Friday, 3 July 2015

Mlevi kushitaki kaya ICC

  • International Criminal Court to deliver first verdict, 10 years and £ ...
                   Taarifa za nesi mshenzi, mnyama, mjinga, mpumbavu na muuaji kumkatalia mjamzito Rhoda Bujiku kule kwa akina Ng’wadila ng’waguku na ng’wa nyingi kujifungulia kwenye zahanati hadi akijifungulia chooni, zimekera hakuna mfano. Hivyo, nimeamua kufanya jambo moja la mbolea hata kama ni kilevi. Nimeamua kuchukua hatua ambayo itawakomboa akina Rhoda popote walipo kayani na ikiwezekana duniani.
           Ngoja kwanza nikuchapie. Vyombo vya umbea viliripoti kuwa nesi aitwaye Constancia John kule Maswa nkoani Simiyu alimnyima huduma mtajwa hapo juu eti kwa vile alikuwa anazaa kila mwaka. Jamani, alitaka azae kila baada ya miaka kumi au asizae?
          Pamoja na kosa hili kuwa kubwa na la kinyama, wengi tulidhani lisirikali lingetoa japo kauli ukiachia mbali kumkamata Constancia na kumnyonga mara moja. Haikuwa hivyo. Baada ya kuona lisirikali limekula pini lisijitetee kwanini lisirambwe bakora, nimeamua kuipeleka kaya kwenye mahakama ya kimataifa ya jinai almaaruf kama International Criminal Court (ICC) The Hague Uholanzi.  Ni mahakama hii iliyomtia jambajamba imla wa Sudani Kaskazi hadi akakimbia bila nguo kutoka Bondeni alikokuwa amekwenda kutanua na walafi na walaji wenzake wenye madaraka ambao hutumia kila sababu kwenda kuzurura. Siju wazururaji wetu wataishi vipi baada ya kuutema ulaji. Naona yule anatikisa kichwa akidhani natumia hii kama gea ya kwenda kutanua kama jamaa aliyeunguza njuluku zetu kwenda majuu eti kuaga utadhani kule ndiko alikopigiwa kura. Kama si kiherehere na kujigonga ni nini? Mtu mzima hovyo!
          Nina sababu za nguvu kadhaa za kuipeleka kaya hii ya Bongolalaland aka Danganyika kule The Hague.
          Mosi, nataka mahakama itangaze unyama wanaofanyiwa wajawazito kama jinai dhidi ya ubinadamu na atakayebainika kutenda kosa hili anyongwe baada ya kucharazwa bakora mia akiwa uchi huku akiwekewa pilipili na chumvi kwenye makalio baada ya kurambwa bakora.
          Pili, naipeleka kaya kwa vile imeshindwa kukomesha mauaji ya halaiki ya watu wenye ulemavu wa ngozi na vikongwe. Pia nitapendekeza watakaopatikana na hatia kwa kufanya mauaji haya ya kishenzi na kinyama watupwe kwenye mto uliojaa mamba ili waone utamu wa mchezo wanaocheza. Nilikuwa nimejitahidi kuvumilia. Hili la kumtesa mzazi limeniuma kiasi cha kuamua kufanya kweli sasa. Anapiga picha huyu aliyetendewa hivi angekuwa bi mkubwa wangu, dada, shangazi , shemeji au yoyote awaye. Je huyu mjalaana aliyetenda unyama huu angemfanyia mkeo au nduguyo zaidi ya kumpiga mapanga ungemfanya nini? Sishauri watu wapigane mapanga. Hasha. Nakwenda the Hague kukomesha mzizi wa fitina. Hivyo, msishangae mkisia rahis wenu ananyea debe mjue kijogoo mimi ndiye nimemsababishia hii kitu.
          Tatu, napanga kuipeleka kaya ICC kutokana na kushindwa kupambana na ufisi, ujambazi na ufisadi ambao kimsingi nao utangazwe kama jinai dhidi ya ubinadamu kwa vile unasababisha vifo vya mamilioni ya watu wetu wasio na uwezo wa kujitibia nje. Huyu bi mkubwa angetoa njuluku hata kiduchu angejifungua kama malkia wa Ukamerunini.
          Nne, nitafungua kesi ya kutaka kumlazimisha rahis kuwakamata mafisadi na kurejesha njuluku zetu zilizofichwa kwenye mabenki ya Uswazi na kwingineko. Maana wanaoficha njuluku nje wanaua wachovu na walevi wengi bila sababu yoyote isipokuwa roho mbaya na uroho wa kishetani. Naana mijitu mingine ina fedha ambayo haiwezi hata kuitumia hata kama ingeishi miaka elfu. Sasa kama si kichaa na roho mbaya mijitu ya namna hii inaiba kupata nini? Je mijitu kama hii ikichomwa moto kama vibaka itakuwa ni makosa? Ukichaa si kuokota makopo tu bali kufanya vitu visivyo vya kawaida. Mijitu yenye njuluku inayoendelea kuiba ni migonjwa ya kichaa inapaswa kuishi Milembe na si Masaki, Mikocheni na Uzitoni ikitanua.
          Katika kesi hii ya mafisadi nitafungua na kesi nyingine ndogo ya kuzuia watuhumiwa wote wa ufisadi ambao ni sawa na ugaidi kwa umma wasimamishwe kugombea cheo chochote hata kama ni cha kifamilia. Hapa ndugu zangu akina Eddy Luwasha, Endelea Chenga, Ni Ziro Kadamage, Hezeh Maige, na wengine wengi lazima wakatwe na kama vyama vyao vitalazimsha, wananchi wawakamate na kuwa-Gaddafi hadharani au vipi?
          Tano, nataka mahakama ya kimataifa itangaze uchakachuaji kama kosa linalokinzana na haki za binadamu. Kwani, kwa kuchakachua uchaguzi na kuzalisha watawala majambazi, wahusika wanakuwa wameua watawaliwa indirectly but maliciously and with malice aforethought. Acha nitumie lugha ya kipilato wajue nami ni learned brother hata kama nakata kanywaji na bangi. Bila bangi huwezi kuwa wakili mzuri.
          Sita, nitafungua kesi nyingine ya kudai uchakachuaji wa katiba ya wananchi ni uuaji wa halaiki ambao unapaswa kupigwa vita dunia nzima. Hii ni baada ya kuona walevi wamesahau kabisa kadhia ya katiba mpya ambayo iliuawa na wale waliofanya hivyo, baadhi yao eti wanautaka urahis. Ili watufanye nini kama si kutuua nasi kama walivyoua katiba? Pia katika kesi hii nitahakikisha mahakama inatangaza kuwa kosa la jinai kwa vikongwe vinavyojifanya vingunge wa vyama kupigwa marufuku kutumia ukongwe wake kuwaunga mkono mafisi na mafisadi kama anavyofanya Kevin Kimdunge Mwehu anayejikomba kwa Eddie Luwasha hadi walevi wanapata shaka kama hakuna zaidi nyuma ya pazia. Maana hata bi mkubwa wake Luwasha hawezi kujimenya kama anavyojitiatia huyu kibabu mwenye miaka mia tano.
          Funga kazi kwenye kesi hii ni kufungua kesi ya kuzuia chama chenye wanachama wote wanaotaka kuwa marahis kipigwe marufuku kushiriki siasa. Maana hakina sifa. Kinapaswa kuzuiliwa ili kiende kikatibiwe kichaa kule Milembe badala ya kuendelea kutujazia mbu. Naona yule anatikisa kichwa akishangaa hili linakuwaje kosa la jinai. Kumbe hajui kuwa wahusika mnaowaona wakijinadi wanatumia njuluku za wizi wanazowaibia walevi ukiachia mbali kufanya vurugu na fujo kiasi cha kuondoa amani kayani?

See you!
Chanzo: Nipashe Julai 4, 2015

No comments: