Wednesday, 29 January 2014

Nenda IGP Mwema na mikono iliyojaa damu


INSPEKTA Jenerali wa zamani wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, amestaafu. Ameacha kiti kinachobubujika damu ya wanyonge.
Ameondoka na mikono iliyojaa damu ya wasio na hatia. Wasio na haki wamemlinda na kumpitisha kimya kimya huku akikabiliwa na tuhuma lukuki za mauaji ya watu wasio na hatia aliopaswa kuwalinda.
Ni ajabu kuwa Mwema ameruhusiwa kustaafu kwa heshima na kufaidi marupurupu na mapochopocho yatokanayo na kodi za wale waliouawa chini ya uongozi wake bila hatia.
Kimsingi hakustahili kufanya hivyo kama historia ya utendaji wake ingetiliwa maanani.
Mwema anaondoka na wingu la kashfa lukuki, moja kubwa ikiwa ni kuzidi kwa mauaji ya raia chini ya uangalizi wake. Ameacha legacy na mfano mbaya wa unyama na ukatili usio na kifani.
Mfano, wengi walidhani Mwema angewajibishwa yalipotokea mauaji mengi ya raia huko Mwanza, Musoma na kwingineko. Lakini hakuwajibishwa.
Hata yalipotokea mauaji ya mwandishi Daud Mwangosi, Septemba 2, 2012, licha ya Mwema kutowajibishwa, hata aliyesimamia mauaji yale, Michael Kamuhanda alipandishwa cheo na kutowajibishwa.
Huu ni ushahidi tosha kuwa Mwema alikuwa akiridhia mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na jeshi lake, huenda chini ya maelekezo yake au wakubwa zake.
Nani mara hii kasahau mauaji ya watu watano kule Arusha kwenye mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mnamo Januari 2011? Nani amesahau utesaji wa Dk. Steven Ulimboka hapo Juni 26, 2012? Nani amesahau hata kusamehe kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda hapo Machi 5, 2013?
Hayo ni machache ya matukio ya jinai yaliyotendwa chini ya uangalizi wa Mwema ambaye matendo yake ni tofauti na kinyume na jina lake.
Hapa hatujagusia matukio ya mauaji yaliyotekelezwa na polisi dhidi ya raia mmoja mmoja kama yale yaliyotokea kule Mara Agosti 29, 2012 kwenye mgodi wa Barrick Nyamongo ambako polisi waliwaua watu wawili, Paulo Sarya ( 26) na Rodcers Nyamboroga (18) kwa kuwapiga risasi na mengine mengi kama hayo.
Sasa tunaambiwa Mwema amestaafu na nafasi yake kuchukuliwa na Ernest Mangu ambaye tungependa ajitenge na utendaji wa kinyama kama huu.
Tunapoandika Mwema ni mstaafu anayekula kuku kutokana na marupurupu ya kustaafu ambayo hakustahili kama nchini mwetu mtu angekuwa analipwa kutokana na stahiki yake.
Je, ni wangapi wameumia au kupoteza maisha na hata wapendwa wao chini ya utawala wa Mwema?
Japo Mwema “amestaafu” kwa amani, ameacha nyuma uchafu mkubwa ambao utamlazimu mrithi wake kufanya kazi ya ziada. Ameacha chuki baina ya wananchi na polisi kutokana na vitendo alivyosimamia vya uvunjaji na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini. Ameondoka na mikono iliyojaa damu ya watu wasio na hatia. Mwema analijua hili vizuri.
Jinamizi la mauaji yaliyofanywa chini yake halitamwacha hata kama watawala wenzake wameamua kumkingia kifua na kumstaafisha kwa amani.
Ukiachia mauaji chini ya Mwema, Jeshi la Polisi lilipata pigo jingine kwa kuwa na sifa ya kuwa kiranja wa rushwa nchini.
Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu cha Dar es Salaam (LHRC) ya mwaka 2011, iliyozinduliwa Mei 28, 2012, Jeshi la Polisi lilikuwa ndiyo kinara wa rushwa nchini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, polisi wanaongoza kwa rushwa kwa asilimia 36.2, wakifuatiwa na mahakama asilimia 32.4, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) asilimia 15.1, hospitali asilimia 8.6, na Wizara ya Ardhi imepewa asilimia 5.3.
Si hilo tu. Polisi wamekuwa wakitajwa kwenye vitendo vingi vya jinai kama vile kushiriki ujambazi, ujangili na jinai nyingine. Rejea kukamatwa hapo Januari 6, 2013 kwa askari David Delina na Gerald Tuti wakitorosha pembe za ndovu.
Japo kila tukio chini ya jua lina funzo, tunajifunza jambo moja toka kwa Mwema kuwa hakuwa mwema kama jina lake.
Tunajifunza kuwa mfumo wetu wa kulindana unazidi kutukwamisha kiasi cha kuwaruzuku watu wanaopaswa kuwa mbele ya mahakama kujibu madai ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu kama ilivyo kwenye sakata la Mwema.
Tunaweza kukubali kuzidiwa nguvu na wenye nguvu. Tunaweza kusamehe hata kwa kulazimika, lakini hatutasahau wala kushangilia wala kushabikia uoza na uovu huu.
Nenda Mwena japo bado kuna maswali mengi kuhusiana na mustakabali wako na utendaji wako. Unaweza kujiridhisha kuwa umestaafu ukiwa huna hatia mbele ya sheria, mioyoni mwa waathirika wengi wewe ni mtu wa kupaswa kushtakiwa.
Laiti ungewajibishwa hata kwa kulazimishwa kujiuzulu kama wengi walivyotaka, hasa baada ya kugundulika madudu ya uvunjwaji na ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili sambamba na mawaziri husika, lakini haikuwa haikuwa hivyo.
Hata hivyo, binadamu ni nini? Tutazidi kuomba Mwenyezi Mungu asiyependelea atende haki kwa niaba ya waathirika. Tunawaombea waathirika wa kazi ya mikono yako nafuu toka kwa Mwenyezi Mungu tunayemkabidhi kesi yao baada ya wenye madaraka wenzio kutuhujumu kwa kukulinda kana kwamba ulikuwa ukiamrisha mauaji ya kuku.
Kwa ufupi ni kwamba Mwema kaa ukijua kuwa umeondoka na mikono iliyojaa damu ya watu wasio na hatia. Hata huyo anayerithi nafasi yako anapaswa aipige deki sana ofisi hiyo na kubadili kiti chako kilicholoa kwa damu ya watu wetu.
Nenda Mwema na legacy ya mauaji na uvunjaji wa haki za binadamu. Sina la ziada la kusema zaidi ya kuzidi kumuomba Mwenyezi Mungu awalipie wahanga wako.
Yeye ni mwema na mwenye kutenda haki. Sina shaka haki itatendeka kwako kama ilivyotendeka kwa mtangulizi wako aliyestaafu na kuishia kukumbwa na kashfa moja baada ya nyingine.

Isipokuwa basi tutajifariji kwa maneno ya Marcus Tullius Cicero, mwanafalsafa wa Kirumi aliyesema; “Amicitiae nostrae memoriam spero sempiternam fore – Nataraji kumbukumbu za marafiki zetu zitaishi milele. Namalizia, Juu ya uovu wako.
Chanzo: Tanzania Daima Jan., 29, 2014.

No comments: