Friday, 24 February 2017

Barua ya wazi kwa FreePerson MboHwe

Image result for photos of mbowe and magufuli
            Bwana Freebinadam
 Salaam; na pole kwa yaliyokusibu hivi karibuni kuanzia kuhamishwa kwenye nyumba ya msajili, kubomolewa Bilcanas, na kubwa katika yote, kutuhumiwa kwa biashara ya madawa ya kulevya. Hata hivyo, kutuhumiwa si jambo la ajabu hasa ikizingatiwa kuwa yeyote anaweza kutuhumiwa ukiachia mbali kuwa kutuhumiwa si kuhukumiwa kisheria; ingawa kilevi ni vinginevyo. Wengi wamesikitishwa na kushangazwa sana hasa na utaratibu uliotumika kufikia hitimisho la kukutuhumu. Tangu lini watuhumiwa wakaitwa kwa vyombo vya habari badala ya summons au kutumiwa ndata kuwadaka na kuwapeleka lupango tayari kwenda kwa pilato? Hapa kilichofanyika ni kutaka kutumia njia chafu kufanya jambo safi. Mwisho wa siku matokeo huwa ni uchafu unaomeza usafi.
            Pili nakupongeza kwa msimamo wako dhidi ya kile ambacho kilevi huita Kangaroo Court ambayo wajivuni wachache tuliodhani wangejua hata sheria za msingi kutaka kuitumia kuadhibu ima wabaya wao au kuitumia kutafutia maulaji. Tangu lini dingi wa mkoa akawa ndata, hakimu, mpelelezi na upuuzi mwingine? Nakushukuru kwa kuwastua.kwani, baada ya kugundua walivyoingia choo cha kike, siku hizi hawataji kiasi cha kushangaza kwanini wengine watajwe na wengine wasitajwe? Hapa dogo Po ameula wa chuya. Kama si kulindana, kibarua chake kilipaswa kiote mbawa. Hata hivyo, huu waweza kuwa mwanzo wa mwisho; hasa ikizingatiwa kuwa mzoea vya kunyonga, vya kuchinja haviwezi. Msimamo wako wa kukataa kuripoti kwa mamlaka haramu umenifurahisha na kunikumbusha mlevi mwingine wa kanywaji kaitwako justice almarhum Chris Mtikisa, ambaye bila shaka, angekuwa hai ashafungua kesi mia kidogo dhidi ya wasaka ulaji na wabangaizaji hawa.
            Tatu, nakushukuru kwa kuonyesha mfano na uongozi dhidi ya ubabaishaji na utaka sifa vinavyoanza kugeuzwa sera na baadhi ya wajivuni na waroho wa madaraka waliojisahau.  Mungu si Mlevi mie. Si juzi nikasoma sehemu kuwa waliotoa taarifa zilizosababisha utuhumiwe kumbe zilikuwa zimeelekezwa kwa Bilcanas kama sehemu ya matanuzi lakini si kwako binafsi. Hili liko wazi. Ila kwa vile wahusika walikuwa na lengo la kupata sifa, na si kupambana na mabwimbwi, waliamua kupinda mambo ili kukukomoa sijui ili iweje? Hapa naanza kuamini kuwa mazonge mengi yanayokuandama kumbe ni ya kisiasa zaidi ya kisheria. Nani, kwa mfano, hajui kuwa magabacholi wengi wanaishi dezo kwenye nyumba za Asajile Mwaijumba na bado familia na biashara zao havijaguswa?
            Bwana Freebinadam, hata nilipoangalia makaratasi uliyosema yameandikwa kwa mwandiko wa darasa la pili, sikuona jina lako zaidi ya Philemon jambo ambalo linaonyesha umaamuma na ukihiyo wa wahusika. Sijua hawa jamaa walipitaje kwenye vyuo wanavyodai kuvipitia wakati walishindwa jambo dogo kama hili; au ni yale yale ya Gus Lyatongolwa wakati wa mzee Ruksa ambapo kila upuuzi ulipewa nafasi katika kusaka sifa zilizogeuka chanzo cha mauti ya mhusika kisiasa?
            Walevi wanaunga mkono mapambano dhidi ya bwimbwi kama hata nawe ulivyobainisha kuwa huna ugomvi na vita hii zaidi ya namna inavyopiganwa kiuonevu, kibabaishaji, kisiasa na si kisayansi. Pia walevi wanakubaliana nawe kuwa vita ipigiganwe kweli kweli lakini si kwa kukomoana, kuzushiana, kuchafuana, kulindana na upuuzi mwingine ambavyo vilijitokeza nje nje kwenye awamu ya kwanza ya vita hii. Walevi wanamshukuru dokta Kanywaji kwa kuingilia na kumteua dingi wa vita hii huku akionyesha wasiwasi juu ya wale walioianzisha japo aliwasifia kinamna ili wasikate tamaa.
            Hata hivyo, kuna mambo ya kujikumbusha. Mithali 16:18 inasema “kiburi hutangulia uangamivu; Na roho yenye kutakabari hutangulia maanguko.” Kwa vile wanaokukamia wanajidai kuamini katika Mungu, tunatoa mstari huu lau uwasaidie hata kama unatoka kwa mlevi. Hakuna kitu kibaya kama kiburi na ulevi wa madaraka. Kiburi na majivuno mara nyingi ni silaha za juha hasa ikizingatiwa kuwa madaraka ni kama koti kwenye mabega ya mvaaji tena la kuazima. Tuliwaona wengi. Wako wapi akina Lyatongolwa? Wako wapi akina Ditto waliofikia hata kupiga walevi risasi na walevi wa maulaji wenzao wakawakingia kifua? Hawa ni vidagaa. Wako wapi akina bwana majivuno aliyewaita walevi wavivu wa kufikiri akaishia kuwa bingwa wa uvivu huo kwa kuwauza na kaya yao? Wako wapi akina Nebukadnezza na wengine wengi waliokuwa miamba na mabingwa wa fitna? Wako wapi akina Richard Nixon? Wako wapi akina Slobodan Milosevic, Nicolae Ceaușescu na wengine wengi waliohaiwa na madaraka? Wako wapi akina Saddam Hussein na watoto wao waliokuwa juu ya sheria wakaishia kufa vifo vya aibu? Kuna haja ya kutumia historia kufanya mambo badala ya kufanya mambo kutafuta nafasi katika historia tena nyingine chafu. Je nani hawajui wauzaji bwimbwi ambao wanahengwa hengwa? Nashauri tupambane na biashara ya bwimbwi kisayansi na kwa haki na si kisiasa na kwa kubambikiana na kupakaziana mambo kama ilivyoanza.
Chanzo: Nipashe Jumamosi kesho.

No comments: