The Chant of Savant

Tuesday 4 August 2015

Kijiwe chajitoa UKAUA


          Japo tulifanya siri, kwa taarifa yenu, Kijiwe kilikuwa ni mmojawapo wa wanachama wa Umoja wa Kaya wa Ukombozi Azimifu (UKAUA). Sasa baada ya wakubwa wake kuonyesha walivyo hovyo na ajabu kwa kukubali kuramba matapishi yao, rasmi kijiwe kinatangaza kujiondoa kwenye genge hili la maigizo.
          Mpemba ndiye analianzisha, “Yakhe sina raha mwenzenu leo. Nina hasira. Hata naweza nyotoa ntu roho Wallahi.”
          Mgosi Machungi anamuuliza, “Kwani kunani hadi utake kujinyotoa loho ndugu yangu?”
Mpemba anajibu, “Wakumbuka kuwa mie ndo nilitoa wazo tujiunge na UKAUA? Sasa kwa walivoua kila kitu kwa kunpwakia yule habithi walotwambia alikuwa fisadi untegemeani?”
“Alaa kumbe! Sasa timekueewa. Kwei nami nina hasia kiasi cha kuweza kupiga mtu zongo waahi. Sikutegemea kuwa wanaume wazima wangejivua nguo tena hadhaani kiasi hiki mgosi. Hapa nakuunga mkono azima kuwa na hasia.”
Mijjinga anakatua mic, “Mimi sikubaliani nanyi. Kwani kila mtu ana haki ya kujiunga na kuhama chama chochote na kila chama kina haki ya kumpokea yeyote. Kama wangemkatalia huyu Luwasha mnayogopa kumtaja ungekuwa ni ubaguzi na kinyume cha demokrasia.”
Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kumchomekea Mijjinga, “Halo halo! Ukisikia kuramba matapishi ndiyo huku. Yaani nyinyi mliokuwa mkisema huyo mpenzi wenu ni fisadi hakuna mfano leo ndiyo mnamtakasa kwa sababu binafsi na uroho wa madaraka! Ama kweli ukishangaa ya Mlema utaona ya Luwasha! Mnadhani mmepata au mmepatikana? Yetu macho na tutaona hapo Oktoba kama hamtalia kilio cha mbwa.”
Kapende anakwanyua mic, “Kusema ukweli hata mimi sijaelewa somo. Maana kwa tulivyokuwa tumembomoa jamaa, itakuwa shughuli kumjenga tena akakubalika mbele ya wachovu. Hili linanitia shaka kweli kweli.”
Mipawa anakatua mic, “Nami naona kama tumekwama kiasi cha kushindwa kujinasua. Ila kwa vile wengi hatukubaliani na uamuzi huu wa hasara, napendekeza Kijiwe kijotoe kwenye UKAUA maana wameishaua matarajio yetu kwa kuendekeza maslahi fiche.”
Msomi Mkatatamaa naye anaamua kula mic, “Kiakili, kimkakati hata kimantiki kilichofanyika ni sawa na kujipaka petroli halafu ukakatisha kwenye moto. Kwanza, Chama Cha Mafisadi (CCM) kinawajua mafisadi wake na  huyu jamaa akiwa kingozi. Hivyo, kitamkaanga kwa kuzidi kumuanika kiasi cha UKAUA kuja kujutia tamaa na upogo wake siku si nyingi. Kwanza, inashangaza kwa wale tuliodhani ni wasomi waliokubuhu kufanya upuuzi kama huu so to speak.”
Anapiga chafya na kuendelea, “Nimependa mlinganisho wa da Sofi hata kama sikubaliani naye kwa mengine. Ni kweli, kuna uwezekano tukashuhudia historia ya Lyatongolwa Mlema na alivyodedisha ENISSIARA Mageuzi ikijirudia. Nadhani anguko la kipindi hiki litakuwa kubwa hasa ikizingatiwa kuwa litahusisha vyama vinne tofauti na Mlema aliyeua kimoja kikaibuka CHAKUDEMA. Kwa ufupi naona kama Mzito Kabwela pamoja na uoza na uhovyo wake anaweza kuibuka kidedea baada ya unne huu kuadhirika na hatimaye kusambaratika. Hii ndiyo analysis yangu.”
Sofia anadakia, “Mmwagie kahawa msomi. Ama kweli leo Msomi umeonyesha usomi usio na kifani kaka yangu.”
Kanji naye anaamua kula mic, “Kumbe Sofi hapana jua Somi. Somi siku yote ongea vitu kuba kuba na ya maana sana. Hata mimi leo Somi nafurahisa sana roho yangu. Nakuna yeye sana.”
Mbwamwitu anadakia, “Kanji tafadhali. Eti Somi nakuna veve sana sasa nakuna vapi veve dugu yangu?” Kanji anacheka sana hasa kuona Mbwamwitu anavyomuiga na kupatia.
Anajibu, “Kwani Somi hapana kuna veve? Kama hapana kuna kwanini hapana pinga. Sasa sikia veve dugu yangu. Somi nakuna kila moja hapa. Hapana ona da Sofi nafurahi sana baada ya Somi kuna yeye?”
“Tafadhai Kanji. Kama Msomi amekukuna wewe siyo useme eti sote timekunwa. Badaa ya kujadii mambo makubwa sasa mmeeta mambo ya kukunwa. Kama amekukuna basi si ufurahi peke yako badaa ya kutiingiza wote?”
Mheshimiwa Bwege ambaye alikuwa akitabasamu anaamua kutia guu, “Waheshimiwa, kwanza tukubaliane. Uamuzi wa UKAUA kujiua kwa kukumbatia fisadi hauna faida kwa yeyote isipokuwa viongozi walioingizwa mkenge. Sijui wamekatiwa kitu hata sielewi. Mimi nadhani kama kuna yeyote ambaye alikuwa na nia ya kusaidi upingaji kuondoa magamba kwenye ulaji alipaswa kufanya kitu alichofanya swahiba yangu wa siku nyingi pale kwa Manyang’au, Laila Odingo ambaye alipoenguliwa KANUU alijiunga na upingaji na kusema, ‘Kibaka Tosa’ ua upingaji ulishinda. Huyu anayeusaka urahis hata kwa kuua upingaji ni tamaa na visasi vinavyomsumbua. Wala hata hafai kusema ule ukweli. Na wakimpitisha mie narejesha kadi na kuachana na siasa za uchumiatumbo.”
Mgosi anarejea, “Ndugu yangu mgosi Bwege hatina haja ya kujitoa kwenye siasa. Maana siasa ndiyo maisha yenyewe. Mie naona tijiondoe na kuanzisha mkakati mwingine peke yetu kama kijiwe badaa ya kupotezeana muda na kuzungukana kama UKAUA ambao kimsingi wamejiua. Tisikubai kufa nao kisiasa.”
Mijjinga hakubaliani na wazo la Mgosi. Anaamua kurejea kwa chati, “Mgosi sikubaliani na ushauri wako. Nadhani, kama tutakuwa wakweli kwenye nafsi zetu,kila mtu angetaka magamba yadondoshwe hata kama ni kwa kumsimamisha shetani ilmradi yaondoke. Nadhani hili ni la msingi.”
Kanji anachomekea, “Sasa kana natumia setani naondoa setani je kama setani yako nageuka veve takwenda vapi? Kama tumia akili basi napanga binu ya kukantrol setani yako. Sasa UKAUA nafungua witu yote kwa setani nategemea nini baada ya chaguzi?”

Kijiwe kikiwa kinanoga si ulipita msafara wa Luwasha akitoka kuchukua fomu. Acha tumjambishie!
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 5, 2015.

No comments: