How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 22 December 2010

Mkapa, Lowassa wameuona mchezo nje ya uwanja

KUNA usemi maarufu kuwa ukiwa nje ya uwanja unapata fursa ya kuuona mchezo vizuri kuliko wacheza wenyewe. Hivyo ukosoaji au ushauri unapotelewa na mtu aliyeko nje ya uwanja tena aliyewahi kuwa kocha mchezaji, unakuwa lulu na uzito wa aina yake.

Hii imejitokeza hivi karibuni wakati rais mstaafu Benjamin Mkapa na aliyekuwa Waziri Mkuu aliyestaafu, Edward Lowassa pamaoja na mapungufu yao na, lau walitoa mchango ambao ni adimu na adhimu na unaopaswa kupewa kipaumbele kikubwa tu.

Mkapa alikaririwa akisema: “…hatuna Katiba zingine zaidi ya zile ambazo tumezirithi kutoka kwa wakoloni, Katiba ambazo hazina umakini, tunahitaji mpya.”

Maneno ya Mkapa ni kweli. Karibu katiba zote ukiondoa za Afrika Kusini, Kenya na kidogo ya Botswana, zilirithiwa toka kwa wakoloni walioendelea kuzitumia kuweka vibaraka wao madarakani ili kuwatumia kuwanyonya wananchi waliodanganywa kuwa wako huru.

Pale ambapo wakoloni hawakuweza kuweka vibaraka wao, waasisi mfano kama Tanzania, walianzisha chama kimoja na kujiimarisha madarakani hata bila ridhaa ya watawaliwa. Chaguzi viini macho zilifanyika na wahusika kushinda kirahisi. Na hii ndiyo sababu ya vyama vikongwe kama CCM kuendelea kuwa madarakani hata bila ridhaa ya Watanzania.

Na hii ndiyo sababu kuu inayofanya CCM kutokubali kubadilisha katiba. Maana inajua fika kuwa kufanya hivyo inamaanisha kifo chake hasa kutokana na katiba mpya kuziba upenyo ambao imekuwa ikiutumia kusalia madarakani hata bila kufanya lolote.

Huwezi kuwa huru bila kupata haki zote za msingi kama kuwa na nguvu na maamuzi katika kuongoza nchi yako. Bila wananchi kuwa na ubavu wa kuilazimisha (kuiwajibisha) serikali kuwatawala watakavyo, maana ya kuwa na katiba na uhuru hupotea kama ilivyo kwenye nchi nyingi za kiafrika.

Hatuwezi kuendelea kuamini kuwa tuko huru tu kwa sababu tuna bendera na rais. Uhuru ni uchumi, huduma bora za jamii, uwajibikaji na maendeleo.

Katiba huru itokanayo na wananchi huwapa jeuri na namna ya kuiwajibisha serikali na serikali huwajibika vilivyo kwao. Hii ndiyo siri ya nchi zilizoendelea kuwa na serikali zinazowahudumia wananchi zikiwajibika moja kwa moja kwao.

Na hii ndiyo siri ya serikali kwa mfano kwenye nchi za Italia na Japan kubadilishwa (kutimuliwa) mara kwa mara.

Ingawa Mkapa alisifika kwa kiburi na urushi, kwa hili nakubaliana naye na kumpongeza huku nikimpinga mzee Ali Hassan Mwinyi aliyekaririwa hivi karibuni akisema eti hakuna haraka kwenye kuandika katiba bali kurekebisha iliyopo.

Tutarekebisha hadi lini iwapo katiba yetu ni viraka vitupu na balaa kwa maendeleo ya taifa?

Turejee nukuu nyingine ya Mkapa: “Katiba ndiyo moyo wa nchi, moyo wa mwanadamu unaofanya mwili mzima ufanye kazi… hivyo kwa kuangalia mbele tunahitaji kuundwa kwa Katiba na mihimili yote ya nchi, tunahitaji Katiba huru itakayotulinda katika hatari.”

Mkapa alisema hayo katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wanasheria wa jumuiya uliofanyika mjini Bujumbura nchini Burundi, Novemba mwaka huu.

Bila kuandika katiba upya tutaendelea kutapeliwa na watawala wababaishaji na mafisadi watokanao na uchakachuaji na jinai nyingine kama kuibia taasisi za umma ili kuhonga wapiga kura.

Lazima tuwe na katiba mpya inayotoa kanuni ya kutatua matatizo yetu na jinsi ya kutawaliwa. Tunataka katiba ambayo inatamka wazi kuwa rais wa Tanzania ni binadamu ambaye yuko chini ya sheria akiwajibika vilivyo kwa waliomchagua na wananchi kwa ujumla.

Tunataka katiba itakayoharamisha rais na wenzake kukataa kutaja mali zao au kuwa na mali zenye kutia shaka zisizo na maelezo kama sasa.

Tunataka katiba inayoainisha haki zote za mwananchi kwa usawa kabisa, katiba inayozuia israfu na ujambazi wa kimadaraka ambao kimsingi ndiyo chanzo kikuu cha umaskini wetu.

Tunahitaji katiba iliyokwenda shule kwa kuazima usemi wa vijana.

Kwa ufupisho tu, mambo tunayokosa kutokana na kutokuwa na katiba mpya itokanayo nasi-umma:

Hakika kwa katiba ya sasa ambapo baadhi ya watu wako juu ya sheria tena kikundi cha watu, umma unakosa haki ya kuishi maisha sawa na wao.

Rejea kwa mfano wanasiasa kujilipa mishahara na marupurupu makubwa kwa kutofanya kazi yoyote.

Wananchi wa kawaida hawana na hawapewi heshima hasa kwenye kuendesha nchi yao. Rejea kwa mfano, umma kulalamika watuhumiwa wakuu wa ufisadi kufikishwa mahakani na serikali-kikundi kidogo cha watu isifanye hivyo.

Uwajibikaji na uadilifu, kashfa zilizoingiza taifa kwenye umaskini kama Richmond-Dowan, EPA, IPTL, CIS, TICTS, SUKITA na nyingine nyingi ziliwezeshwa na katiba mbovu isiyohimiza uadilifu na uwajibikaji.

Uraia wa nchi mbili, wazalendo wamekuwa wakinywa na kuhofishwa kuwa na uraia wa nchi mbili huku wakihimizwa kuwekeza ndani. Ajabu tunao tunaodhani ni raia wenzetu wanaotii katazo hili wenye uraia wa nchi nyingi na si mbili tu.

Mfano, watuhumiwa wa ufisadi kama Sailesh Viran na wenzake wenye asili ya kihindi wasingekuwa na uraia wa nchi nyingi wangewezaji kutoroka toka nchini kirahisi?

Mwanya huu umetumiwa na mamluki na wakimbizi wengi wa kiuchumi wanaoshirikiana na watawala wasio waaminifu kutorosha raslimali na hata pesa zetu nyingi za kigeni bila kudhibitiwa wala kushughulikiwa huku tukishuhudia.

Tutafanya nini iwapo hatuna nguvu kikatiba? Hii ikichangiwa na katiba ya sasa kuwapa wanasiasa madarakana na kinga nyingi, ndicho chanzo kikubwa na ufisadi na umaskini wetu kama nchi.

Tumeona nchi jirani ya Kenya ambapo mawaziri wengi wamepukutishwa kutokana na katiba mpya ya Kenya kutamka wazi kuwa kila atakayeshutumiwa lazima achie madaraka ili achunguzwe na kuwajibishwa jambo ambalo hapa kwetu hakuna.

Kufutilia mbali ufisadi na unyanyasaji wa kitaasisi na mtu binafsi.

Hayo yote hapo juu hayahitaji mtu kuwa na shahada ya utawala wala utafiti kujua. Kila mtanzani anajua fika kuwa kikwazo chetu ni kutokuwa na katiba inayotokana na wananchi wenyewe kwa ajili yao.

Na kila mtu anajua nani anaiba nini wapi hata lini. Na hii ndiyo iliwezesha hata wabunge wa upinzani kuweza kuibua kila aina ya ufisadi kabla ya serikali ya sasa kuhakikisha hili halifanikiwi. Maana yake ni kwamba hata hata whistle blowers wakiwapelekea siri, bungeni watakumbana na kisiki tokana na kuondolewa kwa spika Samuel Sitta. Hii leo hapa si mahali pake.

Ingawa Mkapa alichelewa kuanza mchakato alipokuwa madarakani, aliyosema kuhusiana na kuandikwa katiba upya ni ya msingi na yapewe uzito na kufanyiwa kazi.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 22, 2010.

4 comments:

Anonymous said...

Mpayukaji,

Hivi kuna uwezekano ukatuwekea soft copy ya katiba ya sasa kwenye mtandao wako? au itakuwa ni ukiukaji wa sheria.

Wengi sana tunaimba kuwa katiba ingaliwe upya lakini nikwambie kweli sidhani hata watanzania walioisoma katika ya sasa wanafika hata 1% ya 40+mill.

Hata watanzania walioelimika sidhani wanafika 5%.

By Mpingo

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mpendwa Mpingo,
Kupata katiba yetu viraka ni rahisi. Google katiba ya Tanzania itajitokeza na utasoma hata ukitaka ku-bookmark unaweza kufanya hivyo kirahisi tu.
Otherwise nashukuru kwa kutembelea kibaraza changu na kudondosha ujumbe.

Simon Kitururu said...

@Mtakatifu Mpayukaji: Mpingo anapointi! Unajua nimeuliza Watanzania wengi niwajuao na jibu nilipatalo ni kwamba hawajawahi hata kushika KATIBA mikononi?

Kuna kipindi wakati nasoma somo la uraia wakati mpaka tunanyambulisha katiba na MWALIMU ambaye kwa bahati mbaya hata jina simkumbuki kwa jinsi nilivyokuwa kijinga napuuzia somo lake na la SAYANSIKIMU ingawa najua alikuwa KADA mzuri WA CCM,...
....hata sikuelewa umuhimu wake mpaka baadaye kidogo nilipoondokana na shule hizo ,... ...ila siku hizi ndio kabisaa naona kuna umuhimu sana WA SOMO lijulishalo watu KATIBA na nahisi WACHAKACHUAJI watahakikisha hicho kitu hakifanyiki kwa kuwa haki ya nani hata wadaio KATIBA mpya hawazidi asilimia 15 katika wahitajio kura wawahitajio.:-(

Nawaza tu kwa sauti!:-(

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mt. Kitururu,
Nakubaliana nawe Mpingo ana bonge la pointi. Ndiyo maana nimempa mbinu rahisi ya kuipata KATIBA YETU VIRAKA ya 1977.
Nitajitahidi kuibandika hapa.