The Chant of Savant

Thursday 16 July 2015

Heko Butiku na Warioba japo mnampigia mbuzi gitaa

Image result for photos of warioba and butiku
 Baada ya kung’atuka na hatimaye kuaga dunia kwa Mwl Julius Nyerere, walibaki viongozi wenye udhu wachache sana. Ni bahati mbaya hata wale aliowaamini akawabeba hadi kubezwa amebeba nyago la mpapure walimgeuka wakageuka mafisadi wa kunuka.
Hata hivyo, bado Tanzania ina watu wa kupigiwa mfano. Hawa si wengine bali wanafunzi wa kweli wa mwalimu Nyerere. Mmoja wa watu hawa ni Joseph Butiku ambaye pia ana uhusiano wa damu na Nyerere. Mzee huyu, licha ya kuwa muwazi na muadilifu, si mwoga na anapokuwa au kukerwa na jambo huwa hasiti kulisema.
Hivi kariubuni Butiku alikaririwa akisema, “Sasa tunatoka kwenye utaratibu wetu wa vyama tunashiriki katika kufanya uovu. Kama haki inauzwa, hatuwezi kupata amani. Viongozi wanatoa rushwa hata kabla ya kupewa nchi. Je, wakipewa nchi itakuwaje?”  Tofauti na wakongwe kama vile Kingunge Ngombale Mwiru, Butiku na wengine wachache kama vile Joseph Warioba ni wazee wachache unaoweza kuamini dhati na yale wayasemayo.
Wazee hawa wameshinda vishawishi na kuonyesha uzalendo wao wakati huu ambapo chama chao kinatafuta mtu wa kupeperusha bendera yake. Wamejitenga na ukuwadi uchwara na unepi ambao umewashinda wengi waliopwakia hongo hadi wazee wazima wakajivua nguo hadharani. Kwa lugha nyepesi ni kwamba Butiku analionya taifa kuwa kama halitajirekebisha likaendelea na ugunia wa kumeza kila kiingiacho litajikuta pabaya huko tuendako.
Butiku bila woga wala kumung’unya maneno alionyesha chanzo cha matatizo tunayoshuhudia ambapo watia nia wanatembeza hongo mchana kweupe bila kuchelea lolote. Alisema, “Mtandao huo iliamua kufanya kazi nje ya CCM kwa sababu itikadi zao na sisi zilitofautiana. Eti wanasema CCM ni chama cha mizengwe kinawachelewesha kutajirika. Sasa hao watu ndiyo wameendelea kuwapo na kusababisha haya matatizo yaendelee.” Butiku alikuwa akielezea uchafu ulioasisiwa na wasaka tonge hapo mwaka 1995 kiasi cha kuendelea kuitafuna CCM.
Butiku hakuwa peke yake kukemea uhovyo na uhalifu vinavyoanza kuonekana kama vitu halali na vya kawaida ndani ya CCM na serikali zake. Mzee Warioba naye aliongeza kwa akionyesha chanzo kingine kinachoweza kuleta uvunjifu wa amani nchini. Alisema, “Tunakwenda katika uchaguzi lakini huku tukiwa na viashiria vya uvunjifu wa amani. Hivi nani hajui kuwa kuna rushwa kubwa katika uchaguzi.” Kwa mujibu wa Warioba ni kwamba kinachoendelea kwenye kutafuta atakayepeperusha bendera ya CCM ni rushwa tupu. Hii maana yake ni kwamba watanzania kama hawatajifanya kuwa mataahira wanapaswa kutomchagua mgombea wa chama kinachopata mgombea wake kwa rushwa na kuvunja kanuni walizojiwekea. Kama wanaweza kuwa wazembe kiasi cha kuvunja hata kanuni walizojiwekea, wakipata madaraka si watavunja sheria za nchi kama walivyofanya kwenye kuua katiba ya wananchi? Je watanzania wanataka washikwe wapi au watukanwe matusi gani au kuonyeshwa dalili gani wachukie na kuchukua hatua mujarabu? Je itakapotokea nchi ikaingia kwenye machafuko watamlaumu nani kama si kujilaumu wenyewe?
Watanzania wanapaswa kuzingatia wosia na maneno ya wakongwe hawa wa CCM. Kwani wanachosema ni ukweli ambao hauna shaka. Sasa kama wana CCM tena wakongwe wameishaona hatari na uhovo wa CCM kunaja gani ya wapiga kura kuendelea kuipa hadhi ya kupeleka nchi kuzimu? Nadhani ufisadi ambao CCM imeuasisi, kuusimamia na kuutekeleza vinatosha kuwafanya watanzania wachukie na kutoa hukumu yako ya haki.
Najua baada ya CCM kushikwa pabaya na wanachama wake wenyewe na kuishiwa, kwa sasa watakuja na mzengwe wa kusema fulani tuliyempitisha ni mtu safi. Well, well, mnaweza kuwa na mtu safi je chama ni safi?  Huko nyuma tuliwahi kuonya kuwa hata kama CCM wangemsimamisha malaika, mwisho wa siku watamchafua naye awe kama wao. Watambadili lakini yeye hatawabadili kwa vile chama kina mamlaka makubwa kuliko mtu kitakayemfadhili kugombea ili kulinda maslahi yake hata kama ni maslahi haramu.
Wanaotilia shaka ukweli huu wajiulize Mr. Clean aliishia wapi? Si aliaminiwa na Mwl Julius Nyerere akambeba na kumpatia ushindi lakini akageuka kuwa Mr. Dirty? Je huyu ni nani atakayedhaminiwa na chama kichafu asichafuke au atakayeweza kutumia usafi binafsi kusafisha chama kisichoweza kusafishika. Sijui kama kipande cha sabuni kinaweza kuisafisha bahari. Sana sana kitayeyushwa na kumezwa na kugeuka maji ya bahari basi. Hivyo, wanaoitakia nchi mema wanapaswa kutohadaiwa na yeyote atakayeteuliwa na chama ambacho hata waanzilishi na wakongwe wake wameishakichoka na kukiona hakifai tena kuaminiwa madaraka.
Chama kilichoanzishwa kupambana na uonevu na dhuruma kinapoyatenda haya kinakoma kuwa kile kile. Kwa sasa CCM iliyopo ni chama kingine tofauti na CCM aliyoanzisha Mwl Nyerere ambaye alipokufa na CCM yake ikafa ikabakia ya mafisadi, wala na watoa rushwa kama wanavyobainisha Bujiku na Warioba. Je tusipowasikiliza na kuwaamini hawa wakongwe tunataka tupate ukweli toka kwa akina Kingunge Ngombale Mwiru au Paskari Ndejembi?
Tumalizie kwa kuwapa heko Butiku na Warioba hata kama wanawapigia mbuzi gitaa. Maana, hatujui kama CCM au watanzania watawasikiliza na kujiepusha zahama wanayotaka kuipa ridhaa tena.
Chanzo; Dira Julai 16, 2015.

1 comment:

Anonymous said...

Hi jamani wamechoka hao hata sura zinatisha CCM hiyo
Wamechoka kwa akili hadi sura
Hawa wamechoka kinachowakeka CCM
Pension zao
Tumekwisha