The Chant of Savant

Monday 13 July 2015

Warioba, CCM na sikio la kufa



          
Image result for photos of joseph warioba

 Baada ya kung’atuka madarakani na baadaye chamani kwa muanzilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) marehemu Mwl Julius Nyerere kilipata pigo ambalo pengo lake limeshindwa kuzibika. Maana, tangia wakati ule –karibu kila mwaka –CCM imekuwa ikiendelea kuporomoka hadi kuishi kwa matumaini na ubangaizaji utokanao na mchezo wa rafu kama vile kuchakachua uchaguzi na kufadhiliwa na mafisadi.Hivi karibuni mkongwe mwingine –kati ya wachache waliobakia na waliowashinda makuwadi na wasaka urais –mzee Joseph Warioba alikiasa chama chake ingawa sijui kama kitamsikiliza hasa ikizingatiwa uhuni aliokwishafanyiwa na wakubwa wa chama na serikali.

Warioba alikaririwa akisema, “CCM inakabiliwa na wakati mgumu wa kupitisha jina la mgombea urais kutokana na waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kufikia 38, na mpaka sasa imekuwa ni vigumu kutabiri atakayepitishwa, jambo ambalo halikujitokeza wakati wa upitishwaji wa mgombea urais wa chama hicho mwaka 1995 na 2005.” Anachobainisha jaji Warioba hapa ni kwamba demokrasia lazima iwe na mipaka. Wote tunajua kuwa uhuru bila mipaka ni wendawazimu. Kimsingi, sasa kinachoitwa demokrasia ndani ya chama kisicho na historia ya demokrasia zaidi ya kuipinga si demokrasia kitu bali wendawazimu na uroho wa madaraka wa kawaida. Haiwezekani watu wastaarabu wenye kukubaliana na kuelewana wakaruhusu kila mmoja autake ukuu. Je kama mwili wote ungekuwa sikio kichwa kingekuwa wapi? Mbona vyama vya upinzani ambavyo viliteseka na kuhakikisha taifa linaingia kwenye demokrasia ya vyama vingi havina utitiri wa wagombea?

Wahenga walisema: Sikio la kufa halisikii dawa. Warioba kwa mapenzi na uzalendo wake vilivyotukuka amejitahidi kuwasaidia wenzake. Je watamsikiliza wakati walishamdhalilisha hasa baada ya kuwapa ukweli ambao hawakutaka kuusikia? Nani amsikilize mzee aliyepitwa wakati kama Warioba ambaye badala ya kuchangamkia madili anahagaishwa na maadili? Warioba ni sawa na mtu aliyeko nyikani. Warioba amejitahidi kufanya kile ambacho kimewashinda wengi. Amejitofautisha na akina Kingunge Ngombale Mwiru na Paskari Ndejembi wanaoweza kukodiwa na watia nia kama bodaboda. Amewashinda akina Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Salmin Amour na Amani Karume wanaoonyesha kuvizia upepo. Warioba amefanya kile ambacho waingereza huita to stand up and be counted au kuwa tayari kufanya maamuzi magumu hata yakimaanisha kulaumiwa. Hakika wamebakia wachache wa namna hii. Laiti CCM ingewasikiliza.

Warioba aliongeza, “Waliotangaza nia wamekuwa wakieleza sera zao na ukiwasikiliza unaona kama walikuwa wagombea binafsi hivi kwa sababu CCM ina sera, wanayo ilani ambayo ipo tayari na yeyote atakayepeperusha bendera ya CCM lazima ajikite kwenye ilani ya chama.” Kama siyo sikio la kufa au tuseme kuchanganyikiwa na kuparaganyikiwa ni nini kwa chama ambacho kilitumia kila hila kupinga mgombea binafsi kujikuta kikiwa na wagombea wenye kila sifa za mgombea binafsi? Je ni laana au historia kutaka kurekebisha mambo? Je CCM watauvuka huu mtihani unaolenga kupima na kuonyesha unafiki na upogo wao salama bila kuwasikiliza akina Warioba? Je kama hali ni hii CCM inayokutana hivi karibuni kuteua na kupitisha mgombea wake itampata wapi wakati waliojitokeza wote hawafai na wala hawana mpango na sera zake? Laiti akina Abdulramahan Kinana katibu mkuu wa CCM wasingekuwa wamejiingiza kwenye siasa za usanii walipaswa kuwa na kibarua kigumu cha kuueleza umma mantiki ya kupambanisha wagombea binafsi kumpata mgombea wa chama.

Je kwa CCM kutekwa na wagombea binafsi hadi ikawahalalisha kama wagombea wa chama siyo kuishiwa na kugeuka chama tegemezi ambacho hakina mtaji zaidi ya kutegemea ubabe wa watia nia? Je CCM hii kipofu itashidwa kumpitisha fisadi kama alivyowahi kutahadharisha mmojawapo wa wagombea ambaye pia ni mtoto wa wa mwanzilishi wa CCM, Makongoro Nyerere aliyekaririwa akisema, “Mojawapo ya matatizo ya chama chetu ambayo ni lazima Rais ajaye apambane nayo ni ukweli kwamba kuna majimbo ya uchaguzi hapa Tanzania ambayo kama mtu hutoi rushwa huwezi kupita.” Maneno ya Makongoro ambaye amejizolea umaarufu kwa kusema ukweli ni ushahidi tosha kuwa bila kuwa fisadi au tajiri CCM hupenyi. Je CCM itavuka kikwazo hiki wakati imekaa kimya wakati fedha zikimwagwa hata kabla ya kipenga cha mwisho kupigwa?

Je nini wana CCM na watanzania wengine wategemee? Jaji Warioba ana jibu, “Hawa ndio watakwenda kuchuja, sasa hapa itakuwa kazi ngumu na inawezekana kukawa na mgongano wa maslahi na hilo lisipoangaliwa linaweza kufanya mchujo ukaonekana kuwa haukuwa wa haki. Jambo hili linatakiwa kuangaliwa na hasa kwa kuwa kuna makundi.” Kwa lugha rahisi ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa CCM kuanguka kwenye mtego ikaamua kutokana na msukumo wa mtu na si sera. Hali inazidi kuwa mbaya hasa ikizingatiwa kuwa CCM ina gonjwa kubwa sana la mitandao ya kimaslahi ambapo karibu kila kiongozi ana mtandao wake kuanzia watangaza nia hata wale watakaowachuja.

Tumalize kwa kusema kuwa CCM sasa ni sikio la kufa ambalo halisikii dawa. Je CCM watamsikiliza au kumpuuzia mzee Warioba?
Chanzo: Dira Julai 13, 2015.

No comments: