Monday, 20 July 2015

Tulijua Mahiga na Ramadhan wasingepita


          Baada ya kutangaza au kutia nia kwa wanachama wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wengi tulihoji mantiki ya wageni nao kutaka urais tena kupitia chama chenye kila aina ya mizengwe. Wageni hawa katika siasa za ki-CCM si wengine bali jaji mkuu wa zamani Augustine Ramadhan au mwanadiplomasia ambaye hakuonyesha tangu mwanzo kuwa angejiingiza kwenye siasa Augustine Mahita ni ushahidi kuwa CCM imechafuka kweli kweli.
Kwa wanaojua mchezo huu mchafu wa siasa, walihoji zaidi mantika ya wahusika hawa walioonekana kuwa wanagezi, wasio na mitandao wala uchafu kujiingiza kwenye tanuri la moto. Wapo walioona kuwa CCM baada ya kufilisika kimikakati, kimbinu na kimaadili–tokana na kuwa vigogo mafisadi, wazee, wachovu na wachafu–kama iliwahitaji wahusika lau kuweza kupata mtu safi wa kuinasua kwenye mitego iliyomo.  Kudhani hivyo ilikuwa kosa. Kwani, wapo walioona kuwa wageni hawawezi kuaminiwa madaraka makubwa kama haya wakati wakubwa wa chama wakiwa na skandali kibao ambapo wangetaka mwenzao wa kuwalinda. Nani–kwa mfano–angemwamini mwanajeshi–tena mwenye wa cheo cha juu na mwanasheria jaji–urais ili awaumize wenye maskandali yao?
          Sasa jogoo –sijui bata –limewika Dodoma. Walioonekana kuwa safi wameenguliwa, waliovuma kadhalika. Badala yake, wameletwa wengi ambao hawakutarajiwa. Kwa kuwakatas wasafi, CCM imeonyesha na kuziweka wazi hisia kuwa haiwezi kuhitaji watu wa namna hii kwa kuogopa kuigeuka kuwa kweli.  Kwa kuwaengua makada wake wenye ushawishi mkubwa, si ajabu CCM ikajikuta mahali ilipoishia KANU nchini Kenya kama makada hawa kama vile Edward Lowassa, Fredrick Sumaye na wengine wataamua kujiunga na upinzani kwenye uchaguzi ujao chini ya makubaliano fulani. Je kwa siasa za Tanzania hili linawezekana? Nina shaka nalo.
Pia ukweli kuwa mgombea mmojawapo aliyepenya, John Pombe Magufuri si mwenye mawaa mengi, linafanya kambi zote mbili yaani CCM na upinzani kupata wakati mgumu. Kama mitandao ya CCM itaunganisha nguvu, upinzani utakuwa na kibarua kikubwa japo inategemea kati ya watano waliovuka kihunzi cha kwanza atachomolewa nani. kama tulivyosema hapo juu, CCM itakuwa na kazi ngumu ya kuja na mtu anayeuzika ambaye katika watano waliopita  anajulikana kutokana na utendaji kazi wake. 
Tukirejea juu ya ni kwanini Mahiga na Ramadhin wasingepita, walikuwa na sifa moja kubwa ya usafi tofauti na wenzao. Maana, zaidi yao, wote waliojitokeza walikuwa wachafu bila kujali sifa ndogo ndogo walizojipa ili kuwazuga na kuwaingiza mkenge wananchi na wapiga kura.  Wapo waliochafuliwa na uroho, tamaa, au udokozi kama mwenzao alivyowahi kuwananga. Wapo waliochafuliwa na uongo yaani kusema hili wakatenda hili. Wengine walikuwa na sifa ila umri uliwatupa mkono hasa ikizingitiwa kuwa wengi walianza na awamu ya kwanza na sasa wako na tano. Wapo wababaishaji waliokuwa wakitafuta sifa na namna ya kuwa karibu na atakayepitishwa au kushinda ili wapate mlo wao. Hawa kimsingi, ni waganga njaa au wachumia tumbo wanaotafuta ulaji mdogo na si ulaji mkubwa kama urais. Walikuwapo waviziaji wanaotegemea kubebwa ima na jinsia zao au makundi na upuuzi mwingine. Walikuwapo akina Uvuruge waliolenga kuwakwamisha wenzao kama si kutumiwa na mahasimu wao. Walikuwapo wasaka umaarufu wa shilingi mbili na upuuzi mwingine kama huo, pia wapo wasiojua hata kilichowasukuma kugombea.
          Kwa mfano unajiuliza mantiki ya kapuku aliyetegemea michango ya hisani kugombea tena kwa kutoa milioni moja aliyoomba. Je huyu kweli alikuwa serious? Je alikuwa akitafuta nini kama si umaarufu na wengine kuondoa ushamba kwa kupata fursa ya kuchangiwa waizunguke nchi? Hata ukiwauliza wote waliokuwa wamejitokeza nini sera zao, utaambulia maajabu. Wengi hawakujinadi kwa sera zaidi ya sifa binafsi.
Wageni walikuwa bora. Lakini kuwaamini ilikuwa vigumu kwa kuhofia hatari  ambayo wengeweza kusababisha wakiwa madarakani hasa kufumua uoza uliopo ambao ndiyo njia kuu ya ulaji kwa walio wengi madarakani.Hivyo, hawa walifaa kwa umma lakini  walikuwa hatari kwa mafisadi. Pia upo upande wa pili. Sasa CCM imeonyesha wazi kuwagwana na kutowaamini wasafi. Je upinzani utalitumiaje hili kubadili upepo?
          Kama watanzania wataamua kutorudia makosa, hawana sababu hata moja ya kuichagua CCM tena. Kwani licha ya kuzeeka, kuchoka, imeishiwa na kuisha kiasi cha kustahiki kupumzishwa lau ijifunze. Na hakuna haja ya kuogopa kuiwajibisha CCM.  Kwani, haitakuwa ya kwanza. Tuliona vigogo wenzake kama KANU (Kenya) MCP (Malawi), UNIP (Zambia) na vingine vingi vilivyolizwa na nchi zikasonga mbele. Hivyo, kupata wagombea kama watajawa hapo juu bado si dawa kwa CCM ambayo haina tofauti na sikio la kufa.
Kimsingi Mahiga na Ramadhani wanaonyesha uoza wa CCM ambao hawawezi kuundoa kutokana na kanuni na ushawishi wa ndani ya chama. Hivyo, hata kama mmojawao angepitishwa wasingebadili lolote zaidi ya kubadilishwa. Kwa majina yaliyopitishwa, bado CCM ina kazi hasa kama waliotemwa wataamua kuiadhibu kwa kujiunga na upinzani kama ilivyotokea Kenya mwaka 2002.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 19, 2015.

No comments: