Wednesday, 29 January 2014

Kijiwe chastukia CV ya waziri wa njuluku


BAADA ya msanii, sorry, mkuu kufanya vitu vyake, kijiwe nacho kinakuja kufanya vitu vyake. Haikuwa kwenye ajenda ya kijiwe kama si Mpemba kuibua kitu ambacho wengi hawakuwa wamekiona.
Mpemba anaingia akiwa na gazeti la Danganyika Daima. Anatweta kana kwamba kagundua dawa ya ngoma!
Anasema huku akiwa anatweta: “Assalaam alaykum jamia.” Tunajibu kwa pamoja: “Waleikum Salaam shehe.” Anaendelea: “Yakhe mwaona hili balaa?”
Kabla ya kuendelea, Msomi Mkata tamaa anamuuliza: “Yakhe balaa lipi mbona kuna mabalaa mengi kwenye kaya yetu. Lipi hilo lililoongezwa? Hebu tujuze basi utuondoe mshawasha tashwishi na shaka shehe.”
Anakunjua gazeti na kutuonyesha picha ya Waziri wa Njuluku aitwaye Saaada Mkuuuyaaa Saalimu.
Anasema: “Huyu binti mie namjua sana.” kabla ya kuendelea, Mbwa Mwitu anachomekea: “Umjua sana vipi ustaadh?”
Mpemba hajivungi. Anajibu: “Mie nanjua kama mtu mwenye CViii yenye utata. Kwa vile twajua alivozaliwa Kiembe Samaki na makuzi yake leo twaambwa yu msomi kiasi hiki wakati siyo!”
“Hebu Ami eleza uzuri. Una maana huyu bi mkubwa naye ni kihiyo kama wale ambao wamekuwa wakilindwa na mkuu wakidai wana Ma PhD kama yangu wakati ni feki?”
Mpemba anajibu: “Mie huko siendi. Chukua gazeti weye usome mwenyewe CViii yake uamue.” Anampasia gazeti huku kila mmoja akiwa na mshawasha wa kujua kunani.
“Du! Ukiachia mbali usomi wa mashaka, bi mkubwa alivyopandishwa vyeo si bure. Sorry. Hakupandishwa bali alipaishwa! Ama kweli tunaliwa na kila ajaye!” Anamalizia huku akitikisa kichwa kisha anaendelea: “Hili jamani ni bomu tena la uoza kama sikosei. Kumbe kaya yetu inaliwa na vihiyo wakati wasomi tuko vijiweni!”
Mgosi asiyependa neno kuliwa kulisikia tu anaamua kukwanyua mic: “Hata nawe msomi waiwa siyo?”
Msomi anajibu bila masihara: “Kwani wewe huliwi? Nadhani issue hapa si kuliwa ila kuliwa vipi. Maana hata hao wanaowala wenzao nao wanaliwa au vipi?”
“Mgosi mbona inatifumba. Mie nataka nijue kama unaiwa na anayefanya hivyo ni nani?” “Lisirikali finish!”
Mgosi anaonekana kukubali. Anasema: “Kumbe wanaondoa vihiyo na kuweka mihoyo au ni yale yale ya ondoa kihiyo weka mamihiyo?”
Mie naona wameweka wote. Kwani yule mtoto wa jamaa yake mkuu aitwaye Adamu Milima ya Kigoma si kihiyo anayekwenda kusaidiana na huyu mamihiyo anayesema Ami?” Anachomekea Kapende ambaye alikuwa kimya akisoma gazeti.
Mpemba anajibu: “Kwa huyu binti najua kuna ntu nyuma yake. Hana tofauti na yule mama aliyewahi kuwa waziri wa fwedha aliyepelekwa Marekani kipindi fulani aitwaye Aminia Salimu Alii.”
Mbwa Mwitu anadakia: “Huyo mtu anakaa nyuma yake ili iweje? Akiteleza akaanguka si atamuangukia?”
Wakati mambo ya kula na kuliwa yakiendelea, Kanji anajitia mjuaji kutaka okoa jahazi, anasema: “Sasa somi chukua gazeti, hapana sema nini iko. I know this lady iko na elimu ya fedha sana diyo maana tukufu teua yeye.”
“Wambie mwaya, wamezidisha uzushi hawa,” anachomekea Bi. Sofi aka Kanungaembe.
“Wambea tutawajua Bi. Sofi huna haja ya kutukana watu bila sababu,” anajibu Msomi huku akimpasia gazeti Mchunguliaji ambaye ametumbua mimacho utadhani mbwa kaona nyama.
Mipawa ambaye huwa haziivi na Bi. Sofi anaamua kukatua mic baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu. Anasema: “Hebu wacha niwambiage. Huu mchezo umeota mizizi. Vyuoni tunasikia shahada zikitolewaga kwa rushwa ya ngono. Hata huko nako ni hapa. Hivi hamkumsikia yule muishiwa aliyesemaga kuwa pale mjengoni kila mtu ana mpenzi wake? Mimi naonaga ni hayo hayo hasa ukichukuliaga kuwa ni wale wale.”
Anakunywa kahawa na kuendelea: “Hawa wanaotuitaga wambeya ni wale wale wanaotegemea kubwebwaga na hao hao wabebaji.”
Sofi anamkata mipawa jicho la chuki na kusema: “Taabu ya watu wengine akipata mtu kabebwa. Kwani kosa kubwebwa? Nanyi bebeni wenu mechi droo.”
Mipawa anarejea tena: “Hujakosea kanungaembe. Ila si wote wana tabia za unungaembe. Kwanini kujidhalilishaga kwa ajili ya mambo ya kupita?”
Mzee Maneno naye anaamua kung’ata mic: “Mbona zama za Mchonga upuuzi kama huu haukuwepo?”
Kapende anadandia: “Umemsahau mzee Nchonga nini? Yeye hakupenda mambo ya chini chini wala kuruhusu sirikali yake kufanya hayo. Nani angeona watu wenye kutia shaka wakiteuliwa u-DC kama ilivyo sasa ambapo ukiwaona wengi unajua hapa kimepita kitu?”
“Weweee! Kitu gani hicho na kimepita wapi? Anachomekea Mbwa Mwitu kama kawaida yake.
Mgosi anajibu: “Unauiza jibu. Kinapita hapo hapo kwenye ulaji, unacheza na ulaji nini.”
Baada ya Msomi kuona utani unazidi, anaamua kurejesha mada kwenye mstari. Anachukua gazeti na kusoma: “Hebu tuwe serious. bi mkubwa anasema eti alisomea shahada ya pili bila kutaja chuo. Ajabu eti anasema alipewa cheti badala ya shahada ya pili! Hii inawezekana kweli?”
Mpemba anadandia: “Yakhe hii yawezekana Danganyika tu. Huwaoni wale vihiyo wanaoitwa madaktari wakati ni maamuma watupu?”
“Mie nadhani hata anayewapa ulaji naye ni kihiyo vinginevyo asingefanya hivyo.” Anachomekea Kapende.
“Yakhe washangaa chooni kwanukani!” Mpemba anachomekea huku akiendelea kuangalia picha ya bi mkubwa Saaada kwenye gazeti.
Msomi anaendelea: “Kubwa kuliko pale ni hapa CV yake inaposema eti aliajiriwa mwaka 2006 alikuwa na cheo cha afisa utawala. Huwezi kuamini kuwa ndani ya miaka mitano alishapanda cheo hadi kuwa kamishina wa njuluku wa upande ule! Ama kweli huku ni kupaishwa siyo kupandishwa cheo. Lazima kuwe na namna.”
Mpemba anachomekea: “Si haba bibie nzuri ati. Avutia kiasi cha kuvutia hata vyeo na kuteuliwa haraka haraka.”
“Sasa atakapovutia njuluku msishangae kusikia HEPA nyingine hasa ikizingatiwa kuwa timu aliyonayo inaonekana kuwa hapo kwa ajili hiyo,” anasema Kapende huku akibonyeza iPad yake aliyonunua hivi karibuni kuwakoga wasio nazo. Mambo ni kwenda na wakati.

Kijiwe kikiwa ndiyo kinanoga si likapita shangingi la Mwehu juu Nchembe tukaanza kuzomea na kumsahau Bi. Saaada.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 29, 2014.

No comments: