Thursday, 30 January 2014

Urais: Tuwakatae watoto wa vigogo

 
          Taarifa ambazo hazijakanushwa naibu waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Yusuf Makamba anajipigia debe kugombea urais haziwezi kupita bila kujdaliwa. Taarifa zilizokaririwa na vyombo mbali mbali ni kwamba Makamba ana mpango wa kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao wa 2015. Wengi wanajiuliza Makamba ana sifa gani zaidi ya jina la baba yake ambalo nalo linahusishwa na ufisadi, kujuana, kurithishana madaraka na propaganda tu? Kwa umri alionao na historia yake ya kuingia kwenye siasa kupitia mgongo wa baba yake, sijui kama January ana jingine la mno. Je watanzania wataendelea kubariki utawala wa kifamilia ambapo kila anayepata nafasi serikalini uhakikisha anamrithisha mtoto wake au jamaa yake? Hii ni jinai hata kama imezoeleka na kuanza kukubalika. Hii ni hujuma kwa watanzania wasio na majina makubwa wala mjomba wa kuwabeba ili waingie katika ulaji wa kula kwa mikono miwili tena bila kunawa wala kuona aibu. Ni aina mpya ya ufisadi wa kimfumo inayolenga kuiteka nchi na kuigeuza shamba la bibi la baadhi ya koo zenye majina makubwa.
          Hii si mara ya kwanza wala ya mwisho kuongelea suala hili. Leo utasikia akitajwa Makamba. Kesho utasikia Nchimbi. Kesho kutwa utasikia akitajwa Mwinyi na kadhalika. Namna hii nchi haiwezi kuendelea kwa vile wahusika wanajuana na kulindana ukiachia mbali kulipana fadhila. Tusiruhusu Tanzania kufikia kuwa nchi ya hovyo kama zile ambapo rais anamteua mkewe kuwa waziri huku akimuandaa mwanae kumrithi.  Tuondokane na taifa ambalo kila aliye karibu na mkubwa naye ni mkubwa.
          Je watanzania wataingia mkenge kama Kenya ambao walichagua jina la mwanzilishi wa taifa hilo kwa sababu ya kikabila? Je Makamba anataka kuingia kwenye orodha ya watoto wa vigogo waliopata madaraka simply because baba zao walikuwa wazito kama vile Aman Abeid Karume, Ian Khama, Faure Gnassingbe Eyadema (Togo), Joseph Laurent Kabila (DRC) na Ali Omar Bongo (Gabon).
          Je Makamba hajaridhika na ulaji kwenye kundi lake la wateule watoto wa vigogo la akina Emanuel John Nchimbi, Dk. Husein Ali Hassan Mwinyi, Adam Malima, Mbaraka Abudulwakil, Vita Kawawa, na Zainab Kawawa ukiachia wale waliotamalaki kwenye balozi zetu huko nje?
          Hapa hujawataja wakuu au waliowahi kuwa wakuu wa wilaya watokanao na koo za vigogo kama vile Gerald J. Guninita,Paul Mzindakaya,Festo Kiswaga, Khanifa M. Karamagi, Husna Mwilima, John V. K. Mongella, John B. Henjewele, na Agnes Hokororo.
          Hata ukienda kwenye ofisi nyingine za ulaji wapo kama vile Dk. Hawa Rashidi Kawawa (Mganga Mkuu Msaidizi wa Jiji la Dar es Salaam), Dk. Guni Kate Kamba (Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni), Dk. Asha Omar Mahita – (Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala) na Dk. Amani Kighoma Malima (Mganga Mfadhiwi wa Hospitali ya Temeke).
Ndani ya CCM wapo Ridhiwan Kikwete, Dickson Membe, Freddy Lowassa, Ashura Hussein Mwinyi, Ben Samuel Sitta, Deborah Mwandosya, Irene Pinda, Felister Ndugai, Christopher Ndejembi, Sharifa Bilal, Hawa Kigoda, Judith Mukama, Jerome Msekwa, Mboni Mhita na wengine wengi.
Benki kuu nako hawakosi. Wapo wakihomola na kulinda maslahi fichi ya baba zao. Wapo Salama Ali Hassan Mwinyi, Filbert Tluway Sumaye, Zaria Rashid Kawawa, Blasia William Mkapa, Jerriet Marten Lumbanga, Pamela Edward Lowassa, Rachel Muganda mtoto wa mke wa Daudi Balali aliyeliingiza taifa hasara ya mabilioni ya EPA na aliyekuwa gavana wa Benki Kuu,Salma Omary Mahita,Justine Mungai,Kenneth Nchimbi,Violet Philemon Luhanjo,Liku Kate Kamba,Thomas Mongela na Jabir Abdallah Kigoda. Ni uroho na roho mbaya kiasi gani? Hapa hatujataja walioko kwenye taasisi nyeti kama vile TRA, Ubalozini, Mambo ya Nchi za Nje, Viwanda, Hazina, Uhamiaji, Mizani, na kwingineko kwenhye maslahi manono. Kimsingi, kinachofanyika, ni kwa watawala wa sasa na waliopita kuwaandalia watoto wao na jamaa zao kuendelea kutawala hata baada ya wao kuondoka. Hapa ndipo utawala wa kifalme usio rasmi na kuwalindana unapotengenezwa mchana kweupe huku watanzania wakiendelea kuwaamini kuwa wapo kuwakomboa wasijue wapo kuwakomoa na kujikomboa wao binafsi na koo zao. Huwezi kuwa na kujuana kwa namna hii ukashindwa kuwa nchi ya kifisadi nay a kiukoo (nepotic and clannish country). Huwezi kuliepuka hili hata kidogo.
 Nadhani watanzania wamechoka na utawala wa kurithishana iwe ni serikalini au chamanni. Je hawa watoto wasio na majina mazito watatawala lini nao? Je Tanzania ni nchi ya kifalme chini ya ufalme wa vigogo wa Chama Cha Mapinduzi na serikali yake? Tufikie mahali tuambiane ukweli kuwa kuna haja ya kuwakataa watoto wa vigogo ambao kimsingi wanataka kuendeleza utawala wa familia na mawazo mgando yale yale na sera za kujuana na kulipana fadhila.
          Japo Makamba kama mtanzania yeyote anayo haki ya kugombea uongozi ngazi yoyote, ukiangalia historia na uzoefu wake, unashangaa sifa atazipata wapi zaidi ya jina la baba yake.  Ukiangalia hata jinsi alivyopata elimu yake ya sekondari kuna mazabe. Ningependa kusikia siku moja akijitetea kuhusiana na tuhuma kuwa alinunua jina la mchovu ili kuweza kusoma kidato cha tano na sita. Kama ni kweli alifanya hivi, huyu anaweza kufaa kuwa rais? Akipata urais atawanunua wangapi? Bahati mbaya watawala wetu wanapokabiliwa na kashfa na tuhuma kama hizi huwa wanakaa kimya ili zijifie wasijue kuna watu wasiosahau.
          Tuhitimishe kwa kuwashauri watanzania kuwa macho na watu wanaotumia majina ya baba au mama zao kuusaka uongozi. Tuwafichue, kuwazodoa na kuwaambia fika kuwa hawatufai. Kama wanafaa basi wanafaa kuondolewa kwenye nyadhifa walizozipata kutokana na ukubwa wa majina ya wazazi wao au mitandao ya kujuana ya kiulaji iliyotamalaki nchini. Inatosha basi kumwambia mtu kama Makamba kuwa hana sifa za kuweza kugombea achia mbali kuwa rais wa Tanzania. Walichokula kinatosha. Tuwaachie wengine wenye uchungu na uwezo wasimame lakini si wachovu wanaojificha nyuma ya umaarufu na mitandao ya wazazi wao.

2 comments:

Anonymous said...

Monarchy State!!!?

NN Mhango said...

Nicely put Anon. Bravo.