The Chant of Savant

Wednesday 1 February 2017

Mpayukaji Ahudhuria Kikao cha Wanene Addis Ababa

          Baada ya wanga na woga wengi kudai kuwa nina woga wa kusafiri ughaibuni, nimeamua kuwatoa nishai ili waaibike na kushushuka. Si wapo waliosema kuwa sitakwenda kwenye kuhudhuria genge la wanene wenzangu barani kwa vile ni mwoga wasijue nilikuwa nasukuti na kujipa shule kabla ya kwenda kule na kuchemsha. Mie siyo kama vimbelembele waliozoea kukesha kwenye madege wakienda ughaibuni kutia aibu na kujiaibisha hadi wengine kupewa nishani uchwara na matapeli ukiachia mbali wengine kupewa udaktari uchwara wakautumia kana kwamba wamesomea wakati ni vihiyo wa kawaida.
            Mwenzenu baada ya kumtimua Yaya Jammeh, nimeamua kupitia zangu Addis lau kutia tafu wenzangu kuhakikisha tunaandaa mkakati wa kuwatimua wanene wa wachovu hasa marahis wanaogeuza ikulu kuwa mali binafsi. Haiwezekani watasha wakaendelea kutucheka kwa kukumbatia maimla wakati tunao uwezo wa kuwatoa nkuku kama alivyofanyia Jammeh ambaye huko aliko mafichoni atakuwa anamiss shoptalk ya Addis aliyozoea kuhudhuria na kujidai huku akimwaga pumba zake na kujivisha kama mmanga wakati nimmakonde wa kawaida tena asiye na hata hiyo dini anayopwakia. Atakuwa akitoatoa mimacho na kujilaumu kwa kushindwa kuchakachua uchaguzi uliomtupa nje bila yeye wala dunia kutegemea. Ama kweli kila chenye mwanzo shurti kiwe na mwisho. Hata hivyo, anabahati hakunyotolewa roho kama swahiba yake Kashafi wa Libya aliyekufa akilia kama kichanga baada ya wachovu wa kule kumgeuzia kibao.
            Napanga kutoa mada juu ya demokrasia, uwajibikaji na uchaguzi huru na wa haki bila kusahamu kuheshimu katiba za kaya ambazo sasa zinadhalilishwa na marahis wengi kwa kutaka ulai rahisi utokanao na kung’ang’ania urahis na kubadili katiba. Nakwenda kuwapasha wanene wote waliochakachua ima katiba au uchaguzi na kuendelea kuwa maulajini kinyume cha sheria. Hapa sitajali nani tunatoka ukanda mmoja au rafiki bali kutoa dozi kama sina akili nzuri. Hapa ni mipasho tu kama kazi au vipi?
            Japo wakubwa wezi walionitangulia kuongoza kaya hii ya Danganyika walizoea kuandamana na utitiri wa walaji huku wakiifanya misafara yao kuwa siri, mie sifichi. Nasikia hali ilikuwa mbaya hadi kufikia hata vigagula kuwa kwenye msafara wa munene. Kwa kazi gani kama siyo ujinga na ujuha wa mwaka? Kufanikisha ujinga na ufisadi wao wengi walizoea kuondoka usiku ili kuficha yale mabomu waliyokuwa wakiandamana nayo. Kuonyesha nisivyo na cha kuficha nimeondoka mchan nikiwa nimeandamana na waziri wangu wa Mambo ya Ughaibuni Mghoshi  Machungi na maafisa wachache ili kubana matumizi. Vikao kama hivi siyo sehemu ya kufanyia sherehe na kupeleka washamba kwenda kutoa tongotongo.  Huwa sipendi kutumia njuluku za wadaganyika kwenye  mambo ya kilimbukeni na kishamba wakati wanaihitaji kwa ajili ya mambo mhimu kama vile Afya, Elimu na mambo mengine muhimu. Mie si mchoyo wala sina roho mbaya kama wale walionitangulia ambao walisumbuliwa na roho mbaya na ushamba wakidhani wangeweza kuizunguka dunia nzima. Hata kama walifanya hivyo, ili wapate nini zaidi ya kuendelea kuwa waja kama wadanganyika wengine? Kuoneyesha nilivyo serious, hata bi mkubwa sikuandamana naye hasa ikizingatiwa kuwa hana anachokwenda kufanya kule. Huu ni mkutano wa wakuu na si wake wa wakuu wala waramba makalio ya wakuu.
            Pili,  sikusafiri kwenye business class kama wale washenzi na washamba waliozoa kutumia daraja hili wakati walikuwa wakiongoza kaya kapuku. Huu nao ni ufisadi ambao ulipaswa kufumliwa na walioutenda kuwajibishwa kama siyo kuogopana na kulindana vinavyoanza kuchipuka kimya kimya. Mijitu mingine kwa ulimbukeni sina mfano. Ukienda huko madongo ilikozaliwa usafiri wao ni wa punda na mikokoteni. Lakini ikishapata ulaji hujisahau na kujifanya siyo ile iliyozaliwa na kulelewa kwenye vitanda vya kamba na kulalia ngozi za mbuzi na kondoo. Hawa nao nitawapasha bila huruma wala aibu.
            Tatu, baada ya kumaliza kutoa mada yangu ya demokrasia, uwajibikaji na uchaguzi huru na wa haki, nina mpango wa kutoa pendekezo kuwa ving’ang’anizi wote waliomo maulajini waanze kufungasha virago ili kupisha mawazo mapya yatawale kaya ambazo wamezibaka kwa miaka. Kabla ya kuendelea, hivi juzi mlimsikia M7 akiwazodoa  Wagandaji kuwa yeye si mtumishi wa yeyote utadhani kaya ni mali yake binafsi?  Ana bahati mjivuni huyu. Ingekuwa majuu angefungashiwa virago siku hiyo hiyo ili wachovu wapate kiongozi mtumishi na si bwana kama huyu jamaa aliyeng’ang’ania ofisi kwa zaidi ya miongo mitatu. Inaonekana madaraka yamamempanda kichwani kiasi cha kuanza kujichanganya kutokana na kuchanganyikiwa na kuchanganya mambo. Inawezekana anaanza kutabiri anguko lake kama Jammeh litakalotokea bila kutegemewa na kwa namna isiyotarajiwa. Kwani akina Compaore, Jammeh hata Kashafi walitegemea kung’oka? We ngoja tu. Jamaa yangu Msomi anasema huyu jamaa anaweweseka baada ya kuondolewa maimla wawili japo kwa njia tofauti yaani Blaise Compaore na Jammeh. Anahofia Wagandaji wanaweza kuamka na kumfanyia kitu mbaya kama ambavyo amekuwa akiwafanyia kwa miongo zaidi ya mitatu.
            Kwa vile nina ishu nyingi za kushughulikia, acha niachie hapa ili niende kuwapasha waduwanzi wanaotumia njuluku za wachovu vibaya kwa kujilisha pepo na kutoa tongotongo. Special greetings to all Vasco da Gamas of this world. Tuonane wiki ijayo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
 

No comments: