Sunday, 26 July 2015

Kingunge anaibeep CCM au kuitisha?


 Hivi karibuni aliyekuwa mpambe mkuu wa mtia nia ya urais aliyebwagwa hivi karibuni waziri mkuu aliyeachia ngazi kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa, mzee Kingunge Ngombale Mwiru alitoa mpya.  Alikaririwa akisema, Jitihada zote ambazo zimefanywa za kuvunja taratibu zilikuwa zinaelekezwa kwenye kumzuia Lowassa asipate haki. Badala ya yote nani kashinda? Kashinda Lowassa kwa sababu imeonekana wazi kuwa yeye ndio kipenzi cha Watanzania na hakuna kitu kikubwa kama kupendwa na watu.” Kwanza, Kingunge anaonekana hajaridhika na maamuzi ya vyombo vya juu vya chama chake. Pili, anavituhumu kwa kumdhulumu mgombea aliyetaka ashinde. Tatu, ni kama anatishia chama kimtambue lau kumpa prominence mtu wake akitaka awe kile waingereza huita king maker. Je Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitapokea na kutishwa na kitisho cha Kingunge? Je Kingunge anaongea kwa niaba yake binafsi au ametumwa na Lowassa?
Wapo wanaoona kama Kingunge anajisumbua bure kwani maamuzi yameishafanyika na kupita na CCM kimeishapima upepo na kuona uamuzi wake hautakisababishia madhara zaidi ya faida.  Kingunge anasema CCM imuangukie Lowassa ili isishindwe iwapo Lowassa hatamuunga mkono mgombea wa CCM Dk John Pombe Magufuli. Je hii ni kweli kuwa ili Magufuli ashinde anahitaji kushikwa au kuungwa mkono na Lowassa?  Wapo wanaoona kama Lowassa atajitenga na Magufuli, atampunguzia kazi ya kujinadi hasa ikizingatiwa kuwa tuhuma nyingi za ufisadi zinazomkabili Lowassa zinaweza kumharibia Magufuli hata kama Lowassa anaungwa mkono na watu wengi.
Kingunge aliendelea kusema, “Kuanzia sasa wana-CCM tutafute namna ya kushikamana vizuri, tuimarishe umoja wetu maana ndio nguvu yetu na katika hili ndugu Lowassa ana nafasi muhimu na ya kimkakati ana mamilioni ya Watanzania wana imani naye.” Kama tutakuwa wakweli, nani kati ya Lowassa na Magufuli ni kipenzi cha watanzania na kwa sababu gani? Lowassa anasifika kwa kutimliwa madarakani kwa tuhuma za ufisadi.  Pia kwenye mchakato uliopita alisifika kwa kumwaga fedha ambazo hakuzitolea maelezo alivyozipata ukiachia mbali kucheza rafu hadi akapewe adhabu. Kwa upande wake, Magufuli anasifika kwa uchapakazi, kutokuwa na makundi, kutotumia fedha kwenye mchakato na kutokabiliwa na tuhuma za ufisadi. Sijui kwa kuangalia sifa hizi ni nani anapaswa kuwa kipenzi cha watanzania kweli? Ama kweli mwenye mapenzi haoni. Wahenga walisema.
Wapo wanaoona kama Kingunge anatapatapa bure. Maana wenzie chamani wanaonekana kumzoea ukiachia mbali kumchoka. Wapo wanaoona kama Kingunge la Lowassa wataendelea kutafuta kuwa king makers wanaweza kujikuta pabaya hasa pale CCM ikipuuzia kitisho chao na kuamua kuwashughulikia kulingana na historia yao ya nyuma. Sidhani kama kashfa iliyomhusisha mke wa Kingunge na familia yake pale kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani ilishasahulika na kuuawa kiasi cha Kingunge kuwa salama.
Kwa hali ilivyo, CCM haitakubali kutishiwa na Kingunge na Lowassa. Badala yake inaweza kuamua kuwashughulikia na wakasahulika katika siasa za Tanzania. Kwa mfano, mpaka sasa Lowassa analipwa marupurupu ya ustaafu wakati hakustaafu ukiachia mbali kutofikishwa mahakamani. Je Kingunge na Lowassa hawaoni kuwa wakiendelea kuitishatisha CCM inaweza kuamua kufungua upya mafaili yao na wakajikuta badala ya kuwa king maker wakaishia kuwa washitakiwa?
Pia kwa sifa na tabia ya Magufuli sijui kama anaweza kuwa wa hovyo kiasi cha kutegemea kuungwa mkono na Lowassa ili ashinde.
Inaonekana kushindwa kwa Lowassa kumemchanganya vibaya Kingunge. Wakati akitaka CCM ishikamane na kushinda kwa kishindo, haonekani kuamini kuwa haki itatendeka. Katika hili Kingunge alisema, “Mkitaka nchi ijiongoze lazima chama kijiongoze kwa kufuata misingi ya kidemokrasia. Watu wamehukumiwa katika vikao bila kusikilizwa. Kama makao makuu ya CCM yamepuuza haki ya wagombea, vipi kama hilo likitokea katika katika chaguzi za chama za mkoa, wilaya, kata na tawi.” Kimsingi, anachoonyesha Kingunge ni kwamba project yao ilikuwa kubwa. Baada ya Lowassa kubwagwa, sasa wana wasi wasi na watu wao mikoani na wilayani wanaweza kubwagwa.
Wengi wanaojua utaratibu wa CCM wa kushughulikia malalamiko kupitia vikao na taratibu za chama wanashangaa Kingunge kutumia magazeti badala ya vikao na taratibu husika. Je kwa kufanya hivi haoni–kama anazidi kuwachukiza wakubwa wa chama chake ambao kama wataamua kumjibu–wanaweza hata kumpatiliza zaidi tena kwa kuachana na malalamiko yake na badala yake wakamshughulikia kwa kuvunja na kupuuza taratibu za chama?
Kwa wajuzi wa siasa na staili ya CCM wanadhani anachofanya Kingunge hata Lowassa ni kulilia maziwa ambayo yameishamwagika. Hayatazoleka. Sana sana anaweza kuzidi kuwakorofisha wenzake wakaamua kumvua nguo na akamaliza maisha yake ya kisiasa vibaya. Yeye sasa anawatisha. Hawajamjibu wala kumtisha. Je wakiamua kumtisha kweli kweli atakuwa na utetezi upi?
Kwa wanaokumbuka kilichowafika akina Horace Kolimba, Seif Sharriff Hamad na mzee Aboud Jumbe, wanadhani Kingunge anatafuta la kutafuta na likimfika hatakuwa na namna ya kulikwepa wala kujitetea bali kuzama na kusahaulika ama kwenda kumalizia maisha yake kwenye upinzani. Je kama CCM watawapuuza Kingunge na Lowassa watachukua hatua gani au ndiyo mikakati ya kujiengua CCM kama njia ya kuiadhibu? Je Kingunge na Lowassa wanaibeep au kuitisha CCM? Maswali ni mengi kuliko majibu ingawa hali ilivyo, wawili hawa hawana jeuri ya kuihama CCM.
Chanzo: Dira Julai 2015.

No comments: