Saturday, 22 August 2015

Mlevi ambeep Luwasa


Bwana Eddie Ngonyani Luwasa,
Kwanza, nakusalimu. CCM hoyee sorry, CHANDIMU, sorry, UKAUA hoyeee! Kaka, usidhani nakusanifu au kukuchulia. Unajua mtu akivaa magamba, sorry, magwanda mengi anachanganya kidogo. Mbona huu ulabu na bangi vimenichukua mapema hata kabla ya kusend message? Tuyaache. Kwa vile nimeishawabeep, kuwatweet hata kuwatwangia mkuu na Dk Joni Kanyawaji Makufuli, sasa nimeona ni zamu yangu kuchonga nawe juu ya masuala mbali mbali.
          Mheshimiwa mtarajika, nilikusikia juzi ukiwa kwa akina twambombo tununu kuwa una mpango wa kuibadili Bongo kuwa kama Uswizi wazito wanakoficha mishiko. Nilioposikia hivi nilishangaa kidogo ila nikasema nikiwasiliana nawe utanipa jibu. Naunga mkono mpango wako japo niliwahi kufanya hivyo mara mbili na walevi wenzangu tukaishia kuumia. Mara ya kwanza tuliingizwa mjini na jamaa moja tapeli wa kisiasa aliyejipachika jina la Bwana Mafweza wakati alikuwa msanii na kopakopa wa kawaida. Baada ya kugundulika kuwa kumbe hekalu alilokuwa akiishi lilijengwa kwa mkopo ambao alishindwa kuulipa nilidharau.
           Mara ya pili nilitapeliwa na mtu ambaye unamjua sana. Si walevi tuliahidiwa Maisha Bien kwa Wote Apeche (MBWA) chini ya ANGUKA. Hatukujua kumbe tungeishia kuangushwa na kuwa mbwa kama kifupi kilivyo. Hayo tuyaache.
          Nilivyokusikia juzi nilishangaa na kujiuliza kama nawe hutafanya kama hao matapeli wengine. Je kipindi kile mkipunyua ule uchache wa Richmonduli ndiyo mlikuwa mnaanza sera hii ya kugeuza kaya kuwa Uswizi ama vipi? Maana kuna kipindi nilisikia ukisema kuwa chini ya Richmonduli mliokoa njuluku nyingi wakati waliofaidika ni akina Kagoda na wengine au vipi? Je bado unaweza kusimama mimbarini ukasema kuwa dili la Richmonduli lilikuwa la maana kwa kaya au ni yale yale ya kusema kuwa uhusiki isipokuwa bosi wako aliyekuzuia kuvunja mkataba. Je ni kweli kuwa –kwa usongo wa kaya –ulitaka kuuvunjilia mbali ule mkataba au kamba? Wapo wanaosema kuwa kama ni kweli ulitaka kufanya hivyo, ni kwanini uliendelea kumtumikia njemba mliyepingana badala ya kukitoa na kumchomea utambi kwa walevi au kuna kitu unaficha mkuu?
          Pia nilikusikia ukimkandia swahiba yako ambaye hamjakutana uchochoroni kuwa amebemenda uchumi. Je ulimaanisha nini wakati ulipokuwa Washington kwa Joji Kichaka ukihojiwa ulimwagia ujiko kuwa amejenga barabara na ameweza kuvutia marais wa Uchina, Marikani hata Joji Kichaka mwenyewe? Je wakati ule alikuwa anaonekana mzuri kwa vile mlikuwa timu moja na sasa umejiondoa na kuanza kumtupia mawe. Je unadhani utafanikiwa? Je unadhani walevi watakuamini au watakukaanga kwa maneno yako?
          Juzi nilikusikia ukisema kuwa hutaki mchezo. Ulidhani CCM na Dk Kanywaji wanacheza makidamakida kama yule binti Microphone wa mjengoni? Hebu nimegee kidogo. Hivi yule kitegemezi wako alifanyafanyaje hadi akaukwaa ubalozi? Je yule kitegemezi wa Belly of Tembo (BoT) bado anaendelea kupiga mzigo pale? Mbona hugusii ufisadi kwenye sera yako ya kufanya kaya iwe Uswizi kama siyo Uswazi? Je bado mnawasiliana na kuchat na swahiba yako Njaa Kaya? Juzi nilisikia hata akina Ngeleza na washirika zako wengi wa zamani wakikucheka huku wakimuunga mkono mpinzani wako. Je hili limekustua au umeamua kuwapuuzia kama walivyokushiti?
          Muishiwa, sorry, mhishimiwa, kabla sijasahau, hivi ulimsikia Mapepe Ninaye juzi akitetea uamuzi wa kufyeka jina lako kuwa ulitumia mabilioni kuusaka urahis? Je ni kweli? Kama ulitumia mabilioni je uliyanyakaje kaka? Kama ni rongorongo, unajitetea vipi?
          Kwa vile utanijibu, naomba niishie hapa nikiongoja majibu yako.
Ubarikiwe sana muishiwa.
Chanzo:Nipashe Agosti 22, 2015.

No comments: