Tuesday, 14 October 2014

Hongera Othman kufichua janja ya Shein


 
Japo kukosea ni jambo la kawaida kwa binadamu, makosa mengine yanaweza kuwa na matokeo yenye madhara makubwa kwa mhusika au tuseme mwenye kufanya makosa. Hakuna kosa watakalojutia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na hata marais Jakaya Kikwete na Dk Ali Mohamed Shein kama kumfukuza kazi aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Zanzibar (AG) Othman Masood Othman baada ya kukataa kutumiwa kama nepi na kudhoofisha ofisi na taaluma yake. Kitendo hiki kitawagharimu kwa kiwango ambacho hawakutarajia.
Tofauti na wanasheria nyemelezi wanaotumiwa kama nepi tuliozoea kusikia wakitetea uoza ili waendelee kula kutoka humo, Othman amesimama kidete kutetea haki, katiba, taaluma n ahata watu wake japo si mwanasiasa. Amethibitisha usomi wake ambao ni ukombozi uliomtenga na kutumikia tumbo huku akidhalilika na kuumia. Heri amefukuzwa akiwa na nafsi na dhamira safi kuliko wale wanaoendelea kukaa maofisini kufanya mambo machafu ambayo hata akili zao hazikubaliani nayo zaidi ya njaa zao. Nadhani licha ya kustahili pongezi, Othman anaondoka kishujaa na kwa heshima.
Othman amekataa ukuku na kukumbatia ukanga ambapo kuku hula na kushiba na kulala kwenye banda safi lakini bado akabakia kuwa mfugo tofauti na kanga alaye kidogo lakini akayaweka majaliwa yake mikononi mwake na muumba wake tofauti na kuku ambaye majaliwa yake yako mikononi mwa kiumbe mchafu aitwaye binadamu.
Je ni kwanini waliofukuza Othman watajutia?
Kwanza, kufukuzwa kwake kumefichua msimamo dhaifu wa Shein tokana na ukweli kuwa kumbe kwenye mjadala wa kuandika katiba mpya Zanzibar haikuwa na msimamo wala mtetezi. Je Shein yuko ofisini akilipwa kwa lipi iwapo ameshindwa kutetea maslahi ya taifa la Zanzibar? Je msimamo na tabia ya Shein si ushahidi kuwa amepachikwa pale kama nyampara wa kuwachunga wazanzibari kufuata matakwa ya Dodoma alikotengenezwa? Je wazanzibari watakubali kuwa na kiongozi asiyelinda maslahi yao? Je Shein alinyamazishwa au aliamua kufuata msimamo wa chama akijua fika kuwa bila nguvu ya Dodoma urais wake unakuwa mashakani?
Nadhani kama kuna anayechekelea sasa mbali na Othman si mwingine bali Maalim Seif na CUF ambao bila shaka wamepata hoja nzito na yenye mashiko kwenye kampeni za mwakani.  Je CCM wameliona hili hivyo au walichukua uamuzi kwa hasira wasijue hasira hasara? Je kwa kufichuka ukweli huu kuwa Katiba ya CCM waliyopitisha hivi karibuni baada ya kuchakachua kura haina maslahi na Zanzibar wazanzibari watakaa kimya sawa na wenzao wa bara wenye historia ya ukondoo na kutojali? Je kama wazanzibari wataamua kuungana na CUF kuzuia kufanyiwa hujuma kama ile ya mwaka 2001 CCM na serikali yake itatuma jeshi jingine kuua tena na kuzalisha wakimbizi wengine au kuacha Shein alipie ukimya wake?
Kimsingi, hali hii ni tete na haina jibu moja rahisi. Kinachofurahisha ni kwamba, baada ya rais Kikwete kuwasaliti na kuwazunguka UKAWA akidhani yamekwisha, amepata kikwazokingine ambacho sidhani kama CCM wana watu makini wa kuweza kuwasaidia kukivuka kwa kuwashawishi wazanzibari ambao wameishachoka kutenzwa kama mkoa ndani ya muungano tata wa sasa chini ya katiba tata ya sasa.
Kitu kingine kitakachofanya CCM wajutie ni ukweli kuwa Othman sasa ni mtu huru anayeweza hata kuamua kujiunga na upinzani na kushiriki siasa. Hili likiongezea na sintofahamu baina ya Shein na mtangulizi wake Amani Karume ambaye shemeji yake anakabiliwa na mashtaka ya ajabu ajabu, uwezekano wa upinzani kuwa na nguvu Zanzibar zaidi ya wakati wowote ni mkubwa. Utashindwaje kuwa na nguvu wakati hawa wote watatu adui yao ni mmoja? Lazima wataungana kumkabili na kuzuia asiendelee kuwanyanyasa.
Hili likichanganyikana na ukweli kuwa CCM imegawanyika hasa kipindi hiki inapoisha awamu moja kwenda nyingine, uwezekano wa kutokuwa na mafuta ya kutosha kiakili hata kimkakati kuzuia nguvu ya Zanzibar ni mkubwa. Hapa bila shaka kila mtu atakufa au kupona kivyake hasa ikizingatiwa kuwa rais anayeondoka hana ushawishi wala kipawa cha kufanya hivyo ukiachia mbali kuacha kila mmoja kwenye chama ajifanyie atakavyo huku yeye akiangalia tokana na historia yake ya kutokuwa na udhu.
Kwa sasa CCM ina mitandao inayoviziana na kutishiana uhai huku na uchakachuaji wa katiba ukizidi kuiweka pabaya. Kwa Zanzibar ukiongezea na kufumka kwa ukweli kuwa kumbe kwenye mjadala wa kuandika katiba mpya waliuzwa, bila shaka hakutakalika.  Hivyo, si vibaya kusema kuwa kishindo cha kutimliwa Othman na yale aliyofichua vitaiweka CCM pabaya kuliko ilipowahi kuwa. Ukiongozea na tuhuma za ufisadi wa ESCROW unaoendelea kuitafuna hasa baada ya wafadhili kutishia kugoma kuchangia kapu lake, ndiyo basi tena. Kwa bara wanaweza kufanya mizengwe na ulaghai wao.
Kwa Zanzibar, sitegemei umma uwaruhusu hasa ikizingatiwa kuwa hawakuhusishwa kwenye katiba inayopaswa kuwatawala bila kusuluhisha migongano baina yake na katiba ya Zanzibar. Je tujiandae kumuaga Shein na kukaribisha upinzani au kushuhudia vurugu? La vurugu na mauaji kama ya 2001 ondoa hasa ikizingatiwa kuwa watawala wengi wa Afrika wanaogopa kupelekwa The Hague.
 Hongera Othman. Kufichua hila na jama dhidi ya wazanzibari. Kwani msimamo, ujasiri na ushujaa wako unaweza kuwa nyenzo mojawapo ya kuiangusha katiba kidhabi waliyopitisha kwa maslahi yao. Je Wanzanzibari watagoma kushiriki zoezi ambalo limeishachakachuliwa hata kabla ya kuanza?
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 15, 2014.

No comments: