Saturday, 25 July 2015

Kumbe CCM ni chama kabaila na kifisadi!  • Chama-Cha-Mapinduzi.jpg

Wale waliosoma enzi za ujamaa watakuwa wanakumbuka dhana nzima ya ukabaila ambao ni utajiri unaotaokana na utumiaji ardhi kwa kukodisha kwa wasio nayo. Baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushika hatamu zama zile kwa ajili ya kulinda maslahi ya wananchi, iliishia kupoteza sifa hii pale ilipojiingiza kweye unyakuzi wa ardhi. Tulizoea kusikia unyakuzi wa ardhi nchi jirani tusijue tutatawaliwa na chama nyakuzi chenye kuwa kabaila huku kikiendeshwa na mabwanyenye na mabepari. Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TUKI uk.297, inauelezea ukabaila kama: tabia au hali ya kumfanya mtu amtumikie huku mwingine akistarehe.Tabia ya kumilki majumba na ardhi kupangisha ili kuwanyonya wengine.

Kwa tafsiri ya kamusi ya TUKI, CCM ina sifa zote za kuitwa chama kabaila au cha kikabaila. Haya si madai yetu bali ukweli uliotoka kwenye vinywa vya kiongozi wake.

Akifungua ukumbi wa mikutano Dodoma hapo tarehe 9 Julai alisema kuwa CCM ina viwanja vingi nchini. Mfano, Dar pekee wana viwanja zaidi ya 400. Je huko kwenye majiji mengine kama vile Arusha, Mwanza, Mbeya, Tanga na kwingineko wana viwanja kiasi gani? Je wanavimilki kihalali hasa ikizingatiwa kuwa viwanja vile vilipatikana wakati wa chama kimoja ambapo serikali na chamavilikuwa kitu kimoja? Je kuna mantiki yoyote ya CCM kuendelea kushikilia, kukalia na kupata kipato toka kwenye ardhi ya umma? Je huu si unyakuzi (land grabbing) tuliozoea kuusikia kwenye nchi jirani? Je chama kinachonyakuwa ardhi ya umma kina tofauti gani na viongozi wanaofanya hivyo?

 Kikwete alikuwa akiwahimiza wenzake kuwa waache kuombaomba na badala yake waendeleze vile viwanja kwa manufaa si ya nchi bali chama.

Alilaumu tabia ya kutegemea wafadhili na kutaka CCM waendeleze vile viwanja. Je wataviendelezaje wakati si vyao?  Kikwete alishangaa ni kwanini chama chenye viwanja vingi namna hivi kutegemea wafadhili. Wengi waliona kama anajisuta bila kujua. Kama anashangaa chama chenye utitiri wa viwanja kutegemea wafadhili basi alipaswa kushangaa nchi yenye raslima lukuki kutegemea kuombaomba na kukopakopa. Alichofanya Kikwete kinakubaliana na msemo wa wahenga kuwa nyani haoni kundule.

Kitu kingine cha kushangaza na kusikitisha ni ile hali ya Kikwete akukiri kutojua hata hiyo pesa inayotokana na viwanja chini ya miradi haramu ya kulaza magari anayeipokea na anachoifanyia. Wengi walitegemea rais lau atumia muda ule kama rais na si kama mwenyekiti wa chama kukikumbusha chama chake kurejesha ardhi ya umma. Maana kwa CCM kuendelea kumilki ardhi ya umma kunatoa picha mbaya kuwa chama nyakuzi wa ardhi hakiwezi kupambana na wanyakuzi wa ardhi wakati mchezo wao ni mmoja.

Wengi wanaweza kuona kama tunaiandama CCM bure. Nchini Kenya, chama tawala cha zamani cha KANU kilipotupwa nje, majengo na vitegauchumi kilichokuwa kikimilki wakati wa serikali ya chama kimoja vilirejeshwa serikalini mojawapo ya mradi mkubwa ukiwa Nyayo House yenye ghorafa 27.

Kikwete aliongeza kusema badala ya CCM kuendeleza viwanja viongozi wamekuwa wakivipora na kujijengea majumba yao. Ajabu pamoja na kukiri hivyo, alisita kusema ni hatua gani zichukuliwe kupambana na wezi hao.

Hivyo, tokana na rais ambaye ni mwenyekiti wa chama kushindwa kukiambia chama chake kirejeshe mali za umma serikalini, unapaswa kuanzishwa mchakato wa kuifikisha CCM mahakamani ili iamriwe kurejesha viwanja vyote vya umma. Pia iamriwe kulipa fidia kwa muda ambao imevitumia kwa faida binafsi huku viongozi wake wakizidi kujineemesha kwa jinai hii. Kuna haja ya wapinzani na wanaharakati wa masuala ya ardhi na haki za binadamu kuingia kazini kuhakikisha CCM inarejesha mali za umma haraka sana iwezekanavyo.

Kwa namna ambavyo CCM imekuwa ikiendesha viwanja vya umma kwa faida binafisi, si tusi wala uzushi kusema kuwa CCM ni chama cha kikabaila ambacho hakina uchungu na wananchi kiasi cha kunyakua viwanja vyao na kutumiwa na viongozi waroho na wasioona mbali wala kujali maslahi ya wananchi.

Wakati Kikwete akifichua –sijui kwa bahati mbaya au maksudi –uoza huu wa CCM, katibu mkuu wa chama Abdulrahaman Kinana ambaye mara nyingi amejitia kuwa na huruma na watanzania, alikuwa akichekelea. Wengi tulitegemea –kama mapenzi ya Kinana kwa umma yangekuwa ya kweli –lau kumsikia akitangaza mkakati wa kurejesha viwanja vya umma serikalini. Badala yake alionekana akitikisa kichwa kukubaliana na pendekezo la Kikwete kuwa aunde tume ya kukagua mali za CCM kukiwemo viwanja ambavyo ni mali ya umma. Nadhani kwa kuangalia ukweli huu, tunagundua ni kwanini majengo yaliyojengwa kwenye viwanja vilivyakuliwa au kutoruhusiwa kama lile la Getrude Rwakatare au la uhindini hayaangushwi kwa vile lao wote ni moja.

Tumalizie kwa kuwataka watanzania wailazimishe CCM:

a) Kurejesha viwanja vya umma

b) Kutangaza wazi kuwa sera yake sasa ni ukabaila hasa unaotokana na unyakuzi wa ardhi na utumiaji ardhi nyakuliwa kulaza magari na kupata viwanja vya viongozi wake kujenga majumba binafsi. Huu ni ufisadi wa kiwango cha juu sana kiasi cha kukifanya CCM kuwa chama cha kifisadi.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 26, 2015.

1 comment:

Anonymous said...

http://www.mwananchi.co.tz/habari/habari-ya-ndani/Marais-watano-wanaotajwa-kuongoza-kwa-mishahara-minono-Afrika/-/1724700/2810552/-/jug9pg/-/index.html