Tuesday, 7 July 2015

Kijiwe chastukia “kufuturisha”


Shehe Mrisho  Jakaya Kikwete alipokwenda kufuturu kwa shehe Peter Mizengo Pinda
 Baada ya mwezi wa ramazani kuanza, tumeshuhudia mengi ya kuchekesha na kusikitisha. Umezuka mtindo wa mashirika yanayopaswa kutokuwa na dini eti nayo kufuturisha. Hivyo, kijiwe kimekaa kudurusu kadhia hii na kutoa baadhi ya maelezo na maelekezo kwa wenye kuzifuata na kujua dini.
Mzee Kidevu analianzisha leo, “Leo Sofi dadangu umependeza. Hiyo hijab ilivyokukaa, mashaallah.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anatabasamu na kusema, “Kaka nashukuru. Huu mwezi mtukufu. Lazima tumpendeze Subhanna wa Taala kwa kujipendekezesha kimwili na kiroho ati.”
Mpemba anadandia, “Yakhe naungana nawe. Shurti waja tujipambe kiimani ili kumpendezesha Subhanna.”
Mbwamwitu hangoji Mpemba amalize. Anachomekea, “Ami mbona wewe hujatia hiyo kitu kama kweli lengo ni kumpendezesha Mungu?”
“Wamaanishani? Yaani wataka mie nivae hijabu!” Mpemba anajibu kwa kuchukia kidogo.
“Hasha shehe. Naamisha kuvaa kile kitambaa ambacho wanaume huvaa hasa watokapo hijja au wakati wa mwezi mtukufu.” Anajitetea Mbwamwitu.
Mpemba anajibu, “Yakhe uislam si viremba na hijab bali matendo matukufu ya mja mbele ya Mnyazi Mngu.”
Mijjinga aliyekuwa akisoma gazeti la Cheka Ulie anaamua kutia guu, “Mie nilidhani mtaongelea huu upuuzi uliozuka ambapo mashirika na watu wasio waislamu eti kuandaa futari na kufuturisha. Hivi inakuwaje kama hakuna namna mtu asiyefunga kuwafuturisha waliofunga kama siyo rushwa na kusaka umaarufu?”
Kapende anakula mic, “Shehe Mijjinga imekuwa kama umeyasoma mawazo yangu! Hata nami napinga na kushangaa huu mchezo wa hatari. Iweje mashirika yasiyo na dini kufanya mambo ya kidini kama siyo kutangaza biashara zao?”
Mipawa anaingilia kati, “Hakuna walioniacha hoi kama lile kampuni fisadi la simu ambalo limefunga mitambo mibovu na kutulangua huduma eti nalo kufuturisha.”
Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu, anakwanyua mic, “Msemayo yana mashiko hasa ikizingatiwa kuwa makampuni mengi yanayojitia kufuturisha mengi yanakwepa kodi na kutoa huduma mbovu. Je mnafahamu kuwa kupiga simu kwenye kaya yetu ni aghali na shida kuliko kaya jirani? Heri wangeshughulikia jinai kama hii badala ya kuwatumia waumini kuficha uchafu wao ili waonekane wanawajali wakati wa wanawaumiza.”
Sofi hakubaliani na Msomi. Anakatua mic, “Jamani mnataka mfanyiwe nini ndiyo mridhike? Sasa suala la kulipa kodi au kutolipa kodi kuwa na imani au kutokuwa na imani linaingiaje kwenye kutenda wema kama vile kufuturisha waumini?”
Mheshimiwa Bwege hangoji wengine wavuruge. Anadandia mic, “Da Sofi unamaanisha kuwa hata shetani akifuturisha basi tupwakie kama nguruwe, mbwa na fisi siyo? Kufuturisha kuna sharia na kanuni zake dada. Hata manaswara wanapofunga wanakuwa na namna yao ya kufuturu. Hivyo, nakubaliana na  wanaoshuku mchezo huu ambao nao ni aina fulani ya ufisadi.” 
Mzee Maneno anachomekea, “Wape vipande vyao shehe Bwege wajue kuwa sisi ni mashehe wa nguvu ingawa wapo hata mashehena miongoni mwetu.”
Mpemba anauliza, “Shehe mbona wantisha. Hao mashehena akina nani unosema hapa?”
Mheshimiwa Bwege anasema kwa utani huku akimtazaman Mbwamwitu, “Unadhani kiumbe kama Mbwamwitu ni shehe au shehena?”
Mbwamwitu anacheka na kusema, “Shehe au shehena yote poa tu ilmradi nipate changu au vipi? Mie nikikaribishwa hata na sheitwan naramba tu.”
Mgosi Machungi ambaye alichelewa kutokana na kupitiwa na usingizi anakula mic, “Kwa sisi mashehe azima tiseme wazi wazi kuwa makampuni tena yenye kutia shaka kufutuisha ni kuutukana usiam. Hatiwezi kunyamazia uchafu kama huu eti kwa vie tinapata iziki. Mashehe wa kwei kama sisi tinaogopa kula haamu bwana. Si vizui kwa makampuni tena ya kitwahuti kufutuisha. Na hii ni fatwa natoa kama shehe mwenye msimamo.” Kijiwe hakina mbavu kwa jinsi shehe Mgosi anavyopitisha fatwa.
Kanji ambaye anaonyesha wazi kutovutiwa na mada anaamua kutia guu. Anakomba mic, “Nyinyi dugu yangu nini napata nyinyi. Siku hizi feza iko tabu bwana. Kama kampuni nakaribisha veve futuru nenda future. Napunguzia veve zigo ya nunua futari sasa wakati nalangua kila sokoni.”
Msomi anarejea, “Ngoja tuseme ukweli bila kupindisha. Tatizo hapa ni kubwa kuliko kufuturu na kufuturisha. Tatizo ni kwamba kaya yetu imegeuka taifa la kufadhiliwa hata kwenye vitu vidogo kama milo. Kama tunaishi kwa kuomba omba wakati tumejaliwa uchumi lakini tunaukalia kwanini wanaojua udhaifu wetu wasiutumie kutudhulumu, kutudhalilisha hata kuingilia imani zetu kama mnavyoona? Dini ya makampuni na wafanyabiashara ni faida na mungu wao ni fedha. Hii yote mnayofanyiwa ni danganya toto na kuwaonyesha kuwa hamnazo na ni waroho wanaoweza kupwakia kila kitu hata kama ni halali au haramu. Wapi imeandikwa kwenye msahafu kuwa asiyekuwa muumini anaweza kumfuturisha muumini?”
Sofi leo kapania. Anakwanyua mic na kusema, “Mbona mnauliza majibu badala ya maswali? Kwa taarifa yenu kutenda wema ni uumini tosha bila kujali anayetenda kama ana shahada au la.”
Msomi anajibu, “Uumini ungekuwa rahisi hivyo mbona kila mtu angekuwa muumin! Kutenda wema ni kutenda wema na kuwa muumini ni kuwa muumini. Ni vitu viwili tofauti. Maana ukijumlisha hivyo, unamaanisha kuwa na wakristo au wasio waumini wa dini yako wote ni wa dini yako. Hii ni hatari.”
Kijiwe kikiwa kinanoga si adhana ikapigwa! Acha tuchangamkie tenda hasa usawa huu wa ukapa kutana na ukwete!
Chanzo: Tanzania Daima Julai 8, 2015.

3 comments:

Anonymous said...

Kufuturisha kuna sharia na kanuni zake KAMA KITU HUJUWI ULIZA
HAKUNA KANUNI ZA KUFUTURISHA MWALIMU

Anonymous said...

kufuturisha kanuni zake ndio zipi hiozo wacheni kuambukiza watu

Anonymous said...

huyo harudi hapa yeye anataka anachosema yeye ndio watu wakubali hakuna majadala huuo sio ndio udictetor

pokea maoni ya wenzio pia