Tuesday, 14 October 2014

Kijiwe chawapongeza Mdee na Othman

Siku hizi hakiitwi kijiwe bali colloquium yaani mkutano wa wasomi wakitongoa na kujadili falsafa na madude mengine yaliyowashinda wahishiwa
Leo Mpemba kajilawa kweli kweli. Ana jambo si dogo. Baada ya kufika kijiwe na kukuta watu wachache aliendelea kusoma gazeti lake la Danganyika Daima. Allivuta muda huku akinywa kahawa yake taratibu.
Mara mtu wa mwisho kufika ambaye ni mzee Maneno anatua kwenye benchi.
Mpemba anakula mic, “Yakhe mwaionaje hii ya bwana nkubwa Made in Dom Dokta Shine kumtimua alokuwa mwanasharia wake nkuu shujaa Masudi Osman Osman?”
Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akisoma gazeti la The Mail on Wednesday anakamua mic, “Kwanza huyu bwana shujaa kweli kweli. Pili, nadhani huko aliko anafurahia kufukuzwa kwake. Kwani ametolewa sadaka ili ukweli ujulikane kuwa Mpemba huko kwenu hamna kiongozi zaidi ya nyampara aliyewekwa kuwachuga msibughudhi ulaji wa wale waliomtengeneza na kumsimika pale.”
Kabla ya kuendelea Mheshimiwa Bwege anadakia, “Usemayo Msomi ni kweli. Huyu bwana anaweza kuwa amejipalia mkaa asijue. Nadhani mshirika wake Hamad Madevu wa Kafu sasa anachekelea kwa vile kujulikana kuwa Zenj haikuwa na msimamo wala mtu wa kutetea maslahi yake lazima kutajibiwa kwenye sanduku la kura mwakani. Napendekeza tujadili pia huyu bi mkubwa Halima Mndee aliyeburuzwa lupango kwa sababu za kitwahuti. Laiti wangeburuzwa akina Sam Sixx na Njaa Kaya huenda ingeleta maana.”
Msomi anakatua mic tena, “Uchambuzi wako ni makini sana mkuu. Kwanza nakubaliana nawe kuwa jamaa kajichimbia kaburi kisiasa. Nionye. Kama hawa wajivuni na matwahuti wataendelea na hila zao kwa kutegemea mituringa, kipindi hiki tutashuhudia machafuko zaidi ya yale ya Komandoo na Mkapu ambapo wachovu wengi walinyotolewa roho na kuzalisha wakimbizi kwa mara ya kwanza.”
Anabwia kahawa yake na kuendelea kudema, “Hakika huyu bi mkubwa Halima si mchezo. Naye kama Othman, ameonyesha jinsi mfumo wetu ulivyo wa hovyo sana. Uzuri wote ni wanasharia ambao vitendo vyao vimewaacha uchi wanasharia nyemelezi wanaotumika kama nepi kama vile Mura Freddie Wer-ema ambaye yuko tayari hata kumuuza bi mkubwa wake ilmradi ajaze tumbo lake lisilo na shukrani.”
Mijjinga aliyekuwa ana usongo wa kutia timu hatimaye anakwanyua mic, “Yote tisa. Kumi ni kufichuka ukweli kuwa kumbe ukimya wa Shine haukuwa na neema kwa wale anaodai kuwaongoza. Mie nilishangaa kutomsika kwenye kasheshe hii.”
“Ulitegemea aseme nini wakati bosi wake alikuwa ameishamaliza kila kitu? Nadhani walimnyamazisha ili kusiwepo misimamo tofauti hasa ikizingatiwa kuwa bosi wake huwa si mjenga hoja zaidi ya kuwa mviziaje wa kawaida na mtu asiyeaminika kufanya naye makubaliano kama ilivyotokea hivi karibuni kwa UKAWE.” Anapayuka Kapende huku akibofya kisimu chake cha kisasa.
Mijjinga aliyekuwa akimnong’oneza jambo Mgosi Machungi anaamua kutia guu, “Nadhani mwisho wa ubabaishaji unakaribia. Walidhani nguvu ya kuwang’oa ni UKAWA peke yake wasijue gonjwa limo ndani. Nijuavyo wazenj hawatakubali huu utwahuti unaofanya waendelee kumezwa.”
Mpemba hangoji, “Yakhe msemayo kweli. Sie hatukubali huu upuuzi tena. Kula mwaka waja na ghilba hii na ile. Kipindi hiki nawaapieni lazima tupige ntu chini. Utatendeleaje tawaliwa na jitu liloweka kuwezesha kunyonywa?”
Mgosi Machungi aliyekuwa kimya muda mrefu anaamua kula mic, “Kwanza wenzenu nina huzuni sana baada ya kufiwa na bi mkubwa Mahiza hivi kaibuni. Tilimzika juzi kue Mashindei Vuga. Hayo tiyaache. Mie namshukuu Subhana kwa kumtia hasira Shine akamtimua Osmani ili ukwei ufumke na kutuweka wote huru.”
Kabla ya kumaliza Bi Sofia Lion aka Kanugaembe anachomekea, “Dua la kuku halimpati mwewe. Tutaendelea kutesa na wenye wivu wajinyonge. Hivi mlitaka mheshimwa Shaini asimfukuze mtu muasi ambaye aliamua kujifanyia atakavyo badala ya anavyopaswa kufanya?”
Mipawa anakula mic, “Lawama nyingine hazina hata mashiko. Wewe ulitaka afanye nini wakati umeishaambiwa kuwa sirikali ya Zenj haikuwa na msimamo? Kwa vile yeye ana msimamo si aliamua kuuonyesha kwa wasio na msimamo kiasi cha kufukuzwa ulaji. Hapa hatuwezi kumlaumu Othman bali wale waliokosa msimamo na uchungu na haki za Wazenji.”
“Veve tegemea nini. Iko taka rahisi comment on everything kama Kapa? Hii bwana Sumani kosea rahisi sana paka tia yeye hasira hadi nafuta yeye. Kosa yake hapana laumu rahisi bure bwana,” Kanji anamwaga upupu wake.
Mpembaaliyekuwa akisikiliza kwa makini anaamua kutia guu tena. “Yeye apata wapi udhu wa kufukuza wakati apaswa  fukuzwa yeye aregee kule alikotengezwa? Hebu nyie ngojeni. Mtajaona kile ambacho kilimfanya kuku asikojoe wallahi.”  
“Unadhani wazenji mwaweza mtimua kazi jamaa wakati waliomsimika wapo wanaangalia?” Anauliza Mbwamwitu.
Mpemba anajibu, “Wemezoea vya kunyonga vya kuchinja hawaviwezi. Walizowea kutugawana makundi baina ya wa huku na kule wasijue siku moja watajatuunganisha kwa kukosa msimamo wa kulinda maslahi na utaifa wetu.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si Othman akatia timu kijiweni! Kila mtu alisimama na kumlaki huku tukimpiga kwa ofa za kahawa. Baada ya hapo tulilazimika kuahirisha colloquium kwa vile tulimpeleka jamaa hoteli kufanya party.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 15, 2014.

No comments: