Saturday, 25 February 2017

Tanzania aihitaji kuombewa bali kuambiwa

          Ninapoandika kuna kundi la matapeli wa majoho wanaoandaa tamasha eti la kuombea taifa! Hivi Tanzania inahitaji kuombewa au kuambiwa ukweli mchungu hasa kupambana na vikwazo vinavyoifanya iwe shamba la bibi na ombaomba duniani? Kwanini kuomba badala ya kuyakabili matatizo ya kweli yaani ujinga, umaskini, rushwa, ufisadi, usanii, ukondoo, ukijiko, ukuku na adha nyingine?
            Ni matapeli wengapi wamejificha kwenye uganganjaa kama kutenda miujiza wanaowaibia watanzania maskini na wajinga mchana hadi kugeuka matajiri wa kuktupwa kwa muda mfupi? Si tunawaona kila siku wakijipachika vyeo kuanzia uchungaji, uaskofu hadi udaktari? Nani aliwawekea mikono zaidi ya utapeli na njaa zao?
            Juzi wamejitokeza wengine eti wanabariki mafuta huku wakijifanya kumpenda rais John Pombe Magufuli ambaye huweka picha yake mbele kwa kisingizio cha kumuombea. Japo kuomba siyo jambo baya, kwani lazima mtangaze na kuitisha makongamano kama siyo kutaka kujiweka karibu na rais?  Kama tutaendekeza kuomba, kazi tutafanya lini? Hivi hawa wanaojifanya kuipenda Tanzania kiasi cha kuandaa matamasha na makongamano ya kuiombea, hawawezi kufanya maombi yao majumbani au makanisani mwao bila kutangaza kama siyo kutafuta kuwa karibu na rais?
            Sikumbiki Yesu kuandaa mkesha wa kuombea chochote zaidi ya kufanya kila alichoweza bila kutafuta sifa tena akiwaambiwa walionufaika na huduma yake wasimwambie mtu. Yesu hakutaka sifa wala makuu. Ndiyo maana hakuwa tajiri wala hakuwa na vyeo vya kujipachika na vya kughushi kama vile daktari zaidi ya kuitwa Mwalimu na wanafunzi wake.
            Kama tutakuwa wakweli kwa nafsi zetu, kweli Tanzania inahitaji maombi kama majibu ya matatizo yake? Mbona hatusikii nchi jirani zikiwekeza katika kuomba. Tunapaswa kufanya mambo kisayansi na kwa kuangalia ukweli na uwezekano badala ya ndoto na visingizio kama maombi. Kwanza, maombi hayatuhakikishii majibu ya tatizo kwa muda tunaotaka. Pili, maombi si njia yenye kuaminika ya kupambana na matatizo. Na tatu, tunaweza kuomba lakini kufanyike baada ya kazi na si kwa matangazo na kutafuta sifa kirahisi kwa baadhi ya walioko nyuma ya mradi huu wa sala ambao kimsingi, hauna uhakika.  Kuomba hakuna haja ya kugeuka kazi ya kundi fulani au watu fulani au dini fulani.  Kwa watu wanaoipenda nchi yao, bila shaka watakuwa wakiiombea kila siku kwenye maombi na sala zao iwe ni misikitini, makanisani hata majumbani. Hivyo, hawa wanaokuja na gea ya kuliombea taifa, wanapaswa kujua kuwa walichelewa kujua wajibu wao kama watanzania. Leo tutaanza kuombea taifa. Kesho  tutasikia kuliimbia. Na kesho kutwa tutasikia kulitoa sadaka. Dawa ya matatizo ya taifa letu si maombi bali kuambiana ukweli kuwa kuna wenzetu hawafanyi kazi na wengine wanawaibia watanzania  kwa kushiriki vitendo viovu kama vile ufisadi, biashara haramu ya mihadarati, ubabaishaji, utapeli na maovu mengine mengi ambayo yametamalaki. Kama kuna kitu taifa letu linahitaji, nadhani si kuomba bali kuambiwa ukweli kuwa tusipolipenda na kuchapa kazi, hata tuombe uchi au bila kukoma tutazidi kuumia. Hivi wanaoajiri wageni kinyume cha sheria nao wanahitaji maombi? Mateja nayo yanahitaji maombi? Wauza unga wanahitaji maombi? Polisi na maafisa forodha wanaowezesha wauza unga kupitisha mizigo yao hatari nao wanahitaji maombi kweli? Wanaotumia madaraka vibaya na wababaishaji wa kisiasa nao kweli wanahitaji maombi? Wanaotumia vyeo kuwaumiza, kuwakomoa na kuwachafua wapinzani wao nao kweli wanahitaji maombi? Wanaotukana viongozi wetu kweli nao wanahitaji maombi? Wanaofuja fedha na mali ya umma kweli wanahitaji maombi au kuambiana kuwa tupambane nao kwa udi na uvumba?
            Kuna njia zinazoingia akilini za kushughulikia matatizo yetu kama watu na jamii. Kwa mfano, tunapopambana na ukame, dawa si kuomba mvua tu bali kubuni namna ya kuwekeza kwenye kilimo cha umwagiliaji. Tunaposhindwa kuelewana, njia si kuomba bali kutafuta namna ya kuelewana. Tunapokumbwa na umaskini dawa si kuombeana tena kuombewa na wale wanaotufanya maskini ima kwa kula bila kufanya kazi au kuwaibia maskini bali kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa. Kutofanya kazi lakini baadhi yetu wakatakea kuwa matajiri bila maelezo ni dalili za ufisadi ambao kimsingi, ndicho kikwazo kikubwa kwa taifa letu.
            Hakuna taifa lililopata maendeleo kwa njia ya kuomba iwe ni misaada au maombi zaidi ya uchapa kazi. Kwa vile sera ya rais Magufuli ni ‘Hapa Kazi Tu’ namshauri awaulize hawa wanaopoteza muda na fedha nyingi wakiandaa makongamano na matamasha ya kuombea taifa, wafanya kazi kwanza; maombi baadaye. Anachoweza kufanya rais kulisaidia taifa ni kuwachunguza wote waliojipachika vyeo vya kidini na vinginevyo wenye utajiri wa kutisha ili watumbuliwe.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

6 comments:

Mtwangio said...Mwalimu Mhango,Nakumbuka vyema tu kwamba katika kinyang'anyiro cha mashindano ya kombe la dunia la mpira wa miguu ya mwaka 1982 yaliyofanyika Uhispania ambapo nchi ya Poland iliyashiriki,viongozi wa timu hiyo na wachezaji wake waliamua kwenda kumuona Pope John Paul 11,Mpoland mwenziwao ili awaombee kwa Mwenyezi Mungu ili waweze ushindi wa kulitwaa kombe hilo la dunia katika mashindano hayo.Lakini Pope John Paul 11 aliwajibu kwamba "Katika mpira wa miguu Mwenyezi Mungu apendelei timu yoyote".Kwa msemo huo wa Pope ni kuwaambia viongozi na wachezi wa timu hiyo kwamba ni maandalizi yenu na majuhudi yenu ndio yatakayo waletea ushindi.Kwa mfano huo hai kinyume chake ni kwamba timu za mpira wa miguu zilikuwa klabu binafsi au timu ya taifa utakuta makuhani wa kidini,waganga na wachawi wanaziombea,kuzirogea na kuzichawia timu hizo ili zitoke na ushindi.Sasa tunategemea nini katika jamii kama hizi?Kwa hiyo makuhani hawa wa kidini kusema kwamba wanaliombea taifa ili iweje na je ikiwa makuhani wa kila taifa watamuomba Mwenyezi Mungu kuhusu taifa lao je hapa hatuoni kwamba Mwenyezi Mungu atakuwa na aina moja au nyingine ya ubaguzi kwa kuwapa taifa moja na kulinyima taifa lingine ambayo hii sio sifa yake Mwenyezi Mungu?Katika kitabu cha Waisilamu kuna aya inayosema"Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo naf- sini mwao"
Hapa hata Mwenyezi Mungu anawakumbusha waumini wa dini kwamba hakuna mabadiliko yoyote yale katika jamii au nchi yatakayopatikana kwa MAOMBI TU mpaka waumini hao wabadilike wao wenyewe kwa kuyabadilisha yale yote ambayo yanayo wakwamisha kijamii au katika Taifa na hapo ndipo Mwenyezi Mungu atawapa sapoti yote kwa kubadilika kwao huko.

Ninachoelewa mimi katika historia ni kwamba ni taifa moja tu kama linastahiki kuitwa taifa ni lile taifa la watoto wa Israel alipopewa Mtume wao Moses na Mwenyezi Mungu Jukumu la kuwatoa watu hao kutoka Misri na kuwafikisha katika Ardhi walio ahidiwa.Na ni Mwenyewe Mungu mwenyewe ndie aliekuwa mstari wa mbele kuwaongoza na kuingilia kati katika maisha yao, kuwaadhibu wanapomkosea na kuwapa faraja wanapomtii na hata kupigana vita kwa niaba yao dhidi ya mataifa mengine.Lakini mwisho wa siku watoto hao wa Israel au taifa hilo lilimkana Mwenyezi Mungu wao na wakaamua kujitawala wenyewe kama wanadamu na kumuweka Mwenyezi Mungu wao pembeni na kufuata sababu na visababisha vyote vya kujiendeleza kama wanadamu bila ya kuhitaji MSAADA WA MWENYEZI MUNGU.
Mwalimu Mhango.Msumari wa mwisha umesha ugongomelea kwa nguvu zako zote,je kuna sikio litakalo sikia?kuna akili itakayofahamu na kufanyia kazi maelezo yako haya?Au ndio matapeli wa kidini wataendelea kupeta tu na kutanua katika jamii ya wajinga na washirikina?

Anonymous said...


Salamu Mwalimu Mhango,
Pongezi zangu nyingi sana kwako kwa kuligongomea sanduku la maiti MSUMARI WA MWISHO kuhusu hawa Matapeli wa kidini.Tukumbushe tu kihistoria kwamba tangu jamii za kiduni(Primitive society) waliposhindwa kuelewa jinsi gani tabia(nature) inavyofanya kazi kwa uchanga wao wa kiakili zao kufikiri kisayansi wakaja na fikira kwamba kila tabia(nuture)ambayo wameshindwa kuielewa jinsi inavyofanya kazi na ikawa inawaletea madhara na kushindwa kujitetea na madhara hayo kwa kufikiri kisayansi,wakaja na ufumbuzi wa kwamba kila tabia(nature)inayowadhuru au kuwanufaisha kuuimbia miungu mbali mbali na kuiabudu na hatimae kuifanyia madhabahu ya kuwafurahisha na kuwaridhisha miungu hiyo pale tu wanapogundua kwamba miungu hiyo imekasirika kwa madhara wanayoyapata kwa kuwatoa wanadamu kafara katika madhabahu yao au kuwafikishia mazao yao na wanyama wao kama ni sadaka pale tu wanapoona wamefanikiwa katika maisha yao.Na zilipokuja dini za mbinguni zikaondoa kafara ya wanadamu na kuwatoa wanyama kama ni sadaka au kafara katika madhabahu hayo.Na tunakuta tu kwamba MAKUHANI,WACHAWI NA WATAWALA WALIKUWA NI KITU KIMOJA KATIKA KUHAKIKISHA KWAMBA UTARATIBU HUO UNAENDELEA KWA KUUFANYA KAMA NI DINI NA KUNUFAIKA NA WANANCHI WAO KWA KUWANYONYA KWA KILA NJIA YA HADI HII LEO UTARATIBU HUO UNAENDELEA NA DINI KUWA NI TATIZO KATIKA JAMII BADALA YA KUWA UFUMBUZI NA UFUMBUZI WA DINI NI KWAMBA NCHI NI YA WOTE NA DINI NI YA MUUMINI NA ANACHOKIAMINI NA KUKIABUDU NA BILA YA KULAZIMISHANA,KUUANA,KUCHUKIANA NA KUIINGIZA KATIKA SIASAWA

Watu wa ulaya walipofanikiwa kuzitenganisha taasisi za kidini na kiserikali katika zama za kufikiri kisayansi na baada wanadamu kujua ni jinsi gani tabia(nuture)inavyofanya kazi kwa kupitia nyanja zote za kisayansi.Makuhani wamepoteza nafasi zao au haiba zao za kuombea jamii au kuliombea taifa na kufikisha kafara na sadaka mbele ya madhabahu.Na katika makala yako ya hivi karibuni uligusia kwa kusema kwamba jamii ambayo watu wake ni wajinga na washirikina matapeli wa kidini wataendelea na utapeli wao huu wa kidini.Kwa hiyo Muda wa kudumu jamii yetu bado ina mihimili yote ya jamii duni(primitive society) na hatuna utaratibu wa kufikiri kisayansi ndio upuuzi huu na ujinga huu utaendelea kubaki daima na milele.Swali ambalo linalojiuliza hapa je hivi watawala wetu nao hawashiriki katika kuundeleza ujinga,ushirikina na upuuzi huu?Je ni kweli tumefeli kiasi hiki kwa kushindwa kuwaandaa watu wetu wawe na uwezo wa kufikiri kisayansi tangu mashuleni na sio kuwapa elimu na shahada za kupatia riziki?

Anonymous said...Mwalimu Mhango,Nakumbuka vyema tu kwamba katika kinyang'anyiro cha mashindano ya kombe la dunia la mpira wa miguu ya mwaka 1982 yaliyofanyika Uhispania ambapo nchi ya Poland iliyashiriki,viongozi wa timu hiyo na wachezaji wake waliamua kwenda kumuona Pope John Paul 11,Mpoland mwenziwao ili awaombee kwa Mwenyezi Mungu ili waweze ushindi wa kulitwaa kombe hilo la dunia katika mashindano hayo.Lakini Pope John Paul 11 aliwajibu kwamba "Katika mpira wa miguu Mwenyezi Mungu apendelei timu yoyote".Kwa msemo huo wa Pope ni kuwaambia viongozi na wachezi wa timu hiyo kwamba ni maandalizi yenu na majuhudi yenu ndio yatakayo waletea ushindi.Kwa mfano huo hai kinyume chake ni kwamba timu za mpira wa miguu zilikuwa klabu binafsi au timu ya taifa utakuta makuhani wa kidini,waganga na wachawi wanaziombea,kuzirogea na kuzichawia timu hizo ili zitoke na ushindi.Sasa tunategemea nini katika jamii kama hizi?Kwa hiyo makuhani hawa wa kidini kusema kwamba wanaliombea taifa ili iweje na je ikiwa makuhani wa kila taifa watamuomba Mwenyezi Mungu kuhusu taifa lao je hapa hatuoni kwamba Mwenyezi Mungu atakuwa na aina moja au nyingine ya ubaguzi kwa kuwapa taifa moja na kulinyima taifa lingine ambayo hii sio sifa yake Mwenyezi Mungu?Katika kitabu cha Waisilamu kuna aya inayosema"Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadilike wao wenyewe"
Hapa hata Mwenyezi Mungu anawakumbusha waumini wa dini kwamba hakuna mabadiliko yoyote yale katika jamii au nchi yatakayopatikana kwa MAOMBI TU mpaka waumini hao wabadilike wao wenyewe kwa kuyabadilisha yale yote ambayo yanayo wakwamisha kijamii au katika Taifa na hapo ndipo Mwenyezi Mungu atawapa sapoti yote kwa kubadilika kwao huko.

Ninachoelewa mimi katika historia ni kwamba ni taifa moja tu kama linastahiki kuitwa taifa ni lile taifa la watoto wa Israel alipopewa Mtume wao Moses na Mwenyezi Mungu Jukumu la kuwatoa watu hao kutoka Misri na kuwafikisha katika Ardhi walio ahidiwa.Na ni Mwenyewe Mungu mwenyewe ndie aliekuwa mstari wa mbele kuwaongoza na kuingilia kati katika maisha yao, kuwaadhibu wanapomkosea na kuwapa faraja wanapomtii na hata kupigana vita kwa niaba yao dhidi ya mataifa mengine.Lakini mwisho wa siku watoto hao wa Israel au taifa hilo lilimkana Mwenyezi Mungu wao na wakaamua kujitawala wenyewe kama wanadamu na kumuweka Mwenyezi Mungu wao pembeni na kufuata sababu na visababisha vyote vya kujiendeleza kama wanadamu bila ya kuhitaji MSAADA WA MWENYEZI MUNGU.
Mwalimu Mhango.Msumari wa mwisha umesha ugongomelea kwa nguvu zako zote,je kuna sikio litakalo sikia?kuna akili itakayofahamu na kufanyia kazi maelezo yako haya?Au ndio matapeli wa kidini wataendelea kupeta tu na kutanua katika jamii ya wajinga na washirikina?

NN Mhango said...

Anon,
Kwanza asante kwa mchango wako. Tokana na kiwango chake cha ubora, nimeamua kuuchapisha lau wengine wasome na kunufaika nao. Hivyo, nakushukuru na kukukaribisha sana kuzidi kutoa nasaha zako ili kuielimisha jamii yetu ujuavyo namna ilivyotopea kwenye ujuha na upuuzi wa kuombeana badala ya kuambiana kuwa tutakombolewa na kazi na maarifa kwa kutumia sayansi na kufanya mambo wenyewe badala ya kutegemea miungu. Hata ndege japo ni hayawani, wanatucheka. Tubadilike.

Anonymous said...

Salamu Mwalimu Mhango,

Mimi nikushukuru wewe kwa kutupa sisi wasomaji wako wa makala zako umuhimu wa kushirikiana nawe katika mapambano haya ya kutuelimisha,kutukosoa kutupa nasaha,mwongozo na mwangaza. Hili ni jambo ambalo tuseme tu AHSANTE SANA.Kwani bila ya watu kama nyinyi katika jamii zetu hizi changa tutachelewa sana kufika safari ndefu ya kujikomboa kiakili.Sapoti yako tunaihitaji kama vile unavyoihitaji ya kwetu kuwa bega kwa bega na we ili tufike kwa uchache hata kama si kwa wingi kuwawezesha watu wetu kujijua wapi walipotoka,wapi walipokuwepo na wapi wanahitaji kuelekea.
Nimalizie kwa kuariri tena kwa kusema Ahsante sana kwa sapoti yako kwetu sisi wasomaji wako.

NN Mhango said...

Shukrani zako nimezipokea ukiachia mbali kuzifurahia hasa mchango wako usiokoma kwenye uwanja huu. Hakuna anayejua kila kitu. Ndiyo maana michango ya wasomaji wangu ni mali kuliko hata makala zangu. Karibu tena.