Tuesday, 28 October 2014

Kijiwe chalaani upogo wa vigogo

LEO Mgosi Machungi anaonekana ana usongo na jambo. Alivyoingia mwenye mawazo, si bure. Baada ya kujiridhisha kuwa ni wakati muafaka kusema linalomsimbu, anaangalia huku na kule kujihakikisha kuwa wote tuko naye na kusema, “Mwenzenu leo sina furaha.”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anauliza, “Kunani Mgosi hadi ukose furaha?
Anajibu, “Si huyu mgosi Yusufu anayeendeea kutitia aibu wasambaa wote kwa kutiambia kuwa sisi siyo dijitai utadhani yeye ni hiyo dijitai yake. Anadhani sisi sote ni mataahia?”
Mipawa anauliza, “Mgosi mbona unalalamika na kutuacha Solemba? Kwani tatizo ni nini?”
Mgosi Machungi anajibu, “Ina maana hamisomi magazeti? Hamkusikia kuwa Jose Makamba anataka kumsimika mwanae Jan kuwa rais wa kaya hii wakati hana sifa zaidi ya jina kubwa?”
“Alaa! Kumbe unaongelea hii ya vigogo kutaka kuwarithisha ulaji vitegemezi wao utadhani ni kaya ya kifalme siyo? Huyu anapoteza muda wake. Maana ukimuangalia huyo kitegemezi chake anayesema amesoma hajaifanyia kaya chochote zaidi ya kuitumia kufika hapo alipo.” Anapayuka Mijjinga huku akikunja mikono ya shati lake utadhani anataka kumfundisha adabu Makambale.
Msomi Mkatatamaa hangoji. Anatia guu, “Huu uroho na roho mbaya sasa vimezidi. Umiss watoto wa vigogo. Ubunge watoto wa vigogo.Kughushi vigogo.Epa vigogo.Escrow vigogo.Kazi ubalozini watoto wa vigogo.Shule nzuri watoto wa vigogo.Scholarship watoto wa vigogo.Je hii kaya ni ya vigogo na vitegemezi vyao au wachovu?”
Kijiwe kinamshangilia kwa kupiga makofi na vigeregere kwa jinsi alivyounga mistari utadhani anarapu!
Mgosi anakula mic baada ya vigeregere na hoihoi kutulia, “Umenikumbusha huyu Januai aivokimbia shule ngumu hapa akikimbilia kwa Joji Kichaka. Kama baba yake ni mzalendo kwanini alimkimbizia mtoto wake nje?”
“Nadhani aliogopa kufeli tena. Nasikia kwa Joji Kichaka hata ukimpeleka kilaza wa mwisho hapa kayani atapeta tu kutokana na kuangalia fedha zaidi ya uwezo. Huoni madaktari feki walioghushi vyeti nje wanayotesa kwenye lisirikali?” Anaongezea Kapende aliyekuwa akijiweka vizuri kwenye benchi.
Msomi anarejea tena, “Wameharibu elimu. Wanakimbizia vitegemezi vyao nje. Wameharibu mahospitali wanakwenda kujiangalia afya zao nje. Kimsingi, watu wa namna hii hawapaswi hata kupewa kura ya kuongoza hata mbuzi. Hawafai hawafai hawafai hata kidogo.”
“Jamaa mie kaniacha hoi hasa pale aliposema eti huyo kitegemezi wake digitali. Digitali gani wakati kompyuta yenyewe kaanza kuitumia alipotoshewa huko kwa Joji Kichaka?” Anakamua Mpemba.
Mzee Maneno hajivungi. Anakatua mic, “Nadhani usomi wa kitegemezi cha Yusufu haunipi taabu. Wenye kaya tunataka mtu anayetokana nasi na anayefanana nasi. Mtu ambaye anajua na kuyashiriki matatizo yetu na aliye na uwezo wa kuyatatua na si kuyatumia kuzidi kutuibia. Tunataka mtu atakayeondoa huu uoza uliwawezesha hata wacheza ngoma za kienyeji kuwa vigogo bila hiyo elimu.”
Sofia Lion aka Kanungaembe hakubaliani na wasemaji waliotangulia. “Jamani acheni roho mbaya na wivu. Mbona kijana kasoma tena nje na elimu ya nje ndiyo inayoabudiwa hapa kayani? Halo halo mna dola nyie?”
Kanji anamchomekea Sofia hata kabla hajamaliza, “Ile toto iko soma sana hadi Amerika. Mimi ona faa sana kuwa rahisi ya kaya. Kama nagombea mimi pigia yeye kura.”
Mijjinga hamkawizi. Anakula mic, “Kanji unataka kumdanganya nani? Mbona kwenu mmechagua jitu zee tena lisilo na mke wala mtoto? Nadhani unamshabikia mtoto wa rafiki yenu aliyekuwa akitumiwa na Yusufuuu Maaaaanji kuibia kaya kwani hatujui?”
Kapende anapoka mic, “Hawa wanaounga mkono watoto wa vigogo ni wale wanaofaidika nao. Nani anataka rahisi atakayekuwa kama Joyce Wowowo huku baba yake akiongoza toka nyuma ya pazia kama Joji Kichaka na dingi wake?”
Mheshimiwa Bwege aliyekuwa ndiyo anamaliza kumkabidhi gazeti Mchunguliaji anakula mic, “Inaonekana kuna kitu hamjui hapa. Hamkumsikia Njaa Kaya akisema kuwa rahisi lazima awe kijana kama yeye alipoukwaa utadhani alikuwa kijana. Kama ujana ndiyo sifa ya pekee basi nendeni kwenye shule za sekondari mkatafute wagombea.”
Msomi hajivungi. Anakwanyua mic tena, “Mheshimiwa bwege usemacho ni kweli ingawa huyu Jan anachofanya ni kujijengea sifa ya kuwa kingmaker kwa yule atakayeingia madarakani kumkumbuka kama Ben alivyofanya kwa Njaa Kaya. Janja yake kipindi hiki haitafanikiwa. Nadhani kama ni wasomi tupo tena tulioiva. Hivi unaweza kumlinganisha huyu kitegemezi anayebebwa na jina la baba yake namia ua Dokta Silaha au Prof Ibra Lipu-mba?”
Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anachomekea, “Thubutu. Utamlinganishaje kicheche na tembo?”
Mpemba anaamua kuwavunja watu mbavu, “Nyie wallahi mwanikumbusha yalotokea kwetu pale walipomsimika mtoto wa Karumekenge wakati bomu. Sasa yu ahangaika ataka eti shemeji yake naye awe rahisi utadhani kaya ya kifalme. Tuwakataeni hawa waroho wa madaraka wallahi.”
Kapende anarejea, “Nadhani hatuna haja ya kupoteza muda na wabangaizaji na wasaka tonge. Huyo Joseph mwenyewe anayesema eti atamnadi kitegemezi chake kaya nzima afya yake ugogoro.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la Jan. acha tumzomee hadi atoke mkuku akimuachia dereva kwa kuhogia huenda tungemfanyia kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 28, 2014.

No comments: