Saturday, 4 October 2014

Mlevi kuzuia uchafuzi wa maadili

   Baada ya kugundua kuwa wakubwa wa dunia wamekusanyika New nyoko kuongea na kula kuku, mlevi kwa vile nami rais wa walevi sikujivunga japo sikupokelewa kama kiongozi wa kaya. Nilikwenda kama rais walevi na wavuta bangi wanaoongezeka duniani tokana na uchafuzi wa maadili utokanao na baadhi ya wakubwa kuhalalisha mihadharati, rushwa, ufisadi na ujambazi.
          Kwa vile ajenda mojawapo kubwa ya kikao hiki ambacho kwa wengi ilikuwa ni matunuzi japo hoja ilikuwa kujadili mstakabali wa dunia kutokana na uchafuzi wa mazingira unaosababisha kuchemka kwa dunia, Global Warming, nilitia timu kuanzisha ajenda na hoja mpya ya uchafuzi wa maadili ambao ni hatari kuliko ule wa mazingira.
          Kama kawa, nilitinga na bi mkubwa na washikaji zetu. Ili kutogundulika kuwa tuliandamana na washirika zetu, nilificha orodha yao kwa walevi ili wasistuke kuwa natumia vibaya njuluku zao. Hivyo, kama ada, msafara wangu ilikuwa top secret. Wangeona sura tulizoandamana nazo huenda wangenitimua toka kwenye ulaji. Hivyo, elewa. Ukiulizia majina ya walevi nilioandamana nao nakunyotoa roho kama siyo kukuchukia na kuomba unyotoke roho. Ulaji wetu unakuhusu nini? Kwani niko peke yangu anayeficha majina ya washikaji anaoandamana nao? Akienda na, vitegemeizi, shemeji zangu hata vimada na waganga wa kienyeji nyie inawahusu nini? Kwani nalipia matanuzi haya toka mfukoni mwake? Kama hujui jua. Wanaolipia matanuzi yetu ni walevi wenyewe ambao kwa ulevi wao hawana ubavu wa kugundua janja na kufuru zetu au vipi? Naona yule anatikisa kichwa.   Yule anakukunja ngumi akionyesha kidole cha kati. Koma we! Acha tule tutakavyo.  Mwenye wivu si ajinyonge! Kwani hamjui kuwa kutesa ni kwa zamu siyo? Ngojeni zamu yenu hata kama ni ndoto ya Alinacha.
          Baada ya kugundua kuwa walevi wananisumbua sana wakitaka maoni yangu kuhusu karibu kila jambo kuanzia katiba mchachakachuo, ufisadi, ulaji wa kifisi na upuuzi mwingine, niliamua kwenda zangu kwa Joji Kichaka kupumua japo kidogo. Hivi ungekuwa wewe ungefanya nini? Leo unasikia kelele za Escrew. You screw them up and they come crying seeking your help while you actually are the one that crucified them. Kesho kelele za Katiba Mpya. Kesho kutwa unaulizwa umefanya nini kupambana na mihadarati wasijue nawe ni mnufaika!  Mnadhani mibangi ninayovuta naipata wapi kama siyo kupitia uhalalishaji wake?
          Baada ya kutua kwa Joji Kichaka niliamua natembelea washikaji zangu wote kuanzia wale waliopendekeza nipewe tuzo ya kiongozi bora wa walevi hadi wale wanaopanga kunitunuku shahada za udaktari. Ni kazi kwenda mbele. Bi mkubwa, kwa vile ni rais wa wake za walevi, naye yuko mitaani akisaka njuluku kwa ajili ya kampuni yake ya Maulaji ya Wake za wakubwa (MAWAwa). Kama nilivyosema, kutesa ni kwa zamu. Dingi natesea huku bi mkubwa kule mradi tunachanga njuluku huku tukilipwa Per Diem kwa matanuzi yetu.
          Baada ya kushuhudia mafisadi wa kisiasa wakitoa mapofu kupigania mazingira, nilisukuti na kugundua kuwa kumbe naweza kujenga hoja ya kimataifa kwa kudai baraza kuu la Umoja wa Mataifa liitishe kikao cha kujadili uchafuzi wa maadili yaani kupambana na madili hasa katika kaya kapuku zinazosifika kwa kuomba wakati wakubwa zake ni matajiri wa kunuka. Nilikwenda kwenye viwanja vya ndege vya JFK na La Guardia kuona midege ya madingi wa kaya kapuku iliyoegeshwa pale na kuipiga picha ili uwe ushahidi nitakapokuwa najenga hoja. Ili kunogesha hoja yangu niliomba wachovu wanaoandamana kupinga maovu mbali mbali wafanye kazi hiyo chini ya mradi wa kitaalamu unaioitwa kwa kitaalamu photovoice na photonovella ambapo utafiti hufanywa na walalahoi na si maprofesa kama mimi.
          Lengo la kuanzisha hoja ya kushughulikia uchafuzi wa maadili inatokana na ukweli kuwa kwa Jojo Kichaka kugeuka kijiwe cha kahawa ambapo wakubwa hukutana kila mara kuteketeza njuluku za walevi. Ni juzi juzi walikutana huko na kufanya maonyesho ya ukwasi ambapo wake zao walionyesha vitu vyao hasa mavazi na miposhi ya bei mbaya. Hata mwezi haujaishi wanakutana tena kusaka njuluku na kuongea mambo ya ajabu ajabu wakati wakikwepa yale ya maana. Si walikutana mwezi jana kwenye kikao cha sijui Africon- USO conference. Nani anaongelea yale waliyoazimia kuyatekeleza? Ajadili nini wakati lengo la madingi na washikaji zao kwenda kule ilikuwa ni matanuzi? Waongelee nini wakati wao ziara zao ni juu yao na miradi yao fichi? Ni bahati mbaya nilimpiga bi mkubwa kuwa na NGO ya uongo na ukweli uliojificha kwenye ulaji na ulafi. Huenda ningekua mengi.
          Turejee kwenye mada. Baada ya kufika zamu yangu kuhutubia Baraka Kubwa la Umoja wa Makaya si niliwapa wazi kuwa Afrika isinyanyapaliwe kutokana ugonjwa wa Ufisadi.  Nilizoza hadi wasiojua usanii wangu wakadhani mimi ni mwana falsafa wasijue sina lolote wala chochote bali sanaa. Nilichonga hadi watu wakawa wanasogea huku na kule kwenye viti vyao wakidhani mzee Mchonga amefufuka. Hata hivyo, nikiwa nafaidi ujiko si nikaruka mstari mmoja kwenye hotuba niliyokuwa nimeandikiwa. Nilianza kupayuka na kusoma vitu visivyoingia akilini hadi wasikilizaji wakahoji kama kweli mimi si chizi. Baada ya kugundua nilitetemeka na kutoa jasho kama vile bi Mkubwa wangu afanyavyo aongeapo kimombo kutokana na kutokimanya. Hata hivyo, nilipangua gea na kurejea kwenye mstari na kuupa kibarua Umoja wa Makaya kupanga kikao maalum kwa ajili ya kupambana na uchafuzi wa maadili kwanza ndipo ufuate uchafuzi wa mazingira.
Kwa ufup, pamoja na kutanua kwa njuluku za walevi, angalau nilijenga hoja kuwa tatizo la dunia kwa sasa si uchafuzi wa mazingira bali wa maadili.
Salamu kwa walimu Shombe, Shambula, Selemani, Mtakatifu Zakaria, Kombahaha Lihangwike, Ntandu, Shemkuya, Seria, na Makakala tuliofundisha wote Kinosec. Pia nawakumbuka marehemu Rutaba, Maringo na Jariwalla bila kusahau wanafunzi kwa namna ya pekee.
Chanzo: Nipashe Oktoba 4, 2014.

No comments: