Saturday, 18 July 2015

Urahis: Nusu Mlevi kudedi!

 Baada ya kuangukia pua na kutoka patupu kwenye mbio na harakati za kutia nia ya kusaka urahis, Mlevi nimejikuta kwenye matatizo usipime. Kwani wakati nikitia timu nilitegemea kuwa umaarufu wangu na kutembeza njuluku vingenijenga asijue vingenibomoa. Sasa nipo najuta na kuangua kilio kama Kanji baada ya kupata hasara. Ndoto imeyeyuka hata la kushika na kufanya sijui. Nilichodhani kilikuwa ndoto kumbe kilikuwa jinamizi ambalo sasa limegeuka msalaba mwinge shingoni mwangu. Hata Bi Mkubwa anaishia kunipa karata sorry talaka baada ya kuukosa u-First Rider. Alikamia kuunda bonge la NGO ili achange njuluku kama hana akili nzuri. Marafiki zangu walionizunguka zama za kuusaka urahis wote wamenikimbia na kujiunga na mtarajiwa. Ama kweli sikujua kuwa binadamu wakati mwingine ni wajalaana usipime. Bi mkubwa naye usipime. Naye presha imempanda hadi anazimiazimia kama kisimu cha mchina kwa kuukosa u-first-raider ambao licha ya kumtajirisha ungewatajirisha pia ndugu zake hasa usawa huu ambapo urahis umegeuka enterprise ya kutengeneza njuluku haraka na kwa mazabe bila kunyea debe.
Hivi ninavyoandika nimebaki na mshirika mmoja yaani daktari wangu ambaye amenionya nipunguzi mawazo vinginevyo presha inaweza kuninyotoa roho wakati wowote. Kwani daktari wangu ana wasi wasi sana nami. Anasema presha yangu iko juu kuliko wakati wowote.
Hakuna kinachoniuma na kuniumiza kama kuona washikaji na wapambe zangu wakinigeuka. Njuluku wamekula na sasa hawaniabudii tena. Wamenitelekeza huku wakinionyesha wazi watakwenda kuwapa tafu wabaya wangu.
Kwa hasira na uchungu nimeamua kuvunja kambi. Maana haikuwa kambi kitu bali kamba ya kulia njuluku zangu huku wahusika wakiniegeuza juha na hamnazo kwa kunipa ushauri ulilenga kuwanufaisha wao wakati nikijikaanga mwenyewe kwa mafuta yangu kama ngisi.
Hata jamaa zangu wa magazeti ndiyo usiseme. Walizoea kunizonga kila uchao ukiachia mbali kunibeep na kunitoa mshiko ili waniandike vizuri. Sasa nimeangukia pua hawataki hata kusikia habari zangu achilia mbali kuniona. Kila nikiwapigia simu hawapokei. Wananidengulia anajua Mungu mwenyewe. Zama za mchakato nilifanya kosa moja kubwa. Kwani nilijigamba na kuwa karibu nao nikidhani walikuwa marafiki wa kweli kumbe siyo. Wale niliodhani urafiki wetu haukuwa wa barabarani waliishia kunitosa na kuniacha nikihangaika barabarani hata wasione aibu wala kunionea huruma. Ama kweli siasa ni nchezo nchafu kweli kweli. Nani alitegemea kuwa mshirika wangu kama Njaa Kaya angenichunia na kutumika kama kiongozi wa kunishambulia na kuwahimiza wajumbe wasinipe kura za kula? Leo hii namuona akiwa beneti na Joni  Kanywaji Makufuli wakiangusha vicheko wakati mimi nikiangusha kilio. Hanipigii hata simu kunijulia hali pamoja na kujua kuwa presha yangu na ya Bi Mkubwa zimepanda. Ama kweli penye riziki hapakosi hiana!
Sikujua kuwa wengi walinichukia hadi yaliponikuta. Waliokuwa wakiniita rahis mtarajiwa na mheshimiwa wote wametoweka. Kumbe walikuwa wakinisanifu na kuniingiza mkenge ili wale vyangu halafu waniache Solemba!
Huwezi kuamini kuwa umati niliokuwa nikipata wakati nikisaka wadhani ulikuwa ni wa wabaya wangu walionisanifu na kuniingiza mkenge ili wale njuluku zangu. Nani anaweza kuamini kuwa hata yaliponikuta ya kunikuta wa walishindwa hata kuja kuvunja tanga baada ya msiba huu mzito wa kisiasa?
Hata hivyo, nao wana bahati tena ya mtende. Maana nilivyokuwa nimepanga kuwatumia kama daraja kufikia ulaji kama ningetoboa wangekoma waishie kulia na kusaga meno. Hata hivyo, sikujua kuwa tulikuwa tukicheza mchezo wa karata tatu. Kwa lugha nyingine tulikuwa tukitumiana na kutapeliana huku kila mtu akivutia upande wake. Sikujua kuwa siasa wakati mwingine ni kama ukahaba. Hakuna aliyeniongezea presha kama habithi mmoja kati ya waliokula njuluku zangu. Maana, nilipomtwangia simu kuja tupange jinsi ya kutoka alinitolea nyodo kuwa nisihangaike bure kulilia njuluku zangu zilizoliwa kwa vile nilizichuma kifisadi, kirushwa na kiwizi. Nilipomtaka athibitishe kwa kuleta ushahidi alikata simu na kuniacha nikikosa pumzi.
Nawashauri wenzangu wenye ndoto za Alinacha za kuwa marahis kama mimi wafikirie mara mbili. Heri kufanya mambo kimya kimya kama alivyofanya John Kanywaji Makufuli kuliko kujilisha pepo kwa kuwakaribisha wapembe nuksi na walaji ambao watakuacha pakanga unapoangukia pua kama mimi.
Kwa sasa nikiangalia umri ndiyo umenipiga chenga huku udhu ukiota mbawa. Sijui nitafanya nini ili lau nirejeshe nusu ya mshiko niliopoteza kwenye ndoto uchwara za kuula nikaishia kuliwa? Nadhani kwa sasa lazima nami nijigonge kwa Joni Kanywaji Makufuli ili akipata utukufu wake lau anipe kibarua ukiachia mbali kunyamazia mazabe yangu. Maana juhudi zangu za kuusaka urahis, licha ya kutaka kula kwa dezo kwa mikono na miguu huku nikipiga mbizi kwenye sinia, ilikuwa ni kujihakikisha usalama kwa mustakabali wangu hasa ikizingatiwa maskandali ya wizi wa njuluku za walevi unaoninyemelea tangu zama za Nchonga.
Kwa vile nimeishazoea kubwagwa, lazima nirejee kwa walevi wangu lao nigombee uishiwa niendelee kuwa kwenye gem.
Nimalizie kwa kuwaomba wale wote wenye mapenzi nami lau kuja kunijulia hali hasa wakizingatia kuwa hakuna anayeweza kukataa au kutohangaikia ulaji rahis na wa dezo kama urahis. Hivyo, wasinitenge na kuniona kama ukoma wakati walikula vyangu. Nawashauri walevi waache mchezo wa kuwashawishi wanasiasa kutumia njuluku kuwanunulia kila upuuzi kuanzia kanywaji bangi vibandiko na kanga kwani wanawapa wengi motisha kuwaliza japo nao wanaweza kulizwa kama mimi.
Tukutane wiki ijayo. Pombe kwa urahis, pombe kwa walevi makufuli kwa mafisadi. Kanywaji hoyee! Kanywaji na Makufuli hoyeee!
Chanzo: Nipashe Julai 17, 2015.

No comments: