Monday, 6 May 2013

Kwa hili nampongeza Kikwete

 
Baada ya watanzania kuhuzunishwa na shambulizi la bomu huko Arusha kwenye kanisa la kikatoliki huku wakilalamikia tukio la rais Jakaya Kikwete kufanya ziara nchini Kuwait bila taarifa, angalau watafarijika baada ya rais kukatiza ziara hiyo. Hii itapunguza hasira ya watanzania waliokuwa kwenye mstuko mwingine wa kujua kuwa kumbe rais wao alikuwa amefanya ziara nchini Kuwait tena kinyemela bila kuwataarifu.
Kwa wenye kujua nafasi na umuhimu wa urais, tulitarajia kuwa rais Kikwete angekatiza safari yake na kuwahi Arusha ili kuwafariji wahanga pamoja na kulipa matumaini taifa. Inafurahisha kuwa amefanya hivyo na kutimiza matarajio yetu. Kwa uamuzi wa kukatiza ziara tena yenye utata, tunampongeza rais kwani huu ndiyo wakati watanzania wanamhitaji ili atoe mwelekeo wa kuenenda na tishio hili. Laiti Kikwete angeendeleza uzi huu wa kujifunza kutokana na makosa yake, watanzania wangeweza kumsamehe na kuanza kumuangalia kwa uoni mpya. Kwani yapo maeneo mengi ambayo rais amepwaya na kuendelea kufanya madudu kama vile kubadili mikataba ya uwekezaji wa kijambazi aliyorithi,  kuwatimua kazi mawaziri walioghushi na wale waliosababisha kufeli kwa vijana wetu kati ya mengi. Tunaamini rais atatia maanani hisia zetu na kuzifanyia kazi.

13 comments:

Anonymous said...

Unampongeza kwa kuwa kakatisha ziara na waliokufa ni wakristo? Angekatiza ziara na waliokufa ni waislam angekuwa mdini.unanifurahisha kweli na usomi wwko

Anonymous said...

Unampongeza kwa kuwa kakatisha ziara na waliokufa ni wakristo? Angekatiza ziara na waliokufa ni waislam angekuwa mdini.unanifurahisha kweli na usomi wwko

Anonymous said...

hii pia nzuri
kuwa kumbe rais wao alikuwa amefanya ziara nchini Kuwait tena kinyemela bila kuwataarifu.

na hii pia:
Tunaamini rais atatia maanani HISIA ZETU na kuzifanyia kazi.

Rias wa tanzania wawachiliwe watanzania wenyewe na sio kinyume chake sio watu waloukata uraiya wa tanzania na kuwa raia wa nchi ingine wala matapishi

Anonymous said...

Ano 06:46 humjuwi huyu maalim
ati anampongeza rais ha ha ha ha

JARIBU upo?

NN Mhango said...

Anonymous 6 May 2013 06:46 jaribu kukua kidogo na uwe mstaarabu. Fahamu kuwa rais ni wa watanzania wote. Na usitake watu wajenge hisia kuwa waliotupa hilo bomu ni magaidi wa kiislam. Tusifike huko. Laiti kama Kikwete angechaguliwa na waislam pekee na katiba ikatamka kuwa ni rais wa waislam zaidi ya watanzania mawazo yako yangeingia japo akilini. Hammsaidii Kikwete kufikiri kikale na kibarafu. Kama yeye ametambua umuhimu wake kosa liko wapi kumpongeza? Hata wangeuawa nyani na nguruwe tumbiri na fisi wa nchi yake bado angewajibika kwao. Acheni ukafiri na kufuru zisizo na sababu. Kwani hao wakristo hawakuumbwa na Mungu? Mbona ulipoanzishwa uislam wakristo hawakupiga kelele wala kutowanyima raha? Sitaki niamini kuwa wewe ni muislamu zaidi ya mjinga fulani asiyejua hata maana ya hadhi ya urais. Anon6 May 2013 10:45 si kweli kwamba nimeukana uraia wa Tanzania hata kama thamani yake imefanywa kuwa ndogo. Pia sirambi matapishi. Nashukuru Subhanna kuwa alinijalia akili na elimu vya kutosha. Pia nashauri watu muache unafiki na kujidanganya. Wewe mwenyewe unayenikandia kwa kuishi nje unatamani hata kesho upata japo hata fursa ya kuja na kuona maisha yakoje na si mateso kama mnayosababishiwa na akina Kikwete. Hao mnaowaabudia kila siku wako kiguu na njia kuja huku lau kubadili maisha ukiachia mbali kuwaibieni pesa yenu na kusomesha watoto wao huku. Kalia kujiridhisha lakini nijualo roho inakusuta kwa jinsi unavyojiongopea. Mngekuwa mnachukia maisha ya huku mngesema heri kuzaliwa paka Ulaya kuliko binadamu Bongo? Anyaway, siku nikirejea na vitegemezi vyangu vimeiva kielimu na kuchukua kazi zenu mtajua nilichokuwa nikifanya huku. Na namshukuru Mungu ninavyo vya kutosha na naviandaa kweli kweli. Una bahati. Angekuwa Mkapa angekwambia acha wivu wa kike wewe.

mtwangio said...

Mhango,umeiona hatari hiyo?Majuhudi yako unayoyafanya ya kutaka kuwatoa watanzania upofu na kuwarudishia uoni bado kuna baadhi yetu tunafadhilisha upofu kuliko uoni?Je hao wanaokukosoa kwa kumpongeza Kikwete wanataka kukukwambia nini?au sisi wasomaji wako wanatuambia nini?

Kama ulivyoandika kwamba "Fahamu rais ni wa watanzania wote"nami naongeza kwamba amechaguliwa na watanzania waliomkubali wa matabaka,dini,rangi na makabila yote na kama kuhudumia wananchi anawahudumia wananchi wote wa tanzania bila kujali tabaka,dini,rangi au kabila.Naam hatuwezi tukakubaliana na Rais wetu kwa kila kitu na hatuwezi kumkosoa kwa kila hatua,tunajaribu kutekeleza haki yetu kama wananchi wanaoishi katika nchi ya kidemokrasia(japo tupo mwanzo wa njia)kwa kuangalia kile ambacho rais wetu anachokifanya kwa masilahi ya nchi na wananchi tutampongeza na pale ambapo anapolipeleka jahazi mrama tutaongea na hatutonyamaza hii ni haki yetu hatutorudi nyuma au kukaa kimya.

Mhango,ukweli uliokuwa wazi na dima kwamba watu ambao waliofilisika mawazo au wenye mawazo mgando siku zote wanakuwa hawana cha kuchangia katika kadhia muhimu za nchi na badala yake wanapofunuliwa macho badala ya kujadili au kuchangia hoja kwa hoja wao wanamshambulia mtoa hoja mwenyewe binafsina kusahau kujifanya kusahau hoja zilizokuwepo ubaoni.

Kama ungekuwa katika wale amabao wenye kuangalia masilahi yao na ya familia zao ungebaki Tanzania na ungefaidika na kunufaika sana na utaratibu fisadi,wizi,kudhalilisha na mengineyo hata labda tungekujua kama mbunge,waziri au hata kuwa mwenyekiti wa chama pinzani.Lakini umekua na mission katika maisha yako ya kupigania uhuru,haki,uadilifu na ukweli kwa gharama yoyote ile iwavyo.Na kwa hili nakupongeza sana.

Turudi katika kadhia iliyopo ubaoni,Naam kama inavyoonekana mbele yetu kwamba Rais amekatisha ziara yake Kuwait na kurudi nchini kwa maafa yaliyotokea kama wajibu wake kama rais kiuwazi inabidi tumpongeze kwa hili,lakini kama utakumbuka wakati madaktari walipoanza mgomo wao nakumbuka alikua nje ya nchi na wala hakutikisika na kuamua kurudi nchini kuja kulikabili tatizo hilo na nakumbuka hata aliporudi hakukaa kwa muda akasafiri tena,na nakumbuka nawe hukuliklia kimya utaratibu wake huo na ukakemea.

Lakini hili la kusafiri kinyemela na wananchi bila ya kujua na nyuma yake kulipuka bomu hapa nadhani kuna maswali mengi kuliko majibu.kwanza kabisa nawapa pole wale wote ambao waliojeruhiwa na kuwapa rambirambi kwa familia ambao waliopoteza wapendwa wao katika maafa hayo.

mtwangio said...

Muda si mrefu uliopita nimezisoma taarifa toka katika website moja ya mashariki ya kati zisemazo kwamba kuna wasaudia wanne na watanzania wawiwli wapo chini ya mikono ya usalama wanashukiwa kwamba wanahusika na bomu hilo!!Na habari hizo zimetoka katika chombo cha usalama,je taarifa hizi kutolewa na serikali japo ni hatua ya awali ya uchunguzi hazitii moyo.sina maana kwamba wasaudia hao hawazezi kuhusika na bomu hilo lakini naona ni utaratibu ule ule wa serikali yetu kutuondoa njiani na kutuziba macho na tuanze kushikana makoo wenyewe kwa wenyewe kwa chuki za kidini na sina maana kwamba chuki hizo hazipo chuki zipo na kuna nguvu za kiza toka serikalini wanachochea fitina hiyo,na hata nami nimejaribu kuongele hofu yangu kuhusu tatizo hili la chuki za kidini.

Nakumbuka serikali ya Mubaraka Egypt ilipoona inaanza kuzama ilitumia tactic za aina hiyo hiyo ya kulipua kanisa kule Alexandria na kwa mbegu za chuki na fitina za udini tayari zilishamea waisilamu na wakristo wakaanza kukaliana kooni,lakini wale wachunguzi wa mambo na wenye akili kwa pande zote mbili walishitukia kwamba hizo ni mbinu za serikali za kupeperusha wananchi katika vita vyao halali vya kuiondoa serikali madarakani na badala yake wauane wenyewe kwa wenyewe na serikali izidi kuwa na hoja ya kubaki serikalini.

Wanasiasa ni wanasiasa tu wanachojali ni kubaki kwao madarakani kwa hesabu yoyote ile iwavyo bila hata kujali maadili yoyote yale ya kibinadamu na hata ya kidini.je kuuliwa kwa Padri kule zanzibar,kuanza kwa tabia ya kuchomeana misikiti na makanisa na leo ni bomu je hakuna haja ya kudai tena kwa sauti ya nguvu kwamba serikali ya CCM ipo nyuma ya matokeo yote hayo??waisilamu na wakristo wa Tanzania na viongozi wao wa kidinikama wataendelea nao na opofu na uziwi wao muda si mrefu tutafikia hali ya Nigria,Iraq na Egypt na kama serikali inatumia mbinu hizo chafu kwa kutaka kubaki madarakani watasababisha madhara ambayo mwisho wake Mungu ndio anayejua.

NN Mhango said...

Mtwangio nashukuru sana kwa mchango wako. Naamini walengwa watafaidika watake wasitake. Mie siwezi na wala sitakatishwa tamaa na watu waliopigika kimaisha wakakata tamaa. Hebu angalia hata michango yao. Huwa sivumilii matusi.
Na bahati nzuri hata hayo matusi yao yanapozidi mipaka huwa nayaondoa bila kujali wametumia muda na akili zao hata kama ni mbovu. Uzuri nawapenda kitu kimoja hawa wakosoaji wangu. Huwa ni wasomaji wangu. Kwa hili nawapongeza kwa vile huo ni uoni wao. Naamini taratibu watakuja kuona ukweli siku moja.
Nimalize nawe Mtwangio, nashukuru tena kwa kunisaidia kuwaelimisha hawa wenzetu. Inabidi tuwavumilie ni watu wetu na ni wenzetu. Pia nakushukuru kwa kunipa moyo.

Jaribu said...

Anonymous wa 6 May 2013 10:47

Sidhani kama Mhango au mimi tuna chuki binafsi na Kikwete. Akifanya au akijaribu kufanya kitu kizuri tutampongeza; ingawa kukatisha hii ziara ya kutoroka, I mean ya kiserikali ya siku mbili(mind you "aliondoka" Ijumaa sijui akakatiza jana). Hapo siku mbili zishapita kwa hiyo sijui amekatisha nini.

NN Mhango said...

Du Jaribu umenifungua macho! Hii kamba nyingine acha niipige sasa hivi. Nakushukuru sana.

Jaribu said...

Hamna tabu, bro!

Anonymous said...

Sasa nyie hamtaki mawazo mbadala yaani mnachosema na kufikiri nyie iwe sahihi wacheni watu watowe mawazo yao au vp.

NN Mhango said...

Anon6 May 2013 22:57 hakuna asiyependa kukosolewa isipokuwa Mungu pekee. Ukikosoa na kushambulia mawazo yangu na kuonyesha udhaifu wangu unakuwa umenisaidia na kuwasaidia wengine. Lakini kunishambulia mimi binafsi ni kama kupoteza muda kwa sababu hakuna utata wowote juu mimi kuwa mimi.
Hata hivyo nashukuru kwa mchango wako wa mara kwa mara. Mungu akubariki tuendelee kulumbana kwa hoja elimishi na fikirishi.