Kuna swali moja linalosumbua wachambuzi makini: Kwanini kila serikali inapokabiliwa na kashfa au taasisi zake kama vile TISS hutokea 'filamu nyingine' ya kuwaondoa watu kwenye mjadala? Wakati wa sakata la gesiasilia Mtwara wengi wanajua ilivyozimwa kwa kuleta filamu mpya ya Kibanda ambayo nayo ilizimwa na ya Rwakatare kabla ya hii ya Arusha. Tumeshuhudia filamu nyingi kuanzia ile ya Ulimboka, mauaji ya Padri na uchomaji wa makanisa kule Zanzibar, kuuawa kwa mchungaji kwenye sakata la kugombea kuchinja na nyingine nyingi tu.
Tukiachana na conspiracy theory, tujiulize. Je serikali yetu imechukua hatua gani kukomesha ugaidi kwa namna ya kisayansi? Je mbinu kama kuwa-frame watu kama Rwakatare au hata kutoa taarifa za kukamata wasaudia wanne au mkenya 'aliyemteka' Ulimboka peke yake na nyingine zinatatua tatizo au kulikuza?
Blogu hii imewahi kutoa link ambayo tutarudia kuitoa hapa ambapo mtu mmoja aitwaye shehe Ilunga alikuwa akiwahimiza magaidi na wahuni wenzake waue viongozi wa kidini hasa wakristo bila kujua kuwa anaweza kutokea mhuni mwingine wa kikiristo kama alivyowahi kufanya Christopher Mtikila wakati wa sakata la magabacholi na kuhubiri dhana kinzani. Ukisikiliza maneno ya shenena Ilunga unashangaa: Kwanini serikali imemgwaya kama haijamtuma? Mtu anasema wazi wazi tena kwenye vyombo vya habari lakini hakuna anayemuhoji achia mbali kumkamata! Tunasema hivi kutokana na kushuhudia kasi ya polisi waliogeuka wa CCM walivyokuwa wepesi kumkamata Rwakatare huku wakijifanya hawajui kansa ya Ilunga. Je ni kweli polisi na serikali hawajui sumu anayomwaga Ilunga na wengine kama yeye wanaotumia mihadhara ya kihuni na njaa kuhubiri balaa? Je inakuwaje matukio kama haya yanapotokea watawala wetu wanakuwa wepesi kuwahi kuhani na kutoa faraja wakitoa matamshi mepesi ila wakawa wagumu kushughulikia kiini cha kansa hii? Juzi tulimpongeza rais Jakaya Kikwete kwa kukatiza ziara yenye utata kule Kuwait kuja kutoa msimamo na matumaini kwa taifa--- bahati mbaya hakutoa matumaini wala msimamo zaidi ya kupiga picha na waathirika. Kuna hisia kuwa hakukatiza ziara kama tulivyotangaziwa bali tulipigwa changa la macho hasa ikizingatiwa kuwa rais alikuwa nje kwa zaidi ya siku tatu na ukweli kuwa kila siku anayokuwa kwenye ardhi ya nchi ya kigeni hata kama ni saa moja uhesabiwa kama siku. Hilo leo hatulijadili kuna siku ukweli utajulikana.
Pmoja na yote, inashangaza kuona jinsi rais alivyoshindwa hata kutoa tamko ukiachia mbali lile jepesi lililotolewa na Kurugenzi ya Rweyemamu ya Ikulu ambalo halina kichwa wala miguu. Ukiachia mbali kuonekana kwenye picha akiwasalimia waathirika, hakuna neno tamko lililotolewa na rais kwa uzito unaostahili. Alipaswa ahutubie taifa na kutoa mikakati ya kuenenda na kadhia hii. Lakini wapi! Je namna hii tunaweza kuondokana na uhuni na jinai hii?
Wengi tulidhani baada ya kurejea nchini Kikwete angekaa na vyombo vya usalama na kuja na taarifa ya mpango wa nini kitafanyika. Badala yake amekuja na sanaa zile zile... TUTAWASAKA HADI KUWATEKETEZA. Mtawasaka vipi, lini na wapi wakati mnawajua lakini mnajifanya hamuwajui? Kikwete ana bahati ya mtende. Nilishangaa niliposikia viongozi wa waathirika wasikiwahimiza watu wao wasali sana wasijue kuwa sala pekee si jibu. Nadhani wangeibana serikali kwanza kabla ya kumsukumia mzigo Mungu au kumuomba. Wanadhani Mungu hakuona haya yote? Aliacha yatokee ili wabaya wajulikane na kuumbuka. Ni bahati mbaya kuwa viongozi wa kidini nao wamekuwa na tabia kama za serikali. Badala ya kulielekea tatizo wanakimbilia kusali. Kwani kusali walianza jana? Kwa mayatima na wajane ukiwaambia wasali sana huku ukiogopa kumkamata aliyewahujumu wanakuona kama msanii tu hata kama kusali ni jambo la maana. Sisi tunadhani tungewabana wahusika watuhakikishie usalama wetu na wawakamate wanaoua watu wasio na hatia ndipo kusali kufuate. Hakuna awezaye kuishi kwa mkate tu. Mungu atakusaidia baada ya wewe kujisaidia. Nimependa kauli ya Muadhama Kardinali Polycap Pengo ingawa alifumbufumba alipoonyesha kuwa tatizo ni ombwe la uongozi kitaifa aliposema,BONYEZA HAPA.
Kwa upande mwingine nimeiponda kauli ya rais wa Baraza la Maakofu Tanzania (TEC) Mhashamu askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, aliyekaririwa hivi karibuni akisema, “Tulieni na kufanya tafakari kasha mwambie Mungu hayo yote ayafanyie kazi kwa uweza wake. Sisi binadamu tunategemea nguvu kutoka kwake.”" Sijui huyu kama ana ndugu aliyepoteza maisha kwenye jiani hii. Huyu na Kikwete wasingeweza kusema au kuchukua misimamo husika kama waathirika wangekuwa watoto, wake au ndugu zao. Rejea jinsi polisi wanavyohamanika na kukamata wahalifu wanapowaua polisi au kuwaibia viongozi wazito. Aibu.
Nadhani umefika wakati wa kuwabana watawala wetu waache kututumia kwenye siasa zao chafu. Haiwezekani wahalifu kama Ilunga waachwe waendelee kuhubiri maangamizi. Tumezidiwa na Kenya ambayo ilipogundua kuwa muungu wa Ilunga aitwaye Mohamed Rogo (ambaye muunga wake alikuwa Osama ambaye muunga wake alikuwa Zawahir ambaye muungu wake alikuwa Said Khutb) haikumpa nafasi ya kuhubiri upuuzi wake bali kuhakikisha anawahi anakotaka wenzake wawahishwe. Ndiyo. Dawa ya moto ni moto. Kwanini Tanzania haijifunzi toka kwa Marekani ambayo iliwaumba akina Osama bin Laden na kuwateketeza baada ya kuona wanavuka mipaka? Hata kama akina Ilunga wametengenezwa na serikali, ijue nao wana akili na malengo yao kama ilivyokuwa kwa akina Osama. Wakati wa kuwateketeza akina Ilunga ni sasa sanaa hazitaisaidia serikali na watanzania. Kwa upande wa pili, kwanini watanzania wanakubali kuchezewa mahepe kila uchao bila kukengeuka?
Tumalizie kwa kuishauri serikali na TISS yake waache kutuchezea na kututoa kafara kwenye maigizo yao. Kama kweli wanataka kujua chanzo cha kutupwa mabomu makanisani hata kuchomwa na kuuawa kwa viongozi wa kidini au kumwagiwa tindikali basi wamkamate Ilunga atawataja wenzake. Kwa ufupi ni kwamba magaidi waliolipua bomu Arusha hawajatoka Saudi Arabia bali Tanzania na kiongozi wao anajulikana. Hawa si wengine bali Boko-Al-Qaida Tanzania ya Ilunga na TISS. Sidhani kama akina Igondhu na Zoka hawajuani na Ilunga. Wasingejuana nadhani wangekuwa wepesi wa kumtia mbaroni kama walivyofanya kwa Rwakatare lakini wakashindwa kuwashawishi watanzania kuwa ni gaidi wakati magaidi wanajulikana. Ni uhuni na utoto na ujuha kiasi gani!It is time to call a spade a spade; not a big spoon.
Tunangoja tamko linaloingia akilini toka kwa rais Kikwete.
2 comments:
Huyo aliyempa Ilunga "UUstadhi" ndiye aliyempa Nchimbi uDakta. Ustadhi mzima anaita Koran "Koroani!"
Naona "Wasaudia" hao watakuwa ndugu wa mmiliki wa Dowans, Brigadia Mpemba.
Na hao jamaa wa Tanzania Incarnation of Savage Spies wanahitaji mwandishi mzuri. Hizo plots zao za kibuda sidhani kama zitawapatia Oscar
Jaribu sitaki niongeze neno ila umeniacha hoi eti unasema Tanzania Incarnation of Savage Spiues! Mie huwaita Taifa Institute of Sabotage and Setbacks. Kweli umempata huyu shehena aitaye Koran Koroani. Hawa ndiyo mashehe ubwabwa wanaosumbuliwa na njaa. Heri angeungana na Ponda wakapondwe huko gerezani badala ya kuponda raha.
Post a Comment