The Chant of Savant

Monday 31 August 2015

Kwanini Mkapa anakataa kukua?

Image result for photos of benjamin mkapa 

          Matusi yaliyoporomoshwa na rais mstaafu mwenye kashfa ya kujitwalia Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira Benjamin Mkapa hivi karibuni kwenye kufungua kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) yameacha wengi vinywa wazi.  Mkapa alikaririwa akiwaita wapinzana malofa na wapumbavu asijue alikuwa akijichamba asijue? Hatutachambua maneno malofa na wapumbavu kutokana na urahisi wake kueleweka. Je tukiangalia hawa wapinzani na Mkapa aliyekwisha achia dola tena kwa aibu ya wizi wa kijinga nani lofa na mpumbavu? Ngoja tuache wasomaji waamue wenyewe. Kwani hatutaki kumlaumu Mkapa kwa kurudia alichofanya.

          Pili, kwa rekodi ya Mkapa kisiasa, wengi hawakutarajia kama angepata mshipa achia mbali jeuri ya kutukana wenzake hadharani tena bila sababu. Wapo wanaoona kama Mkapa alipaswa abwate ili kuwaridhisha watakaoingia madarakani wamkingie kifua kama alivyofanya rais anayeondoka Jakaya Kikwete baada ya kubainika yeye marafiki na familia yake walivyotumia uwekezaji kulihujumu taifa. Ni aibu kiasi gani kwa mtu anayetegemewa awe mfano wa kuiga anaongea kama wahuni na wapiga debe wa vijiweni.

          Tatu, kwa hadhi ya Mkapa kama rais wa zamani–hata kama ana madudu na mazabe yake aliyotenda kutokana na upogo na tamaa–hakupaswa kuwa bingwa wa matusi na mipasho jambo ambalo linaweza kufanya wenzake wamuite mtu mzima hovyo.

          Nne, kwa umri wake alipaswa awe ameishajua jinsi ya kuchagua maneno ya kuongea na ya kutoongea. Si jambo la maana kwa mzee tena wa hadhi ya Mkapa kuongea kama watoto wa vijiweni au wale wazee waliokataa kukua. Sijui kwa matusi ya Mkapa ametufundisha nini kama jamii aliyowahi kuitawala baada ya kushindwa kuiongoza?

          Tano, Mkapa alipaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kutenda makosa ya jinai mojawapo likiwa ni matusi na kutumia lugha za shari. Sijui Mkapa amekumbwa na nini? Maana huko nyuma hakuwa hivi! Hata mwl Julius Nyerere aliyempigia kampeni baada ya kugundua kuwa alikuwa hauziki bila kubebwa, hakutumia lugha za hovyo na aibu kama hizi anazotumia Mkapa.

          Sita, Mkapa anapaswa aambiwe kuwa lugha aliyotumiwa licha ya kutokuwa saizi yake si ya kistaarabu wala haina cha maana cha kulifundisha taifa zaidi ya kumvua nguo na kumuonyesha kama mtu muhuni na mpayukaji asiyejua jinsi ya kuzuia ulimi wake. Kama hakuwa na la kusema si angejinyamazia kuliko kumwaga upupu.

          Saba, kama Mkapa atataka asiendelee kueleweka vibaya, basi awaombe msamaha wapinzani aliowatukana na watanzania aliowanyosha utovu wa nidhamu tena hadharani. Hivi kama ni ulofa na upumbavu, kuna ulofa na upumbavu kama kuingia kwenye mikataba ya kijambazi ya uwekezaji ambayo haina maslahi kwa taifa? Je kuna ulofa wa kisiasa kama kutumia matusi na maguvu kama ambavyo inaanza kubainika bila sababu ambapo wahusika wameishaanza hata kutumia polisi kuwahujumu wapinzani? Ama kweli mzoea vya kunyonga vya kuchinja haviwezi. Sijui kama wapinzani ni malofa na wapumbavu kama anavyowaelezea Mkapa wakati wameizidi CCM yake kete wakawasomba mawaziri wao wakuu wawili kwa mpigo akiwamo mshirika , rafiki na waziri mkuu wa pekee wa Mkapa Fredrick Sumaye ambaye ameamua kujitenga na dhuluma na kushindwa kusoma alama za nyakati.  Hivi ikitokea wapinzani wakashinda Mkapa ataweka wapi sura yake? Tulitegemea wazee aina ya Mkapa wahubiri haki ,upendo, amani, heshima, maadili, haki, kumbe wapi. Badala yake wanahubiri maangamizi, matusi, uchokozi na vurugu. Tunamshauri Dk John Pombe Magufuli ajitenge na watu wa namna hii asionekane yu sawa na wao au ni kikaragosi chao. Hatudhani kama Magufuli ni mchovu hivi kiasi cha kuhitaji kubebwa na wale waliobebwa.

          Namheshimu sana mzee Mkapa ila kwa hili alilofanya, kwa mapenzi yangu makubwa kwake, sitamuogopa wala kumdanganya, amechemsha tena vibaya sana. Hata huyu aliyempigia kampeni kwa lugha za mipasho, kashfa, matusi na ukosefu wa busara hamsaidii zaidi ya kumuumiza. Badala ya kujifunza kwa Nyerere aliyewahi hata kuambiwa amebeba kinyago cha mpapure bila kurusha ngumi wala matusi, Mkapa anazidi kujivua nguo tena hadharani. Hakika hii siyo saizi yake.  Hata mzee Jangala kwenye maigizo yake hawezi kufikia uhovyo kama alioonyesha Mkapa.

          Tuamalize kwa kumtaka Mkapa aombe msamaha yaishe. Maana waingereza wana msemo kuwa ukiishi kwenye nyumba ya vioo usiwachokoze vichaa. Bado watu wanajua madudu yake ya NBC, Kiwila, EOTL na mengine mengi. Ashukuru Mungu tuna siasa za kulindana tokana na wote kuwa waovu. Vinginevyo angepata wapi hiyo jeuri mtu kama yeye.  Wapinzani wanaweza kuamua kama mbaya mbaya wakamjibu kizembe kama alivyofanya akaumbuka zaidi. Tunawashauri wasimjibu Mkapa kwa vile lugha aliyotumia siyo saizi yao. Sana sana walipaswa kwenda mahakamani kuweka katazo Mkapa asishiriki kampeni kwa vile hana udhu wala uwezo wa kufanya hivyo bila kuvunja sheria.
Chanzo: Dira Agosti 31, 2015.

2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Hakika Mungu ubariki uchaguzi huu, watu wote pia nchi yetu Tanzania!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Da Yasinta,
Naamini mhusika amesikia ingawa ni jukumu la watanzania hasa watawala kutenda haki.