Sunday, 5 July 2015

CCM inapowaandaa watanzania kuwachakachua


 
          Tambo na mipayuko ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Nape Nnauye kuwa  itashinda hata kama ni kwa bao la mkono, ni tangazo la  hatari lililopaswa kuwachefua na kuwahamasisha watanzania kuingia mitaani. Lakini wapi! Ama kweli aliyeiroga Tanzania alishajifia miaka mingi. Nnauye alikaririwa akiwa Sengerema akisema, “Rangi inayoenda Ikulu ni hii (anaonyesha shati lake la kijani ambayo hutumiwa na chama hicho). Tuna uhakika na ushindi wa Rais. Kwa namna yoyote ile, CCM itarudi Ikulu hata kama ni kwa bao la mkono... bao ni bao tu ili mradi refa hajaona.” Kwanza, sijui alipitiwa au ni tabia ya kuropoka tu bila mdomo kuwasiliana na ubongo.  Pili, je alipitiwa au kuropa kweli au ni ile hali ya kuwaona watanzania kama mabunga unaoweza kuwatukana tusi lolote liwe la maungoni na au juu ya wazazi wao wasikufanye kitu? Tatu, je Nnauye alisema aliyosema kama namna ya kupima maji ili aone watanzania watalichukulia na kuitikia vipi?
          Ingawa ukisema kuwa kiama cha CCM kinakaribia unaonekana kama mnazi na shabiki wa upinzani, kimsingi, CCM imeishiwa kiasi cha kuwapa silaha wapinzani waibomoe kirahisi. Maana sikutegemea kusikia uoza kama huu toka kwa kiongozi wa juu wa chama hasa wakati huu ambapo CCM imeparaganyika kiasi cha kuwa na wasaka urais wanaoibomoa bila huruma wala adabu. Ama kweli la kufa halisikii dawa.
          Je kitendo cha watanzania kukaa kimya si kuhalalisha njama hii ya kuiba kura na kuhakikisha CCM inashinda? Nadhani alichotaka kusema Nnauye ni kwamba kuandaa uchaguzi ni kama kupoteza muda na fedha au kutimiza mradi. Maana CCM lazima ishinde kwa goli la mkono kwa vile refa hataona. Je Nnauye anamaanisha refa atakayesimamia mpambano huu atakuwa kipofu au ameishakatiwa chake kiasi cha kuwaahidi waliomhonga tayari kuwa wafanye watakavyo yeye hataingilia kati?
          Kitu kinachochanganya na kukatisha tamaa ni namna wapinzani wanavyochukulia mambo mazito kirahisi na kimzahamzaha kama alivyokaririwa katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbrod Slaa aliyekaririwa akisema, “Kwa bahati mbaya kauli za Nape siwezi kuzijibu. Kauli za Nape zichukue kama zilivyo, ingekuwa ni (katibu mkuu wa CCM, Abdulraham) Kinana, ningemjibu lakini ajue kuwa tutakutana Oktoba.” Kwangu mimi hili si jibu mujarabu hasa ikizingatiwa kuwa Slaa anaogopa kupambana na mbwa akingoja amuone aliyemtuma. Sioni kama kuna haja ya wapinzani kuchukua msimamo legelege kama huu hasa ikizingatiwa kuwa Nnauye aliyesema haya yuko kwenye ziara moja na huyo Kinana wanayemtaka.
          Nadhani jambo ambalo walipaswa kufanya wapinzani, ni kuwashitaki CCM kwa wananchi haraka bila kujali uzito wa aliyetoa kauli hii hatari. Nadhani, hata kama maneno yaliyosemwa na Nnauye yangelisemwa na kunguru hata paka wa CCM wapinzani walipaswa kuyapa uzito. Maana, alichofanya Nnauye ni kufikisha ujumbe aliopewa na wakubwa zake ili kupima maji kama tulivyosema hapo juu. Kimsingi, mtoto wa jirani akikutukana huwezi kunyamaza kwa kuogopa kukabiliana na mtoto. Badala yake utafunga safari uende kwa mzazi wake ili uone anajibu nini ili uamue kama udharau mambo ya kitoto au ule meza moja na mzazi mwenzako.
          Wengine waliopaswa kusimama na kutoa melezo ikiwamo kupinga kauli hii chafu ni Tume ya Uchaguzi (NEC). Lakini pamoja na uzito na uzushi wa hoja husika, NEC hawajapoteza muda kujibu wala kujadili. Hii inaweza kutafsiriwa kuwa wote wawili yaani CCM na NEC lao moja. Hivyo, wanauandaa umma kisaikolojia kuupiga bao la mkono si la kisigino kama tulivyozoea. Je namna hii tunalipeleka taifa wapi kama siyo kwenye machafuko kama alivyoonya Naibu mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya ambaye alikaririwa akisema, “Lakini CCM wajue kuwa kutatokea machafuko makubwa iwapo wamejipanga kuingia Ikulu kwa njia hiyo ya bao la mkono. Kauli ya Nape ni ya kidikteta na inaonyesha dhahiri kuwa wamejikita kwenye utawala wa mabavu.” Kama kuna sehemu ambayo inaweza kukomesha mchezo huu mchafu si nyingine bali upande wa pili wa Muungano yaani Zanzibar ambao siku zote wameonyesha kiwango kikubwa cha kujitambua na kusimamia haki zao. Hivyo, tuombe Mungu haya wanayopanga wayafanye pande zote za Muungano waone cha moto.
          Lugha wanayotumia CUF ni ya kujitambua zaidi kuliko waliyotumia CHADEMA ya waache tutakutana Oktoba. Mtakutana Oktoba ili iweje iwapo kutoshupalia kauli ya Nnauye ni ushahidi tosha kuwa hamkujiandaa kukabiliana na  kadhia hii? Hata hivyo, akina Nnauye na CCM wanapaswa kukumbuka. Kama alivyowaonya mwenyekiti wao rais Jakaya Kikwete, mambo yanaenda yakibadilika. Wanaweza kudhani kuwa watanzania ni kichwa kile kile cha mwendawazimu ambacho wamekuwa wakijifunzia kunyoa kumbe siyo. Kimsingi, kauli za CCM zinaelekeza nchi kwenye machafuko tena ya kupangwa na CCM hiyo hiyo inayojinadi kuwa ni chama cha amani.
          Tumalize kwa kuwaonya wapinzani kuamka na kupambana hata kabla ya hiyo Oktoba. Pia tunawaasa watanzania waache kujifanya kama hamnazo kiasi cha kufanyiwa kila upuuzi tena kwa majigambo. Wasimame na kutoa tamko ili kufikisha ujumbe kwa kuingia mitaani japo kwa siku moja. Pia tunawaasa CCM waangalie mchezo wanaopanga kuufanya na madhara yake. Nani alitegemea kuwa Burkina Faso wangemtimua rais king’ang’anizi, wa muda mrefu na aliyeogopewa sana? Nani alijua kuwa miamba ya udikteta kama Muamar Gaddafi wa Libya angekufa kwa kipigo kama kibaka huku akilia kama kichanga? Tieni akilini na chonde chonde, tamaa zenu za madaraka zisituletee machafuko.
Chanzo: Dira Julai 2015.

No comments: