Tuesday, 21 October 2014

Makamba anapomchimba Kikwete

NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Januari Makamba, mtoto wa Katibu Mkuu wa zamani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba aliyemtabiri angeteuliwa kuwa waziri, aliwaacha Watanzania hoi kwa kuonesha utoto na uhovyo wake.
Alikaririwa akisema, “Kiongozi anayetumia fedha kununua uongozi hawezi kupambana na rushwa hawezi kuleta mabadiliko ya aina yoyote katika nchi hii”. Je, Makamba anamlenga nani zaidi ya Jakaya Kikwete, japo hajawahi kukiri au kukanusha, ila ndiye aliyetuhumiwa kuingia madarakani kwa kununua wapiga kura kwa fedha ya EPA iliyoibwa toka Benki kuu?
Je ni kwanini Makamba ameliona hili au ni kwa vile hana fedha za kutosha kuhonga katika mbio zake za urais? Japo kiongozi aliyepatikana kwa rushwa na kuibia umma hafai, hata hawa wanaoona hili kama tatizo kwa sasa wakati walikuwa na nafasi ya kuliongelea zamani hawafai pia.
Je, Makamba ameishiwa hoja? Maana gia yake kubwa ilikuwa ni ujana bila kujali kama mhusika ni fisadi wala nini.
Makamba hakuishia kwa mtu binafsi bali hata mfumo mzima unaoelea uoza ingawa naye ni tunda na matokeo ya mfumo huo huo anaoushambulia kwa sasa kama janja ya kutaka aonekane mwana mapinduzi wakati siye.
Alisema, “Kama mfumo wa uchaguzi unaingiza viongozi kwa rushwa au viongozi waliowahi kula rushwa, tusahau kabisa nchi hii kuondokana na rushwa. Hapo ni pa kupafanyia kazi sana.” Je, aliyebariki jinai hii zaidi ya chama chake ni nani?
Hivi kweli anaweza kutoka mtu yoyote ndani ya CCM akafanya tofauti na mazoea yaliyoiweka madarakani miaka yote tena kinyume na utashi wa wapiga kura na wananchi? Rejea ambavyo imekuwa ikichakachua kila uchaguzi tangu kuingia mfumo wa vyama vingi.
Je, Makamba ameyasema hayo ndani ya chama akapuuziwa akaamua kumwaga mtama au ni ile hali ya kutaka kujipatia umaarufu kwa kujionyesha kama mtu anayepiga vita rushwa wakati yeye ni matokeo ya mfumo ule ule?
Je, Makamba ameanza kuunda mtandao wake unaojifanya kuwa tofauti na chama kama alivyojaribu Samuel Sitta akaangukia pua? Sijui kama konokono anaweza kukana gamba lake akaishi.
Makamba ni tunda na kizalia cha mfumo huu anaoushambulia. Anaweza kuukana. Ila bado hataukimbia kwa vile uko kwenye damu yake. Angekuwa anataka kueleweka, basi angejitoa CCM kwanza.
Je, January angeweza kuyasema haya wakati baba yake akiwa madarakani akimuandalia nafasi ambayo aliipata kama baba yake alivyotabiri wakati akijivuna kuwa amezaa watoto wenye akili?
Makamba alizidi kuonyesha kuwa anayajua mengi ingawa wengi wanaona kama amechelewa kiasi cha kuuliza: Kwanini anayesema sasa na si siku za nyuma kama kweli ana nia njema.
Alisema, “Kuna wizi na ubadhilifu mkubwa siyo tu kwa viongozi wa kisiasa, hasa kwa watendaji na watumishi wa kada za kati na chini. Watu wanawatizama wabunge na waziri pekee wakati wapo wahasibu wa wizara na halmashauri.” Zaidi ya chama chake, nani anawalinda wabadhirifu hawa?
Nani amesahau kashfa ya uuzaji wa madawa feki inayomkabili  mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Dar es Salaam Ramadhani Madabida, anayeendelea kukaa ofisini pamoja na tuhuma nzito kama hizi?
Makamba aliongelea sifa za anayepaswa kuwa rais ajaye. Alisema,“Awe na uwezo wa kuwaunganisha Watanzania kwa sababu kama mnavyoona chembechembe za mgawanyiko zimeanza, mgawanyiko kati ya Tanzania bara na Tanzania Visiwani, mgawanyiko wa kidini na kikanda.”
Inashangaza Makamba kuongelea mgawanyiko wakati chama chake kimeuridhia kwa kuchakachua rasimu ya wananchi. Je, ina maana kuwa Rais Kikwete ameshindwa kuwaunganisha watanzania kiasi cha waziri wake kulalamika?
Kauli ya Makamba inaonyesha hata mgawanyiko ndani ya serikali ambapo waziri anaweza kumnanga bosi wake wakati ana uwezo wa kukutana naye akaeleza maoni yake au hiyo nafasi hawapewi?
Je, Makamba anataka nani abebeshwe mzigo wa hizi tuhuma zote ambazo zinaonyesha wazi kuwa mambo si sawa zaidi ya Kikwete? Je, Makamba anaanza kujitofautisha na Kikwete baada ya kugundua kuwa muda wake wa urais umekwisha?  Kwanini alingoja saa ya lala salama kama kweli ni mtu makini na wa kupaswa kuaminiwa?
Kwa wanaojua madudu yaliyofanyika chini ya utawala wa Kikwete, hawashangai madai ya Makamba zaidi ya anayemlenga. Bila shaka hapa anayelengwa si mwingine bali Rais Kikwete.
Je, Kikwete atayachukuliaje madai haya ya waziri wake ambaye alipaswa kuyatoa kwenye vikao vya chama? Je, wakati wa kila mtu kufa kivyake umefika ambapo marafiki watakanana na kuumbuana kama alivyoanzisha Makamba?
Kweli ulaji tena wa dezo mtamu kweli! Nani alitegemea watu kama Makamba waugeuke mfumo uliwaumba na kuwafikisha pale walipo. Je, wanadhani kuwa watanzania wamesahau historia zao na matendo yao? Je, watanzania ni wepesi wa kusahau hivi?
Ni raha namna gani Makamba anapomchimba Kikwete akitegemea kumrithi. Je, Kikwete atamsamehe kwa kosa hili? Yetu macho. Muhimu ni kuwaasa watanzania wasihadaike na maneno mazuri. Wakumbuke kuwa hata nyoka husifika kwa kuimba nyimbo nzuri kuwavutia wadudu ambao hatima yao ni kugeuzwa kitoweo.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 22, 2014.

2 comments:

Anonymous said...

Pinda naye anataka
Afya yake spana mkononi
Janja yenu CCM tushaijuwa mnataka UKAWA tutawanyike hamtupati ngo 2015 mwisho wenu mkichakachuwa hapakaliki bongo

NN Mhango said...

Anon omba wenye ugogoro wa afya wapukutike ndipo tupate rais anayefaa badala ya hawa spana mkononi kiafya na kimaadili.