Chama
nambari wani kilipokuja na sanaa za kujivua magamba niliogopa. Magamba yalipo
kipiga mkwara kikanywea. Badala ya kuyashughulikia yalikishughulia na
yakaendelea kufanya vitu vyake. Nami naona heri nijigeuze gamba
lau nifaidi wafaidicho magamba. Siku hizi kuwa gamba dili babkubwa. Unageuka
gamba na kukomba ili uzidi kutuna. Katika ugamba wangu nitaanzisha biashara ya
kusafirisha madawa ya kulevya, pembe za ndovu na nyara za taifa. Kwa vile
nitakuwa na gamba nene, hata uwanja wa ndege hawatanikamata. Simpo. Kama nitaona
wale dog wa polisi wanaanza kunisumbua, nitaongea na jamaa zangu wa zima fire
waniingizie kago yangu. Watashindwa nini iwapo nitawapa dau kubwa?
Tuache utani,
taarifa kuwa watu wa zima fire wanatumia migari yao kuvusha bidhaa za wizi pale
mwalimu Mchonga International Airport zilinfungua akili. Nilizibuka na kugundua
ni kwanini mibwimbwi inajaa kwenye kaya. Kumbe jamaa ndiyo wanakula dili! Badala
ya kuzima moto wanahangaika na wizi siyo? Ipo siku wataungua motoni waangalie.
Ila waliniboa niliposikia kuwa wanachana mizigo ya abiria tena waliotoka majuu
na kuiba vijisimu na vipapakatishi vyao. Wajua vipakatishi ni nini? Laptop au
kompyuta lapa. Hayo tuyaache. Leo siwafundishi Kiswahili.
Nataka niwe
gamba tena lile la nguvu. Najua nikishaunyaka ugamba nitapata mshiko wa nguvu
kiasi cha kuficha kiasi kule Jersey na Uswazi ya Uswizi kabla ya kugeuka
mfadhili wa miradi mbali mbali ya kiroho na uroho kama magamba. Nitakuwa
nikiabudiwa kama magamba mengine. Nitatisha kama ukoma achia mbali miwaya.
Lazima niwe gamba nifaidi bwana. Unadhani kuwa gamba mchezo?
Kuanzia leo
naitwa mlevi Nkwazi Gamba nene na la haja. Raha ya kuwa gamba ni
kwamba unageuka mtakatifu. Dhambi zako zote zinasafishwa na unakuwa mweupe kama
theluji. Nani hapendi kuwa kama theluji? Niongeleapo gamba hapa simaanishi lile
jeusi la kobe na kasa. Ni gamba jeupe la utakatifu liliojaa utakakitu. Gamba la
kitu si la kinyama mwitu kama kobe. Gamba na neema na zali na si gamba la
konokono au kakakuona. Gamba langu lina nguvu kuliko hata magamba ya vyuo au
shahada ambazo nimejaza nyumbani kwangu. Lazima nivae gamba.
Ukiwa na gamba
wenye gwanda na magwanda hawakutishi. Badala ya kukutia adabu wanaishia
kukujadili huku wewe ukijinoma na maulaji yatokanayo na kuwa gamba. Gamba bwana.
Ujanja kupata gamba na si vinginevyo. Raha ya kuwa gamba ni kwamba unalinda
kokwa ambalo mara nyingi ndilo humuihifadhi mdudu. Unahifadhi kokwa na kokwa
linakuhifadhi. Mnahifadhiana. Maana ukibanduliwa ujue ndiyo mwisho
wa kokwa. Na gamba haliwezi kuota bila kuwepo kokwa. Kokwa haiwezi kuishi bila
gamba. Hivyo, tunatumiana na kutumiana hadi tunaishi. uzuri wa kuhifadhi na
kuhifadhiwa na kokwa si kama ule wa malkia wa mchwa ambaye huwaruhusu walume
wampe urodas halafu akawaua ili wasijishaue kuwa walishiriki kikombe na bi
mkubwa.
Uzuri wa kuvaa
gamba au kuwa gamba ni kupata ulinzi toka kwa watukufu wenye magamba mazito.
Mara hii mmesahau jinsi gamba lilivyomuokoa Eddie Ewassa na Andy Chenge baada ya
wapingaji kuwashupalia? Risasi za wapingaji hazikuwapata kwa vile zisingepenya
kwenye magamba yao mazito. Hakuna kitu hunifanya ninywe na kucheka kama sanaa za
jamaa yangu Njaa Kaya. Wajua? Akiwa ameuchapa ulabu si alijisahau akapayuka kuwa
lazima genge lao lijivue gamba asijue gamba la kwanza yeye! Baada ya magamba
mengine kuinyaka yakapanga mikakati ya kumvua nguo ili kila mtu aone gamba lake
lilivyo nene kama yao.
Akiwa amemtuma
Mapepe Napepea Ninaye kuwashambulia magamba wenzake bila kujua na yake
wanayajua, Njaa Kaya aliishia kuuchomoa na kunywea huku Mapepe naye akizodolewa
kwa kimuhe muhe na unywanywa wake. Mapepe alinywea kadhalika akakosa hata la
kuwaambiwa waandishi wa umbea. Aliona aibu kuongea utadhani alikuwa na kiseyeye.
Magamba yaliendelea kundunda hadi kutishia hata ulaji wa mweyewe. Asingestuka na
kuufyata angeishia kuvuliwa gamba lake na kuadhirika huku wao wakiendelea kupeta
kutesa na kusepa.
Kimsingi,
rafiki yangu Njaa Kaya huwa na kaugonjwa ambako kitaalamu huitwa Payukayosis
mental marasmus. Huu ni ungonjwa hatari ambao ukimpata mtu huadhirika mchana
kweupe. Nakumbuka ugonjwa huu uligunduliwa mara ya kwanza nchini toka kwa
mgonjwa aliyeitwa Yusifu Makambae Ngosi. Huyu bwana alikuwa ana kaugonjwa haka.
Alikuwa akipayuka huku kinywa na ubongo vikikosa mawasiliano. Hata Mapepe Musa
Nnaye naye ana kaugonjwa haka ingawa hakajafikia kiwango cha wagonjwa wawili wa
kwanza.
Gamba ni kinga
kuliko hata tunguli. Ukiwa na gamba hata ndata hawakuoni na wakikuona wanapumbaa
wakikuacha ukifanya vitu vyako. Kama si gamba rafiki yangu Andaraman Kinamna
angekuwa akikunyea mtondoo lupango. Baada ya zali lake la kusafirisha vipusa
Mbali ya Mashariki kufichuka, ndata walitaka wamtie mikononi. Walipogundua kuwa
kumbe naye gamba wakanywea. Kuwazodoa zaidi Njaa Kaya alimpa ulaji kwenye genge
na kutuacha wengine vinywa wazi. Jamaa anazidi kutanua hata kwenda kutembelea
miradi yake huko alikouza nyara za umma. Wajua? Nyara za umma hata ukiziteka
nyara hakuna wa kukuuma maana huwa nyara za umma, sawa na mali ya umma, haziumi.
Unaziuma na hakuna chombo cha dolari cha kukuuma angalau ukakoma.
Kayani kwetu
lazima uwe gamba ndiyo uishi vinginevyo utajiishia sawa na walalanjaa. Nani
alijua kuwa Roast Tamu La Aziz angeweza kufanya yote aliyofanya kuanzia
Kagodamn, Downs, Richmonduli na uchafu mwingine na akaendelea kuula bila kuliwa?
Gamba bwana! Ukiwa na gamba una kinga ya uhakika. Ndiyo maana nami napanga kuwa
gamba ili wenye magwanda wakinilenga wanoe kama walivyonoa kwa magamba tajwa
hapo juu. Nataka niwe gamba nono na zito kama mzee wa Kiwila anko Njomba Ben
Nkapa wa Bill.
Chanzo: Nipashe Jumapili Mei 11, 2013.
No comments:
Post a Comment