Tuesday, 7 October 2014

Tukatae katiba ya kifisadi

Hali ilivyo, na mambo yanavyokwenda, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama nyemelezi na washirika zake wamepania kutubambikia katiba. Hili halikubaliki na halipaswi kukubalika wala kuvumilika. Katiba ni mkataba wa kudumu baina ya watawala na watawaliwa unaolenga kuonyesha jinsi ya kutawala na kutawaliwa. Uzoefu unaonyesha kuwa katiba viraka ya zamani imetumiwa na genge la watu kulihujumu taifa bila kushitakiwa.  Watanzania wakiendelea na ujinga, ukimya, woga na kutojali wataendelea kuumizwa. Hili nalo halikubaliki.
          Ili kujinasua na jinai hii ambayo walaji wetu wanapania kutenda, lazima umma usimame na kuizuia.  Ni bahati mbaya. Wananchi wamewaachia wanasiasa kazi ya kupinga jinai jambo ambalo linafanya mapambano kuwa magumu. Kuendelea kuwa watazamaji na mashahidi wa uovu huu ni kujiruhusu kuhujumiwa si sisi tu bali na vizazi vijavyo. Jamii yoyote yenye watu wanaofikiri sawasawa isingeacha kikundi kisicho na uhalali wowote, kimantiki na kisheria, kujitwisha jukumu la kuandika katiba ya watu yao. Nani kawapa madaraka ya kufanya hivyo? Jibu ni rahisi. Wamepora madaraka na kuteka mstakabali wa taifa. Wanasema kuwa katiba inayopendekezwa huko Dodoma ni aslimia 75. Hizo aslimia 25 zimekwenda wapi? Andrew Chenge Mwenyekiti wa Kamati bandia ya Uandishi ya Bunge la Katiba, alikaririwa akisema, “Bunge hili limeboresha Rasimu ya Katiba vizuri sana. Rasimu hii imebeba asilimia 75 ya maudhui ya Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba (Joseph) na nyie wajumbe mmeboresha kwa asilimia 25 tu.” Huku “kuboreshwa” kunamaanisha nini wakati hayo maboresho si mawazo ya wananchi? Je hawa walioondoa haya maoni na utashi wa wananchi kweli wanaweza kuboresha kitu au kuboronga? Bila shaka jibu ni kuboronga. Je jamii inayojiruhusu kuhujumiwa na kutekwa na kikundi kidogo cha watu ni hai kweli? Tunashindwa nini kuwaambia tena kwa sauti moja kuwa inatosha? Sidhani kama hili nalo linahitaji wafadhili au msaada toka nje.
          Kwa kujiruhusu kuchezewa sisi na mstakabali wetu hivi, tumeonyesha udhaifu mkubwa kiasi cha nchi nyingine kutucheka. Tumezidiwa na hata viinchi vidogo kama Hong Kong ambao wamekatalia mizengwe ya taifa kubwa, China? Tumezidiwa na majirani zetu wa Kenya waliofanyiwa mizengwe wakakataa kata kata hata kwa kutishia kufanya nchi isitawalike? Watawala wetu ni ving’ang’anizi. Hawajui lugha ya majadiliano. Yako wapi matunda  ya majadiliano na makubaliano ya hivi karibuni baina ya rais Jakaya Kikwete na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA)? Aliwaita na kuwahadaa ilia pate muda wa kuendeleza jinai hii. UKAWA wametimiza jukumu lao. Je wananchi wamefanya nini kuwaunga mkono?
          Wapo wanaojidanganya kuwashawishi wananchi wapige kura ya hapana kupinga kupitishwa katiba hii feki. Uzoefu unaonyesha kuwa CCM imekuwa ikiiba kura (kuchakachua). Tukifanya kosa kuruhusu hichi kiini macho ilichotengeneza CCM na kukiita katiba ya wananchi, tutajilaumu na kujuta. Watashindwaje kuchakachua, kama kawaida yao, ilhali tume itakayosimamia kura ya maoni ni ile ile iliyobariki uchakachuaji? Watashindwaje iwapo polisi na vyombo vyote vya ulinzi na usalama ni washirika wakuu wa jinai hii kwa umma? Tuguswe wapi kama jamii ndipo tustuke? Tufanyiwe maudhi kiasi gani tustuke?
          Kwa tuliosoma rasimu ya tume ya Kukusanya na Kuratibu Maoni ya Jaji Joseph Warioba (CRC), tulijiridhisha: Katiba iliyokusudiwa baada ya kukusanya maoni ya wananchi ilikuwa ya kimapinduzi na ya umma. Ilionyesha nia ya wazi ya kupambana na ufisadi uliotamalaki kiasi cha kuanza kuhalalishwa na watawala wanaoufanya na kunufaika nao. Hili liliwaudhi na kuwatisha watawala. Wapo waliohofia kusimamishwa mahakamani kujibu mashtaka ya hujuma na ufisadi waliofanya wakiwa madarakani. Wapo walioona kama mipango yao ya kupora madaraka imevurugwa. Hivyo, kwa pamoja, chini ya CCM, waliamua kuhujumu rasimu ya Warioba huku wakimtisha na kumshambulia asitishike wala kutetereka. Bahati mbaya, Warioba hajaungwa mkono vilivyo. Wametumia fedha na muda wetu kufanya mambo ya ajabu katika karne ya 21 nasi tunaendelea kujifanya kama hayatuhusu!
          Ajabu, umma unapoendelea kujifanya hahuhusiki, utakuwa wa kwanza kulalamika kama katiba hii feki itapitishwa! Kwanini kungoja majuto kuwa mjukuu ilhali ipo kila fursa ya kupinga dhuluma na jinai hii? Tunaogopa nini iwapo tumeshuhudia nchi nyingine umma ukiingia mitaani na kuzuia jinai kama hii tunayotendewa? Je sisi ni kisiwa au kuna tatizo katika mkusanyiko unaoitwa Tanzania?
Je ni kwanini watawala wetu hawajali? Aliwahi kusema Earl Derr Bingers, “Careless shepherd make excellent dinner for wolf.” Yaani mchungaji asiyejali hugeneza kitoweo kizuri kwa mbwa mwitu.
Je ni kwanini umma wetu haujali? Imesemwa, “When is a revival needed? When carelessness and unconcern keep the people asleep,” Billy Ashley Sunday (1862-1935), mwanariadha maarufu na mwinjilisti wa kimarekani aliwahi kusema. Yaani, uamsho unahitajika pale kutojali kunapowafanya watu walale. Je watanzania hatujalala? Tuamke basi. Kuna kila sababu ya kukataa katiba feki nay a kifisadi iliyoandikwa na CCM. Tuna kila sababu na uwezo wa kufanya hivyo. Sana sana hatuna cha kupoteza bali hasara ambayo tutaipata kama tutaruhusu katiba hii ipitishwe kwa mizengwe, ulaghai na uchakachuaji ili kukidhi matakwa ya hovyo na hatari ya kundi dogo la watu ambao wameshindwa kuona mbele wakadhani wataishi milele.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 8, 2014.

No comments: