Saturday, 11 July 2015

Mlevi atabiri kufunjika ndoa za kipolitiki

Leo gwiji natabiri kuvunjika kwa ndoa za kipolitiki. Huu ni utabiri sahihi japo wa hatari. Hivyo, yawapasa kutafakari na kuchukua tahadhari. Natabiri bila kusita lau mchukue tahadhari. Utabiri huu ni hakika. Hivyo, uzingatieni ili kuiepuka nakama. Ada yangu ni kusema. Sitaki mseme hakusema wakati nilisema. Najua mtalaumu japo sitaki mnilaumu. Nasema mtajilaumu kama hamtazingatia. Najua mtasikia mjifanye hamsikii. Ila siku ikijiri mtasema alisema tena nazidi kusema kuwa ndoa nyingi za kisiasa zitavunjika
Nitabiri Mzito Kabwela kutalikiwa akiisha kuadhiriki. Kwani siku zilipita? Si mnamuona anavyohaha na kuadhirika. Juzi kaja na yada yada. “Oh nitataja majina ya walioficha fedha Uswizi ya Uswazi.” Alipoambiwa taja kwani alitaja. Ataje nini wakati hana la kutaja? Mbona Dokta Silaha pale Mwembe Yanga alitaja hata ndege wakamsikia na wote wakamwamini. Nini kinamzuia kama siyo kukosa la kusema na wale wa kuwataja? Badala ya kutaja aliishia kujing’ata huku akisaka sifa asizipate.
Kwa kitaalamu hawa nyemelezi na wasaka tonge huitwa political hookery whores. Wapo wengi na mtawajua. Hamkusikia mmoja toka CHAKUDEMA akitangaza kuomba talaka ufikapo wakati wa uchakachuzi. Nani aliamini kuwa zee zima lingekuwa hovyo kama Kimdunge Ngumbaru Mwehu aliyejigeuza nepi ya Luwasha?
Sasa nasema bila kumung’unya kuwa ndoa nyingi ziko msambweni. Kule kwa akina yakhe mambo yeshaanza. Yule bi harusi mwenye madevu keshapewa vipande vyake akibaki kutishatisha kuwa muhula huu patachimbika bila jembe. Utabiri wangu unanionyesha kuwa kule kutakuwa na zali usipime hasa ikizingatiwa kuwa mmoja wa mabibi harusi umri ushamuacha. Hivyo, shurti afe na mtu hata kama ni kung’ang’ania lau aoelewe kwa lazima.
Gwiji sifanyi usanii. Nafanya kweli tena kweli haswa. Natabiri tena si kwa kuokotaokota kama yule shehe kidhabu aliyekuwa akitumiwa na waganga njaa na matapeli wenzake kutishia watu kifo asijue kitamnyakua. Natabiri bila kuficha kuwa uchakachuaji utakapokwisha msishangae watu kufikishwa The Hague baada ya kutembeza undavandava na kila aina ya vipigo.
Nilitabiri wengi hawakunielewa. Wakumbuka nini nilitabiri? Nilitabiri utitiri wa wasaka urahis toka Chama Cha Mafisi (CCM).  Nilitabiri kuwa wataibuka wengi wakiutaka ulaji rahisi kiasi cha kuacha chama kimegawanyika na kuparaganyika kisijue nini cha kufanya. Nilitabiri marafiki kugeukana. Kwani mara hii mmesahau vilio vya wale waliowahi kujinadi kuwa urafiki wao na wanene si wa barabarani. Wako wapi sasa kama si barabarani wakihanikiza wale wale waliosema ni washikaji wao wawaunge lau mguu kama si mkono?
Nawatabiria CHAKUDEMA wakae mkao wa kukosa baadhi ya vidhabi. Naona kidhabi mmoja kule Simiyu akijiandaa kuomba talaka. Mwamjua kwa jina. Basi kama hammjui ngoja niwatonye. Anaitwa Joni Magalele Ni Buda na kweli ni buda kweli kweli.
Kwa ndugu zangu wa KAFU ukweli ni kwamba ngoma ni nzito.  Hapenyi mtu hasa usawa huu. Mtatoana ngeu na kuishia kuwa washitakiwa. Kisa? Kutaka ulaji rahis.
Je mnakumbuka kuwa nilitabiri kuwa mbayuwayu atawatema wale waliomtegemea huku akihangaika kuokoa roho yake?  Kwani hajui aliyofanya kwa miaka yote ya uzururaji na utanuaji? Anajua na wote mnajua kuwa aendako pakanga asipopata mtuwe ili amsitiri kama alivyomfanyia Tunituni ilipoibuka Kiwila.
Natabiri hali itabana. Wengi wataumia kwa presha. Wapo watakaopoteza mishiko mikubwa baada ya kuwekeza kwenye ndoto za kupata urahis ili wale kirahisi. Naona laana ya mwenyewe asiyetajwa hovyo aliyeniamuru kutabiri. Naona ikiwatafuna wengi walioba na kujilimbikizia minjuluku wasijue wataitema kwenye mambo ya hovyo na ya ndotoni kama kuwania urahis. Naona wengine wakilazwa baada ya kipenga cha mwisho kupulizwa. Wengi watavuka mipaka ya vyama vyao wakihamia vingine. Wapingaji watapata mtihani mkubwa wa kuwapokea au kuwakataa makapi na makahaba wa kisiasa wanaotafuta pa kuponea. Watajikuta kwenye kishawishi kikubwa cha yupi wampokee na yupi wamwengue. Wataanza kugombana wao kwa wao tokana na ujio wa wageni wao watalikiwa watarajiwa. Hali itakuwa tete usipime. Patakuwa hapatoshi kwenye uringo wa siasa. Visasi visa na mikasa vitahanikiza.
Natabiri kuwa rushwa itatembea kwa kiasi ambacho wengi hatukutarajia wala hatujawahi kushuhudia. Sarafu ya Bongolalaland itahujumiwa na kushuka kama vile inaharisha. Nadhani niliwahi kulitabiri hili japo wengi walidhani ni bangi zangu na ulabu. Ngoja yatakapowakuta ndipo watanikumbuka wasijue nini cha kufanya. Msifanye mchezo na maisha hasa usawa huu mnapohenyeka kutafuta walaji wengine. Nawaonea huruma hasa kipindi hiki ambapo urahis umegeuka ulaji rahisi. Wengi sera yao ni it is our time to eat. Wataitana kila aina ya vinyamkera na nyemelezi wawageuze asusa kama mtachagua kwa pupa. Msikubali tena kuingizwa mkenge kama huu unaoisha. Chagueni wale mnaofafana nao ili wawafae hapo baadaye. Najua wengi hawataambua kitu kwa vile naongea kinabii. Sina jinsi ya kuwasaidia zaidi ya kuwanasihi wajielimishe ili lau waweze kujua mambo makubwa kama haya nitabiriyo.
Nasema bila kusita kuwa jihadharini na vyangudoa wa kisiasa. They are looking for someone to hook on. Wakishatimiza haja yao wanawapiga kibuti ding ding ding na mnabakia kulia na kulalama huku wao wakiwacheka. Manaowaona kondoo sasa ni mbwa mwit wa kesho watahadharini. Wasikilizeni kwa makini mkitia nukta kila hoja ili muepuke mitego ya kipumbavu.
Namaliza kwa kurejea angalizo langu. Sitaki mseme sikusema wakati nilisema. Nataka siku ikifika mseme hata kwa kujilaumu kuwa gwiji alisema japo hatukumsikiliza. Nataka mseme alituonya ila hatukuonyeka. Msema tulisikia ila tukajifanya hatukusikia kama hamnazo.
Kwa leo ni hayo tu. Ni masahibu ya kuvunjika ndoa za kipolitiki.
Chanzo: Nipashe Julai 11, 2015.

No comments: