Sunday, 23 August 2015

Dk Bilal hana sababu kujitoa CCM
              Kuna uvumi uliokuwa umezagaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa makamu wa rais Dk Gharib Bilal angejitoa kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM). Baada ya uvumi huu kuzagaa, ofisi ya Makamu wa Rais iliwahi kuzikanusha jambo ambalo ni jema na lenya nafuu kwa mhusika.
          Jambo ambalo ni vigumu kuelezea ni kwanini uvumi huu umemlenga Bilal na si waziri mkuu anayemaliza muda wake, Mizengwe Pinda, waziri mkuu wa zamani Fredrick Sumaye au vigogo wengine? Je ni wapinzani wake aliowahi kuwapa hali ngumu visiwani hadi akapewa umakamu wa rais au system iliyompa ulaji huo bila kutaka walioanzisha uvumi huu ili kupima maji au kuzidi kumbomoa mhusika? Je kuna chembe za ukweli kwenye uvumi huu? Je ni vyama vya upinzani ambavyo hivi karibuni vimevuna baadhi ya vigogo wa CCM baada ya kumaliza kwa mchakato wa utafutaji atakayepeperusha bendera yake?
           Kama utamuangalia Bilal kwa makini sana kufuatana na historia yake kisiasa, walioanzisha uvumi huu walipoteza muda wao kwa vile–kama ni kuleta changamoto mpya Visiwani kama alivyofanya kabla ya kunyamazishwa kwa kupewa umakamu wa rais–ameishazidiwa kete; au tuseme kuwekwa sawa. Kwani mchakato wa kumtafuta atayepeperusha bendera ya CCM visiwani ulishakwisha.       Kumbuka, Bilal aliteuliwa–si kwa sababu ya kupendwa–bali kuepusha balaa Zanzibar. Kwa wanaokumbuka sekeseke alilozua Bilal –akiungwa mkono na rais wa zamani Salmin Amour na alivyotaka kuipasua CCM –wanajua fika alivyokuwa mwiba kwa CCM pamoja na kupewa umakamu wa rais ili kufunika kombe mwanaharamu apite. Kwa vile Bilal alikubali kuwekwa sawa, hana tena ubavu wa kufanya lolote kisiasa hasa ikizingatiwa kuwa umri nao umeishamuacha. Uzuri ni kwamba Bilal na wapambe zake wanalijua na kulikubali hili. Hata yule aliyempa nguvu na support, hana tena ubavu zaidi ya kuuguza mavune ya ugonjwa na uzee ukiachia mbali kuondoka kwenye hadhira kisiasa.
          Pia Bilal anafahamu kuwa kwenye siasa za Tanzania ni mtu mmoja tu aliyekuwa na ubavu na ushawishi wa muda mrefu yaani Mwl Julius Nyerere.  Hivyo, kubebwa kwake na Amour–aliijua fika–lilikuwa ni suala la muda kabla ya historia kumweka kwenye kapu lake la sahau.
           Wapo wanaoona kuwa Bilal bado ana ubavu wa kuweza kulianzisha kama alivyofanya awali kiasi cha kuilazimisha CCM kumtengenezea ulaji wake wa miaka mitano.  Je ukweli na hali halisi ikoje? Hata akirejea Zanzibar, hana tena ule mvuto aliokuwa nao dhidi ya rais Dk Ali Mohamed Shein ambaye alichomolewa kwenye Muungano na kurejesha Zanzibar ili asiwavurugie wapakwa mafuta wa upande wa bara.  Sasa wakati wa kukaa kando umefika sawa na wengine kama vile Pinda na wengine wengi ambao walitemwa kwenye mchakato uliomuibua John Pombe Magufuli huku CCM ikimpoteza Lowassa na wapambe zake.
           Hata ukiangalia muda wote aliokaa ofisini, alibanwa na kuwa mtu wa kufungua makongamano na matamasha. Haijulikani kama ni kwa makusudi au bahati mbaya, Bilal hakujijengea umaarufu kama aliokuwa ameujenga makamu wa rais wa zamani marehemu Dk Omar Ali Juma aliyekufa kwenye mazingira ya utata kutokana na mitandao ya urais kumuona kama tishio.  Kwa muda wote aliokaa madarakani, alijiandalia hili. Kwani, hakuonyesha wala kuruhusiwa kuonyesha makeke. Je Bilal alijua na kulikubali hili hasa baada ya kujua kilichompata marehemu Dk Juma baada ya kuonyesha makeke ingawa hakuwa na nia mbaya?
          Hata hivyo, kwa wanaojua siasa za visasi na kuviziana, ilikuwa dhahiri kuwa Bilal alikuwa mtu wa kuja kwenye ofisi ya makamu wa rais aliyewekwa pale kwa lengo maalumu ambalo wengi wanalijua kuwa ni kutaka kuepusha shari ambalo kuendelea kwake kutaka kusimama dhidi ya Shein, chaguo la Dodoma kungesababisha visiwani na kwa muungano mzima. Nani angeendelea kumzawadia kwa ujeuri wake huo hata kipindi hiki alichochukua fomu za kugombea urais? Sioni tofauti ya Bilal na Augustine Ramadhani au Augustine Mahiga waliogombea wakiwa watu safi lakini wakabwagwa kwenye awamu ya kwanza huku hata watoto wa jana kwenye siasa wakipitishwa jambo ambalo ni aibu kwa wakongwe hawa.  Inashangaza ni kwanini wakongwe hawa kwenye fani zao hawakuliona hili sawa na ambavyo Dk Bilal hakuliona.
           Kwa kuzingatia ujio wa Bilal kwenye siasa za bara kama makamu wa rais, ingekuwa jambo la ajabu kama CCM wangempitisha kumrithi Kikwete. Pia litakuwa jambo la ajabu kama Bilal bado ana ndoto ya kulianzisha ima akiwa CCM au nje. Anachoweza kufanya –kama anahisi alitumiwa ili kuzuia mbio zake baadaye –ni kijiunga na upinzani kuongeza nguvu kwa Lowassa ambaye pia naye anatisha shaka kama atafikia malengo yake ya kuiadhibu CCM kwa kukataa kutumika kumfikisha kwenye malengo yake binafsi.
          Tumalizie kwa kusema wazi kuwa–kwa sasa–Bilal hana mvuto wala ubavu wa kuweza kufanya lolote kisiasa. Hivyo, wanaozusha kuwa ana mpango wa kuhamia upinzani–hata kama anao–wajua hautayumbisha CCM.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 23, 2015.

No comments: