa kuwa huna shughuli nyingi sawa na ulizokuwa nazo ukiwa kiongozi wa nchi. Hili ni muhimu hasa kwa sasa ambapo imejengeka imani kuwa wauza mihadarati wana serikali yao ndani ya serikali. Isitoshe, kujitokeza kwako kuelezea mapungufu ya utawala wako dhidi ya jinai hii kutaisaidia serikali ya sasa kupambana na kadhia hii kwa kuchota kwenye uzoefu wako hasa pale ulipoacha kuwakamata watuhumiwa ambao orodha ya majina yao unayo.
Naomba kutoa hoja na ombi kwako ili utusaidie kwenye vita hii kama mtanzania na kiongozi mstaafu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili juzi.

No comments: