Friday, 17 October 2014

Katiba-chakachuliwa ikipitishwa najinyonga


          Uhuru wa kufanya unavyotaka ilmradi usivunje sheria ni haki kidemokrasia. Japo kujiua ni kosa la jinai, ni pekee kwa walio hai. Hivyo, kwa vile waliochakachua rasmu ya jaji Jose Warioba wanasema wamefanya hivyo kwa misingi ya kidemokrasia basi nami natumia misingi hiyo hiyo kujinyonga kama katiba yao itapita. Siko tayari kufa kwa ugonjwa wa moyo hivi hivi. Heri nawaachie wenye nchi yao wawafanyie watakavyo waliojiruhusu kufanyiwa kila upuuzi na ushenzi. Mie ni muungwana na lazima nife kiungwana kwa kujitia kitanzi kama Mkwawa.
          Hata hivyo, kama mwamko na wimbi la kupiga kura ya hapana vilivyoonyeshwa na baadhi ya mashujaa wa  katiba vingeendelea na kuipiga chini hii rasimu habithi, huenda waja hawa wageokoa maisha yangu sawa na yale ya vizazi vijavyo, kwa kukataa hujuma na jinai ya kutubambikia katiba inayolenga kulinda maslahi ya kikundi kidogo cha watu tena wasio na huruma. Wakitishwa au kupewa ulabu wakabadili msimamo wajue wameniua.
Naona yule anatikisa kichwa akidhani bangi ishanibangua kiasi cha kuongea kibangi na kigongogongo. Shauri yako! Mie ni shujaa asiyeogopa kifo. Naogopa aibu kuliko kifo. Hivyo, we kaa ukidhani ni bangi na gongo wakati nafanya kweli. Heri mie anayejinyonga kuliko nyinyi mnaonyongwa na kuishi kama punda vihongwe na watumwa. Hata hao wanaowatumikisha na kuwaibia nao ni watumwa wa hayo wanayofanya. Heri nijinyonge kuliko kuliwa na mafisadi utadhani mie samaki au ujaka.
          Nina sababu za kufanya hivyo:
          Mosi, mawazo na utashi wangu vimedharauliwa na kutupiliwa mbali. Nikikumbuka nilivyokesha na kusafiri kwa punda kwenda wilayani kutoa maoni nasikia kichefu chefu. Iweje niingizwe gharama kusafiri mwendo mrefu hivyo tena kwa mateso nitoe mawazo yadharauliwe?
          Kwa vile nina hasira na ufisadi ambao nilidhani katiba mpya ingepambana nao badala ya kuupamba kama ilivyo, nahofia nisipojinyongwa wataninyonga hasa baada ya kumtoa fisadi roho kwa mapanga na marungu. Hivyo, heri nijimalize mwenyewe.
Tatu, niliwashawishi walevi tulianzishe wakagwaya wakijuruhusu kuliwa na kufanyiwa mahepe na kugeuzwa asusa kana kwamba mtoto si riziki. Hivyo, kwa kuogopa aibu hii lazima nijinyotoe roho na kuwaachi amauza uza yao ya kuibiana na kulana kama ilivyo.  Kama waliochakachua katiba hawakuogopa kuua vizazi vijavyo, nikijiua mlevi kama mimi nani anajali? Sana sana wabaya wangu wanaosoma madude yangu yakawaita jokomoyo watasherehekea kuwa hakuna mlevi na mvuta bangi wa kuwapigia kelele na kuwaghasi kwa mauzauza wanayofanya mchana kweupe tena watu wazima ambao usingetemea kuwa wangekuwa hovyo hivi.
Wabaya zangu msikonde. Kama upuuzi huu ninaoona na kutamani kumtoa mtu roho utaendelea mie sishiriki wala kushuhudia wala kuuabudia na kuruhusu upite kwa kutumia jina langu safi. Heri nijifie kwa heshima kuliko kuishi kwa aibu. Heri kulala kaburini kuliko kutembea kwenye kaya ya dhuluma na hujuma huku nikigeuzwa punda kihongwe. Heri nioze na kuliwa na wadudu kuliko kuliwa na mafisadi. Heri nimwachia bi mkubwa wangu majonzi ya kunikosa kuliko mimi kukosa heshima na haki katika kaya yangu. Hivyo, natoa taarifa rasimi kuwa kuna wakati mnaniona na kuna wakati hamtaniona.
Wenye kusherehekea mauti ya wenzenu sherehekeeni utadhani nanyi hamtakufa.  Mnadhani ni mchezo? Ipo siku nanyi mtakufa tu. Maana imeandikwa, “Kullu nafsin zallikat umaut.” Naona yule anacheka asijue mie bonge ya shehe. Hayo tuyaache. Japo mnaweza kudhani natania, hebu jiulizeni. Wamekufa watu wema kama Madiba na mzee Mchonga itakuwa nyinyi mahabithi na mabaradhuli ambao hata shetani akiwaona kutokana na wingi na ukubwa madhambi yenu huenda atawakataa. tokana na uchafu wenu. Wamekufa watu na utauwa wao itakuwa nyie mnaochakachua hata utashi na mawazo ya wenzenu kulinda aibu na tamaa zenu? Heri mie ninayejinyonga kwa kutetea haki kuliko wale wanaoishi kufanya na kuunga mkono au kuuvumilia uovu. Heri ya mlevi na mvuta bangi mwenye mapenzi na taifa lake kuliko kiongozi mwenye kuliteketeza kwa tamaa upogo na roho mbaya vyake. Heri ya mlevi mwenye kulaumu kuliko wapumbavu wawasifuo watesi wao. Kwani hamkuambiwa kuwa cha mjinga huliwa na mwelevu wakati cha juha na bunga huliwa na mjinga.
Sitaki wale mabingwa wa kushambulia vyombo vya habari kuwa vinawachukia vinapokosa jinai yao waanze kunishambulia. Sifi kwa vile nina hila wala chuki na katiba zaidi ya ilivyopatikana na yale inayosimamia ambayo ni kunila mimi kama ujaka na changu. Katiba ya walevi lazima ifanane na kutungwa nao. Katiba ya walevi haina gharama za kulipana mabilioni wala kuiba mengine ki-Escrow ili kutunisha mfuko wa uchakachuaji na uhongaji. Katiba ya walevi hupitishwa baa bila kuhitaji miezi ya kulipana mabilioni. Katiba ya walevi ni nafuu kuliko hata maji. Kwani unawapa michupa kidogo wanakutana chap chap na kuja kitu kinachoingia akilini. Ukiwapa pombe na bangi nyingi nao wanaweza kuvuta muda ili wapate zaidi sawa na hawa waliopoteza muda mwingi kwenye mipasho ili bora liende wapate mshiko. Wanadhani hatukumbuki hujuma hii kwa walevi? Tunajua sema tunawalimbika tu.
Siko tayari kuishi na kutawaliwa na katiba iliyopatikana kwa ghilba na laghba ili kulinda ufisadi ulafi na kila aina ya jinai.  Siko tayari kuramba matapishi yangu kama Ali Kesi aliyekandia Katiba feki akaishia kuipigia kura. Nani anayetaka kutawaliwa na katiba ambayo imepatikana kwa njia haramu na chafu na kupuuzia mawazo ya walevi? Mie japo nina roho ngumu, siyo kama hawa wanaoweza kutumiwa kwa ahadi uchwara na zisitekelezwe wasijue wanaowaita na kuongea nao walikuwa wakivuta muda ili madude yao yapite.
Kabla sijafa naacha wosia. Nimemwambia bi mkubwa ashiriki kwenye kura yoyote ya kupitisha vitu vilivyosababisha kifo cha mumewe. Nichukue fursa hii kuwaasa walevi wasishiriki. Wakikaidi wakashiriki kitakachowakubwa wasinikumbuke wala kunililia wala kulalamika. Salamu za leo ni kwa wanafunzi wangu wa Kinondoni, Biafra na kwingineko.
CHANZO: NIPASHE

No comments: